Sinoni
JF-Expert Member
- May 16, 2011
- 6,191
- 10,672
Rais Park Geun-hye ni rais wa kwanza wa Korea Kusini kuizuru Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika ziara hiyo rais huyo wa kike anaongoza ujumbe wa watu zaidi ya 200 wanaojishughulisha na masuala ya kiuchumi kutoka mashirika tofauti ya serikali na ya watu binafsi.
Korea Kusini ilikuwa ikiendesha vizuri shughuli zake za kiuchumi nchini hapa kabla ya taifa hili kuwekewa vikwazo vya kidhalimu. Hatua ya Wairan kuridhia bidhaa za Korea Kusini imechangia msukumo wa kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili hizi hususan baada ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia.
Kwa mujibu wa Amir Hossein Zamani-Nia, Naibu Waziri wa Mafuta anayeshughulikia masuala ya kimataifa na biashara, katika kipindi cha safari ya siku tatu ya Rais Park Geun-hye nchini hapa, mikataba minne ya ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi baina ya Tehran na Seoul itatiwa saini.
Mikakati ya muda mrefu ya ushirikiano katika sekta ya mafuta na gesi baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Korea Kusini itaandikwa, chini ya usimamizi wa marais wa nchi mbili mjini Tehran.
Si vibaya kuashiria kuwa, Korea Kusini ni moja ya wanunuzi wakubwa wa mafuta ya Iran. Uingizaji wa mafuta ya Iran nchini Korea Kusini hadi kufikia mwezi Machi mwaka huu, uliongezeka kwa asilimia 18 ikilinganishwa na muda kama huo mwaka uliopita wa 2015.
Viongozi wa Seoul wametangaza kuwa, wameazimia kuongeza kiwango cha ununuzi wa mafuta ghafi kutoka Iran mwaka huu ili waweze kujidhaminia mahitaji yao ya nishati hiyo muhimu. Kufikiwa makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) hapo tarehe 17 Januari mwaka huu, kumeongeza kiwango cha ununuzi wa mafuta ya Iran na sasa Tehran iko katika mchakato wa kutafuta soko la bidhaa hiyo hasa baada ya kuondolewa vikwazo dhidi yake.
Ukweli ni kwamba masoko ya zamani ya mafuta ya Iran katika eneo la bara la Asia hususan mashariki mwa bara hilo, bado yanakubali sana mafuta ghafi ya nchi hii.
Ushirikiano wa sekta ya mafuta kati ya Iran na Korea Kusini utaboresha pia uchumi wa nchi mbili sanjari na kuongeza kiwango cha mabadilishano yao ya kibiashara. Kiwango cha mabadilishano ya bidhaa nyingine mbali na mafuta cha nchi hizi kilifikia dola bilioni 4 na milioni 100 mwaka 2013.
Kwa hakika kuondolewa vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kupatikana tena wawekezaji wa Korea nchini hapa na kadhalika kupanuka ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara wa nchi mbili, kumeandaa fursa nzuri ya kuongezwa kiwango cha mabadilishano ya kibiahara baina ya Tehran na Seoul.
Katika uwanja huo, Kim Sung-ho, balozi wa Korea Kusini mjini Tehran amesema kuwa, zaidi ya mikataba 30 ya makubaliano baina ya serikali mbili inatazamiwa kutiwa saini chini ya usimamizi wa marais wa nchi mbili mjini Tehran.
Kwa mujibu wa Kim Sung-ho mikataba hiyo inajumuisha sekta za mafuta na gesi, miundombinu, ubaharia, afya na matibabu na baadhi ya miradi mingine mahimu yakiwemo pia masuala ya utamaduni. Kwa hakika safari ya kihistoria ya Rais Park Geun-hye nchini Iran, ni nukta muhimu katika uhusiano wa nchi mbili, kama ambavyo pia inafungua ukurasa mpya katika mahusiano ya jadi kati ya mataifa haya muhimu ya Asia.
Nafasi muhimu ya kiuchumi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na iliyochanganyika na teknolojia ya Korea Kusini, ni nukta nyingine itakayostawisha zaidi mahusiano ya nchi mbili, na viongozi wa Seoul wanataraji kuona malengo muhimu ya safari ya Rais Park Geun-hye nchini hapa yakifikiwa.
Kuongezeka kiwango cha ununuzi wa mafuta ghafi ya Iran, uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya kiteknolojia, uwekezaji katika miradi tofauti ya gesi na kadhalika ushirikiano katika sekta ya petrokemikali, ni mambo mengine muhimu yanayotajwa kuwa yataboresha uhusiano wa Iran na Korea Kusini.
Kufanyika kongamano la kuchunguza njia za kustawisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya Tehran na Seoul baada ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia, katika safari ya Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini nchini Iran, ni ishara ya kuwepo azma thabiti ya pande mbili kwa ajili ya kupanua uhusiano wao wa kiuchumi na kibiashara na kuufikisha kwenye kiwango kinachotakiwa.