Ushauri Kwa Viongozi Wakuu Wa Serikali – Awamu Ya Nne, Hususani Mhe Meghji, Karamagi,

ilboru1995

JF-Expert Member
Oct 4, 2007
2,329
268
USHAURI KWA VIONGOZI WAKUU WA SERIKALI – AWAMU YA NNE, HUSUSANI MHE MEGHJI, KARAMAGI, MRAMBA, YONA N.K KUHUSU UWAJIBIKAJI NA UADILIFU.


Baada ya kufuatilia kwa karibu sana matamshi mazito ya kukemea ufisadi na ufujaji wa rasilimali nchini Tanzania, yaliyotolewa hivi karibuni na Mhe Rais J.M Kikwete, Kadinali Pengo, Askofu Kilaini, Padri Victus Sichwale, Askofu Thadeus Ruwa, Sheikh Suleiman Gorogosi, Sheikh Mkuu Sheikh Shaaban Bin Simba, Askofu Dr. Valentino Mokiwa, Mhe Jaji Mstaafu Sinde Warioba, Waheshimiwa waandishi wa habari k.m Jenerali Ulimwengu, Joseph Mihangwa, Mbwambo, Conges Mramba, Jackton Manyerere, Said Kubenea, Ayubu Rioba, Majid Njengwa, Innocent Mwesiga, Padri Privatus Karugendo, D. John, Muhingo Rweyemamu na wengine wengi wakiwemo wananchi, na hasa kutokana na umma wa Watanzania kuguswa na yaliyotokea BoT, nimeona ni busara nami ni ungane na wote hao ktk kupaza sauti ya kuchukizwa na matendo haya yenye kurudisha nyuma juhudi za maendeleo ya nchi yetu.


Nianze kwa kusema mimi ni mtumishi mstaafu niliyekuwa nimeajiriwa na serikali ya Tanzania kuanzia tarehe 01.01.1969 hadi tarehe 02.06.2005. Ngazi ya juu niliyofikia ni kubahatika kuwa katibu ( msaidizi mkuu kiserikali ) wa Mwalimu J.K Nyerere. Nimeishi naye hadi alipofariki dunia 14.10.1999. Kubwa nililozingatia katika utumishi wangu serikalini katika kufanya maamuzi madogo na makubwa ni kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za serikali ambazo msingi wake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( Sheria mama). Niharakishe kusema mapema kuwa nilipotambulishwa na kupokelewa na Baba wa Taifa kama msaidizi wake mkuu , baada ya Butiku na Batao , Baba wa Taifa kwa maneno yake mwenyewe aliniasa kwa kusema “ KASORI, KARIBU SANA. NAOMBA USIFANYE KAZI KWA KUNIOGOPA. MUNGU AKUSAIDIE KTK KUNILEA KISERIKALI; KUWA MWAMINIFU NA JASIRI KTK KUNISHAURI”

Jambo jingine ambalo lilinisaidia katika utumishi wangu serikalini ni kujitahidi mara kwa mara kudurusu kurasa za nyuma na madokezo katika kila jalada liliokuja mezani kabla ya kufanya maamuzi ya suala jipya ndani ya jalada hilo. Nilizoea kufanya hivyo kwa lengo la kuepuka kutoa maamuzi yenye kuleta utata ambayo labda huko nyuma tayari yalikwisha kutolewa maamuzi ya busara na kufangwa. Nathubutu kusema kuwa hili ni moja ya yale yaliyonijengea heshima kubwa kwa Baba wa Taifa.


Jambo la tatu nililoliweka maanani daima ni kutambua na kuheshimu alama kuu za serikali ambazo ni taasisi kama vile URAIS, UWAZIRI, UKATIBU MKUU, na KATIBA ya Jamhuri yetu. Niliishi kwa kutambua kuwa Rais au Waziri au Katibu mkuu n.k wote wanafanyakazi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu na siyo “hisia” au “mawazo yao”.


Kwamba Mhe. Meghji mwenye dhamana kubwa ya KAPU la fedha za serikali anatuambia Watanzania na dunia nzima kuwa aliidhinisha malipo ya Tsh billion 40 kwa kampuni ya Kagoda Agricultural ltd kwa kumuamini Gavana Ballali, inatia kichefuchefu hasa inapozingatiwa kuwa Meghji naye alihudhuria semina elekezi Ngurudoto na kupata heshima ya kutembelewa wizarani kwake na Rais J.M. Kikwete. Ni kweli kufanyakazi kwa kuaminiana ni moja ya vigezo vyenye kuleta ushirikiano mzuri katika sehemu za kazi. lakini kuaminiana siyo mbadala wa sheria, kanuni na taratibu za serikali. NAKATAA! Mhe Zakia Meghji si mgeni katika kazi za uwaziri. Haiingii akilini eti baada ya Boss ( Rais) kukasirishwa na yale yaliyojiri BoT, yeye Meghji anasema alidanganywa na gavana. Mhe Meghji ofisini kwake katika makabati au mezani anazo sheria , kanuni za utawala wa fedha . Pia Waziri anao wasaidizi, manaibu mawaziri wawili, katibu mkuu, manaibu katibu mkuu wawili, wakurugenzi, makamishna na wengine wengi, tena wasomi wazuri tu. Hivyo anao uzoefu wa kutumia hizo rasilimali nzuri za serikali( wataalam na nyaraka)! Mhe. Mgonja (KM) ni mtaalam mzuri tu wa masuala ya BoT na uchumi. Meghji anamtumia vizuri?


