VITA BARIDI YA PILI?

VITA BARIDI YA PILI?

Joined
Oct 5, 2015
Posts
90
Reaction score
483
VENEZUELA: MTAFARUKU MPYA NA MUENDELEZO WA VITA BARIDI YA PILI - 1

Jumatano ya Tar. 23 Januari 2019 kiongozi wa bunge la Venezuela Bw. Juan Guaidó alijitangaza kuwa Rais wa mpito wa nchi hiyo ya Amerika kusini na kumtaka Rais aliyeyekuwa madarakani Bw. Nicholus Maduro aachie madaraka haraka. Bw. Guaidó alihamasisha umati wa wananchi wanaomuunga mkono kuandamana na kushinikiza Rais Maduro ajiuzulu. Kufuatia uamuzi huo, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza mara moja kumuunga mkono Bw. Guaidó na kumtaka Maduro aachie madaraka la sivyo nguvu za kijeshi zitatumika. Naye waziri wa ikulu ya Marekani, Mike Pompeo alitangaza katika ukurasa wake wa Twitter kuunga mkono uamuzi wa Bw. Guaidó na kueleza mpango wa Marekani kuisadia Venezuela kiasi cha dola Mil. 20 endapo Maduro ataachia ngazi na kumpisha Guaidó aongoze nchi angalau kwa mpito.

Hata hivyo Rais Nicholus Maduro hakuonesha dalili za kung'atuka madarakani, wiki chache baada ya kuapishwa kuongoza Venezuela kwa awamu ya pili. Pamoja na kwamba Kauli ya Marekani iliungwa mkono na Canada na mataifa mengine ya Amerika ya kusini yakiwemo Brazil, Argentina na Colombia lakini nchi za Mexico na Bolivia zinaendelea kumuunga mkono Rais Maduro. Nje ya Amerika, huko mjini Moscow msemaji wa ikulu ya Kremlin ameionya Marekani isithubutu kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Rais aliyechaguliwa na wananchi la sivyo, mgogoro mkubwa utaibuka. Naye waziri wa mashauri ya kigeni wa Russia, bwana Sergei Lavlov ameoneshwa kushangazwa na kitendo cha Marekani na washirika wake kuingilia siasa za ndani za Venezuela wakati wakiilaumu Russia kuingilia siasa za ndani za Marekani. Mr. Lavlov amekiita kitendo cha Marekani kumuunga mkono Bw. Guaidó kuwa ni kudharau sheria za kimataifa na kuingilia mambo ya ndani ya nchi zingine.
Taarifa zaidi kutoka Russia zinadai Rais Vladimir Putin ameongea kwa simu na Rais Maduro na kumuhakikishia kuwa yupo upande wake kwa hali na mali.

Uturuki hali kadhalika imeonesha kumuunga mkono Rais Maduro huku Rais Erdogan akimtaka Rais Maduro kuwa imara dhidi ya waasi. China imetoa kauli ya kidiplomasia zaidi ikitaka majadiliano na maridhiano ya pande mbili wakati India inajipanga kutoa tamko la kumuunga mkono Rais Maduro. Iran nayo imetangaza kumuunga mkono Rais Maduro.

Nchini Spain kuna jitihada za kuhamasisha nchi za Ulaya kumuunga mkono Bw. Guaidó, japo Uingereza ilikwisha onesha dalili za kuunga mkono Marekani. Bado nchi nyingi za Ulaya hazijaonesha kuwa na upande wowote.

Maandamano makubwa ya kumpinga Rais Maduro yaliendelea kwa siku mbili huko mjini Caracas, na miji mingine lakini yameonesha kupungua nguvu siku ya tatu leo. Awali, nguvu ya upinzani ilikuwa kubwa kiasi cha kutikisa utawala Rais Maduro lakini kitendo cha Jeshi la Venezuela kumuunga mkono Rais Maduro kumemuongezea nguvu mara dufu na kumfanya Bw. Guaidó kujificha na kutoa matamko machache. Waziri wa Ulinzi wa Venezuela Bw. Vladimir Padrino Lopez amekiita kitendo cha kiongozi wa bunge kujitangazia Urais kuwa ni kichekesho lakini ameonya kuwa kitendo hiko kinaweza kufanya ndugu wa Venezuela kuuana wenyewe kwa wenyewe. Waziri Lopez alitamka maneno hayo mbele ya vyombo vya habari huku akiambatana na maafisa wa ngazi za juu wa jeshi wakionesha kumuunga mkono Rais Maduro.

