WAMILIKI na madreva wa bajaji wanaofanya shughuli za usafiri katika Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi,wamefanya mgomo na kusitisha kutoa huduma za usafiri katika maeneo ya Manispaa ya Mpanda na nje ya Manispaa baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi na Majini ( SUMATRA), kupiga marufuku bajaji kufanya safari zake kupitia barabara kuu.
Mwenyekiti wa wa madreva wa Bajaji, Rashid Juma alisema wameamua kusitisha kutoa huduma ya usafiri kwenye maeneo ya Manispaa ya Mpanda, baada ya SUMATRA kupiga marufuku bajaji zote ili kupunguza wingi wa ajali.
Alisema wameamua kusitisha huduma hiyo kuanzia juzi, ingawa walikuwa wamepata agizo, bali wamesitisha kutoa huduma kwenye maeneo yote hata yale ya barabara ndogo.
Alisema kitendo cha kuwazuia, kitawafanya wakose mapato na kusabisha kushindwa kulipa kodi kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mwenyekiti wa wasafirishaji ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani wa Mkoa wa Katavi, Nassor Arfi alisema amepata taarifa za kusimamishwa huduma za usafiri wa bajaji kupita kwenye barabara kuu za Mpanda- Kigoma,Mpanda Sumbawanga na Mpanda – Tabora na amefanya mawasiliano na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Raphael Muhuga.
Alisema mkoa huo, hauna nyingine mbadala za kuwafanya madreva wa majaji kutumia, hivyo ni vema mamlaka hiyo ikatumia busara kumaliza suala hilo.
Meneja wa SUMATRA wa Mkoa wa Katavi, Amani Mwakalebela alisema mambo yote yanaendeshwa kwa sheria halali.
Mkazi wa Mtaa wa Kazima, Aglipina Petro alisema ameshindwa kumpeleka mgonjwa wake hospitali, baada ya kukosa huduma ya usafiri.
Mkazi wa Kijiji cha Ibindi, Joice Longino alisema kitendo cha bajaji kusitisha huduma ya usafiri kumesababisha wafanyabiashara kushindwa kufika mjini Mpanda kununua bidhaa kwa ajiri ya biashara zao.
Chanzo: Mtanzania