Ukishangaa ya Balotelli, Utastaajabu ya Kiemba!

Ukishangaa ya Balotelli, Utastaajabu ya Kiemba!

Hussein Massanza

JF-Expert Member
Joined
Dec 26, 2012
Posts
1,016
Reaction score
2,195
George Oppong Weah ndiye mwanasoka pekee barani Afrika ambaye ameshatwaa Tuzo ya Fifa Mchezaji Bora wa Dunia ambayo siku hizi inatambulika kama Ballon d'Or. Pamoja na mafanikio hayo, hakuwahi kufanya maajabu yoyote akiwa na Timu ya Taifa ya Liberia.

Mwaka 1995 ambao Weah alishinda Tuzo ya Fifa Mchezaji Bora wa Dunia, alitunukiwa pia Tuzo ya Uefa Mchezaji Bora wa Ulaya. Vilevile ameshinda Tuzo ya Caf Mchezaji Bora wa Afrika mara tatu, mwaka 1989, 1994 na 1995. Kwa nini hakuifanya Liberia itishe kwenye ulimwengu wa soka?

Haishii hapo, Weah alichaguliwa na jopo la waandishi wa habari za michezo duniani kote kuwa Mchezaji Bora wa Afrika wa Karne ya 20. Tuzo kama hiyo alitunukiwa Pele (wa Brazil) kwa upande wa Bara la Amerika Kusini, wakati Ulaya, ilikwenda kwa Johan Cruyff.

Mafanikio yake yote akiwa na Klabu ya Tonnerre Yaoundé ya Cameroon ambayo yalimvutia Arsene Wenger wakati huo kisha kumsajili kwenye Klabu ya Monaco ya Ufaransa ambako alitikisa kabla ya kunyakuliwa na Paris Saint-Germain (PSG), yanabaki kuwa binafsi na si kwa taifa lake.

Miaka mitatu aliyocheza PSG ilikuwa ya neema sana lakini haifii rekodi aliyoweka AC Milan ambako alicheza kwa miaka mitano (1995-2000). Wakati soka lake linaelekea ukingoni, alicheza Chelsea kwa mkopo mwaka 2000 ambao alisajiliwa Manchester City. Msimu wa wa 2000-2001 alinunuliwa na Marseille kabla ya kutundika daruga Falme za Kiarabu akiwa na Klabu ya Al-Jazira, Abu Dhabi kati ya 2001-2003.

Endapo utakatiza mitaa mbalimbali ya majiji makubwa ya Afrika na kuuliza swali hili kwamba ni kwa nini Weah hakuwika akiwa na Timu ya Taifa ya Liberia, utakutana na majibu mengi mepesi ambayo yamezoeleka pindi wanapozungumzwa mastaa wa soka wa Afrika wanaowika klabu kubwa Ulaya.

MAJIBU RAHISI YA MASHABIKI WA SOKA AFRIKA

Kwa kawaida, mashabiki wa soka Afrika wanapoona mataifa yao hayafanyi vizuri, kitu ambacho hukimbilia kukisema ni lawama kwa wachezaji wanaosakata kabumbu Ulaya kwamba hawajitumi kama ambavyo hufanya kwenye klabu zao.

"Mastaa wa soka Afrika wanajituma sana kwenye klabu zao Ulaya kwa sababu wanalipwa vizuri, wakiwa na timu zao za taifa wanategea kwa vile wanaogopa kuumia. Wakiumia ajira zao zinakuwa shakani katika klabu zao," hivyo ndivyo husema.

Mashabiki wa soka na hata wachambuzi wengi Afrika huwa hawaangalii na kutoa tathmini za kitaalamu. Hujikita zaidi kwenye shutuma na lawama. Hata Zinedine Zidane angechezea Timu ya Taifa ya Algeria, angelaumiwa hivyohivyo.

Lawama za aina hiyo zilishavuka Afrika mpaka Amerika Kusini, zikatua Argentina na kumwandama Lionel Messi kwamba haisaidii timu yake ya taifa. Eti akiwa na Albicelestes hajitumi kama anavyokuwa kwenye klabu yake ya Barcelona.

Hivyo ndivyo baadhi ya watu walithubutu kumsema Weah, vivyo hivyo mastaa wa sasa Afrika kama Yaya Toure, Didier Drogba, Mikel Obi na wengine wengi wanavyoshutumiwa. Ni lawama ambazo hazijafanyiwa tathmini. Ni maneno tu ya kuvunjana moyo.

