Rubawa
JF-Expert Member
- Dec 25, 2015
- 2,055
- 3,266
Na Ahmed Rajab
YALIYOTOKEA wiki iliyopita Dar es Salaam, Tanzania, na Moroni, Comoro, ni muendelezo wa hadithi moja. Visa vilikuwa tofauti lakini hadithi ndiyo hiyo hiyo — yayo kwa yayo, maji ya futi kwa nyayo. Ni hekaya ya mapambano baina ya watawala wakaidi na umma usiokubali kuonewa.
Kilichojiri Dar ni hatua nyingine ya jeshi la polisi ya kuzuia mkutano wa ndani wa chama cha upinzani. Safari hiyo ulikuwa ni mkutano wa chama cha ACT-Wazalendo.
Kama ilivyo kawaida yao, polisi walikuwa na kisingizio kwa hatua walioichukua. Walisema waliwajibika kuuvunja mkutano wa ACT kwa sababu walikuwa na taarifa zao za kiintelijensia zilizoonesha kwamba wafuasi wa chama cha Civic United Front (CUF), chenye kuongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba, walikuwa wakijiandaa kufanya vurugu katika huo mkutano wa ACT.
La kushangaza ni kwamba polisi badala ya kuwachukulia hatua hao waliokuwa wakipanga kufanya kosa la jinai, waliwachukulia hatua waliokusudiwa kuonewa. Kama waliyosema polisi ni kweli basi kwa mara nyingine wametoa ushahidi bayana kwamba dola ilitumia chombo chake cha polisi kumbeba Lipumba. Unajiuliza: kwanini?
Naive iwavyo, ni wazi kwamba polisi kwa hatua waliyoichukua walikikaba chama cha ACT. Unajiuliza tena: kwanini?
Yasitoshe hayo lakini wiki hiyohiyo ACT-Wazalendo iliandikiwa barua na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa akikionya kwamba kitafutwa endapo baada ya siku 14 hakitotoa maelezo ya kuridhisha kuhusu madai matatu.
La kwanza ni la wanaosemekana kuwa wanachama wa ACT kupiga “Takbir” (Allahu Akbar, Mungu Mkubwa) wakati wa kupandisha bendera ya chama hicho.
La pili ni shtuma kwamba wanachama wa ACT walichomoa bendera za CUF na dai la tatu ni la kutowasilisha taarifa ya hesabu za mwaka 2013/14 kwa kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CGA. Tena unajiuliza: Kwanini?
Ni dhahiri kwa yeyote mwenye kuzifuatilia siasa za vyama vingi Tanzania kwamba nguvu za dola zinatumika kila uchao kuuhujumu mfumo huo. Dhamira ya watawala ni kukiandama kila chama cha upinzani na kukiua au angalau kukidhoofisha.
Watawala wamekuwa wakitumia njama tofauti lakini lengo ni lilelile moja la kuviua vyama vya upinzani. Zanzibar kililengwa chama cha CUF na katibu mkuu wake wa siku hizo, Maalim Seif Sharif Hamad.
Jaribio hilo lilishindwa. Badala yake liliudhoufisha upande wa Lipumba aliyetangazwa na mahakama kuwa ndiye mwenyekiti halali wa chama hicho. Kati ya hatua za mwanzo alizochukua Lipumba ilikuwa ya kumfukuza chamani katibu mkuu wa chama.
Hapo ndipo Maalim Seif alipohajiri kwenda ACT-Wazalendo. Alihamia chama hicho akifuatwa na mkururo wa wafuasi wake wa Unguja na Pemba. Kwa Zanzibar Lipumba alikuwa kama aliyeachiwa kifuu kitupu.
Mgogoro wa uongozi ndani ya CUF, baina ya kambi ya Lipumba na ile ya Hamad, badala ya kuwakatisha tamaa wafuasi wa chama hicho uligeuka na kuwa chanzo cha kiu kipya cha kutaka mabadiliko, kiu ambacho wengi wanaamini karibu kitakatwa.
Namna Seif alivyoungwa mkono kumeonyesha nguvu kubwa za kisiasa alizonazo, hususan Zanzibar. Licha ya mapungufu yake sidhani kwamba kwa sasa kuna mwanasiasa yeyote anayeweza kumzidi nguvu kisiasa. Kama yuko hatujamuona bado akichomoza.
Kuhamia kwa Hamad ACT-Wazalendo kumeziamsha hamasa za Wazanzibari wenye kumuunga mkono na kumewapa matumaini mapya. Siasa visiwani humo zimebadili umbo na sasa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinachotawala kinakabiliwa na hasimu yake mkubwa akiwa na umbo jingine la ACT.
Kama tulivyoashiria wiki iliyopita, uongozi wa Seif Sharif Hamad unategemea zaidi juu ya haiba yake. Haiba hiyo pamoja na msimamo wake juu ya suala la muundo wa Muungano ndio wenye kuwavutia wafuasi wake na kuufanya uongozi wake uwe kitisho kwa watawala na chama chao cha CCM.
Kwa kujiunga na ACT-Wazalendo uongozi wake hauna budi ila kuzidi kuimarika kwa vile katika mazingira ya chama kipya utalazimika uwe na uhalali wa kisheria na ufuate urasimu mpya anaoukuta katika chama chake kipya. Uongozi wa aina hiyo ni madhubuti zaidi ya ule wenye kutegemea haiba ambao unaweza ukayumbayumba endapo hautoengwaengwa na uhalali wa kisheria.
Kwa viongozi wa CCM kuibuka kwa ACT-Wazalendo kuwa ndicho chama kikubwa cha upinzani Zanzibar kumetokea wakati mbaya kwa sababu ya mivutano miongoni mwa viongozi wa CCM/Zanzibar. Mojawapo ya masuala yanayosababisha mivutano ni hofu waliyonayo wengi wa viongozi hao kwamba kwa mara nyingine tena, kama ilivyo kawaida, suala la nani awe mgombea wao wa urais wa Zanzibar katika uchaguzi ujao wa 2020 litaamuliwa Dodoma, kwenye makao makuu ya CCM.
Wiki iliyopita kwa hatua ya kuuzui mkutano wa ACT na kwa vitisho mbalimbali vilivyotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali dhidi ya chama hicho ni wazi kwamba serikali imedhamiria kukifuta chama hicho. Wenye macho wanaiona kuwa kwa nguvu inatafuta visingizio vya kuchukua hatua hiyo.
Hilo litakuwa pigo kubwa kwa demokrasia kama tuijuavyo. Tayari hivi vitisho vinavyotolewa na wakuu wa serikali dhidi ya wapinzani na wengine wenye mawazo huru vinaitia walakin mkubwa demokrasia inayosemekana kuwako Tanzania.
Mara kwa mara viongozi wa upinzani wamekuwa wakifikishwa mahakamani na kushtakiwa kwa makosa mbalimbali, magazeti yamekuwa yakifungwa au kusimamishwa na hofu imewajaa wananchi kwa jumla wenye kutaka kueleza fikra zao dhidi ya watawala.
Ungewasili Moroni kwa mtumbwi wiki hiyo iliyopita baada ya kuuvuka Mkondo wa Msumbiji katika Bahari ya Hindi, ungekutana na mabavu ya utawala wa Rais Azali Assoumane.
Mji wa Moroni uligubikwa na machafuko makubwa yaliyosababishwa na ukaidi wa Azali wa kutaka kung’ang’ania madaraka hadi 2036. Utafikiri mabavu ya Tanzania yamevuka bahari nayo na kuwasili Comoro. Huko pia katika miezi ya karibuni wapinzani wamekuwa wakitafutiwa vijisababu vya kutumbukiziwa jela
Kwa mujibu wa katiba Azali, mzalia wa Ngazidja, alikuwa amalize muhula wake wa urais 2021. Na uchaguzi ujao wa urais uwaniwe na wagombea walio wenyeji wa Nzuwani.
