Uboreshaji huduma ya afya ni habari njema

singidadodoma

JF-Expert Member
Nov 11, 2013
4,394
1,536
MOJA ya habari njema kwa Watanzania ni Serikali kutangaza kuboresha huduma za afya zikiwemo za Hospitali za Rufaa, Maalumu, Kanda na hasa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na hasa kuiwezesha kutoa huduma ya kupandikiza figo.

Habari hii si tu kwamba itaiwezesha Serikali kuepuka gharama kubwa za kuwapeleka baadhi ya viongozi na maofisa wake nje ya nchi, lakini pia itaongeza mapato na kupunguza misongo kwa Watanzania wenye uwezo mdogo wa kifedha ambao kwao kwenda nje ya nchi kupata matibabu ilikuwa ni ndoto.

Habari hii njema kwa Watanzania ilitolewa bungeni Dodoma juzi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Waziri Ummy hakuishia hapo, alibainisha pia kwamba maboresho hayo kwa upande wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni pamoja na kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) kutoka 21 hadi vitanda 75.

Pia akasema Serikali imeazimia kununua vifaa tiba vya upasuaji na kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 13 vya sasa hadi 18. Akaongeza kwamba itapanua huduma za kusafisha figo kwa kuongeza vitanda kutoka 15 hadi vitanda 50 na kuanza kusafisha figo kwa wagonjwa wenye Virusi Vya Ukimwi na virusi vya ini.

Tunasema ni habari njema kwa Watanzania kwa kuwa huduma za afya zimekuwa hazikidhi haja kwa Watanzania. Mbali na kuwepo uhaba mkubwa wa dawa mahospitalini hasa zile za rufaa pia vifaa tiba, vyumba vya wagonjwa na madaktari vimekuwa ni kikwazo kwa wananchi kwa muda mrefu.

Wapo Watanzania wengi ambao wamepoteza maisha kwa kuwa hawakuwa na jinsi ya kupata msaada kwa kuwa ama hapakuwa na huduma za kutosha kwa maana ya kuwepo na wagonjwa wengi au kwa kutokuwepo kabisa kwa huduma hiyo hapa nchini na ndio maana wenye uwezo wa kifedha tu ndio waliweza kupelekwa nje ya nchi hasa India.

Magonjwa yanayohusiana na figo kwa mfano, yamekuwa ni hatarishi kwa wananchi walio wengi, na hasa kwa kuwa magonjwa hayo yamekuwa yakihitaji gharama kubwa kutibiwa. Ni katika hali hii, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imeliona hili na kuamua kulivalia njuga.

Kweli kuna kila haja ya kuendelea kuwaombea viongozi wa awamu hii waweze kulitumikia taifa kwa mwendo huo huo wa kasi bila kikomo. Katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Muhimbili itaanzisha huduma mpya ya upandikizaji figo na upandikizaji wa ‘cochlea’ kwa wagonjwa ambao ni viziwi…itajenga jengo la kisasa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa binafsi na viongozi wa kitaifa na watu mashuhuri litakalokuwa na vitanda 170 na kuongeza mapato kutoka Sh bilioni 2.6 za sasa hadi Sh bilioni 5 kwa mwezi.

Pia Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) katika mwaka huu wa fedha 2016/17, itaongeza nafasi ya wagonjwa wanaolazwa kutoka vitanda 150 hadi 340 ambapo katika chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) vitaongezeka kutoka vinane hadi 32.

Serikali imeazimia kununua mashine mpya za uchunguzi ikiwa ni pamoja na MRI, CT Scan na Xray za dijitali na kwamba MOI itatoa mafunzo ya upasuaji wa marejeo kwa nyonga na goti.

Kama tulivyobainisha hapo juu, kwamba kupanua wigo kwa huduma za afya, kunaenda sambamba na uboreshaji wa mapato ya Serikali lakini pia kunalenga moja kwa moja kuwaondolea kero Watanzania wa kada zote.
 
Back
Top Bottom