MAMLAKA ya Usafirishaji Majini na Nchi Kavu (Sumatra), imesema Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), kipindi hiki linawapa wakati mgumu kutokana na kushindwa kutii taratibu zilizowekwa barabarani.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mfawidhi Sumatra Kanda ya Mashariki, Conrad Shio, alisema hadi sasa kuna mabasi ya UDA 150 ambayo yanafanya safari bila kusajiliwa na mengine ambayo yamesajiliwa, bado hayajapakwa rangi na kuwekwa vibao vinavyoonyesha yanakotoka na yanakokwenda.
Alisema mwitikio wa UDA kuweka rangi na vibao hivyo haupo huku makondakta nao wakikaidi kuvaa sare, sambamba na kukatisha njia.
"Bado tunasisitiza UDA zipakwe rangi na pia ziwekwe vibao ambavyo vinaonyesha sehemu zinakotoka na zinakokwenda, tunaomba UDA kufanya utaratibu unaofanywa na daladala ili kuweza kwenda sawa," alisisitiza Shio.
Aliongeza kuwa kwa sasa wana vikao vya mara kwa mara na UDA na siku za usoni muafaka utapatikana.
Alibainisha kuwa kwa wastani wamekuwa wakizikamata UDA tatu kwa siku na huzipiga faini kati ya sh. 150,000 na 250,000 kulingana na makosa husika.
Shio, alitoa wito kwa abiria kuendelea kutoa taarifa pale magari hayo yanapokatisha njia ama kupandisha nauli.
Alipotafutwa Msemaji wa UDA, George Maziku, alisema kwamba si kweli kuwa kuna mabasi yao 150 hayajasajiliwa na akahoji kama yapo kwanini washindwe kuyakamata.
Kuhusu sare, alisema madereva na makondakta wao wote wamepewa, ila kama ni suala la kutozivaa ni ukaidi wao wenyewe.
Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kutokana na jinsi UDA inavyofanya kazi zake, ikiwamo njia zake kutoeleweka, kukatisha njia na kutoza nauli kubwa.