Nimesoma barua na taarifa za Mhe. Meghji katika gazeti la raia mwema la tarehe 16-22 Jan.2008 toleo la 012, uk. 12. Nimeshikwa na butwaa maana zote hazina nukuu za sheria , kanuni na taratibu za serikali ndani ya maelezo yake yote. Katika uandishi wa barua za serikali, unapoandika; kinachokupa mamlaka kwa hoja yoyote ile mara zote ni nukuu za sheria, kanuni na taratibu za serikali. Lazima zitajwe. Kinyume chake ni ngonjera na mawazo binafsi tu! Ndiyo maana barua za serikali nyingi siku hizi ni ndefu mno!


Hata alipo omba ukaguzi kwa Mthibiti Mkuu wa Hesabu za serikali alipashwa kunukuu vifungu vya kanuni za ukaguzi wa mahesabu ya serikali. Mhe Utoh alifanyakazi kizalendo. Nampongeza. Mwandishi mmoja kati ya hao niliowataja mwanzoni aliwahi kuandika kuwa “baadhi ya viongozi wetu wanapoteuliwa kushika madaraka makubwa hujiona kuwa wana akili maalum, nzuri kuliko za walio chini yao” Ni ukweli usiopingika kuwa leo hii tunao viongozi wenye tabia ya kudharau kutumia nyaraka rasmi za serikali na ushauri wa wataalam walionao. Tabia hii imefikisha taifa letu kukodi kwa gharama kubwa wataalam wengine wenye sifa duni kutoka nje kuja kushughulikia hata matatizo madogo! Ni kwanini hao wanaaminiwa na kuheshimiwa kuliko wataalam wetu na sheria zetu, mimi sijui! Ni aibu kwa Mhe. Meghji na hata prof. Maghembe kusema kuwa walidanganywa!


Angalia hawa mawaziri ni wasomi wenye hata makabrasha muhimu ya Ngurudoto ambapo fedha nyingi zilitumika kuwa gharamia! Je, waliyaacha Ngurudoto? Nadhani kwa siku za usoni ni busara kuanza na kozi za Ngurudoto kabla ya kugawa madaraka ili wasio elewa wasipewe madaraka KABISA. Serikali makini haijengwi na viongozi wenye kubahatisha juu ya uendesheji na uongozi wa serikali, HAPANA! Ndiyo maana tuna Permanent Secretaries. Eti anafanya hisani kupata ushauri wa katibu mkuu! Mawaziri hawapashwi kufanyakazi na permanent secretaries kwa misingi ya hisani. Kila mmoja analazimika kuona kuwa anamhitaji mwenzake katika uendeshaji wa serikali. Wote wanapashwa ku-review flimsy files kila wakati, kujua ni nini kinaendelea ndani ya wizara/idara.

Watanzania wamechoka kuona/ kusoma maamuzi ya cabinet na wizara au idara yanakinzana. Pia ni muhimu mawaziri wetu wajenge tabia ya kuelewa kuwa maamuzi ya wizara moja yanagusa wizara nyingine na serikali kwa ujumla. Inauma sana kuona warsha/semina za mara kwa mara hata pale Bungeni wanalipana posho za Jumamosi juu ya posho za kila siku wawapo bungeni, baada ya hapo hakuna tija ya maana na badala yake mtu anaishia kumwambia Rais na watanzania kuwa “nilidanyanywa” Kumbukumbu zinapofutika haraka ng’atuka. Ni Mhe. Meghji huyo huyo alituletea mwekezaji wa kununua shamba la mikoko yetu. Wataalamu wa misitu na waandishi wa habari Mungu bariki walipaza sauti kweli kweli na agenda hiyo mufilisi ikafa kifo cha mende. Katika hilo nani alimdanganya? Kwa tabia hii kuzoea kudanganywa, hivi mhe.Rais wetu hajadanganywa na wakubwa hawa? Ndiyo! Kwani Msabaha hajadanganya juu ya umeme? Je alijiuzulu?Ona! Mwaka jana wakakwepua posho na kuzunguka nchini eti wanaeleza ubora wa bajeti! Mungu wangu! Danganya ya aina yake tu. Sasa kazi ya wabunge wetu ni nini? Si hao ndio wenye kujua lugha na shida zetu? Si walikuwepo Bungeni na ndio walioichambua? Meghji na wenzake wanafikiri hatujui somo la URAIA? Mhe. Meghji, kwa vile ni fundi wa kiingereza naomba nimwambie kuwa “People can be fooled for a while, they can for a while believe stories (rhetorics), that while the pain is here to-day, the gain is around the corner but after a quarter century or more, such stories lose their credibility”

Ya BOT tumeyaona! Dr. Slaa na Hamadi walipo anzisha sakata la BOT, hadithi, ngonjera kutoka kwa Meghji na Wenzake zilikuwa nyingi. Mimi ni mwana CCM mwenye kadi Na. Ab1478743 kwa vile niliyajua kiasi fulani wote hao wawili Hamad na Slaa niliwatumia message kuwa semeni kwa nguvu tu bungeni. Nilifanya hivyo kwa mapenzi makubwa niliyonayo kwa nchi yangu. Tanzania si nchi ya viongozi tu. Ni yetu wote. Hapa nimethubutu kutaja namba yangu ya CCM kwa kujiamini sana kwa vile nilifundishwa kusema ukweli tu na marehemu J.K. Nyerere – nitatoa mfano hai. Waulizeni wahusika nitakao wataja hapa.

