singidadodoma
JF-Expert Member
- Nov 11, 2013
- 4,394
- 1,536
WAKATI Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe akijisifu kumteua Katibu Mkuu wa chama hicho mwenye kiwango cha elimu kinacholinga na cha Dk. Willibrod Slaa aliyeng’atuka, Mwenyekiti wa kanda ya Dar es Salaam Kuu, Mwita Waitara ana mtazamo tofauti.
Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga mkoani Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Uenezi wa Chadema, haamini kwamba kitendo cha kumteua Dk. Vincent Mashinji kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kina taswira ya kumuenzi Dk. Slaa aliyeng’oka kwenye nafasi hiyo siku chache kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
“Sidhani kitendo cha Mbowe kumteua Dk. Mashinji atakuwa amemuenzi Dk. Slaa, isipokuwa imeangukia tu katika mtazamo wa Mwenyekiti na sifa alizoziangalia. Ni kweli naye (Mashinji) ni daktari, lakini siyo kwamba Mwenyekiti amemteua kumuenzi Dk. Slaa, na siyo kwamba daktari pekee ndiye anaweza kuongoza.
“Mtu yeyote mwenye uwezo anaweza kuongoza chama hiki, hii ni fursa imetokea, huyu aliyeteuliwa ni daktari, lakini hata mtu mwenye digrii moja, stashahada, profesa ingewezekana kuteuliwa. Elimu ni kigezo muhimu, lakini siyo lazima awe daktari, ni ilimradi ana uelewa wa kutosha, hiyo ndiyo factor (kigezo) kubwa,” alisema Waitara katika mahojiano na Raia Mwema wiki hii jijini Mwanza alikohudhuria vikao vya Kamati Kuu na Baraza Kuu la Chadema vilivyobariki uteuzi wa Dk. Mashinji.
Wakati mtazamo wa Waitara ukiwa huo, Mbowe alipomtambulisha Katibu Mkuu mpya kwa wananchi katika uwanja wa Furahisha jijini hapa Jumapili iliyopita, alijipongeza kwa umakini wake katika uteuzi alioufanya akisema “Nimemtoa daktari (Dk. Slaa) na kumweka daktari (Dk. Mashinji).”
Katika mkutano huo, Mwenyekiti huyo wa Chadema alikiri kwamba elimu ni nyenzo muhimu katika uongozi, ingawa si lazima kila kiongozi awe msomi.
Itakumbukwa kwamba wakati wote ambao Dk. Slaa amekitumikia Chadema, Mbowe alikuwa mstari wa mbele kusifia utendaji wake, hivyo kitendo cha kutofautiana naye katika misimamo ya kuelekea Uchaguzi Mkuu uliyopita hakitoshi kumfutia kumbukumbu ya uongozi mahiri wa daktari huyo aliyewahi kuwa ukasisi.
Chanzo: Raia Mwema