Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
Utafiti uliofanyika hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebaini kwamba asilimia 71 ya watanzania wanatumia muda mwingi kufanya shughuli zisizokuwa za uzalishaji mali wala tija binafsi kwao na kwa Taifa kwa ujumla.
Akizundua taarifa ya utafiti huo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa idadi hiyo hufanya kazi zisizoleta tija kwao na taifa na muda mwingi huutumia kujihudumia binafsi kwa kulala na starehe nyingine.
Ameeleza kuwa takwimu hizo zinaonesha wazi ni kwa namna gani watanzania wanashindwa kujishughulisha katika kufanya kazi zenye kuwaingizia kipato na badala yake wanatumia muda wao mwingi kufanya shughuli zisizo za uzalishaji hasa kufanya starehe mbalimbali.
“Ndugu zangu watanzania unakuta mtu amekaa baa au anacheza “poll table” kuanzia asubuhi mpaka jioni na hujui anafanya kazi gani ya uzalishaji, ndugu zangu tuone aibu basi tujishugulishe tulijenge taifa letu ili kujiletea maendeleo yetu na nchi yetu.”
Aidha, matokeo hayo yamebainisha kuwa asilimia 18.5 ya wananchi wanafanya kazi za uzalishaji na asilimia 10.6 ni wale wanaofanya shughuli za nyumbani zisizo na malipo huku uchambuzi wa kijinsia ukionesha kuwa wanaume asilimia 23.8, wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi ikilinganishwa na asilimia 13.5 ya wanawake.
Source: Ripoti: Asilimia 71 ya Watanzania hupoteza muda kufanya yasiyo na tija kwao wala Taifa - wavuti