Wabunge waikubali kasi ya Magufuli

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
HOTUBA ya ufunguzi wa Bunge ya Rais John Magufuli, imeanza kujadiliwa bungeni huku wachangiaji wengi wakieleza kuridhishwa na kasi yake ya uongozi.
Wamesisitiza kwamba kama yako mambo ambayo hayaendi vizuri, wabunge wanapaswa kumjulisha, yafanyiwe kazi.
Pamoja na wabunge kuainisha maeneo kadhaa ambayo Serikali inapaswa kuyafanyia kazi, wachangiaji wengi wamempongeza Magufuli na kuendelea kusisitiza Watanzania wamwombee atimize malengo yake.
Michango ya wabunge hao, ambao baadhi waliweka bayana kuwa wananchi wana imani naye kubwa kutokana na kuonesha kuwa analosema analitekeleza, ilitolewa baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwasilisha hoja bungeni ya kujadili hotuba ya Rais, aliyoitoa Novemba 20 wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema hotuba ya rais imetoa mwelekeo na dira ya serikali ya kutekeleza ahadi, alizotoa katika mikutano ya kampeni. Alisema hotuba ya Rais imeeleza vipaumbele mbalimbali, vinavyotakiwa kutekelezwa katika miaka mitano ijayo na kusisitiza kuwa serikali imejipanga kikamilifu kuvitekeleza.
Aliomba wabunge wa vyama vyote, kutoa michango itakayosaidia serikali katika utekelezaji wa mambo mbalimbali yaliyoainishwa, ambayo utekelezaji wake umeshaanza kwa kasi kubwa.
“Bado serikali inahitaji sana michango na mawazo ya wabunge kwa ajili ya kuboresha maeneo na yanahitaji usimamizi wa karibu na utekelezaji,” alisema Waziri Mkuu.
Aliahidi kwamba michango yote ya wabunge itaheshimiwa na kufanyiwa kazi. Wabunge wasifu Mbunge wa Mvomero, Suleiman Murad (CCM) alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake za kupambana na mafisadi, kuimarisha uchumi na kukusanya mapato.
Alisisitiza kuwa yako mambo mengine ambayo hayajui hivyo wabunge ndiyo wanaopaswa kumjulisha yafanyiwe kazi. Murad alizungumzia tatizo la ardhi kwa wakulima na wafugaji na kusema eneo hilo, linahitaji kazi ya ziada.
Alishauri wizara zote zenye dhamana ya ardhi, mambo ya ndani ya nchi, kilimo, mifugo na maliasili, zishirikiane kwa pamoja kukabili tatizo hilo. Akizungumzia mikakati ya kuimarisha uchumi, alisema lipo suala la baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa waaminifu.
Aliomba wanaohusika na masuala ya bajeti na uchumi, kuwa macho na watu wa namna hiyo, aliowataja kuwa wanacheza na Kamati ya Bajeti, kuingiza mambo yao kwenye bajeti.
Akizungumzia vocha za pembejeo za kilimo, alisema lipo tatizo kubwa vijijini kutokana na kuwapo watendaji serikalini wasio waaminifu ambao ndiyo wamekuwa wakinufaika nazo.
Mvutano Zanzibar
Wakati suala la mvutano wa kisiasa lilikuwa miongoni mwa mambo ambayo baadhi ya wabunge walilijadili kwa mtazamo tofauti wakiwemo waliotaka Rais Magufuli aingilie kati aamuru mshindi wa urais atangazwe, mbunge huyo wa Mvomero aliwakosoa, akisema suala hilo ni la kisheria.
Murad alisema, “Suala ni la kisheria, tuwatakie kila la heri wafanye uchaguzi wao (Zanzibar) kwa amani. Rais hawezi kuingilia tena. Tume (ZEC) imetangaza Machi 20 ni uchaguzi…Mizengwe ndiyo imesababisha hali hii.” Aliendelea,
“Tumtake rais afanye makubwa, tusimchanganye, tumepata rais asiyeogopa, mkweli, mwaminifu kwa taifa na ana ndoto nyingi. Tumpe ushirikiano tuache maneno maneno, tumuache asonge mbele.”
Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea (CUF) katika kuchangia kuhusu suala la Zanzibar, alionesha imani kwa Rais Magufuli, akisema wananchi wana imani naye kubwa kutokana na kuonesha kuwa analosema analitekeleza.
Mbunge huyo wa Temeke pia alizungumzia matatizo katika sekta ya afya jijini Dar es Salaam na kusema licha ya hospitali za Temeke, Mwananyamala na Amana, kupandishwa hadhi na kuwa za mkoa, zimeendelea kuachwa zikihudumiwa na halmashauri huku zikikabiliwa na ukosefu wa vitanda, dawa na maslahi ya watumishi.
Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda (CCM), alimpongeza Rais Magufuli kwa hotuba aliyosema ni nzuri iliyosheheni weledi na iliyoangalia kila sekta na maono mapana ya maslahi ya taifa. Aliomba Watanzania waendelee kumuombea azma yake ya kuleta maendeleo ifanikiwe.
 
Back
Top Bottom