Ili ajipatie muradi wake alifanya mageuzi kadhaa ya kikatiba. Miongoni mwayo ni kuufuta ule utaratibu wa kuuzungusha urais wa Comoro kwa kila kisiwa kati ya visiwa vitatu vilivyobakia kuwa pamoja (Ngazidja, Nzuwani na Mwali). Kisiwa chane cha Comoro, Mayotte, bado ni sehemu ya Ufaransa.
Azali pia aliyavunja Mahakama ya Kikatiba na aliteua Tume mpya ya uchaguzi aliyoijaza wateule wake. Kama tulivyoandika hivi karibuni Azali alijitangaza mshindi katika duru ya mwanzo ya uchaguzi wa urais uliofanywa Machi 24.
Inasemekana kuwa wajumbe wa Tume ya Uchaguzi ndio wenyewe waliokuwa wakipokea masanduku ya kura pamoja na fomu ambazo zikistahiki zijazwe na wawakilishi wa vyama pamoja na mwenyekiti wa kituo cha kura.
Wao wakitakiwa wapeleke taarifa zao kwenye ofisi inayoendesha uchaguzi. Lakini wajumbe wa Tume ya Uchaguzi wamekuwa wakifanya wao kazi hiyo.
Tume hiyo baadaye ilitangaza kuwa Azali ndiye aliyeibuka Rais kwa ushindi usiohitaji pafanywe tena duru ya pili ya uchaguzi. Pia walitangazwa magavana waliochaguliwa wa Ngazidja, Nzuwani na Mwali. Wote walikuwa wagombea wa chama chake.
Takriban wachunguzi wote wa uchaguzi, wakiwa pamoja na wale wa Muungano wa Afrika (AU), Comesa na ESAF walitoa ripoti wakieleza jinsi ufisadi ulivyopita katika uchaguzi na kwamba uchaguzi haukuwa wa uwazi na wa kweli. Ni wachunguzi wa taasisi moja tu Umoja wa Nchi za Kiarabu waliotangaza kwamba uchaguzi ulikuwa sawa.
Wagombea wote wengine 12 wa urais walikataa kuyakubali matokeo hayo ya uchaguzi wa urais, wakisema kwamba yaliyotokea ni “mapinduzi” na wakidai uchaguzi huo ubatilishwe. Baada ya mashauriano waliunda Baraza la Taifa la Mpito.
Alhamisi iliyopita mmoja wa wagombea hao Mohamed Soilih “Campagnard” alikamatwa muda was aa moja tu baada ya kutangaza hadharani kwamba yeye ndiye atayeliongoza Baraza hilo, ambalo bila ya shaka lingeunda serikali mbadala ya mpito.
Siku ya pili baada ya kukamatwa Soilih utulivu wa Moroni ulitobolewa kwa milio ya risasi. Wafungwa katika jela ya Moroni walitoroka na kambi kuu ya kijeshi ya Kandaani, mjini Ntsudjini, ilivamiwa na wanajeshi walioasi. Inasemekana kwamba walijaribu kumfungua Soilih pamoja na wafungwa wa kisiasa na wengine waliofungwa katika kambi hiyo. Wanajeshi wane walikufa katika mapigano kambini humo. Wengine kadhaa walijeruhiwa.
Jumatatu ya wiki hii magazeti matatu yalikosekana Comoro: Alfajr, Masiwa na La Gazette des Comores. Yote yalitiwa adabu na kufungwa na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Dadoud “Kiki” baada ya kuandika kisa cha mwandishi wa magazeti Toufeyli Maecha (Toufé) aliyekuwa amekamatwa na wanajeshi tangu asubuhi ya Jumamosi iliyopita. Inasemekana kwamba aliteswa.
Yaliyojiri Tanzania na Comoro katika kipindi cha wiki iliyopita tu yamezidi kuupaka tope ukanda mzima wa Afrika Mashariki. Na kama wenye busara hawatowatanabahisha watawala wa hizo nchi mbili basi tujiandae kuwaona watawala wakizidi kuikanyaga demokrasia na wananchi wakizidi kushajiika na kukataa kuonewa.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
Sent using Jamii Forums mobile app