Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,870
- 34,352

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako.
MATOKEO ya Kidato cha Nne yametangazwa, shule zilizoaibika kwa matokeo mabaya ni za serikali zinazosomesha watoto wa maskini.
Tukioanisha mantiki, ufaulu wa wanafunzi miaka ya hivi karibuni ni sawa na vita ya matajiri na maskini; mwaka huu tena walalahoi wamevuna aibu ya ufukara wao. NANI MWENYE KUJALI KATIKA HILI?
Wakati mwingine fikra ni kitu cha ajabu, ndiyo maana katika muktadha huu wa matokeo mabaya ya shule nyingi za wasio nacho ni wachache waliotafakari taifa letu linaelekea wapi?
Ni wazi kabisa, taifa lipo kwenye mtikisiko mkubwa wa ki-hali! Maisha na mafanikio bora yanachukuliwa mikononi mwa maskini walio wengi na kurasimishwa kwa matajiri wachache.
Fedha hivi sasa inaongea! Ukitaka elimu bora, tiba nzuri, huduma za kijamii za kisasa usitumie kinywa chako; mfuko uteme noti; kila kitu ni murua! Hata nafasi za kisiasa bila fedha hupati.
Nawasihi Watanzania wenzangu, tusikubali kurudi enzi za ukoloni wa Wazungu waliopora utashi wetu kwa kutumia utajiri na maarifa yao kwa kuwapa nafasi matajiri weusi kuwa watawala wetu wapya kwa mfano wa Wazungu tuliowatimua wakati tukidai uhuru.
Kama ilivyokuwa enzi za ukoloni, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, aliwaongoza wananchi wanyonge walio wengi kupigania usawa wa huduma na haki kwa wote na kufanikisha vita ya kujikomboa iliyotufikisha hapa.
Shime wanyonge wote wa leo! Tuungane na Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli aliyeonesha nia ya kuwatetea wanyonge kuutokomeza mfumo wa ‘fedha inaongea’.
Ni wazi kuwa nchi hii si ya matajiri, bado ni ya wakulima na wafanyakazi maskini, hivyo ni vyema kuhakikisha kuwa huduma bora haziendi kwa matajiri wachache bali kwa Watanzania wote.
Ni muda wa kila mwananchi kutafakari kwa nini shule za matajiri zinaongoza ufaulu kitaifa? Tujiulize ziko wapi shule za umma za watoto wenye vipaji, mfano Tabora Boys, Mazengo, Ifunda, Ilboru, Msalato na nyingine nyingi?
Shule hizi si tu zilikuwa mkombozi wa watoto wa maskini kupata elimu bora lakini ndizo zilizozalisha wataalamu na viongozi wengi ambao taifa linajivunia hivi sasa.
Watanzania wenzangu; wanafunzi waliopata divisheni 0 hawapo huko kwenu tu, hata kwetu wapo! Ni kilio cha taifa zima; vipi hisia zetu zisiumizwe na hili na kuona ipo haja ya kuunganisha nguvu zetu kuisaidia serikali kupambana ili kurejesha nchi mikononi mwa wanyonge!
Tukiacha shule za ada za milioni 3 kwa mwaka ambazo wananchi wengi hawawezi kupeleka watoto wao huko ziwe ndiyo njia ya kupata elimu bora, maana yake tunakubali watoto wa maskini wawe watawaliwa na wachunga ng’ombe maisha yao yote.
Nahamasisha; ukombozi wa elimu bora kwa wote unaanzia katika jamii zetu, tujitoe kadiri tuwezavyo kuchangia ubora wa elimu kwa watoto wetu.
Tuwahamasishe watoto wapende shule, tukatae utoro na tuwape msaada uwafaao katika maisha yao ya shule kamwe tusikwepe majukumu yetu kwa kisingizio cha serikali kuwahudumia.
Tukumbuke serikali ni watu, tukifanyacho sisi imefanya serikali. Si vibaya tukijenga nyumba bora za walimu na madarasa kwa kujitolea halafu serikali kuu ikachangia tulipokomea lengo ni ushiriki wa wananchi wote katika vita hii. Tumuunge mkono rais Magufuli kwa uwezo wetu wote.
Natoa wito kwa watendaji na viongozi wote wa mitaa na vijiji kuhakikisha kuwa shule zilizopo maeneo yenu zinafanya vizuri, msikubali zishike mkia kwa kufelisha wanafunzi, wenye hasara na matokeo mabaya ni ninyi wakazi wa eneo husika na taifa kwa ujumla.
Nachochea tu.
Chanzo: GlobalPublishers