Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni chombo kilichopewa jukumu la kuhakikisha kuwa Utumishi wa Umma unakuwa na watumishi wenye weledi wa hali ya juu kupitia mchakato wa ajira. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa inapata waombaji wenye sifa kitaaluma, uwezo na ujuzi ili kuufanya Utumishi wa Umma kuendeshwa na watumishi wenye weledi na maadili mema katika kuiwezesha Serikali kutimiza malengo yake kwa ufanisi.
Sekretarieti ya Ajira katika tathmini yake imebaini mapungufu mbalimbali yatokanayo na ubora wa wahitimu wanaoomba kazi kupitia chombo hiki ambao wamehitimu ngazi mbalimbali za elimu ikiwemo wanaotokea kazini.
Aidha, tofauti ya mapungufu yao hutofautiana kutoka ngazi moja na nyingine, uwezo wa kitaaluma, ufahamu, Kuamini vyeti peke
yake vinaweza kuwapa kazi pasipokuwa na uelewa mpana wa kile walichoombea kazi, kutotilia maanani sifa/vigezo na masharti ya tangazo husika, kutokujiamini, kukosa uzoefu kwa kazi inayohitaji uzoefu, uwezo mdogo wa mawasiliano ikiwemo matumizi ya lugha sahihi, uwezo mdogo wa kutumia nyenzo za utendaji kazi hususan vifaa vya kielekroniki, kutokujiandaa vya kutosha, kukosa mbinu za usaili na kutozingatia muda.
Changamoto nyingine ni kutokujitambua, kusoma kwa kufuata mkumbo, kukosa sifa halali za kitaaluma, kutokujua namna ya kuandika barua za maombi ya kazi, namna ya kuandika wasifu wao(CV), kutokuwa na maandalizi sahihi pamoja na kughushi baadhi ya sifa kwa lengo la kujipatia ajira.
Kwa upande wa wahitimu wanaoomba kazi wakitokea kazini baadhi yao wameonyesha udhaifu wa kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto hivyo kuona ni bora atafute kazi nyingine, kutokupitisha barua kwa waajiri, kukosa uelewa mpana unaoendana na uzoefu wake kazini ili kuweza kuonyesha tofauti yake na waajiriwa wapya, kukimbilia serikalini ili kupata fursa ya kusomeshwa lakini si kwa lengo la kwenda kuongeza tija kiutendaji.
Hali hii inadhihirisha kwamba wapo waombaji kazi ambao wanasoma ili kuhitimu au kufaulu na sio kuelewa kwa ufasaha fani wanazosomea ili kuweza kuleta utaalamu wao katika nyanja mbalimbali za maendeleo. Jambo ambalo limekuwa likichangia wengi wao kushindwa kufikia hatua ya kuitwa kwenye usaili kutokana na kukosa baadhi ya vigezo na wengine kufikia hatua ya usaili na kushindwa kufaulu usaili husika kutokana na kutojiandaa ipasavyo.
Sekretarieti ya Ajira katika kukabiliana na changamoto ya upungufu unaotokana na ubora wa wahitimu kabla ya kuingia katika mfumo wa kutuma maombi kwa njia ya Kielektroniki imeamua kuweka mapungufu haya kwa uwazi ili kusaidia wahitimu husika na wadau mbalimbali wa elimu katika kuzitatua changamoto hizo.
Aidha, Chombo hiki kitaendelea kutembelea sekta za elimu ikiwemo kushauriana na mamlaka na wadau mbalimbali wa elimu kuhusu namna ya kukabiliana na changamoto hizo kwa pamoja ikiwemo kuandaa programu ya elimu kwa umma ili kuwawezesha waombaji wa kazi kuweza kutimiza vigezo vinavyohitajika ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata kazi husika wanazoomba.
PSRS