SoC03 Wabunge kuwa wafuasi kunaathiri utawala bora na uwajibikaji katika serikali

Stories of Change - 2023 Competition
Dec 10, 2020
15
14
Bunge ni sauti ya watu, bunge si sauti ya serikali kuu, bunge ni sauti ya taifa zima la leo na lijalo kwa vizazi, bunge ni dira ya sheria, sera na mambo mbalimbali yanayohusu nchi. Serikali inaweza kubadilika kulingana na awamu lakini misingi ya bunge la awamu moja ya serikali inaweza isibadilike kwa miaka mingi.

Misingi ya bunge la awamu moja ya rais inaweza kuathiri awamu za marais wawili au zaidi. Kwa kawaida bunge linatakiwa kuwa na mwelekeo wa kuwa makini katika kutazama na kumulika masuala mbalimbali ya kitafa bila kujali wingi wa viti vya chama fulani bila kujali ni cha upinzani ama chama tawala.

Mara nyingi tumeona wabunge wa nchi mbalimbali zilizoendelea wakijenga hoja mbalimbali na kuibua mambo mbalimbali ambayo ni ya msingi katika jamii lakini pale tu wabunge wanapokuwa wafuasi wa serikali nafasi hiyo hupunguza nguvu ya uwajibikaji katika mihimili mingine ya serikali.

Katika hali ya taifa letu, bunge mara nyingi limekuwa ni sauti ya serikali, bunge hata kupitia kwa wabunge wengi na spika wake ukifatilia mikutano mingi utasikia mara kwa mara wabunge walio wengi na hata spika wake wakitamka kwa wazi kuwa lengo ni kumsaidia rais na kuunga mkono juhudi za serikali.

Maneno ya kumsaidia rais yamekuwa ya kawaida katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hili ni suala la wazi ambalo hata ukifatilia katika mikutano mingi utasikia maneno haya ama kutoka kwa baadhi ya wabunge tena wengi wao na hata spika wa bunge. Wakiongoza hoja kwa kuunga mkono juhudi za serikali hii inaashiria kuwa wafuasi wa serikali hiyo tu. Na, kumsaidia rais si hadi kusema unamsaidia.

Kuwa mfuasi wa kitu fulani kunanyima haki na uhuru wa baadhi ya mambo ya msingi ambayo hata kama ulitakiwa kuyasema basi kwa kuwa wewe ni mfuasi utalazimika kuacha ili uendelee kuwa mfuasi hata kitu ambacho hautakiwi kukifuata kwa wakati huo. Hili ni tatizo kubwa hata kwa wabunge kuwa wafuasi kwani inapunguza kwa kiasi kikubwa mno nguvu ya utawala bora na uwajibikaji katika nguzo nyingine za kiserikali kwa kuwa bunge la namna hii.

Bunge linapokuwa na wabunge wengi walio na ufuasi wa serikali ama chama ndani yake bunge hilo linakuwa bunge lenye kulenga kitu fulani kiende kama kilivyo katika serikali kuu au chama hata kama linaona kuna haja ya kuionesha serikali mapungufu ambayo haijayaona iweze kuyaona na kuweka mwelekeo wa namna gani serikali iweze kuepukana nayo kama kwa bahati mbaya haikuyabaini. Matokeo yake uwajibikaji unapungua katika serikali kuu na vyombo vingine vya dola.

Jamii yetu imekuwa na mtazamo kuwa chama kimoja kuwa na wabunge wengi ndiyo nguvu ya kuweza kuendesha serikali kuu kiurahisi, hapa ndipo tatizo la ufuasi linapoanzia. Ifahamike kuwa, kumsaidia rais katika baadhi ya maswala muhimu si kitu kibaya lakini kuwa mfuasi ni tatizo. Nia za wabunge wengi wamekuwa ni kwa ajili ya kusaidia chama chake kitu ambacho si kizuri kwa uhai wa taifa.

Kusaidia chama si jambo baya lakini kuna wakati wa kusaidia chama na kuna wakati wa kusimama kama mbunge ili kutetea maslahi ya taifa.