Siku moja Naibu Katibu Mkuu wa CCM Mhe. Ameir akifuatana na Mhe.Maokola Majogo walikuja Butiama bila taarifa. Walipofika nilikwenda kumwita Mwalimu shambani na njiani alisema kwa masikitiko kwa nini nilichelewa kumpa taarifa kuhusu ujio wa wakubwa hao. Nilimwambia wamekuja ghafla. Kabla ya kuwasalimu Mwalimu alikwenda kusali chumbani kwake na alipotokea aliwauliza kuna jambo gani kubwa ambalo liliwaleta pasipo taarifa. Walijibu kuwa wametumwa na Kamati kuu ya CCM kumweleza kuwa anaaibisha CHAMA kwa kuzungumza na wapinzani Mrema na Sharif. Mwalimu aliuliza walikuja kwa njia gani? Wakajibu kuwa kwa ndege. Akauliza ndege gani? Wakajibu Jet ya Rais. Akauliza tena: ile ambayo nilikuwa natumia? Wakasema ndiyo! Mwalimu aliuliza hivi mnapo niita Baba wa Taifa nilileta maombi (application) serikalini au katika chama niitwe hivyo? Hivi Mrema na Sharif siyo watanzania? Hivi kuunda vyama vya upinzani ni usaliti? Hivi nyinyi CCM kama hamnihitaji kwa ushauri kwa vile mnajua kila kitu basi nisizungumze na vyama vingine? Hivi hamjui kuwa mimi Baba wa Taifa ni above political parties? Mmesema nina kadi namba moja, sawa kwa hiyo mmekuja kunikamata hapa kwetu nilipozaliwa? Maana wewe Ameir ni Waziri wa Mambo ya Ndani na Majogo Ulinzi? Aliendelea kwa kusema kuwa, kama hilo ndilo lililowaleta na kama mmetumwa na mwenyekiti Mhe.Ali Hassani Mwinyi na kamati yake ya CC basi kuleni chakula na baada ya hapo nitawapa kadi yenu kisha ondokeni! Mimi naijali na kuipenda Tanzania kuliko vyama vyenu, mnasikia?

Hapo Mhe. Maokola Majogo alijiengua haraka kwa kusema kuwa Mhe. Mwalimu mimi nilipata lift tu kwenye ndege ili nije kukagua ujenzi wa nyumba mpya tunayokujengea wanajeshi. Kisha nilimfuata Mwalimu chumbani kwake na kumsihi asirudishe kadi na akakubali. Hakurudi kuwaaga!

Nimelazimika kutoa mfano huu wa kweli kwa kuenzi hekima/busara hizo za Baba wa Taifa kwamba wapinzani wanapojenga hoja za msingi zenye maslahi ya Taifa mimi huwapa shime kwa kuongea nao. Hata CCM pia huwapa shime. Nilifanya hivyo kwa mbunge wa Mbarali kupinga ubinafsishaji na kuuzwa kwa mwekezaji wa nje mashamba ya mpunga, pia nilimpongeza kwa simu Mhe. Beatrice Shelukindo katika hoja ya uteuzi wa mabalozi kuwa baadhi hawana sifa na hawaandaliwi. Katika haya niliyoyasema kama yameudhi viongozi wa CCM basi kama Mwalimu alivyofanya kwa Mhe. Ameir nami nitakuwa tayari kurudisha kadi ya CCM!

Naipenda na kujali Tanzania kuliko vyama ambavyo havina uchungu na UBAKAJI WA RASILIMALI ZETU na vyenye viongozi waliojaza pamba masikioni na macho yasiyoona ukweli! Tunaimba kumuenzi Baba wa Taifa lakini matendo hayafanani! Nasema nje ya nchi yapo mataifa yanayomuenzi Mwalimu kuliko sisi. Nendeni kwa Mhe Kagame. Pamoja na matatizo ya vita uchumi wao haupangwi na kuendeshwa kisanii kama Tanzania. Hata wanavyo sherehekea Mwalimu DAY utafikiri alikuwa Rais wao! wametumia mawazo yake vizuri zaidi kuliko sisi! Na hayo mnayo yafanya (BOT) kwenye rasilimali za nchi kama Madini n.k angekuwa hai, nasema huo ndio ungekuwa ugonjwa wa kumua haraka kuliko ugonjwa wa LUKIMYA. Kuna wakati aliniambia juu ya mambo ya ovyo yanayofanywa na viongozi serikalini na akalia machozi. Tusema nini ndipo msikie sasa? The poor in Tanzania are now left to fend for themselves. When they speak no one listerns. When someone listerns they are told nothing can be done! Tunaambiwa sisi ni wavivu!


Naomba niseme kwa msisitizo mkubwa kuwa CCM na serikali, vyote vina taratibu nzuri tu. Maandishi hayo kimsingi yanalenga viongozi maalum kama hao wanaovuruga nchi hii kwa rhetorics za kuondoa umasikini kudumisha amani na mshikamano….eti Tanzania kisiwa cha amani n.k. huku wakitumia kiburi kuvurugwa kwa raslimali za nchi.

Kwa mfano wote hao wamekopeshwa magari (mawaziri, makatibu wakuu) wote. Lakini kwenda kazini na kurudi nyumbani bado wanatumia magari ya serikali, pia wanazurura nayo hata likizoni bila aibu. Hata kama ni stahili je hizi zina morals?. Katika hili nashauri viongozi wetu waende kwa Mhe KagameRwanda waone magari ya serikali yanavyotumika. Kule hakuna mzaha!. Kwetu hapa katika Wizara moja tu utakuta aina ( miundo) zaidi ya sita na hili limeshuka hadi kwenye halmashauri za Wilaya n.k. Nani katuloga? Je, katika haya huwa tunafanya faithful decisions? kwanini tumekuwa ni mafundi wa kuiga mambo ya hovyo kila wakati? Bungeni kwanini tumeharakisha kutunga sheria za ugaidi na haya tunayapuuza? Hivi ni lazima kila kitu tuaambiwe na mataifa makubwa au mashirika ya wakubwa? Hivi ndivyo tunavyojenga amani na mshikamano? Stahili zao ni pamoja na kuishi nyumba za serikali bure, wanalipiwa umeme, maji, simu, watumishi wawili, dereva wa kuendesha gari binafsi na samani za nyumba na vyombo vya chakula. Ona sasa tumepandishiwa bei ya umeme wakati tunalalamikia mafuta ya taa!


