Wapinzani wanena

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,009
Wapinzani wanena

na Peter Nyanje, Dodoma
Tanzania Daima

WAKATI Rais Jakaya Kikwete akikuna kichwa kuhusiana na muundo wa Baraza la Mawaziri analotarajia kuliundwa upya, kambi ya ya upinzani bungeni jana ilitoa ushauri kwake na kusema itamshangaa sana Rais kama atawateua watu ambao wao waliwataja katika orodha ya mafisadi.
Hayo yalibainishwa jana na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF) na msaidizi wake, Dk. Wilbrod Slaa (Karatu-CHADEMA), walipozungumza na waandishi wa habari hapa.

Dk. Slaa alisema Rais anapaswa kutambua hata kama watu hao yeye anawaona safi, lakini jamii inaweza kuwaona vinginevyo na ni vema sasa baada ya kashfa ya Richmond, kuunda timu itakayosaidia kulijenga taifa.

Alisema wao kama wapinzani, waliwataja kwa majina viongozi kadhaa wa serikali na kuorodhesha tuhuma zinazowakabili, jambo lililozusha mjadala mkubwa nchini.

Kwa upande wake, Hamad Rashid alimuonya Rais Kikwete kuangalia ukubwa wa Baraza la Mawaziri, kwani imedhihirika kuwa baraza lililopita, lililokuwa na zaidi ya watu 60, lilikuwa mzigo kwa Watanzania.

Alisema yaliyotokea katika siku za hivi karibuni yanaonyesha kuwa sasa wananchi wameanza kujua haki zao nyingine, kama ile ya matokeo ya kura zao baada ya kuzipiga.

"Awali wananchi walikuwa wanajua haki moja tu - ya kupiga kura. Hawakuwa wanajua haki yao baada ya kupiga kura, lakini kwa juhudi zetu (wapinzani) na kwa hakika kazi kubwa iliyofanywa na vyombo vya habari, wananchi sasa wameanza kujua haki zao nyingine," alisema.

Alisema inashangaza kuwa nchi maskini kama Tanzania ina Baraza kubwa la Mawaziri, wakati nchi tajiri kama Uingereza inayoongoza kwa kusaidia bajeti ya Tanzania, ina baraza dogo la mawaziri.

Alisema kwa mujibu wa taratibu za Uingereza, Waziri Mkuu anaruhusiwa kuchagua mawaziri wasiozidi 20 na anakuwa na ruhusa ya kuchagua mmoja wa ziada iwapo atatoa hoja inayoonyesha kuwa anamuhitaji mtu wa ziada katika baraza lake.

"Baada ya hao 21, akiongeza mwingine Waziri Mkuu anawajibuka kulipia gharama zake zote yeye mwenyewe binafsi kutoka katika fedha zake na si za ofisi yake au serikali," alisema.

Wakizungumzia suala la sakata la ufisadi katiba Benki Kuu ya Tanzania (BoT), walisema wametaka Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, naye ajumuishwe kwenye uchunguzi katika suala hilo.

Dk Slaa alisema suala la Richmond linapaswa kuwa mwanzo wa kuwashughulikia mafisadi nchini.

Alisema anazo taarifa kuwa baadhi ya watu waliotajwa kwenye kashfa ya EPA wameshaanza kuhojiwa na akaunti zao zimefungwa.

Hata hivyo, alisema kuwa zipo taarifa pia kuwa kuna njama za kupoteza nyaraka ili kuwalinda watu kadhaa waliohusika katika kashfa hiyo.

Alisema kilichogundulika katika Richmond na EPA ni masuala madogo mno yanayomaliza rasilimali za nchi na kutaka uchunguzi upanuliwe kwenye maeneo mengine, ili kuhakikisha kuwa wote wanaotumia rasilimali hizo kibinafsi ‘wanasafishwa'.

Akifafanua, alisema kuwa kwa mujibu wa katiba, Mkapa ana kinga ya kutoshitakiwa kwa mambo aliyoyatenda kama Rais, lakini linapokuja suala la yeye kujihusisha na biashara binafsi, kinga hiyo inaondoka.

Alisema wanazo taarifa kuwa Mkapa alijichukulia asilimia 85 ya hisa la Kiwira Coal Mine na kuanzisha kampuni ya kibiashara wakati akiwa Ikulu.

Alisema kumbukumbu katika wakala wa kuandikisha biashara yaani Brela, zinaonyesha kuwa Mkapa aliandikisha kampuni hiyo si kama Rais, bali kama Benjamin Mkapa aliyetajwa kuwa ni mjasiriamali.

"Hili halimhusu Rais mstaafu, linamhusu mjasiriamali, hatuwezi kuliweka suala hili katika kazi za urais wa Mkapa kiasi kwamba nalo liwe na kinga. Hatuwezi kumshitaki alipofanya kazi zake za urais lakini akifanya biashara tunaweza kumshitaki.

"Ni vema sasa kwa kuwa tumeanza na Richmond tukaendelea mbale na kuhakikisha tunawafikia wale wote waliozitumia vibaya rasilimali za nchi hii," alisema Dk. Slaa.

Alisema matendo ya Mkapa yalilibebesha taifa mizigo mikubwa, na mtu aliyelibebesha taifa mizigo mikubwa kama hiyo hawezi kuachwa bila kuwajibishwa.

Wakati huo huo, kuna taarifa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (Takukuru), Edward Hosea, amemwandikia Rais Jakaya Kikwete akiomba kujiuzulu.

Akizungumzia hilo, Dk Slaa alisema iwapo ni kweli Hosea amemwandikia barua Rais Kikwete kuomba kujiuzulu, haitoshi.

Dk Slaa alisema kama viongozi wote wa Takukuru hawataondolewa na badala yake kuundwe timu mpya, yeye binafsi hatokuwa na imani na chombo hicho.

Alisema yaliyotendeka ndani ya chombo hicho hayakufanywa na mtu mmoja, hivyo kumwondoa Hosea itakuwa ni sawa na kuendelea na mtandao uliokuwapo tangu awali.

Habari ambazo hadi jana mchana zilikuwa hazijathibitishwa, zilieleza kuwa Hosea alikuwa ameomba kujiuzulu na msaidizi wake, Lilian Mashaka, aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo.

Aidha, Dk. Slaa alisema matokeo ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge kuhusu Richmond, yanaonyesha kuwa taasisi zilizopewa dhamana ya kuchunguza suala la EPA, hazina uwezo wa kuifanya kazi hiyo ipasavyo.

Taasisi hizo ni Ofisi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Mkurugenzi wa Takukuru walioagizwa na Rais kuifanya kazi hiyo kwa muda wa miezi sita, ili kupata ushahidi wa kimahakama utakaosaidia kuwafikisha wahusika mahakamani.

Dk. Slaa alisema ripoti ya Richmiond imeonyesha kuwa kiuadilifu, watu hao wote wamekosa sifa ya kuifanya kazi hiyo na kushauri kiundwe chombo kingine huru au kialikwe chombo kingine kutoka nje kuifanya kazi hiyo.

Alipotakiwa afafanue, Dk. Slaa alisema iwapo itapenda, serikali inaweza kuialika Interpol kuifanya kazi hiyo kwa sababu ufisadi wa EPA unavuka mipaka ya Tanzania.

Pia alisema BoT ilipoungua, Scotland Yard ya Uingereza iliitwa kuja kusaidia upelelezi na haitashangaza iwapo wataitwa na sasa ili kusaidia katika upelelezi wa EPA, hasa katika mazingira yanayoonyesha kuwa hakuna chombo hapa nchini kinachoweza kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi unaotakiwa.
 
Back
Top Bottom