Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Tumeshakika adabu, mwanakwetu tusamehe,
Hizi si bure adhabu, kwa maamuma na shehe,
Ndururu kupata tabu, hali zetu hohehahe,
Ulipo pashika pashike, lakini usipafunge.
Kiumbe umakinike, panapo vuja paunge,
Vizuri upazindike, lipate kuiva dunge,
Riziki siifutike, haramu sawa uchunge,
Ulipo pashika pashike, lakini usipafunge.
Unga kupata kibaba, mtihani hivi sasa,
Sukari 'mekuwa haba, aghari kama kipusa,
Ili mradi kushiba, vyakula tunatokosa,
Ulipo pashika pashike, lakini usipafunge.
Ukali wote wa simba, kumbe naye anazaa,
Ati akitaka mimba, mchezo hato kataa,
Mikwara uliyochimba, haijashusha bidhaa.
Ulipo pashika pashike, lakini usipafunge.
Mikutano wakataza, ikiwa ya kisiasa,
Jirani wamcharaza, mwandani wamtomasa,
Mbaguzi hana jaza, mwenzangu ninakuasa,
Ulipo pashika pashike, lakini usipafunge.
Sitaki mie semina, kuielewa sinema,
Milioni saba sina, hapa nakoma kusema,
Sina baba wala nina, wa furusi kuzitema,
Ulipo pashika pashike, lakini usipafunge.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
Call/whatspp 0622845394 Morogoro.