Hawa tukiwasema ati wanajibu kwa kiburi tunatukana serikali au CCM! Hapana huo ni uhuni. Ni ukweli CCM na serikali hawako hivyo. Hawa ni wahuni waliojificha katika CCM na kana kwamba hayo hayatoshi wanachezea kapu kuu la fedha zetu za serikali (BOT). Kweli tunyamaze??


Ona alivyosema CASTILLO wa Guatemala kuhusu wabakaji/wakwepuaji wa raslimali za nchi; namnukuu kiingereza (naomba radhi): -“One day the apolitical intellectuals of my country will be interrogated by the simplest of our people. They will be asked what they did when their nation died out slowly like a sweet fire small and alone. No one will ask them about their dress their long siestas after lunch. No one will want to know about their sterile combats with the ideas of nothing. No one will care about their higher financial Learning. They won’t be questioned on Greek mythology or regarding their self disgust when someone within them begins to die the coward’s death. They will be asked nothing about their absurd justifications born in the shadow of total lie. On that day the simple men will come.Those who have no place in the books and poems of the apolitical intellectuals but daily delivered their bread and milk, their tortillas and eggs those who mended their clothes, those who drove their cars, those who cared for their dogs and gardens and worked for them and they will ask: WHAT DID YOU DO WHEN THE POOR SUFFERED WHEN TENDERNESS AND LIFE BURNED OUT IN THEM? We, the African students and intellectuals, what shall we say when we are asked by simple MEN AND WOMEN; WHAT DID YOU DO WHEN THE POOR SUFFERED, WHEN TENDERNESS AND LIFE BURNED OUT IN THEM?


Oneni hekima hiyo. Meghji kasoma ana elimu nzuri tu. Pamoja na hayo ya elimu yake, je ana hekima kusema alidanganywa? Na wote wale wanaofanana naye ni vema wakazingatia pia mawaidha ya Charles Mloka (16/01/1983) aliposema: “Ingawa elimu ni bora, hekima bora zaidi. Hekima ndiyo heshima, ya elimu ikafaa. Hii ndiyo sifa njema, hata ukisoma sana. Hekima huleta jibu, watu linalovusha. Babu zetu hapo zamani hekima walithamini.Uongozi wa hekima ulileta kuungana. Watu waliishi vema, wakiwa wanapatana. Hii tushike sana, utu ufike kilele. Hekima ndiyo uhuru wa watu wowote wale hekima huleta nuru, ya watu kuenda mbele ingawa elimu bora. Hekima bora zaidi!” (nimenukuu vipengele vihusuvyo mada yangu tu)
Marehemu Baba wa Taifa katika mojawapo ya hotuba zake kwa viongozi wenzake kuhusu maadili na uwajibikaji aliwahi kusema “Mtu unapofanya kosa na ukalikubali na kuomba radhi bila kusingizia wengine… wewe unahesabika kuwa una hekima, uungwana na busara ni mtu wa kutumainiwa kwa kupewa hata madaraka makubwa hapo baadaye”. Mwishoni mwaka jana katika taasisi moja Uingereza zilipotea nyaraka muhimu. Waziri mkuu G. Brown alikwenda Bungeni haraka kuomba nchi radhi. Huu ndio uadilifu. Ndiyo uungwana. Kwa vile mada yangu inahusu UADIIFU NA UWAJIBIKAJI WA VIONGOZI WETU.

Sasa kwa kuzingatia yote haya na hekima za Baba wa Taifa nachapisha hapa kikamilifu barua ya Mhe. Ali Hassani Mwinyi kwa yale yaliyotokea shinyanga mwaka 1975 yeye akiwa Waziri wa Mambo ya ndani kwa lengo la kuona kama huo utakuwa ni msaada wa mwisho kwa Mhe. Meghji na wenzake kufuata nyayo. Barua yenyewe inasema hivi; tufuatane kwa kuisoma kwa makini tafadhali.

Baada ya kusoma barua ya mhe. Ali Hassani Mwinyi, unaona uadilifu, uwajibikaji na unyenyekevu uliotukuka? Hiyo ndiyo hali halisi inavyotakiwa yaani; hayo yaonekane yakitendeka! Hivi tunaposema kuenzi busara za viongozi wetu maana yake nini hasa? Ni kweli tunawaenzi kwa vitendo? Yetu ni masikio na macho. Kujiuzulu kama alivyofanya Mhe. Ali Hassani Mwinyi sio ujinga. Ni uungwana , ustaarabu na ni kusafisha njia ili haki iweze kutendeka pasipo kuharibu imani ya wanachi ndani ya taasisi husika. Kurudisha imani iliyopotea kuna gharama kubwa. Wakubwa hili mnalijua.

