Urais rahisi...

Nov 11, 2007
10
74
URAIS RAHISI!
1.1 Kuna mambo yanisuta, njia ya kukwepa sina,
1.2 Nguvuze zinanivuta, niwanene hawa wana,
1.3 Cheo wanokitafuta, japo huwezo hawana,
1.4 Nusura wakikipata, mjuwe nchi hatuna,
1.5 Urais si kupeta, kazi rahisi hauna.

2.1 Chonde chonde tutajuta, tukidhihaki amana,
2.2 Nchi akiikamata, kiumbe asiye maana,
2.3 Mali zote atachota, apelekee 'mabwana',
2.4 Si gesi wala mafuta, faida hatutaona,
2.5 Urais si kubweta, kazi rahisi hauna.

3.1 Apitae akibwata, watu wengi kawabana,
3.2 Mapesa aliyochota, agawa rushwa bayana,
3.3 Kuzimu hakuna nyota, anayagawa mchana,
3.4 Akute la kumkuta, hapa Rais hatuna,
3.5 Urais si kubwata, kazi rahisi hauna.

4.1 Huyu anomeremeta, tumchunguze kwa kina,
4.2 Mshaharawe kitita, wakidhi mke na wana,
4.3 Vipi awe kaukata, ana nyumba kila 'kona'?
4.4 Na hata tukimsuta, hajuti anajivuna,
4.5 Urais si kupeta, kazi rahisi hauna.

5.1 Mdomo walia mbwata, anaunadi ujana,
5.2 Atarukaje ukuta, kamwe uzoefu hana,
5.3 Mbio zake zitagota, wapambe wakimkana,
5.4 Hapo ndipo atajuta, mdomowe kuushona,
5.5 Urais si kubweta, kazi rahisi hauna.

6.1 Katu haimili vita, jaribuni kumbana,
6.2 Utaona akitweta, ahaha kama mtwana,
6.3 Ana tafuta tafuta, mnyonge wa kumchuna,
6.4 Atamaliza mafuta, na mambo hayatafana,
6.5 Urais si kubwata, kazi rahisi hauna.

7.1 Tumshukue matata, tuwe wazi kumkana,
7.2 Ubaguzi auleta, hanayo nyingine zana,
7.3 Udini ndio karata, hana nyingine namna,
7.4 Tumkane katakata, kama twataka kupona,
7.5 Urais si kupeta, kazi rahisi hauna.

8.1 Huyu naye anaota, tunamuelewa sana,
8.2 Apitapo ananata, hana sifa moja chana,
8.3 Visasi avitafuta, akitangaza twaguna,
8.4 Atatuendesha puta, tubaki twatafutana,
8.5 Urais si kubweta, kazi rahisi hauna.

9.1 Urais kuupata, ukabila sio dhana,
9.2 Jambo hilo litagota, sio sifa ya kufana,
9.3 Muwe wengi kama nyota, ushindi hamtavuna,
9.4 Mtabakia kusota, kujibagua ni laana,
9.5 Urais si kubwata, kazi rahisi hauna.

10.1 Urais unapita, wajibu kupokezana,
10.2 Kuutaka sio vita, vya ndugu kuchafuana,
10.3 Sera zisizo utata, nadi bila kutukana,
10.4 Mwenye sifa atapita, kwa sifa si kung'ang'ana,
10.5 Urais si kupeta, kazi rahisi hauna.

Eur Ing. Omari Rashid Nundu
Dodoma
12 Novemba 2014
 
Huyu ni Omar Nundu yule aliyewahi kuwa Waziri wa Miundo Mbinu ?
 
Ahsante.... Mhe Eng. O.R.Nundu ujumbe mzuri nimependa kwenye mstari 2.1-3.5 tafakuru ya kina yahitajika kuyatilia maanani maoni yako.
zidi kusambaza tenzi hizi hasa kwa waheshimiwa wenzako hata kwa sms na e-mail
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom