Ofisi ya uhamiaji mkoani Njombe imefanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 12 kutoka mataifa mbali mbali ikiwemo Rwanda,Somalia na Burundi wakitokea mkoani Dodoma kuelekea Tunduma mkoani Songwe kwa malengo ya kufika nchini Afrika kusini kwa ajili ya kutafuta Maisha.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya uhamiaji mkoa wa Njombe Afisa uhamiaji mkoa wa Njombe ABBAS ABEID MISSANA amesema katika wahamiaji hao saba ni raia wa Rwanda,wawili ni raia wa Burundi na watatu ni kutoka Somalia.
“wahamiaji hawa wote kwa pamoja walikuwa wakitokea mkoani Dodoma na walikuwa wakisafiri kwa mabasi ya SATCO,SUPER FEO na SHABIBY wakielekea tunduma hadi Zambia na Afrika ya kusini kwa ajili ya kutafuta maisha,idara ya uhamiaji inatoa wito kwa wamiriki wa vyombo vya usafiri na wananchi kwa ujumla kutoa ushirikiano wa taarifa kwa mtu yeyote ambaye una mashaka na uraia wake au ukazi wake hapa Tanzania ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa”alisema MISSANA
Aidha MISSANA amesema kuwa kwa wote waliokamatwa idara inakusudia kuwafikisha mahakani na kuwafungulia mashtaka ya kuingia nchini kinyume cha sheria na kuwataka wananchi kuwa na mapenzi na nchi yao huku akisisitiza kutoa taarifa kwenye vyombo husika pindi anapoonekana mtu yeyote anayetiliwa na mashaka.
CRISTIAN MWAKINGA na DATSAN MAKOGA ni miongoni mwa wananchi mjini Njombe waliozungumza na mtandao huu,wamesema kuwa watanzani tumekuwa na tabia ya wema licha ya kukubali wito wa ofisa uhamiaji wameiomba idara ya uhamiaji mkoani Njombe kuendelea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kuelewa sehemu sahihi ya kuwapeleka.
“wananchi tunahitaji elimu kwa kuwa sisi watanzania tunatabia ya wema tunatabia ya kumuona kila mmoja ni rafiki kwa hiyo ni lazima tujifunze juu ya wema wetu kwa kuwa tunaweza kujikuta tunaishi na wageni bila kujua ni watu gani,na hii idara iendelee kutoa elimu ili tujue zaidi watu kama hawa tukiwaona ni wapi tuwapeleke”walisema wananchi.