Ushauri: Jinsi ya kuwashawishi watu wajiunge na biashara ya mtandao unayofanya

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,407
Habari za leo rafiki yangu?

Watu wengi wamekuwa wanajiunga na biashara ya mtandao (network marketing) wakiwa na matumaini makubwa sana ya mafanikio. Baada ya kupewa habari za biashara hiyo, na kuoneshwa namna wanavyoweza kutengeneza kipato kikubwa, wanaondoka na hamasa kubwa.


Lakini hamasa hii inaisha ghafla kama maji ya moto yanavyopoa, pale wanapowashirikisha wengine biashara hii. Wanakataliwa na watu ambao waliwategemea wakubali, na hapo ndipo wanapoona biashara hii haifai na kuacha na nayo.

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kufanikiwa.

Kama ambavyo nimekuwa nakukumbusha mara kwa mara, changamoto siyo ukomo wa safari yetu, bali ni kichocheo cha safari yetu ya mafanikio. Ni namna ya kutukumbusha tujifunze yale ambayo hatujajua bado. Na iwapo hatutajifunza basi hatuwezi kupiga hatua. Kama ambavyo mtoto anajifunza kutembea kwa kuanza kuanguka, hivyo pia kwenye safari ya mafanikio, kuna kuanguka hapa na pale. Muhimu zaidi ni kujifunza na kuchukua hatua ili safari iendelee.

SOMA; Njia Mbili(2) Rahisi Unazoweza Kuzitumia Kutengeneza Kipato Kupitia Mtandao Wa Intaneti.

Kwenye makala yetu ya leo tutakwenda kuangalia jinsi gani unaweza kuwashawishi watu wajiunge na biashara ya mtandao unayoifanya. Kwa sababu kama nilivyosema hapo juu kwenye utangulizi, wengi wamekuwa wakikata tamaa mapema pale ambapo watu wanaowaambia wanakataa. Kabla hatujaangalia kipi cha kufanya, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili.

Mimi nimejiunga na biashara ya mtandao, changamoto Yangu ni kwamba ninavyo washirikisha watu hawaielewi fursa ya biashara wengi wanasema ni ngumu hiyo biashara na wengine wanajiunga na kuenda kutulia tu nyumbani hawafanyi biashara. Sadick L. K.

Katika kumshauri Sadick, na watu wengine wanaofanya au wanaotarajia kufanya biashara ya mtandao, nitakwenda kugusia mambo matano muhimu sana. Ukishayajua mambo haya matano, utakuwa umeelewa vizuri kuhusu biashara ya mtandao na kuweza kuifanya kwa mafanikio.

Moja; ijue vizuri biashara ya mtandao.

Biashara ya mtandao ni moja ya fursa za kibiashara ambapo bidhaa inauzwa moja kwa moja kutoka kwa anayezalisha kwenda kwa mtumiaji wa mwisho. Bidhaa haipiti kwenye mtiririko wa kawaida wa kibiashara, kama kupitia kwa wauzaji wa jumla, wauzaji wa reja reja na hatimaye kwa mteja. Inatoka inapozalishwa na moja kwa moja anaipata mteja. Mteja anapata bidhaa hii kupitia mtandao wa watumiaji wa bidhaa hiyo. Hivyo mtu mmoja anayetumia bidhaa na ikamsaidia, akiwaambia wengine na wao wakapenda kuijaribu, basi wanaponunua, yule aliyewaambia watu mpaka wakanunua, anapewa kamisheni na wanaotengeneza bidhaa hiyo.

Hivyo kadiri mtu anavyowaambia wengi na wakanunua na kutumia bidhaa hiyo, analipwa kamisheni kubwa zaidi. Kwa njia hii mtu anaweza kutengeneza mtandao mkubwa wa watumiaji wa bidhaa hiyo, na kwa pamoja kama mtandao wakanufaika sana.

Mfumo huu wa biashara ni halali kabisa, ila wapo watu wachache wanaokuja na biashara zao zisizo halali na kuzificha kwenye mfumo huu. Biashara hizo zinakuwa na muundo wa upatu, ambapo wengi wanapoteza na wachache wanafaidi. Kwenye biashara halali ya mtandao, kila mtu aliyepo kwenye mtandao ananufaika na bidhaa husika pamoja na kupata kamisheni kutokana na manunuzi yanayofanyika.

SOMA; Kuhusu Kujiunga Na Biashara Ya Mtandao(Network Marketing) Na Mambo Muhimu Ya Kuzingatia.

