Wapinzani hawaelewi kwamba siku ya kufa nyani miti yote msituni inateleza?

security guard

JF-Expert Member
Sep 27, 2011
799
603
Wapinzani hawaelewi kwamba siku ya

kufa nyani miti yote msituni inateleza?


Na Charles Charles


MKUTANO wa tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza Aprili 19 mjini Dodoma, unaendelea mjini Dodoma huku kilio cha wabunge wa upinzani kikiwa ni kilekile; kupinga kwa nguvu zao zote kutotangazwa ‘live’ na vituo vya redio na televisheni kwa vikao vya chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi.


Wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, (Utawala Bora, Utumishi na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa au Tamisemi) kwa mfano, wabunge takribani wote wa upinzani waliopata nafasi hiyo walipinga vikao hivyo kutotangazwa moja kwa moja wakidai wananchi hawavioni!


Hatua ya wabunge hao kuanza tena kuchangia hoja bungeni, inakuja baada ya awali kususia kufanya hivyo wakati wa mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa ili kumuunga mkono bosi wao ambaye ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.


Mbunge huyo wa Hai mkoani Kilimanjaro ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), aligoma kusoma hotuba mbadala ya kambi yake na kutoka nje ya ukumbi ili pamoja na mambo mengine, kupinga bunge hilo kutorushwa ‘live’ redioni na katika televisheni.


Kati ya wabunge waliozungumza na kuunga mkono hoja hiyo ya Mbowe wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa aliyekwenda mbali zaidi kwa kulisifia bunge la tisa kwa kurushwa ‘live’ na vyombo hivyo vya habari.


“Enzi za (uspika wa Mheshimiwa Samwel) Sitta wabunge walikuwa na uhuru na bunge lilirushwa ‘live’, lakini serikali hii (ya Awamu ya Tano) inakandamiza uwazi na kuficha madudu (ambayo hata hivyo alishindwa kuyataja). Huo ni woga na inachokificha hakieleweki, huku ni kukanyaga utawala bora”, alisema na kuongeza:


“Bunge siyo mkutano wa unyago. Hapa tunazungumzia maslahi ya Watanzania na matumizi ya fedha zao za kodi. Mnaficha nini (ili) Watanzania wasikione?”


Mbunge huyo alisema “pamoja na udhaifu wa Serikali ya Awamu ya Nne, bado Rais (Jakaya) Kikwete (wakati huo) alikuwa na ujasiiri wa kuruhusu wabunge kuikosoa serikali yake kwa uwazi.


“Leo mnakuja na kusema ‘Hapa Kazi Tu’ huku mkiogopa kukosolewa. Wakati tunamkosoa Kikwete mliufyata na kukaa kimya. Inawezekana leo hata (Rais John) Magufuli akidondosha kijiko mtampigia makofi kwa ajili ya woga wenu”, alisema, kauli iliyokuwa ikiwalenga zaidi wabunge wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi au CCM.


Kana kwamba haitoshi, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema naye alidai kuwa bunge la hivi sasa halina uhuru na tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani pia hakuna utawala bora na tatu, mawaziri wake wote wamekuwa wakifanya kazi kwa woga.


“Mawaziri (wa sasa nao) wanafanya kazi kwa woga na wengi wanapinga (pia) utaratibu wa utendaji wa serikali hii ikiwemo kutorushwa ‘live’ matangazo ya bunge”, alisema, madai ambayo hata hivyo yalipingwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dk. Khamis Kigwangalla aliyemwomba Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kumtaka mbunge huyo athibitishe ama afute kauli yake.


“Aweke ushahidi hapa ili tuwagundue wanafiki katika serikali hii na kama mbunge amesema uongo aondoe maneno hayo katika hotuba yake”, alisema naibu waziri huyo, jambo ambalo Lema alishindwa kulithibitisha huku akiokolewa na wabunge wenzake wa kambi hiyo waliopiga kelele kama watoto wa chekechea kwa kusema “wa kwanza ni wewe mwenyewe”.


Katika orodha hiyo pia wamo Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Tunza Malapo na Mbunge wa Konde kutoka chama cha Civic United Front (CUF), Khatibu Saidi Haji aliyefikia mpaka hatua ya kumshutumu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye kuwa ndiye ameishauri serikali isitishe matangazo hayo ya ‘live’ kwa vikao vya bunge.


Hiyo ndiyo michango iliyotolewa ukumbini na wabunge hao wa upinzani, wale ambao badala ya kuwasemea wananchi ili serikali ifahamu matatizo au mahitaji yaliyopo kwenye majimbo yao, wao waliishia ‘kulialia’ kama watoto walionyimwa pipi.


Nimekuwa nikieleza mara kadhaa kuhusu ukweli kwamba Msigwa yuko bungeni siyo kwa sababu ana uchungu sana na maendeleo ya jimbo la Iringa Mjini, na pia hana udhati wala uthabiti wowote wa kutaka kutatua changamoto zinazowakabili wananchi, badala yake anatanguliza kwanza mbele maslahi ya kisiasa au familia yake.


Aidha, nimekuwa nikieleza mara kwa mara kwamba hata Lema na wabunge wengine wa Chadema, CUF na ndugu yangu James Mbatia wa NCCR – Mageuzi wanachofanya ni kuwadanganya wapiga kura wao kwa kupiga kelele nyingi ama ‘kuwachezea mazingaombwe’ ya kisiasa, lakini wanachotaka hasa ni kuendelea kushika nafasi hizo ili wazidi kujinufaisha wao wenyewe.


Ndiyo maana siuoni uhusiano wowote uliopo kati ya shughuli za bunge, wabunge na kutangazwa au kuonyeshwa ‘live’ kwa vikao vyao na vituo vya televisheni ama redio nchini.


Kama nilivyowahi kubainisha huko nyuma, Ibara ya 63(3)(a) – (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Toleo la 2005 inayotumika sasa inaeleza kuwa “Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake bunge laweza-


(a) kumuuliza waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika wajibu wake;


(b)kujadili utekelezaji wa kila wizara wakati wa mkutano wa bunge wa kila mwaka wa bajeti;


(c) kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo;


(d)kutunga sheria pale ambapo utekelezaji (wake) unahitaji kuwepo sheria; na


(e) kujadili na kuridhia mikataba yote inayohusu Jamhuri ya Muungano na ambayo kwa masharti yake inahitaji kuridhiwa” (mwisho wa kunukuu).


Hayo ndiyo majukumu makubwa matano ya bunge hilo la bajeti ya serikali kwa mwaka 2016/2017. Hayo ndiyo mambo yanayopaswa kujadiliwa na wabunge bila ya kujali kama vikao vyao vinatangazwa au kuonyeshwa moja kwa moja na redio na televisheni na siyo vinginevyo.


Msigwa aliyesema kwamba “bunge siyo mkutano wa unyago” ila linazungumzia maslahi au mahitaji ya Watanzania na matumizi ya fedha zao za kodi hata miye ninakubali, lakini sikubaliani hata kidogo na juhudi zake za kutaka kupotosha ukweli kuwa vikao vyake navyo lazima vitangazwe ‘live’ na vyombo hivyo vya habari.


Mfano ni vikao vyote vya Kamati za Kudumu za Bunge ambavyo hakuna hata kimoja kinachorushwa ‘live’ na TV wala kutangazwa moja kwa moja na kituo chochote cha redio nchini, lakini siku zote zinaendesha mikutano yake yote na kumalizika kwa usahihi.


Mbali na vikao vya kamati zao hizo, Msigwa anafahamu pia kuwa hakuna kikao chochote kwa mfano cha Kamati Kuu ya Chadema kilichowahi kurushwa ‘live’ iwe na kituo cha televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC 1), Star TV, ITV, Azam TV, Clouds TV na kadhalika, lakini hakuna hata siku moja ambayo amewahi kuipinga hali hiyo kwa sababu ni Mjumbe wa Kamati Kuu hiyohiyo.


Bunge kama chombo cha uwakilishi wa wananchi kinachotajwa katika Ibara za 62(1) – (2) na 66(1)(a) – (f) za Katiba ya Tanzania madaraka yake yameelezwa, tena kikamilifu katika Ibara ya 63(3)(a) – (e) na hivyo kusema vinginevyo ni uzushi, uongo na upotoshaji mkubwa unaolenga kuivuruga nchi yetu kwa misingi ya kisiasa.


Wote wanaofanya hivyo kama akina Peter Msigwa, Godbless Lema, Khatibu Saidi Haji, Tunza Malapo na wengineo wanataka Tanzania isambaratike kama kishada kilichokwenda harijojo, hatua ambayo hata wao haiwezi kuwanufaisha iwe kisiasa, kidini wala kiuchumi katika kipindi hiki ama baadaye.


Katika hali hiyo, wabunge hao wanataka Tanzania ibaki nyuma kwa maendeleo ya uchumi na mahitaji mengine, jambo ambalo litasababisha wananchi wazidi kubaki masikini na kuishi kwenye nchi isiyokuwa na mbele wala nyuma.


Tofauti na madai hayo ya uzushi, uongo na upotoshaji yanayotoka kwenye vinywa vya wabunge hao wa genge linalojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Watanzania duniani kote wanaridhika kwa kiwango kikubwa kabisa na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano iliyoanza kazi hapo Novemba 5, mwaka jana.


Wanaridhishwa kwa namna zote na uongozi wa Rais John Magufuli, utendaji wa mawaziri wake au serikali katika ujumla wake wote, hivyo wabunge wanaosimama na kuchangia upotoshaji hawawezi kuwadanganya ama kuwashawishi wananchi ili waunge mkono uongo wao.


Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano unatimiza wajibu wake wote siyo kwa maneno isipokuwa kwa vitendo, hivyo umejipenyeza katika mioyo ya Watanzania nchini kote na mtu anayekuja na malengo ya kutaka ‘aichafue’ kwa namna moja ama nyingine huyo atakuwa adui yao mkubwa.


Wakati akigombea nafasi hiyo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka jana, Magufuli aliyekuwa Waziri wa Ujenzi aliahidi kufanya kazi kubwa ya kupambana na kero zote zilizokuwa zikiwakera wananchi ukiwemo ufisadi, rushwa, tatizo la ajira na kupambana na umasikini, mambo ambayo kila Mtanzania hivi sasa anaona jinsi yanavyokabiliwa kwa nguvu na serikali iliyopo madarakani.


Wanaona jinsi Serikali ya Awamu ya Tano inavyopambana kwa namna zote na wafanyabiashara ambao kwa miaka mingi walijijengea utamaduni wa kutolipa kodi zao, wengi wakifanya hivyo siyo kwa sababu hawajui ila kutaka kutajirika kinyume cha sheria.


Ushahidi wa kazi kubwa inayofanywa na serikali ya sasa ni pamoja na ongezeko la makusanyo ya kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kupanda kwa ufanisi wa kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kurejea kwa nidhamu na uwajibikaji kazini kwa watumishi wa sekta yote ya umma na kadhalika.


Leo tunapoona wabunge wakidhani eti mahitaji ya wananchi ni kuonyeshwa ‘live’ kwa vikao vyao kama akina Peter Msigwa, Godbless Lema, Khatibu Saidi Haji au Tunza Malapo kwa hakika wamejeruhiwa kisiasa na utendaji ama kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo wanahofia vyama vyao kwamba ‘vitakufa’ kama NCCR – Mageuzi ‘ilivyokufa’ mwaka 1999.


Tofauti na ilivyokuwa katika kipindi kile cha kuanzia mwaka 2008 – 2015 wakati vyama vyao vilipopata nguvu nyingi kisiasa hasa kwa Chadema, mambo hivi sasa ni magumu huku wafuasi wao wakimiminika CCM au kuachana mbali na ushabiki wowote wa itikadi na kuimba “Hapa Kazi Tu”.


Msigwa kwa mfano anajua alivyoshinda ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa hisani au kwa kubebwa na wana CCM, na pia anaelewa jinsi alivyopata ushindi huo mwaka jana kwa njia zote haramu.


Anafahamu mwaka 2010 alizawadiwa ushindi huo na mgogoro wa kijinga uliokuwa ukiitafuna CCM na viongozi wake, halafu ilipofika mwaka jana akashinda siyo kwa sababu anapendwa sana ila waliompa ushindi huo ni viongozi waandamizi wa CCM waliokuwa mamluki wa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.


Yeye na wasaliti hao wa CCM waliingia ‘mkataba’ wa maneno kwamba agombee ubunge kwa mara yake ya mwisho hapo Iringa Mjini, halafu ikifika mwaka 2020 ahamie Isimani na kumwachia mmoja kati ya viongozi hao mamluki katika jimbo lake hilo la sasa akidhani atashinda.


Ndiyo maana kilichofanywa na wasaliti hao wa CCM ni kutumia nguvu zao zote ili kumpa ushindi huo wa hujuma kwa chama chao, kazi iliyofanyika mchana kutwa mpaka usiku wa manane ili kukidhi matakwa yao hayo.


Hata hivyo bahati mbaya ni kuwa ‘mchezo’ wao ule ulifanikiwa katika uchaguzi huo mkuu wa rais, wabunge na madiwani uliofanyika Oktoba 25, 2015, lakini hauwezi tena kufanikiwa mwaka 2020, hivyo ‘kigogo’ huyo wa CCM aliyekuwa ‘kocha’ na mfadhili mkuu wa ‘gemu’ hilo ni vizuri angefahamu kwamba ‘imekula kwake’.


Sitaki kulijadili suala hilo kwa kina kwa sababu lina muda wake lenyewe, lakini ninachotaka kieleweke ni ukweli kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ‘imekaba’ kona zote iwe NCCR – Mageuzi, CUF au Chadema, hivyo kilio chote kinachotaka matangazo ya ‘live’ redioni ama katika televisheni siyo lolote wala chochote ila ni kisingizio tu.


Nataka wananchi wafahamu ukweli kuwa kinachofanywa na wabunge hao sasa ni kutunga kila aina ya uzushi, uongo na upotoshaji wowote unaoweza ‘kuwabeba’ ili kukidhi matakwa yao ya kisiasa, lakini inawezekana hawaelewi kwamba “siku ya kufa nyani miti yote msituni inateleza”.


Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0787 088 870
 
Wapinzani wanahangaika na 30% ya watanzania wenye TV.

70% ya watanzania( wapiga kura) hawana TV wala muda Wa kuangalia mbunge wa upinzani akihubiri kuhusu shanga..
 
Imekugharim siku ngapi kuandika ujinga huo?
+baada ya siku si nyingi itakubidi ubadili huo wimbo
±wenye akili ndani ya chama wameshagundua hili la kuzuia bunge live lina hasara kubwa kwa CCM na sio wapinzani
+ haihitaji gharama kubwa kujua hilo ni janga kwa chama angalia tu nape anavyo jitetea mbele ya wana habari kama lingekuwa jambo jema asingejitetea angesimamia msimamo
+ ukiona viongozi wako wamenza kuteteleka kusimamia maamuzi ya pamoja. Wewe mpambe anua matanga.
± nashangaa wewe mpambe wa aina gani bado unatetea huo upuuzi unaoanza kukimbiwa pole sana amka hujachelewa
 
Gazeti halina jina.Mmebakia kujipendekeza tu na kushikiwa akili basi.
 
Back
Top Bottom