Sambamba na barua ya Mhe. Mwinyi hapo juu, Professor Joseph Stiglitz, mtaalamu wa uchumi, ona aliyoyafanya kwa kuona kuwa Ikulu Marekani sera za Rais Clinton juu ya utandawazi zilikuwa zinakandamiza nchi masikini sisi tukiwemo. Kwa maneno yake anasema: “ When I was about to leave the white house for the world bank, President Clinton asked me to stay on as chairman of his council of Economic Advisors and as member of his cabinet. I declined, because I thought the task of designing policies and programs that would do something about the abject poverty which plagued the less developed world was a far more important challenge… I had seen countries where poverty was increasing rather than decreasing, I had see what that meant-not just in statistics but in real lives of people”.
Huyu sasa ni mwalimu tu-professor of economics and finance University of Columbia. Catrina ilipotokea marekani nako viongozi kadhaa walijiuzulu.

Unaona wenzetu wanavyojiuzulu kistaarabu. Msabaha, Mramba, Karamagi, Meghji, Ballali nchini Tanzania wamekataa kujiuzulu. Hapa kwetu hotuba zimejaa takwimu ambazo hazina uhusiano kabisa na hali halisi ya maisha ya watanzania! Tunazunguka nchi eti tuna bajeti nzuri n.k na uchumi unapaa! Tunamdanganya Rais na tunawadanganya Watanzania mchana kweupe na kwa kiburi. Vipaumbele katika bajeti zetu vinatisha! Kana kwamba hayatoshi Mramba juzi juzi kama Karamagi kaweka sahihi mkataba wa hovyo wa EPA. Huyu sasa kaleta sumu kali - TINDIKALI MACHONI ya kuua biashara na viwanda vyetu. Tarehe 26/01/2003 Rais Lula Da Silva alisema;
Any export we might make will be worth nothing if rich countries continue to preach free trade and practice protectionism.
Mhe. Mramba ona; Nothern governments now spend $ 1 billion a day on agricultural subsidies. Amounting 6 times their spending on aid. Subsidies generate large surpluses that are dumped on world markets at prices bearing nothing to production costs. Millions of farmers in developing countries receive lower prices for their products and get pushed out of markets of the powerful nations. To add insult to financial injury, rich countries impose higher taxes on processed goods than on raw materials. Mramba ajue kwamba advanced industrial countries which dictate the direction of globalization have not yet developed the underlying sympathies which are necessary to make the global economy work. Kwanini Mramba hatumii wataalam ofisini au chuo kikuu kabla ya kukurupuka?
Hivi haya, Mhe. Mramba na ujanja wote alionao wa kutwambia tule majani hayajui kweli? Amuulize Prof Samwel Wangwe MNEC, prof Ndulu, prof Shivji, prof Baregu, Iddi Simba kwa yaliyojiri DOHA, Joseph Mihangwa, prof Joseph Stiglitz na prof A.Safari maana ya nukuu hiyo hapo juu. Kwa hapa watanzania walipofikia sampuli hii ya mawaziri na watendaji wanaofanana nao ni muhimu wakajua kuwa kama nchi tayari kuna idadi isiyo haba ya informed citizensary which is more likely to provide some checks against abuses of power/ office! Si busara kumkasirisha Rais, si busara kukasirisha viongozi wa dini. Si busara wananchi kupoteza imani kwa serikali waliyochagua. Bunge letu lina wasomi wengi wazuri . Muhimu wachangamkie maendeleo. Serikali ijue wajibu wake katika kuleta maendeleo. Muhimu kwa akina Mramba, Karamagi, Meghji wasaidiwe kuona njia sahihi ya maendeleo.

Mwisho nasema watu walipokufa shinyanga mwaka 1975, mhe. Mwinyi kwa kusutwa na dhamira yake ya kukosa amani moyoni ( yeye hakushiriki mauaji wahusika walimficha) kwa hiari yake na kwa unyenyekevu mkubwa tarehe 22/01/1977 aliandika barua kwa Rais Nyerere ya kujiuzulu uwaziri. Tayari tumesoma hapo nyuma. Katika hili sakata la BOT na uporaji wa raslimali zetu ikiwa ni pamoja na wanyama kuuzwa kwa bei za kutupwa, waheshimiwa Meghji, Mramba, Karamagi, Yona, Msabaha tayari wamekwisha fanya mauaji makubwa ya watanzania kuliko yale ya Shinyanga. Kuua si lazima iwe kwa silaha au sumu tu. Unaweza kuua kwa kutotoa fedha za kununulia dawa na zana nyingine za tiba kwa wakati. Kwa kipindi ambacho mabillioni hayo ya fedha yalipoibwa BOT na kwingineko, hospitali zingetoa takwimu za watanzania waliokufa kwa kukosa nyenzo muhimu za tiba taifa letu lingetikisika. Kwa kutojali sasa ni kawaida mawaziri na vigogo wengine wanatibiwa India, Marekani na ulaya hata kwa ugonjwa wa mafua tu. Mwalimu alianzisha mradi wa hospitali ya Lugalo (JWTZ) kwa lengo la viongozi pamoja na Rais kutibiwa hapo kama inavyofanyika Marekani, lakini nani anajali kupaendeleza? Yawezekana nako tukabinafsisha, nani ajuae kwa staili hii ya viongozi wenye kuabudu utandawazi (MJOMBA MWEKEZAJI)! Tunao madaktari wenye ujuzi mkubwa tu lakini shida ni vifaa na miundo mbinu. Someni hotuba ya Mwl JK. Nyerere bungeni ya mwaka 1985

