UTAFITI: Ndoa za mitala zimeanza miaka milioni 3.66 iliyopita

Interest

JF-Expert Member
Apr 11, 2015
3,434
7,067
Wakuu, kumbe ndoa za mitala ni kitu chetu cha asili eeh!??

Unaambiwa Zamadamu wa kale amegundulika kuwa alikuwa na familia ya Wake kadhaa na watoto..

Yaani ile maisha ya kidume kukamatia fursa na kuweka ulinzi kwa mawaifu ilianza toka enzi hizo za kuishi miaka milioni tatu na ushee..

Mzee wa Upako, Rais Mstaafu Mwinyi na Rais Dk Magufuli wameshagundua siri hii..

Ukitaka kuwa Imara na kuishi miaka mingi, mathna/mitala inakuhusu!
=============

IMG_20161226_102343_774.JPG

Nyayo za Zamadamu ‘Lucy’ kutoka Laetoli zinaonesha hivyo.


Mwaka mmoja uliopita, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na washirika wao kutoka nchini Italia, waligundua nyayo mpya za zamadamu aliyeishi takribani miaka milioni tatu na laki sita iliyopita. Watafiti hawa wameendelea kufanya utafiti zaidi na kugundua mambo kadha wa kadha kuhusiana na nyayo hizo.

Kwenye Makala iliyochapishwa tarehe 14 Disemba 2016 kwenye Jarida la kitaaluma na maarufu duniani liitwalo eLife, wanaonesha kwamba zamadamu walioacha nyayo hizo Laetoli walikuwa na miili yenye ukubwa tofauti. Utofauti huu wa ukubwa wa miili yao unadokeza taarifa mbalimbali za kijamii hususan uhusiano wa kimapenzi.

Mmojawapo kati ya watafiti waliogundua nyayo hizo Dk. Fidelis Masao anasema kuwa visukuku (mifupa na meno) vinatoa taarifa nyingi sana juu ya babu zetu hao walioishi takribani miaka milioni 3.66 iliyopita.

Hata hivyo nyayo za zamadamu ni tofauti na mifupa na meno kwa sababu upatikanaji wa nyayo ni mgumu sana kwani zimefukiwa ardhini na zimekuwa huko kwa muda mrefu na kuvumbuliwa baada ya mamilioni ya miaka baadaye kutokana na upekee wa mazingira yaliyochochea uvumbuzi. Uvumbuzi huu ni muhimu sana kwa nchi yetu na hatuna budi kuutangaza duniani kote.

Nyayo hizi, ambazo zimegunduliwa Laetoli ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, eneo ambalo mwanaakiolojia Mary Leakey na wenzake katika miaka ya 1970 walivumbua nyayo zinazohusishwa na Australopithecus afarensis (ajulikanaye kama Lucy), zinatoa taarifa juu ya: matembezi na ukubwa wa miili ya mababu zetu, utofauti wa tabia zao na namna walivyokuwa wakizaliana. Zikiwa zimezungukwa na nyayo za wanyama na ndege mbalimbali pamoja na viashiria vya matone ya mvua, nyayo mpya zilizogunduliwa Laetoli ni za zamadamu wawili waliokuwa wakitembea juu ya mwamba kwa mwendo na uelekeo ule ule sawa na zile nyayo zilizogunduliwa miaka ya 1970.

Naye mgunduzi mwingine wa nyayo hizi Dk. Elgidius Ichumbaki ambaye pia ni mhadhiri kutoka idara ya Mambo ya Kale na Urithi wa Utamaduni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema nyayo hizi pamoja na zile zilizogunduliwa miaka ya 1970 kwa pamoja zinatoa ushahidi usiokuwa na mashaka kwamba zamadamu (babu zetu) walianza kutembea wima na katika makundi miaka takribani milioni 3.66 iliyopita. Nyayo hizi zinaonesha kwamba zamadamu mmojawapo alikuwa na mwili mkubwa kuliko zamadamu wengine wote.

Matokeo ya tafsiri na uchambuzi wa data vinaonesha kwamba zamadamu huyo mwenye mwili mkubwa kuliko wenzake alikuwa mwanamume.

Vilevile, zamadamu huyu ndiye mwenye mwili mkubwa kuliko zamadamu wengine wote waliotambuliwa siyo tu kwa Tanzania na Afrika bali duniani kote.

Naye Dk. Marco Cherin ambaye ni mtafiti mshiriki kutoka Chuo Kikuu cha Perugia nchini Italia, anahitimisha kwa kusema kuwa walioacha nyayo hizo Laetoli ni mwanamume mmoja, wanawake wawili au watatu na mtoto mmoja au wawili. Matokeo haya yanaonesha kwamba zamadamu aitwaye Australopithecus afarensis maarufu kwa jina la Lucy alikuwa na mitala. Tafsiri ya matokeo haya ya utafiti inaonesha kufanana kwa kiasi kikubwa katika uhusiano wa kingono baina ya zamadamu na sokwe.
 
Back
Top Bottom