UKWELI NI UPI?

Soka linachezwa kwa ‘kombinesheni', ndiyo maana inaitwa timu. Haingii mtu mmojammoja na kucheza kivyake halafu utarajie ushindi. Lazima wachezaji wajumuike pamoja na kucheza kitimu kulingana na mfumo unaotokana na mafundisho au maagizo ya mwalimu (kocha).

Soka linachezwa kwa ‘teamwork'. Ili timu ifanye vizuri inabidi kuwepo na wachezaji wanaoelewana kiuchezaji, maelewano ambayo hutengeneza muunganiko bora (good chemistry). Hapo ndipo utaona matokeo mazuri ya ndani ya uwanja.

Timu inaweza kuwa na wachezaji wachache wazuri sana na wengi wenye viwango vya kati (average), hivyo kutengeneza timu nzuri kutokana na jinsi ambavyo kila mchezaji anavyosoma kwa haraka na kuelewa jinsi ya kucheza na mwenzake.

Timu ikiwa na wachezaji wachache wenye viwango vikubwa na kati halafu wengi wakawa hohehahe uwanjani, huwezi kupata timu nzuri. Wakijitahidi sana hiyo timu itacheza kwa kiwango cha wastani. Yaani wakali, kati na wengi wenye viwango duni, watavutana kwenda kiwango cha kati.

Tena afadhali kufikia kati, wakati mwingine mvutano huo husababisha timu kuwa dhaifu kabisa, matokeo yake hata wale wakali wasioneshe uwezo wao. Timu bora huundwa na wachezaji ambao viwango vyao vinashabihiana au kukaribiana.

Kabla ya kumlaumu Messi kuwa hana mchango timu yake ya taifa, jiulize kwamba kule anacheza na akina nani? Ni kweli kwamba Messi akiwa Barcelona ni ‘nyoka mwenye sumu kali', huko nako anaoshirikiana nao uwanjani ni akina nani?

Kule Barcelona, Messi anakutana na akina Iniesta, Xavi, Neymar na wengine wengi ambao ni daraja la kwanza, je, unataka asioneshe kiwango? Ni rahisi mchezaji kuonekana bora anapokuwa anacheza katika timu bora, yaani yenye muungano wa wachezaji bora.

Utaona kwamba japo mashindano yalimchosha sana kwa sababu ya udogo wa kikosi, angalau Fainali za Kombe la Dunia mwaka huu, Messi aliweza kuifikisha Argentina fainali. Peke yake asingeweza, walikuwepo wengine daraja la kwanza duniani kama Angel Di María, Javier Mascherano, Sergio Agüero ‘Kun' na wengine waliotengeneza timu yenye afadhali.

Kwa tafsiri hiyo ni kuwa hata Weah kama asingechezea klabu bora wakati huo, AC Milan asingepata nafasi ya kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Dunia. Alionekana straika hatari kwa wakati wake kwa sababu alishirikiana uwanjani na wachezaji bora.

Kama Wenger asingemuona Weah na kumpeleka Monaco, angeendelea kucheza soka la Afrika. Na kwa mantiki hiyo, angekuwa anashirikiana na wachezaji wa kiwango kidogo. Ni vigumu sana kumtambua mchezaji bora anapocheza na wacheza dhaifu.

Kadhalika Weah, ubora wake kiuchezaji uliongezeka siku baada ya siku tangu alipotua Monaco kwa sababu alicheza timu moja na wachezaji wazuri na kwenye ligi alikutana na wakali ambao walimpa changamoto iliyomfanya aongeze juhudi zaidi na kuonesha uwezo wote aliokuwa nao, mwisho akawa Mchezaji Bora wa Dunia.

SASA NAJIBU KWA NINI HAKUISAIDIA LIBERIA

Pale Liberia Weah hakukutana na wachezaji wa kiwango chake. Ilikuwa ni sawasawa na Bill Gates kumuweka meza moja na Matonya (marehemu), yule ombaomba wa Dodoma aliyetikisa Dar miaka ya nyuma. Ukweli ni kwamba kimawazo wasingeshabihiana, isipokuwa kila mmoja angemshangaa mwenzake kwa namna yake.

Weah alijitolea sana kwa ajili ya timu yake ya taifa, lakini nchi hiyo ilikosa wachezaji ambao wanaweza kuendana na kasi yake. Matokeo yake alikuwa anatumia nguvu nyingi uwanjani lakini ikawa kazi bure. Hakuwahi kuiwezesha Liberia kucheza Kombe la Dunia, alifanikisha kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika mara mbili na zote walitolewa kwenye makundi.