Fedha zilizoporwa na tunazopoteza kupitia mikataba mibovu zimeua/zimedhoofisha asilimia kubwa tu ya watoto wetu waliostahili kupata elimu nzuri/bora hapa nchini. Fedha hizo kama walivyokwisha sema waandishi wa habari (tunaowadharau na kuhujumu juhudi zao na kusifia waandishi wa nje) zingesaidia kuboresha majengo ya vyuo vikuu vya mlimani (DSM), Muhimbili na Sokoine. Hali ilivyo sasa mlimani, binafsi naona aibu kusema kuwa nilisoma hapo! Kwa taarifa yenu yale majengo ya awali ya mlimani yalikuwa na hadhi ya kimataifa ikiwa ni pamoja na chakula tulichokuwa tunapata kama wanafunzi. Hata Baba wa Taifa ilikuwa ni kawaida yake kuja kushiriki nasi katika chakula cha jioni kila mwaka-ANNUAL DINNER! Pia ilikuwa ni kawaida yake mara nyingi kuja kuzungumza nasi (siyo kutuhutubia na kufoka)
Mwaka jana nilibahatika kutembelea chuo kikuu cha sokoine morogoro. Ukiona majengo ya kitengo cha mifugo, karakana na sehemu za kuhifadhi vyakula vya mifugo n.k. hutaamini kuwa hiyo ndiyo taasisi namba moja ya kutoa wataalamu wa kilimo tunacho imba kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Madaraja muhimu yaendayo kwenye mashamba muhimu ya majaribio ndani ya chuo yamekatika. Gharama za kuyarejesha katika hali yake chuo hakiwezi kumudu. Lakini wakubwa wamekwapua BOT. katika hatua ya kuchukiza sana utakuta baadhi ya viongozi wakitembelea chuo hicho au mkoa wa Morogoro wanachota miche, madume au mitamba yenye ubora wa hali ya juu ati kama zawadi! Kuna wakubwa fulani wamezoea kutumia raslimali za vyuo vikuu kuendeshea kampeni zao za uchaguzi. Hali ya sekondari zetu hasa zile za kabla na baada ya uhuru sina la kusema!! Nilibahatika pia kutembelea sekondari za Musoma, Ilboru, Mzumbe, Pugu, Bwiru, Old Moshi na Minaki. Niliyoyaona ndani ya madarasa, maabara, mabweni na nyumba za walimu ni siri yangu yenye kusababisha kilio cha machozi ya damu. Basil Davidson aliwahi kuandika kitabu chake cha historia akakiita WHICH WAY AFRICA, Hayo niliyo yaona katika shule zetu na sasa kusikia ukwapuaji wa mabillioni BOT natamani kuandika kitabu na nikiite WHICH WAY TANZANIA! Kabla sijafanya hivyo niombe tu kwa unyenyekevu kuwa fedha hizo zitakaporejeshwa, na iwe mapema, basi nyingi zimwagwe kwenye kuwekeza katika elimu na afya.
Sambamba na hayo nitoe ushauri tu kuwa ili kufanya gawio la busara katika wizara mbali mbali, Waziri wa fedha ajenge tabia ya kutembelea maeneo yenye matatizo makubwa. Pia wakuu wa mikoa/wilaya waache taabia za kumpangia Rais ratiba zenye mafanikio tu: sehemu kubwa ya ratiba zao wamwonyeshe yeye na Waziri Mkuu mambo yenye utata ili wakuu wetu waachane na aibu ya kutumia fedha za wafadhili kujengea vyoo shuleni n.k

Naomba kuhitimisha kwa kutoa mchango wangu kwa chief Whipp, Mhe Dr. Batilda na Mwanasheria Mkuu Mhe Mwanyika kuwa kwa haya yaliyotokea BoT na tatizo la madini. Si busara kumfanya Rais kuchukua nafasi zao bungeni. Wao walishiriki kwa nguvu kubwa kuua sauti za wabunge wa upinzani Bungeni. Kwa haya yaliyotokea wanalo la kusema? Mijadala yenye maslahi ya nchi siyo ya kufanyia usanii/mzaha Bungeni. Ni muhimu hawa wawe “ focused” wamsaidie spika na Taifa. Kwa wabunge kama Gallinoma, Dr Mwakyembe,Anne Kilango, W.Shelukindo, Ibrahim Sanya, Hamad, Dr Slaa, Zito hawa ni watu very serious, tujifunze kutoka kwao tafadhali.

Kwa waandishi wa habari nawashukuru kwa dhati na nawatakia kazi njema. Katika kitabu chake “ UONGOZI NA HATIMA YA TANZANIA” marehemu baba wa Taifa alisema: “OLE WAKE TANZANIA TUSIPOISAIDIA” Niwezalo nimefanya, kushauri na kuonya. Nasi tumsaidie (Rais J.M. Kikwete) Mhe. Meghji na wenzake kwa unyenyekevu nawaomba mtafakari haya tafadhali. Haitoshi kutuambia Ballali alidanganya. Mlikuwa wapi? Watanzania bado tunasubiri kuambiwa na Meghji ni kikao gani cha serikali na ni sheria zipi za serikali zilimruhusu Meghji kutenda aliyoyatenda. Hata anaposema maswala nyeti yenye usalama wa nchi – hayo yote atueleze ni kwa mujibu wa sheria na vikao vipi? Je barua hiyo ya Mhe. Mwinyi itakuwa ya msaada na angalizo mwafaka katika medani za uadilifu na uwajibikaji? TAFAKARI!!

