Utata kuhusu miamala unahitaji kauli ya pamoja

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
Tangu Julai Mosi, ulipoanza utekelezaji wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa katika Bunge la Bajeti mwezi uliopita, wananchi wamekuwa katika mkanganyiko mkubwa kutokana na kauli zinazokinzana kutoka taasisi za fedha na vyombo husika vya Serikali.

Juzi, Mamlaka ya Mapato (TRA) iliitaka Benki Kuu (BoT) izichukulie hatua taasisi za kifedha zilizotangaza kufanya makato kwenye miamala ya wateja wao kwa madai kuwa Serikali kufanya marekebisho kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

TRA, kupitia kwa kamishna wake mkuu, Alphayo Kidata imesema taasisi hizo za fedha zimeonyesha kuwa na nia ovu dhidi ya wateja wao kwa kisingizio cha VAT. Ilisema kumekuwa na taarifa za upotoshaji ambazo zimekuwa zikiendelea kwenye mitandao ya kijamii kwa benki kadhaa kuwatangazia wateja wao kwamba kutokana na marekebisho ya sheria hiyo, wanaanza kukata gharama kutoka kwenye miamala ya fedha ya wateja.

Taarifa hiyo imekuja baada ya baadhi ya benki na kampuni za simu zinazotoa huduma ya fedha kutoa maelezo kwa wateja wake juu ya kuwapo kwa makato zaidi kwenye miamala yao, zikisema kutakuwa na ongezeko la asilimia 18 katika gharama za huduma zake. Zilisema ongezeko hilo la VAT litakatwa kutoka katika akaunti na kama muamala hautapitia kwenye akaunti, mteja atalipa kwa fedha taslimu.

Lakini kuhusu hilo Kidata alisema: “Ukweli ni kwamba kiasi cha VAT kinachotozwa ni asilimia 18 ya kiasi cha gharama ya huduma iliyotolewa na benki au taasisi za fedha.”

Alitoa mfano kwamba mteja ambaye amefanya muamala na kukatwa Sh1,000, fedha hiyo ilikuwa inachukuliwa yote na taasisi hizo, lakini sasa Serikali itachukua asilimia 18 ya VAT, ambayo ni Sh152.50 tu, hivyo fedha inayobaki kwenye taasisi husika ni Sh847.50. Hivyo mteja hatakiwa kutozwa zaidi.

Alisema ni jambo la kushangaza kwamba TRA na Wizara ya Fedha na Mipango ambao ndiyo wasimamizi wa utekelezaji wa sheria hiyo hawajatoa mwongozo, lakini taasisi hizo bila sababu za msingi zimetoa matangazo yasiyo sahihi.

Lakini Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndullu alikaririwa na gazeti hili akisema kwamba taasisi hizo za fedha hazikufanya kosa kuwatangazia wateja wao ongezeko hilo la kodi kwa kuwa zina wajibu wa kufanya hivyo na si BoT.

Alisema taasisi hizo zinatekeleza tu sheria ya fedha iliyopitishwa na Bunge ya kukusanya kodi na kwamba kila anayekusanya kodi anawajibika kuwajulisha wateja wake.

Utata huu umesababisha wananchi kutojua nini hasa kinaendelea na kuhofia kutumia huduma rasmi za fedha, jambo ambalo tunaamini kwamba litakuwa na athari kubwa kwa pande zote.

Kitendo chochote kinachoweza kuwatisha wananchi juu ya huduma hizo, maana yake ni kwamba kitawafanya wasitumie taasisi hizo rasmi za fedha na hivyo kuziathiri kimapato.

Lakini pia, njia yoyote mbadala itakayotumiwa na wananchi inaweza kuwa na athari kubwa kwa maendeleo na usalama wao, kwa kuwa kwa vyovyote vile watadunduliza fedha zao katika sehemu moja hivyo kushawishi wahalifu kuwashambulia. Lakini pia kitendo cha kuwa na fedha taslimu mkononi, hushawishi matumizi yasiyokuwa na msingi hivyo kuathiri mipango ya muda mrefu ya mwananchi.

MY TAKE:

Wito wangu kwa Serikali na taasisi zote za kifedha ni kukaa pamoja kujadili suala hili na kisha kutoka na tamko la pamoja na kuwaondoa hofu wananchi kuhusu huduma hizo za kifedha ambazo zimeshaanza kuwa sehemu ya maisha yao.
 
Back
Top Bottom