Biashara ya mtandao inaweza kufanywa na mtu yeyote ambaye yupo tayari kuweka juhudi kwenye biashara. Haina vikwazo vingi kama biashara za kawaida, huhitaji mtaji mkubwa, huhitaji uwe na fremu, huhitaji uwe na leseni au namba ya mlipa kodi. Hayo yote yalishafanywa, unachofanya wewe ni kutengeneza mtandao wako wa watumiaji wa bidhaa husika na kuweza kunufaika nao.

Wapo watu wengi ambao wamenufaika na mfumo huu wa biashara, ila pia wapo wengi ambao wameshindwa kunufaika na kukata tamaa. Wapo ambao wakisikia tu biashara hii, au baadhi ya majina ya kampuni zinazofanya biashara hii, husema ni utapeli au uongo. Lakini ukiangalia kwa undani, biashara ipo sahihi, ila wapo ambao wanaongopewa.

Mbili; usiwadanganye watu.

Moja ya makosa makubwa ambayo watu wanaofanya biashara ya mtandao wanayafanya ni kuwadanganya watu kuhusu biashara hii, hasa kwenye kipato. Watu wengi wanaohudhuria semina zinazohusu biashara ya mtandao, huoneshwa chati ya fedha watakazotengeneza kupitia biashara hii. Na wengi huwa na aina ya mafunzo yanayofanana. Kwamba ukiingiza watu watano, unapata laki tano, hawa watano nao kila mmoja akileta watano, unapata milioni tano, wale 25 nao kila mmoja akileta watu watano, unapata milioni 50, hesabu zinaendelea hivyo mpaka mtu anaona utajiri si ndio huu hapa! Mtu anatoka akiwa na hamasa kubwa ya kuhakikisha anaingiza watu wengi zaidi, kweli anawaingiza, lakini hayo mamilioni hayaoni.

Ni kweli hizo hesabu watu wanapewa ni sahihi, lakini hawaelezwi ukweli kuhusu hesabu hizo. Na ukweli wenyewe ni kwamba siyo tu kuwaingiza watu, bali watu hao wanunue bidhaa ya kampuni husika, na wale wanaowaingiza pia nao wanunue. Kampuni inakulipa kamisheni kutokana na faida inayotengeneza, na faida inatokea pale watu wanaponunua bidhaa. Hakuna fedha za bure.

Zipo kampuni ambazo kwa kumwezesha tu mtu kujiunga, kuna kamisheni unapewa, lakini hii ni ndogo, kamisheni kubwa ni ile inayotokana na watu kununua.

Watu pia wamekuwa wanawadanganya watu kwamba hii ni biashara rahisi, unayoweza kuifanya kwa masaa machache kwa siku na wakapata mamilioni. Utasikia nafanya biashara masaa mawili tu kwa siku lakini napata mamilioni. Kwa kifupi ni uongo. Siyo biashara rahisi, unahitaji kuweka juhudi, unahitaji kutokukata tamaa na unahitaji muda mrefu kuliko unavyoambiwa.

Uongo mwingine mkubwa unaofanyika kwenye biashara hii ni watu kujinadi kutengeneza kipato kikubwa ambacho siyo kweli. Wapo watu wanajiunga, hawatengenezi kipato ila wana matarajio hayo. Ili kuwavutia watu kujiunga, wanawaambia kwamba tayari wao wanatengeneza kipato kikubwa. Lakini ukiangalia wanayosema na uhalisia, haviendani, watu wanapogundua hilo, wanaona hiyo ni biashara ya uongo na utapeli tu.

SOMA; Business @ The Speed Of Thought. (Mbinu Za Kufanya Biashara Kwenye Zama Hizi Za Taarifa).

Hivyo wewe binafsi, unapowaambia watu kuhusu biashara hii, usiwadanganye, waambie ukweli kama ulivyo, na waoneshe njia ya mafanikio ni ipi, kisha wakaribishe msafiri pamoja.

Tatu; siyo biashara ya kila mtu.

Watu wakishapata hamasa ya biashara hii, kwa kuoneshwa picha ya mamilioni na safari za kifahari, wanatoka wakiwa na moto kweli na wanataka kumsimamisha kila mtu barabarani na kumweleza kuhusu biashara hii, wakitegemea watajiunga haraka na kuanza kutengeneza mamilioni. Mambo hayaendi hivyo, hii siyo biashara ya kila mtu na hivyo kukazana kumwambia kila mtu na wakati mwingine kulazimisha wajiunge, wanaweza kufanya hivyo lakini usipate zile faidia ulizokuwa unategemea.