Kwa kifupi ni ndoto za mchana kutegemea Weah angefanya mambo makubwa akiwa na Liberia. Alihitaji wakali kama wale aliokutana nao Ulaya ndipo aoneshe makali yake. Kwa kombinesheni ile ya Liberia, hata angejitahidi vipi asingeshinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa Dunia.

Hayo ndiyo mateso aliyonayo Cristiano Ronaldo na Ureno yake, hapati wachezaji wa aina yake. Ndiyo maana Messi analaumiwa kwenye timu yake ya Mawingu Meupe na Bluu. Neymar aliteseka sana na Brazil yake katika Kombe la Dunia 2014. Kadhalika akina Toure, Drogba, Obi na wengine wengi watasemwa sana.

SHANGAA YA BALOTELLI SASA

Kocha wa Liverpool, Brendan Rodgers alipomsajili Mario Balotelli, alisukumwa na vitu viwili, kwanza ni kwa sababu alikuwa ametoka kumuuza Luis Suárez kwenda Barcelona, hivyo alitaka kutuliza presha kama siyo mizuka ya wazee wa You'll Never Walk Alone.

Pili ni baada ya kusikia kwamba AC Milan wanamuuza Balotelli. Ni mambo hayo tu mawili! Hakuangalia aina ya uchezaji wa Liverpool na staili ya Balotelli. Rodgers hakuzingatia aina ya wachezaji alionao kama wanaweza kuendana na Balotelli.

Tazama aina ya wachezaji ambao Balotelli aling'ara nao akiwa Inter (Internazionale) Milan na Manchester City na baadaye AC Milan. Kote huko alifanya vizuri ila aliponzwa na utovu wa nidhamu. Liverpool wanataka Balotelli afunge, kwa mpira upi? Kwa chemistry ipi?

Mbaya zaidi Liverpool wanategemea Balotelli acheze kama Suarez, huo ni utani. Balotelli ni mfungaji mzuri lakini lazima apate wachezaji wa aina yake ambao wanaweza kumlisha. Anahitaji wachezaji wakubwa, siyo utitiri wa ‘wavulana' kama waliopo Liverpool kwa sasa.

Ambacho Liverpool wanapaswa kufanya, ama wanunue wachezaji wengine daraja la kwanza kama Balotelli kisha wabadili mfumo au wamuuze na kutafuta mwingine (wengine) kuziba pengo aliloacha Suarez. Kwa kutegemea maneno yatasaidia, hatafunga ng'o, zaidi watamjaza ‘stress' mwisho aanze kutukana kama kawaida yake.

STAAJABU YA AMRI KIEMBA

Hivi karibuni uongozi wa Simba uliwasimamisha kwa muda usiojulikana wachezaji Amri Kiemba, Haruna Chanongo na Shaban Kisiga kwa madai kwamba eti ndiyo sababu ya sare mfululizo ambazo timu hiyo imekuwa ikipata tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Hata hivyo, Jumamosi iliyopita Simba ilipata sare ya sita wakati wachezaji hao hawakuwepo. Mchawi kaondolewa na bado timu haifanyi vizuri. Uongozi wa Simba unashindwa kugundua tatizo la msingi na kulifanyia kazi, unakimbilia kushikana uchawi na wachezaji.

Hivi, uongozi wa Simba umeshafuatilia na kugundua kuwa wachezaji wao hawana stamina ya kuwatosheleza kumudu dakika 90? Hili ni tatizo kubwa, na ndiyo maana mara zote huwa wanatangulia kushinda halafu wanasawazishiwa dakika za mwishoni.

Katika mechi hizo sita, nimefanikiwa kuangalia mbili tu. Zote nimejionea jinsi ambavyo Simba huanza kwa nguvu sana lakini kipindi cha pili kuanzia dakika ya 70 na kuendelea, huanza kujigongagonga, kuonesha kuwa tayari wameshachoka.

Tatizo lingine ni utitiri wa wavulana ambao kiukweli wana vipaji lakini hawajafunzwa inavyotakiwa. Badala ya kucheza mpira wenye lengo la kutafuta ushindi, wao wanachezacheza tu! Wanapoteza mipira bila sababu, wanajigongagonga sana!

