Kutoka Gazeti la Habari Leo.
KENYA imetajwa kunufaika zaidi na Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hivyo kujipatia fedha nyingi za kigeni kutokana na kuuza nje bidhaa zinazotokana na malighafi inayozalishwa Tanzania ambayo inasuasua katika kutumia fursa zinazotokana na soko hilo.
Hayo yamebainika jana Dar es Salaam wakati Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alipozindua Kamati ya Kitaifa ya kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la EAC.
Sitta alisema Tanzania iko nyuma katika kutumia fursa zinazotokana na soko hilo, na kuitaka kamati hiyo ambayo wajumbe wake ni makatibu wakuu na wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali kuhakikisha Watanzania wanawezeshwa kutumia fursa hizo vema.
Akitolea mfano namna Kenya inavyofaidika na Soko hilo la Pamoja, Waziri Sitta alisema machungwa mengi yanayozalishwa Muheza mkoani Tanga yanakwenda kuuzwa Kenya ambako wao hutengeneza juisi na kuisindika na kisha kuuza nchi za Mashariki ya Mbali na kujipatia fedha nyingi za kigeni.
Mbali na kunufaika na machungwa kutoka Tanzania, nchi hiyo jirani pia imekuwa ikinufaika na mifugo kwani imebainika kuwa asilimia 80 ya nyama ya ngombe inayosindikwa Kenya na kuuzwa nje, inatokana na ngombe waliouzwa Kenya na wafugaji wa Kitanzania, tena kwa bei nafuu.
Wenzetu Wakenya wana benki yao ya KCB hapa nchini na ambayo sasa tunaelezwa kuwa tayari ina matawi takribani 13 katika taifa jipya la Sudan Kusini, lakini sisi kutokana na sera, benki zetu haziwezi kufanya hayo, hivyo tunashindwa kunufaika na biashara hiyo, alisema Sitta.
Changamoto nyingine iliyoelezwa kuwa kikwazo cha utekelezaji wa soko hilo ni nchi wanachama kuchelewa kukamilisha zoezi la kuhuisha sheria zina