Unaweza kusaidia chama kwa kutekeleza mambo ya taifa kama mbunge. Inatakiwa, kila anayetaka kuwa mbunge kufahamu kuwa hatakiwi kuwa mfuasi wa upande fulani baada ya kuwa mbunge. Kutokuwa mfuasi kunamfanya mbunge kuweza kuchakata mitazamo mingi chanya na hasi kuhusu kile kinachojadiliwa bungeni na kuweza kuona kwa kina kikubwa madhara ambayo yanaweza kutokea kama tu atafanya kosa la ama kukubali au kukataa kitu hicho na hii inajenga uwajibikaji na utawala bora katika serikali.

Jukumu la mbunge kusimama katika kuliangalia taifa na kutokufungamana na upande wa ama kuwa katika mwelekeo wa kuunga mkono serikali kuu ama kuunga mkono masuala ya chama chake pekee ni la kila mbunge anayechaguliwa na wananchi wa jimbo lake kwa ajili ya jimbo lake na taifa kwa ujumla.

Makosa mengi ya kiserikali yamekuwa yakitokana na jicho la taifa kutokuwa makini kwa kuwa wabunge wengi wa bunge wanaingia bungeni tayari wakiwa au wanakuwa wafuasi wa uongozi wa serikali ya awamu hiyo, hapa nitatolea mfano, katika kipindi cha awamu ya sita wabunge wengi walikuwa wakisema tunaunga mkono juhudi za rais wetu na kupiga kura za ndiyo na hali haijabadilika baada ya kuingia awamu nyingine wabunge wengi wamekuwa wakisema tunaunga mkono juhudi za rais.

Hili swala ni baya bila kuwa makini kwani linapunguza sana uwajibikaji na utawala bora. Bunge haliwezi kukaa kuunga mkono jitihada za rais pekee anayekuwa madarakani kwa muda wake, bali linatakiwa kukaa makini na kuangalia mwelekeo wa taifa na si wa rais pekee.

Bunge linapoangalia mwelekeo wa taifa litamsaidia hata rais bila hata wabunge kusema kuwa wanamsaidia rais. Ikumbukwe kuwa, rais anaweza kumaliza madaraka yake ya miaka kumi ama isifike lakini yale mambo yaliyopitishwa na bunge yanaweza kukaa miaka zaidi ya hiyo anayokaa madarakani. Je hapo ni sahihi kumsaidia rais tu? Jambo hili si sawa kwa maana kama bunge linakaa kumsaidia rais pekee, pale anapomaliza madaraka yake, kuna mambo yanapitishwa kumsaidia nayo yanaisha muda wake pengine kuna mengine yamepitishwa kukaa miaka zaidi ya muda wa madaraka ya rais anayehusika.

Kwa maana hiyo, kamwe bunge halitaliwa kuwa na wabunge wafuasi wa mhimili fulani katika kujadili masula ya kitaifa. Wabunge wanapaswa kutambua kabisa kuwa bunge ni mhimili tofauti wa serikali ambao unatakiwa kutengenishwa katika kufanya mijadala yake na masuala ya ufuasi wa ama chama au mhimili fulani na linapaswa kuendesha vikao vyake kwa ajili ya taifa zima na si kuangalia kipindi cha utawala wa awamu hiyo tu bali wafahamu kuwa kuna awamu na awamu zinaweza kupita katika baadhi ya misingi ile ile bora inayowekwa na bunge linalokuwepo hata kabla ya awamu nyingine.

Suala hili ni muhimu sana kwa taifa zima, mawaziri nao wafahamu kuwa wana nafasi mbili hivyo nafasi ya ubunge isiathiriwe na nafasi ya uwaziri.

Bunge imara ni msingi wa serikali imara na taifa imara na endelevu, ni nguzo muhimu katika utawala bora na uwajibikaji na ni mhimili wenye kuliongoza taifa kwa kuweka misingi mizuri baina ya uongozi mmoja na mwingine kwa kutokuruhusu mabadiliko mengi yasiyo ya lazima kutokana na awamu ya serikali moja na nyingine kwa kuweka misingi bora ya kitaifa kwa taifa na kuzuia mianya ya serikali dhaifu kutokuathiri taifa kama itatokea na kuhakikisha utawala bora na uwajibikaji unakuwepo.
 
Back
Top Bottom