Hapohapo nikamsikia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zachariah Hans Poppe akisema kuwa Kiemba anacheza vizuri sana akiwa Timu ya Taifa kuliko anavyokuwa anaitumikia Simba. Niliposikia hivyo nilicheka, nikakumbuka yaleyale ya Weah kuisaidia Liberia.

Kiemba ni mchezaji mkubwa, ana sifa zote kama kiungo. Anakaba, anajua kukaa na mpira, ni mtaalamu wa kutoa pasi, anaelewa wajibu wake wa kuichezesha timu, vilevile anafunga. Ili uone raha ya Kiemba ni lazima akutane na wanaojua.

Akiwa Taifa Stars anakutana na akina Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto na wengine kibao wakali. Je, kwa kombinesheni hiyo, unataka aoneshe kiwango kidogo na wakati anakutana na wenzake wanaojua?

Simba wanapaswa kutafuta mchawi badala ya kuzungumza mambo mazito kwa hoja nyepesi. Timu haina kikosi kizuri, hilo wanapaswa kukiri na kulifanyia kazi haraka kuelekea dirisha dogo la Januari.

By Luqman Maloto
 
umeshasikia wapi kuwa LFC wanataka Balotelli acheze kama Suarez??
 
Swadaktaaaa!huo ndo ukweli,tatizo lingine lipo ndani ya uongozi kama uliiona mechi yao na mtibwa utagundua kunatatizo,
 
Mi naombea tim yenyewe ife kabisaa tupumzike!!
 
Mchambuzi mzuri kuliko wanaojiita wachambuzi!
 
Huu ndio uchambuzi.

Simba wamepaniki. Kupaniki huku kutaiharibu timu zaidi na zaidi kama juhudi za makususi hazitachukuliwa.
Kwa upande wangu naona wanachovuna Simba ni haki yao. Mpira usingekuwa fair kama Simba wangekuwa wameshinda na kuongoza ligi kwa sasa.

Huwezi kuwa na timu mpya kila baada ya miezi sita halafu uwe na matokeo mazuri. Huwezi kuwa na kocha mpya kila baada ya miezi minane halafu uwe na matokeo mazuri. Huwezi kuwa na wachezaji karibu saba ktk kikosi cha kwanza ambao hawana hata miezi 18 ya tangu waanze kucheza ligi kuu halafu eti uwe na kikosi tishio. Mpira usingetenda haki.

Wanachopaswa kutambua Simba ni kuwa wana timu nzuri ya vijana wadogo wenye uwezo mkubwa wa kucheza mpira. Vijana hawa wanahitaji tu kucheza kila mara na kuvumiliwa angalau kwa msimu huu tu kisha matokeo yatakuja yenyewe.
Simba wanahitaji kukaa na Patrick Phiri na kumwacha aendelee kusuka timu ktk ngwe ya pili na hata msimu mpya wa 2015/2016 kisha watakuwa wanasubiri matokeo yakija bila jasho. Phiri anahitaji angalau miezi 8 mingine kuirudisha Simba kwenye ubora wake.

Na tayari dalili zimeanza kuonekana. Uelewano wa timu iliyocheza dhidi ya Mtibwa ulikwa ni mzuri sana. Matokeo yaliyopatikana ilikuwa ni mojawapo ya matokeo ya kimpira. Kiemba Kisiga na Chanongo wanahitajika sana Simba. Hawa wote ni wachezaji wa kiwango cha juu kwa soka la Tanzania. Kuwaondoa saa hizi kwenye timu ni kuihujumu timu.

Kiemba anacheza mpira huo huo miaka yote lakini hawezi kustawi kwenye pressure kubwa. Ana hitaji mpira wa nafasi na uhuru. Hana tofauti sana na Haruna Moshi. Na ndio maana anafanya vizuri timu ya taifa maana mechi za kimataifa wanchezajai wanatanua uwanja na kucheza kwa nafasi. Chanongo anapoteza uwezo wake wa kujiamini kutokana na maneno maneno yasiyoisha dhidi yake. Amepewa majukumu makubwa kuliko umri na uwezo wake. Kisaikolojia hayuko sawa. Kisiga yuko vizuri sana lakini umri unakwenda kwa hiyo anahitaji kupewa free role uwanjani.

Simba ina kila sababu ya ktengeneza mazingira ya vijana wao ambao wameanza kuaminika ktk timu, wapevuke na kocha wao Phiri na watakuwa wameitendea haki timu yao na taifa lao kwa ujumla.
 
Back
Top Bottom