Chachu Ombara
JF-Expert Member
- Dec 11, 2012
- 6,042
- 10,787
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera limewasimamisha kazi Watendaji sita wa Halmashauri kupisha uchunguzi wa upotevu na ubadhirifu wa milioni 851 za mfuko wa barabara, Mfuko wa Afya, na Mfuko wa Jimbo zilizotumika bila kufuata utaratibu na kanuni za wa fedha.
Watendaji hao sita waliosimamishwa katika kikao cha Baraza la Madiwani cha tarehe 28.01.2016 walihusika na ubadhilifu wa fedha hizo kwa kuzitumia bila kufuata kanuni, taratibu na sheria za kuomba idhini ya kuhamisha vifungu vya fedha au kubadilisha matumizi yake kutoka fungu moja kwenda fungu lingine.
Hayo yalibainishwa na Kamati ya Wataalamu sita iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa Mhe. Mongella katika kikao cha Bodi ya Barabara kilichofanyika tarehe 21.01.2016 Mkoani Kagera na kuiagiza Kamati hiyo kuchunguza upotevu wa fedha hizo mara baada ya Mhandisi wa Halmashauri hiyo kuwasilisha taarifa ya matengenezo ya barabara na madaraja kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Kamati hiyo ya wajumbe sita iliyoongozwa na Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera Bw. Sabora Wambura na ilipewa siku tano iwe imekamilisha taarifa yake. Aidha, taarifa ya Kamati hiyo iliwasilishwa mbele ya Mkuu wa Mkoa, Baraza la Madiwani, Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Kamati ya Ulinzi na Usalaama ya Mkoa na Wilaya tarehe 27.01.2016.
Katika kikao hicho cha kupokea taarifa ya ubadhirifu wa shilingi milioni 851, Watendaji waliohusika walihojiwa mara baada ya taarifa kuwasilishwa na kuonekana walitumia fedha hizo kinyume na utaratibu wa fedha, katika mahojiano hayo walikiri kuwa utaratibu wa fedha haukufuatwa na kukiri makosa yao.
Mkuu wa Mkoa Mhe. Mongella mara baada ya kuwahoji alikubaliana na Baraza la Madiwani kuwa watendaji hao wanatakiwa kuwajibishwa na kuliagiza Baraza hilo kukaa kikao na kuamua hatua ya kuchukua kwa wahusika wote kwani mamlaka ya kuwawajibisha Wakuu wa Idara wa halmashauri ipo kwa Madiwani wenyewe.
Aidha, alimwagiza Katibu Tawala Mkoa kumwadikia barua Katibu Mkuu TAMISEMI ili aweze kumchukulia hatua Mkurugenzi Mtendaji Bi Gradis Dyamvunye aliyekuwepo wakati huo na kuomba aliyekuwa Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri hiyo Robert Massoro kurudishwa kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za mfuko wa barabara pia kuomba ufanyike ukaguzi maalum mara moaja.
Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika tarehe 28.01.2016 kikiongozwa na Mwenyekiti wake Mustapha Ngeze kiliamua kwa kauli moja kuwasimamisha kazi kupisha uchunguzi wa upotevu wa milioni 851 watendaji wafuatao; Idara ya fedha ni Bw. Jonathan Katunzi (Mweka Hazina), Selialisi Mutalemwa, Idara ya Ujenzi, Bw. Deus Bizibu, Elimu Sekondari ni Bw. Lucas Mzungu, Mifugo ni Dk. Kisanga Makigo na Bw.Mustapha Sabuni Afisa Mipango.
Mchanganuo wa fedha zilizotumika bila kufuata utaratibu na kanuni za fedha ni Shilingi milioni 200 za mfuko maalum wa barabara zilizokuwa zimeletwa kwa ajili ya kujenga daraja la Kyamabale, Milioni 176 za mfuko wa barabara kwa ajili ya kutengeneza na kukarabati barabara, Milioni 168 za mfuko wa Jimbo, na Milioni 307 za mfuko wa Afya (Busket Fund)