Kila kampuni ina bidhaa zake, kuna ambazo bidhaa ni za urembo, nyingine virutubisho, na vitu vingine muhimu. Sasa unapojiunga na kampuni fulani, jua vizuri bidhaa zake na zinawafaa watu wa aina gani. Kisha rudi kwenye maisha yako, na angalia kwa watu unaowafahamu, ni kina nani ambao wanaweza kusaidiwa na bidhaa za kampuni husika. Hao sasa ndiyo unaweza kukaa nao chini, na kuwaeleza manufaa watakayopata kwa kutumia bidhaa hiyo. Kwa kufanya hivi, mtu anaweza kuanza kwa utumiaji, halafu ikimsaidia anaweza kuwaambia wengi zaidi, hivyo akanufaika kifedha pia.

Usikimbilie kumwambia kila mtu kuhusu biashara hii, bali chagua watu ambao itawasaidia na ukiwa na watu wa aina hii mtaweza kutengeneza mtandao mzuri.

Nne; ni mchezo wa namna.

Biashara ya mtandao ni mchezo wa namba. Hata baada ya kuwachagua watu wanaoweza kunufaika na biashara hii na kuwaambia, bado siyo wote watakaojiunga na biashara hii. Hivyo unapaswa kuelewa hili ili usikate tamaa. Ukiongea na watu kumi na kuwaeleza vizuri kabisa kuhusu biashara hii, mmoja atakuwa tayari kujiunga na biashara hii. Na kama una bahati nzuri, unaweza kupata mpaka watatu.

Tuanze na mmoja kati ya kumi, sasa angalia ni watu wangapi unahitaji wajiunge na biashara yako, kama unahitaji watu 10, basi jiandae kuongea na watu zaidi ya 100, ukiwaeleza vizuri kuhusu biashara hii, kuwafuatilia na kujibu changamoto zao. Hao kumi watakaojiunga nao pia wasaidie kwenye kupata watu zaidi. Kadiri unavyowaambia wengi kuhusu biashara hii, ndivyo unavyoweza kupata watakaojiunga.

Usitegemee kila utakayemwambia akimbilie kujiunga na biashara hii, na pia usiache kuwaambia wengine kwa sababu wote uliowaambia wamekataa. Ni mchezo wa namba, endelea kuwapa wengi zaidi taarifa, na utawafikia wale wanaofaa.

Pia kuwa tayari kuambiwa hapana na kukatishwa tamaa, ni sehemu ya mchezo wa namba.

Tano; lengo ni kufanya biashara, siyo kuingiza watu.

Kama nilivyoeleza kwenye maana ya biashara hii ya mtandao, lengo siyo kuingiza watu, kama ambavyo wengi wamekuwa wanakazana kufanya. Lengo ni kufanya biashara, watu wanunue bidhaa, kampuni ipate faida, halafu itoe kamisheni kwa wale waliopo kwenye mtandao wa kampuni hiyo. Hivyo basi, kazi yako kwenye biashara ya mtandao, haiishii pale mtu anapojiunga, bali hapo ndipo kazi inapoanza. Kwa sababu kwa kila mtu anayeingia kupitia wewe, unahitaji kumhamasisha anunue bidhaa, na pia kumsaidia aweze kupata watu wa kujiunga kwenye mtandao wake pia. Hivi ndivyo faida inavyopatikana kwenye biashara hii.

Wengi wamekuwa wanakazana kuingiza watu na baadaye wanaachana nao, wakifikiri kazi imeisha. Kila unayemwingiza ni kama mtoto wako, unahitaji kumlea, unahitaji kumfundisha biashara hiyo aelewe kwa undani. Wakati mwingine unaweza kumwambia awakusanye watu anaotaka kuwafundisha kuhusu biashara hiyo, na wewe ukaenda kusaidiana naye katika kufundisha. Ni kazi hasa, ndiyo maana nimekuambia anayekuambia anafanya masaa mawili tu kwa siku anakudanganya.

Haya ni mambo matano muhimu ambayo kwa kuyafanyia kazi, utakuza biashara yako ya mtandao, kwa kupata watu wazuri wanaofanya biashara na kisha kupata faida kubwa kwenye kamisheni.

Kama unafanya biashara ya mtandao, na ungependa kutumia vizuri mtandao wa intaneti kupata watu wa kujiunga na biashara yako, tuwasiliane kwa njia ya wasap namba 0717 396 253. Ninao mpango mzuri kwako wa kukuwezesha kutumia mtandao wa intaneti kukuza zaidi biashara yako ya mtandao.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.
 
Shkamoo Kocha, narudi kwnye biashara hii baada ya kusoma huu uzi, ntajipanga na kuja na mpango kazi ambao hakika utanisaidia sana
 
Back
Top Bottom