Mjadala.
Inaonekana kama vile Marekani ilikurupuka kumuunga mkono Bw. Guaidó aliyejitangazia Urais, na bila kujali hilo washirika wake wa Amerika na ulaya waliunga mkono haraka jambo hilo. Vitisho vya kupeleka jeshi nchini Venezuela pamoja na ahadi ya msaada wa dola Mil 20, vingeweza kuongeza nguvu ya upinzani kwa Rais Maduro, lakini haikuwa hivyo. Marekani ilitumaini jeshi la Venezuela kubaki katikati bila kuunga mkono upande wowote au ikibidi kuunga mkono wapinzani wa serikali ya Rais Maduro, pia haikuwa hivyo. Sababu za wazi za uamuzi wa Marekani wa kumuunga mkono Bw. Guaidó ni kwamba serikali ya Rais Maduro imeshindwa kuwasaidia wananchi wake, sawa na tuhuma alizopatiwa hayati Hugo Chaves kabla ya kifo chake. Venezuela ni nchi ya kijamaa, ambayo uchumi wake umedorora hasa kutokana na vikwazo vya kiuchumi kutoka nchi za magharibi. Mikopo na misaada kutoka Urusi na China ndio imesaidia angalau kuendesha serikali.

Hata hivyo Marekani yaweza kuwa na ajenda ya siri. Ifahamike kuwa Venezuela, pamoja na mdororo wa uchumi lakini ndio nchi yenye akiba kubwa ya mafuta kuliko nchi zote duniani, ikifuatiwa na Saudi Arabia na Canada. Hadi kufikia miaka ya 1990 makampuni ya Marekani yalikuwa yakifanya shughuli za uchimbaji mafuta nchini Venezuela. Lakini kushika hatamu kwa Hayati Hugo Chaves mwaka 1999 kulipelekea kutaifishwa kwa rasilimali ya mafuta nchini Venezuela, sera iliyokuwa mwiba kwa Marekani. Tangu wakati huo mahusiano ya Marekani na Venezuela yamekuwa ya kuwekeana vikwazo na kumekuwa na majaribio ya mauaji ya aliyekuwa kiongozi wa Venezuela, Hyt Hugo Chaves.
Russia kwa upande wake imekuwa rafiki wa karibu wa Venezuela. Misaada ya dola Bilioni 10 kutoka Russia na biashara ya silaha yenye thamani ya dola bilioni 11 baina ya Venezuela na Russia vimeongeza chachu ya mahusiano. Kampuni ya uchimbaji mafuta ya Russia, Rosneft ina mkono wake ndani ya sekta ya nishati ya Venezuela. Zaidi ya hayo, Desemba 2018 ndege mbili zenye uwezo wa kurusha mabomu ya Nyuklia (Tupulov 160) pamoja na ndege zingine za kivita za Russia zilisafiri umbali wa maili 6000 hadi nchini Venezuela kwa ajili ya mazoezi ya pamoja. Wakati kitendo hicho kikipokelewa kwa hisia tofauti nchini Mareani, taarifa mbaya zaidi zilifikia ikulu ya Washington kwamba Russia inapanga kujenga kambi ya jeshi nchini Venezuela. Ikiwa jambo hilo litatokea basi jeshi la Russia litakuwa limeweka kambi 'mgongoni' mwa Marekani, kama ilivyokuwa wakati wa vita baridi ambapo Russia iliweka makombora yake yake nchini Cuba. Uamuzi wa Russia kuweka kambi la kijeshi nchini Venezuela unatokana na ukweli kwamba Marekani na washirika wake wa NATO wamejenga Makambi mengi ya kijeshi katika nchi zinazopakana na Russia.

Kwahiyo mgogoro wa Venezuela si wa Venezuela Bali ni mgogoro wa kidunia. Mafahali wawili, Marekani na marafiki zake ambao ni matajiri wa dunia dhidi ya Urusi na Marafiki zake ambao ni wababe wa teknolojia ya anga na silaha, wanacharuana kama walivyocharuana nchini Syria.

Sasa yamebaki masaa 24 tangu Rais Maduro atangaze kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Marekani, na kuwataka maafisa wa Marekani wote waondoke nchini Venezuela ndani ya muda huo. Ingawa Marekani walikataa kuondoa wanadiplomasia wao wakidai kuwa watabaki kufanya kazi na 'Rais Mpya' Bw. Juan Guaidó, lakini taarifa zinaonesha maafisa wa ubalozi wa Marekani nchini Venezuela wameanza kurudi nyumbani. Waliosalia ni maafisa wa ngazi za juu, ambao nawo familia zao zimerejea Marekani. Raia wa Marekani waliopo nchini Venezuela nawo wametakiwa kuondoka nchini humo kwa sababu za kiusalama.
Kwa upande wake Venezuela imeshafunga ubalozi wake mjini Washington na balozi ndogo zilizopo Texas na Florida.

Itaendelea...
 
Back
Top Bottom