Ulimi Rangi Saba

Robert Heriel Mtibeli

Platinum Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
40,274
Reaction score
93,304
ULIMI RANGI SABA.

Na, Robert Heriel

Ukumbi wote ulikaa kimya. Giza totoro lililokuwa mule ndani lilitosha kuvuta hisia za mtu mwoga. Wote walikuwa wamesujudu wakiwa na majoho meusi yenye makofia makubwa yaliyowafunika usoni.Mbele ya ukumbi kulikuwa na jukwaa kubwa lililokuwa linalofuka moshi uliokuwa ukitoka kwenye chungu cheusi tii. Moshi na lile giza lilileta taswira ya kusisimua mno.

Sauti ya paka ilisikika ukumbini. Ilikuwa ni kama paka huyo alikuwa akitembea ingawa alikuwa haonekani kutokana na giza. Bado wale watu walikuwa wamesujudu sakafuni kwa utulivu na heshima zote. Kitendo cha sauti ya paka mmoja kulia kilivungulia sauti za paka wengine ambao hata hivyo walikuwa hawaonekani. Eneo lote lilizizima sauti mbalimbali za paka hao waliolia kwa mfanano wa sauti za watoto waliapo.

Nje ya jengo upepo ulivuma huku anga likitawaliwa na vimulimuli. Hii iliashiria kuna jambo linaenda kutokea na jambo hilo ni hatari na lakutisha. Punde upepo ulikoma ukiacha vimulimuli vikiendelea kumulika angani hali iliyofanya ndani ya ukumbi kumulikwa mulikwa kama vile mtu apigaye picha mahali penye giza.Sauti za Paka nazo zilinyamaza kukawa na ukimwa wenye kuleta mashaka.

Mara kengele ililia, kengele iliyotoa sauti ambayo hata kichaa angeelewa kuwa inaashiria jambo baya. Baada ya sauti ya kengele iliyodumu kwa takribani dakika moja kumalizika punde mishumaa iliyomo mule ndani ilianza kuwaka mmoja mmoja bila kuwashwa na mtu. Hapo hapo ngoma ilisikika na saut ya vicheko ikafuatia.

Sasa jambo lililokuwa linatazamiwa lilikuwa limewasili. Mbele alisimama mtu mrefu mwenye ulimi mrefu wenye rangi saba. Kwa kawaida ulimi wa binadamu unarangi nyekundu lakini mtu huyu aliyetisha alikuwa na ulimi mrefu wenye rangi saba.
Yule mtu akasema:
"Sauti kwa sauti, ala kwa ala, maneno kwa maneno. Mimi ndiye mwenye kutawala. Nawapa shari wenye kutaka shari. Ni nani mwenye nguvu ya ulimi isipokuwa mimi ULIMI RANGI SABA?"(Anapaza sauti kwa nguvu)
Wanitukuze! Wanihimidi!"
Kisha wale waliovalia majoho waliitikia:
"Twakutukuza! Twakutukuza! Twakuhimidi"

Jengo zima lilitetemeka kwa sauti hizo na popo wakaruka ruka mule ndani wakishangilia.
"Mimi Rangi saba natawala majumbani. Huko ndoani waumen na wake wanisujudu. Naharibu nyumba nikitaka kwa sauti ya ulimi wangu. Matusi na masimango hunifanya nizidi kustawi huko chumbani. Ulimi Rangi saba ukicheza nakuharibu"
Lilibwatuka huku ulimi wake ukilamba lamba pua na masikio yake.
"Twakutukuza! Twakuhimidi! Twakusifu"
Wenye majoho waliongea tena kwa pamoja wakionyesha heshima.

"Mimi ninazungukwa na meno thelesini na mbili upande upande. Chini maji maji kama mito ya Kongo. Naharibu taifa kwa sumu ya maneno. Naleta husda na fitina siasani. Viongozi wananitumia, Hekaluni nimeweka kiti changu. Huko nasujudiwa na kafara natolewa"
Mara hii alizungumza huku ulimi wake akilamba vidole vya mikononi.
"Utawala ni wako Daima twakuhimidi"
Wenye majoho walijibu.

"Mimi naleta vita, ubaguzi na unyanyasaji. Mataifa nayapiganisha. Damu nazo kumwagika. Hakuna kinishindacho. Dunia yote yanijua"
Hapa liliongea huku ulimi ukiwa umeshika panga linalong'aa kwa ukali.
"Tuhurumie Rangi Saba"
Walijibu huku wakiogopa upanga ulioshikwa na ulimi wa yule mtu.

Mbele ya jukwaa ukutani kulisomeka maandishi haya:
"Ulimi ni nyama peke iliyondani iwezayo kutoka nje. Nyama laini iliyozingirwa na meno na kulala chini ya maji ambayo ni mate. Ulimi huweza kuharibu na kubomoa. Kujenga na kuimarisha.
Tukiutawala ulimi wa hao tutatawala akili zao"
"Nendeni! Nendeni huko kwao. Huko waishipo. Huko wakaapo na huko walalapo. Pia muende huko wasemapo. Nawatuma hivi leo nendeni mkashike ndimi zao. Nimewapa heshima ile niliyokuwa nayo mimi tangu hapo awali.
Shikeni makoo yao wasipatane. Kwani kushika kwenu ndimi zao ndipo watakapo farakana. Nao hawatakuwa kitu kimoja kama sisi tulivyo wamoja. Wapeni kusikia kuwili kuwili kulingana na masikio yao. Wasema wasiyoyafikiri kwa ndimi zao hata watakapo hitilafiana na kuchafuana kwa hila
Nami buchani wakinila waone ulaini na utamu wangu. Wajilambe mpaka mikono kwa utamu wa hila. Watabiri na kusemeana uongo. Nami ni nyama iliyondani itokayo nje. Hivyo nao watoa vya ndani ya nyumba zao wapeleke nje. Kusudi mifarakano isiishe hata watakapo umia.
Nasi tukijua yakuwa ulimi ni kiungo muhimu nacho twakitukuza. Tukihakikisha tunatawala midomoni mwao daima dawamu."
Yule mtu alimaliza kuzungumza na kutoweka baada ya kuwaachia kazi wale watu waliovalia majoho meusi yenye makofia makubwa.
Kengele inalia na mishumaa inazima mwisho kunakuwa giza kuu.

 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…