S. H. Kasori

0754372141
 
Baba asante kwa kazi nzuri ya kukumikia kwa uaminifu,wape shule vilaza wa CCm hawa
 
barua ya alhaji mwinyi nimeshindwa kuiweka hapa .....
inatia moyo sana kuona yale matone yaletelezayo mafuriko ya ukombozi yanazidisha ubichi wa ardhi tayari kabisa kutengeneza mkondo wenye nguvu nyingi za kuondoa ufisadi ndani ya ardhi takatifu ya watanzania.
 
barua ya alhaji mwinyi nimeshindwa kuiweka hapa .....
inatia moyo sana kuona yale matone yaletelezayo mafuriko ya ukombozi yanazidisha ubichi wa ardhi tayari kabisa kutengeneza mkondo wenye nguvu nyingi za kuondoa ufisadi ndani ya ardhi takatifu ya watanzania.

Mzee wetu S.H Kasori heshima mbele, nakushukuru sana kwa hii post imenitoa tongotongo nyingi, sasa nini kifanyike jamani kila kitu ovyo ovyo tu Tanzania...kuna wengi sana wanatakiwa kuwa na Accountable responsibility tunaishia kupewa bla bla..Karamagi, Meghji, Mramba, Yona, Mkapa, Balali, Rostam list ni ndefu mno jamani turudishieni pesa na utajiri mlo tupola kabla hatujaanza warushia mawe, pinde na mishale!! Hivi kuna raha gani kuwa na mapesa mengi wakati jirani zako wanakufa kwa njaa ama kwa kukosa huduma muhimu, wanasahau kuwa masikini siku wakimua kurudisha utajiri wao itakuwa hatari...
 
Mimi nadhani Tz we need Bunge la Pili kama Senate- na constituion members iwe Jaji Mjuu msataafu, Maaskofu wa dini, Shehe Mkuu, Chancellors wastaafu wa Vyu Vikuu, n.k, na watu wengine maarufu wasiohusiana na executive directly!

Hawa wawe na uwezo to question maamuzi ya Bunge! Hii itahitaji katiba ifanyiwe marekebisho!

Taabu sasa hata serikali ikichemsha- na kufanya kama wanavyopenda hakuna wa kukumea! Na kuwajibika kwa kujiuzulu!

Ktk demokrasia ya kweli sakata la BoT Waziri wa Fedha inabidi ajiuzulu!

Huu utamaduni wa kujiuzulu wakati wa JK mbona hauonekani?
 
Very strong, kama ni kutuma ujumbe kwa mafisadi na umma kwa ujumla, it can not get better than this.
 
Najua wengi wetu humu ni wavivu wa kusoma,lakini nashauri msome hii article iko very interesting!
 
Nimeambatanisha barua ya Mhe. Mwinyi kuomba kujiuzulu, tafadhali isomeni muone uadilifu na uwajibikaji wa kuigwa na watajwa hapo juu.
 

Attachments

  • Mwinyi25.pdf
    682.7 KB · Views: 158
Mzee wetu kuna haja ya kuichapa hiyo article yako kwenye gazeti kwani bila hivyo ujumbe huu utawafikia watu wachache tuliopo hapa naomba pia uwasilishe ujumbe wako kwa magazet kama mwanahalisi.tanzania daima ,mwananchi na raia mwema naamini wataandika ujumbe wako.

Wosia wangu kwa vijana mliopo hapa ni kuwa humu wanakuja watu wazee kama mimi na wenzangu ---hivyo lugha za matusi hatuzipendi hata kidogo, mtawafukuza wazee wenye mambo mengi mazuri kama huyu mzee wangu.
 
Naomba kuhitimisha kwa kutoa mchango wangu kwa chief Whipp, Mhe Dr. Batilda na Mwanasheria Mkuu Mhe Mwanyika kuwa kwa haya yaliyotokea BoT na tatizo la madini. Si busara kumfanya Rais kuchukua nafasi zao bungeni. Wao walishiriki kwa nguvu kubwa kuua sauti za wabunge wa upinzani Bungeni. Kwa haya yaliyotokea wanalo la kusema? Mijadala yenye maslahi ya nchi siyo ya kufanyia usanii/mzaha Bungeni. Ni muhimu hawa wawe " focused" wamsaidie spika na Taifa. Kwa wabunge kama Gallinoma, Dr Mwakyembe,Anne Kilango, W.Shelukindo, Ibrahim Sanya, Hamad, Dr Slaa, Zito hawa ni watu very serious, tujifunze kutoka kwao tafadhali.

Huu ni ujumbe wenye maana sana kwa taifa hili , kama CCM hamtajifunza kutoka kwa hawa mtajifunza kutoka kwa nani?

Mazingaobwe hayasaidii chochote muda huu ambao kila mmoja wetu anataka kupata haki yake ya msingi.
 
We have to circulate this message to our leaders and those who are in power,

Kamataifa viongozi wake hawaoni hata aibu kuongoza watu ambao wanashindwa kupata mlo mmoja kwa siku ni aibu sana na naamini kilka kiongozi alipaswa kujisikia vibaya juu ya hali hii kuwepo nchini mwetu hapa.
 
Tunahitaji wazee kama hawa ambao wanaweka mbele maslahi ya Taifa badala ya unafiki.
 
Thanks Ndugu kasori. Wapambe wa Meghji, karamagi, mramba, batlida, nk mnao ubavu wa kumjibu bwana kasori???
 
Ona alivyosema CASTILLO wa Guatemala kuhusu wabakaji/wakwepuaji wa raslimali za nchi; namnukuu kiingereza (naomba radhi): -“One day the apolitical intellectuals of my country will be interrogated by the simplest of our people. They will be asked what they did when their nation died out slowly like a sweet fire small and alone. No one will ask them about their dress their long siestas after lunch. No one will want to know about their sterile combats with the ideas of nothing. No one will care about their higher financial Learning. They won’t be questioned on Greek mythology or regarding their self disgust when someone within them begins to die the coward’s death. They will be asked nothing about their absurd justifications born in the shadow of total lie. On that day the simple men will come.Those who have no place in the books and poems of the apolitical intellectuals but daily delivered their bread and milk, their tortillas and eggs those who mended their clothes, those who drove their cars, those who cared for their dogs and gardens and worked for them and they will ask: WHAT DID YOU DO WHEN THE POOR SUFFERED WHEN TENDERNESS AND LIFE BURNED OUT IN THEM? We, the African students and intellectuals, what shall we say when we are asked by simple MEN AND WOMEN; WHAT DID YOU DO WHEN THE POOR SUFFERED, WHEN TENDERNESS AND LIFE BURNED OUT IN THEM? JK upo?
Naomba kuhitimisha kwa kutoa mchango wangu kwa chief Whipp, Mhe Dr. Batilda na Mwanasheria Mkuu Mhe Mwanyika kuwa kwa haya yaliyotokea BoT na tatizo la madini. Si busara kumfanya Rais kuchukua nafasi zao bungeni. Wao walishiriki kwa nguvu kubwa kuua sauti za wabunge wa upinzani Bungeni. Kwa haya yaliyotokea wanalo la kusema? Mijadala yenye maslahi ya nchi siyo ya kufanyia usanii/mzaha Bungeni. Ni muhimu hawa wawe “ focused” wamsaidie spika na Taifa. Kwa wabunge kama Gallinoma, Dr Mwakyembe,Anne Kilango, W.Shelukindo, Ibrahim Sanya, Hamad, Dr Slaa, Zito hawa ni watu very serious, tujifunze kutoka kwao tafadhali. Tafadhali wana JF huu ni ujumbe na tafakuri nzito kwa umma wa watanzania. Naomba wakongwe wa JF wakishirikiana na adm wafanye juhudi za makusudi kuusambaza dunia nzima ikibidi!!!! well done mzee KASORI.
 
Professor Joseph Stiglitz, mtaalamu wa uchumi, ona aliyoyafanya kwa kuona kuwa Ikulu Marekani sera za Rais Clinton juu ya utandawazi zilikuwa zinakandamiza nchi masikini sisi tukiwemo. Kwa maneno yake anasema: “ When I was about to leave the white house for the world bank, President Clinton asked me to stay on as chairman of his council of Economic Advisors and as member of his cabinet. I declined, because I thought the task of designing policies and programs that would do something about the abject poverty which plagued the less developed world was a far more important challenge… I had seen countries where poverty was increasing rather than decreasing, I had see what that meant-not just in statistics but in real lives of people”.
Ujio wa mhe Kichaka utainufaisha Tanzania au ndiyo ukwapuaji na ubakaji wa rasilimali zetu? Najua viongozi wetu wengi ni vilaza au hawana uzalendo ! ktk nyakati hizi tunahitaji hekima, busara na watu wenye maono/mtazamo mpana kama wa mzee wetu kasori. JK mwendo mdundo tuko nyuma yako!!
 
Mzee S.H.Kasori [Heshima Kwako]... Hii post yako imenikumbusha hotuba ya mwanaharakati wa haki na uhuru wa binadamu [the late] Martin Luther King Jr.-- maarufu kama "I Have a Dream". Kama ulivyoweka bayana, wakati umefika viongozi kubadilika ki-fikra,ki-utendaji na ki-mienendo. Raia wa nchi wamechoka kupigiwa gitaa kama Mbuzi. Raia wanependa kuona yale wanasiasa wanaya-hutubia yanatokea kwa uhalisia wake na sio visingizio na sababu kedekede!

Bwana awe Nawe.
 
Mafisadi wa nchi hii wana vichwa vigumu na utahangaika kuwashauri, hata ripoti ya Mwakyembe imetoka kwa nguvu za wananchi. we acha tu.
 
We acha tu, viongozi wetu wana vichwa vigumu, Unajua hata unayoongea hawawezi kuyathamini kamwe na kama Baba wa Taifa alivyosema, mtu akila nyama ya mtu, haachi, ndivyo ilivyo kwa mafisadi, hawawezi kuacha.

Mungu wangu, na huyo jamaa ya Mamvi aliyetaka kutuletea Mvua alipinduliwa sasa nafikiri hii ni zamu yake, kudadadeki.

Mzee hawa mafisadi dawa yaho ni kama hii ya Mwakyembe, na isitoshe Mwakyembe ana nguvu ya wananchi, siyo JK, maana yeye amewachekea kwa muda mrefu.

Bye
 
"Kijinai, Mimi binafsi nisingehusika kwani sikuhusika wala kushauri, sikuagiza wala kuelekeza kwamba mambo yafanywe kama hivyo yalivyofanywa. Kwa kweli hata mimi nilifichwa, kwani niliarifiwa baada ya tume yako kuteuliwa. Hata hivyo, Kisiasa nakiri kuwa na husika, siwezi kukwepa kwasababu dhamana yangu wa uwaziri inaambatana na wajibu inao nitaka nijue yanayotendeka wizarani na pia niweze kudhibiti na kuhakikisha mwendo mwema wa jeshi la polisi........ Kwafedheha hii naomba kujiuzulu".. Mhe. LOWASA, NA WOTE MLIYOYATENDA IGENI MFANO HUU WA BABA WA DEMOKRASIA .... Thank you so much mzee Kasori.
 
Kwa barua hii ya alhaji mwinyi natumai viongozi wengi zaidi watajiuzulu!
Kasori- God bless the work of your hands...
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom