MEYA wa Jiji la Dar es Salam, Isaya Mwita amesema anafikiria kama inawezekana kuweka sheria ndogo zenye kuwabana wakazi wa jiji hilo ili kuacha mazingira katika hali ya usafi na watakaokamatwa wakitupa takataka hovyo walipishwe faini.
Mwita amesema hayo Dar es Salaam jana wakati akizindua kituo cha kutoa taarifa kuhusu hali ya uchafu na athari zake kwa afya ya binadamu, kinachoratibiwa na Taasisi ya Nipe Fagio inayohamasisha jamii kuwa na utamaduni wa kufanya usafi maeneo mbalimbali.
Kituo hicho kimejengwa kwa chupa za plastiki, ikiwa ni maandalizi ya Siku ya Usafi Duniani itakayofanyika Septemba 15, mwaka huu ambapo kitatumika kama sehemu ya uhamasishaji kuhusu uchafuzi wa mazingira kupitia plastiki na umuhimu wa kupunguza plastiki kwa kuzitumia kutengeneza bidhaa ikiwemo ujenzi wa nyumba.
Mbali ya uzinduzi huo, pia vikundi 11 vya wakimbiaji kutoka Manispaa ya Kinondoni wamefanya usafi wa mazingira katika ufukwe wa Coco.
Akizungumzia suala la usafi, Mwita alisema anafikiria kuhusu sheria hizo kwa kuwa ipo mikoa kama Arusha na Kilimanjaro imefanikiwa kuwa misafi na kutunza mazingira hasa baada ya kufanikiwa kuwabana wakazi wake na wale wanaokiuka kutozwa faini.
"Hata miji kama Nairobi na Mombasa ukifika mitaa yao ni misafi na yenye kuvutia mazingira kwa ujumla," alisema na kuongeza kuwa suala la usafi limekuwa halitiliwi mkazo badala yake limekuwa suala la kusukumana.
Alisema wananchi wamekuwa hawatilii mkazo usafi mazingira yao, mpaka wasukumwe na serikali, huku kila kata ikiwa na mkandarasi wa taka ambaye naye amekuwa akipata shida kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa wananchi wa eneo husika.
"Tumekuwa tukipata malalamiko kutoka kwa wakandarasi hao ya wananchi kutokutoa taka majumbani na kusababisha kazi ya kuzoa taka kuwa ngumu," alisema na kuongeza kuwa suala hill linachangia magonjwa ya milipuko kama kipindupindu kushindwa kutokomezwa kabisa.
Alisema kwa jiji la Dar es Salaam lina idadi ya watu wanaokadiriwa kufikia milioni sita hadi saba na wakizalisha taka tani 4,000 kwa siku huku zinazopelekwa katika dampo la Pugu zikifikia takribani tani 2,000 na nyingine zikizagaa tuu mitaani.
Amesema fukwe zimejaa takataka, wakazi wa jiji hilo wakidhani kuna Malaika anayeweza kushuka kwa ajili ya kufanya usafi na kuwataka wawe mabalozi wa usafi popote.
Kuhusu Taasisi ya Nipe Fagio alipongeza jitihada za kuelimisha kuhusu kufanya usafi na kuitaka kazi hiyo kuwa endelevu ili kila mwananchi aweze kuokota takataka kila wazionapo badala ya kufikiria kuwa wapo wanaohusika kwa suala hilo.
Mkurugenzi was taasisi hiyo, Anna Rocha alisema Tanzania ina fursa kubwa ya kutumia taka za aina mbalimbali ikiwemo plastiki kutengeneza vifaa vya ujenzi na kuongeza kuwa hatua hiyo inatokana na mbinu mpya ya ubunifu na yenye gharama nafuu.