Walimu wapasuka: Acheni chokochoko, heshimu CWT

Mzee wa Code

Member
Joined
Sep 23, 2024
Posts
78
Reaction score
216
Walaani wastaafu wanaokikimbiza chama mahakamani… Wamtaja Rais Samia, Kikwete na Majaliwa kama mifano ya kuigwa

Na Mwandishi Wetu
Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wameibuka kwa sauti moja na kulaani vikali chokochoko zinazoanzishwa na baadhi ya viongozi wa zamani waliowahi kushika nafasi ndani ya chama hicho, wakisema kuwa vitendo hivyo ni tishio kwa mshikamano, umoja na mafanikio ya chama hicho kikongwe cha wafanyakazi.

Katika mahojiano yaliyofanywa na wanahabari mwishoni mwa wiki, walimu kutoka mikoa mbalimbali waliwaomba waliostaafu uongozi wa CWT kuheshimu misingi ya taasisi hiyo na kustaafu kwa heshima, badala ya kuibua migogoro isiyo na tija kupitia vyombo vya sheria.

“Ni jambo la kusikitisha kuona watu waliowahi kushika dhamana kubwa ndani ya chama hiki leo hii wanakimbilia mahakamani, kana kwamba hawajui taratibu. Hii ni kukosa uadilifu na heshima kwa chama walichokihudumia,” alisema mmoja wa wanachama kutoka Mwanza.

Walimu hao walisema kuwa vitendo hivyo vinahatarisha mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ambapo chama hicho kimekuwa na uongozi uliojaa maono, usikivu na mshikamano na Serikali ya Awamu ya Sita.

“Uongozi wa sasa umeonyesha dira ya kweli. Kwa kushirikiana na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, tumeshuhudia kupandishwa madaraja, kulipwa madeni ya muda mrefu na kuboresha mazingira ya kazi. Huu ni uongozi wa kutunzwa, si wa kupigwa vita,” alisema mwalimu kutoka Ruvuma.

Baraza la Taifa liliazimia kwa nia njema

Wanachama hao pia walikumbusha kuwa Baraza la Taifa la Chama cha Walimu lililokaa mwaka 2023, chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu Maganga na aliyekuwa Rais wa CWT, Madam Leah Ulaya, liliidhinisha mkopo wa shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ununuzi wa T-shirt, ikiwa ni maandalizi ya sherehe za Mei Mosi. Walisema kuwa hatua hiyo ilikuwa na nia njema kabisa kuhakikisha kuwa maandalizi ya tukio hilo muhimu la kitaifa yanafanyika.

Aidha, Baraza la Taifa la mwaka 2024 lilikutana na kupitia kwa kina maamuzi yote ya awali, ambapo Mwanasheria wa CWT alitoa maelezo ya wazi kuhusu uhalali wa uamuzi huo na kuthibitisha kuwa taratibu zote zilifuatwa kwa mujibu wa katiba ya chama.

“Mdhamini kwenda mahakamani ni fedheha”

Katika kile kilichoonekana kama ukosoaji mzito, walimu walieleza kusikitishwa kwao na hatua ya kiongozi mstaafu mwenye hadhi ya Mdhamini wa Chama kupeleka mashauri kwenye vyombo vya sheria. Walieleza kuwa kama hakuridhika na maamuzi ya Baraza Kuu, alipaswa kuwasilisha hoja zake kwenye Mkutano Mkuu wa CWT Taifa wa mwaka 2025, ambao ndio chombo cha juu kabisa kwa mujibu wa katiba ya chama.

"Cha kushangaza ni kwamba walikaa kimya katika Baraza Kuu, ambako walikuwa sehemu ya maamuzi, lakini sasa wanajitokeza kulalamika nje ya taratibu, tena kwa mtu ambaye si sehemu ya uongozi wa chama," alisema mmoja wa wanachama kutoka Iringa.

Walimu walieleza kushangazwa na hatua ya kupeleka malalamiko kwa Mwenyekiti wa Maandalizi ya Uchaguzi, ambaye hana nafasi yoyote ya kikatiba ya kushughulikia masuala hayo. Mbaya zaidi, wamemlaumu kwa kuanza kuwatuhumu viongozi waliopo madarakani, waliopatikana kwa kura nyingi kutoka kwa wanachama waliowaamini.

“Tuache chokochoko, tulinde taaluma yetu”

Walimu hao waliendelea kueleza kuwa CWT ni taasisi ya kitaaluma ambayo haipaswi kuingizwa kwenye migogoro ya watu binafsi. Wamesisitiza kuwa chama hicho kinabeba sura ya walimu wote nchini, hivyo lazima kiendelee kuwa kielelezo cha nidhamu, mshikamano na maadili mema.

“Tunaomba waliostaafu wakae pembeni kwa heshima. Wapumzike kwa amani na wajivunie kazi yao. Kazi ya chama si ya mtu mmoja; ni ya wanachama wote,” walisema kwa sauti ya pamoja walimu hao.

Wamehitimisha kwa kutoa wito kwa walimu wote nchini kuendelea kuunga mkono juhudi za uongozi wa sasa na kuhimiza mazungumzo badala ya migogoro.

“Tusikubali chokochoko zidhoofishe chama. Tuilinde CWT kama sehemu ya taaluma yetu na urithi kwa walimu wa vizazi vijavyo,” ulisema ujumbe wao wa pamoja.
 
Daah!!! yaani vizazi vijavyo tuwarithishe CWT ?? Kweli sisi watanzania ni wagonjwa wa akili.

CWT ni wezi, walafi na wabinafsi wanachukua pesa za walimu kibabe Kwa kusaidiwa na serikali halafu wanalipana posho na marupurupu kufuru.

Sema Walimu nao ni WAOGA, CWT ilitakiwa kiwe hakina wanachana mpaka sa hivi.

Mnachukua 250,000/= ya Mwalimu halafu mnampa T shirt na kofia ??? Pathetic!!
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…