Tundu Lissu: Kama risasi 16 za 'watu wasiojulikana' waliotumwa kuniua hazikuninyamazisha, kuninyang'anya mshahara hakutaweza kuninyamazisha

Johnny Sack

JF-Expert Member
Jan 21, 2017
8,813
18,793
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ameibuka tena na waraka mwingie kuhusu kunyanganywa mshahara wake pamoja na posho zote

Tundu Lissu anasema alikuwa ameshasitishiwa mshahara wake huo kabala hata ya Spika Ndugai kutangaza Bungeni

Lissu ameeleza kuwa kama hawkumtingisha kwa kukosa kosa kumuua kwa risasi 16 basi hawatamtingisha kwa kumnyima mshahara wala posho Tundu Lissu ameendelea kusema mshahara wake umesitishwa kwa chuki tu na wala hajavunja kanuni wala sheria yoyote ambayo angestahili kuondolewa mshahara na posho

Hado sasa hajaandikiwa barua yoyote ya kumueleza kuwa sababu ya mshahara wake kusitishwa

Tundu Lissu amemtaka Spika Ndugai kumrudishia mshahara wake huo kwa kuwa ameuondoa isivyo halali
pia amewaomba watanzania kumchangia ili aendelee na matibabu yake kama walivyofanya awali



YA SPIKA NDUGAI, MSHAHARA WANGU NA UKIUKAJI WA SHERIA
Tundu AM Lissu, MB

Watanzania wenzangu na marafiki wa haki popote mlipo,

Salaam,

Mapema ya mwezi uliopita, tulimsikia Spika wa Bunge la Tanzania, Job Yustino
Ndugai, akitoa kile alichokiita 'mwongozo' kuhusu Bunge kunifutia mshahara na
posho za kibunge ambazo kila Mbunge hulipwa kila mwezi.

Katika 'mwongozo' wake huo, Spika Ndugai alieleza sababu ya kunifutia
mshahara na posho za kibunge kuwa ni kutokuwepo kwangu Bungeni 'bila
ruhusa ya Spika.'

Leo napenda kuthibitisha kwamba uamuzi wa Bunge kunifutia mshahara na
posho zangu ulifanyika kabla hata ya Spika Ndugai kuombwa, na kutoa, mwongozo huo. Ndio kusema kwamba Bunge la Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai limezuia mshahara na posho za kibunge tangu mwezi January ya mwaka huu.

Kwa hiyo, kitendo cha kuombwa, na papo hapo kutoa, mwongozo kulikuwa ni mpango tu wa kuhalalisha maamuzi yaliyofanywa nje ya Bunge kabla hata ya
kikao chenyewe cha Bunge kuanza.
Iwe itakavyokuwa, uamuzi wa kunifutia mshahara na posho za kibunge ambazo
kila Mbunge hulipwa, awe anaumwa au mzima, awe amehudhuria vikao vya
Bunge au hajahudhuria, ni uthibitisho mwingine wa utamaduni wa ukiukaji wa
Katiba, Sheria na taratibu ambao umekithiri sana katika Tanzania ya Magufuli
na Bunge la Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai.

Aidha, kitendo hicho ni uthibitisho mwingine wa chuki kubwa ambayo
imetamalaki dhidi yangu binafsi, na dhidi ya wote ambao tumekataa kumsujudia Magufuli na watu wake, na ambao tumekuwa tukisimamia misingi ya Utawala wa Sheria na Katiba ya nchi yetu katika kutetea haki za wananchi wetu.

Ninaadhibiwa na tunaadhibiwa sio kwa sababu ni wavunja sheria za nchi yetu;
bali ni kwa sababu ya kusimamia Katiba na Sheria za nchi yetu katika kutetea haki za wananchi wetu.

Ninaadhibiwa na tunaadhibiwa sio kwa sababu sisi ni wasaliti wa nchi yetu; bali
ni kwa sababu ya kukataa kunyamaza kimya na kufumba macho wakati maslahi halisi ya nchi yetu na wananchi wetu yanahujumiwa na watu waliojipachika vyeo vya uongo vya 'watetezi wa wanyonge.'

Kwenye hili, msimamo wangu hautayumba. Kama risasi 16 za 'watu wasiojulikana' waliotumwa kuniua hazikuninyamazisha, kuninyang'anya mshahara na posho za kibunge hakutaweza kuninyamazisha.

Kama kuninyima stahili yangu ya fedha za matibabu na za kujikimu hakujanipigisha magoti kwa watesi wetu, kuninyang'anya mshahara wangu na posho za kibunge hakutanibadilisha msimamo kwenye masuala ya msingi ya nchi yetu. Hata hivyo, nina wajibu wa kuonyesha uovu na uharamu wa vitendo hivi kwa wananchi na kwa dunia nzima, na kudai haki itendeke.

Mshahara na posho za kibunge ambazo kila Mbunge hulipwa kila mwezi sio
fadhila za Rais Magufuli na CCM; bali ni haki ya kikatiba na kisheria ya kila Mbunge wa Tanzania.

Aidha, haki hiyo haitegemei utashi binafsi wa Spika Ndugai na Katibu wa Bunge
Kagaigai. Vile vile, haki hii haiwezi kufutwa ama kusimamishwa kwa sababu ya Mbunge kutohudhuria vikao vya Bunge au kwa sababu nyingine yoyote. Naomba kufafanua.

Kwa mujibu wa ibara ya 73 ya Katiba yetu, "Wabunge wote wa aina zote ... watalipwa mshahara, posho na malipo mengine kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge."

'Sheria iliyotungwa na Bunge' inayozungumzwa hapa ni Sheria ya Uendeshaji wa Bunge, 2008, Sura ya 115 ya Sheria za Tanzania. Kifungu cha 19 cha Sheria hiyo kimefafanua 'stahili' za Mbunge kuwa ni mshahara na posho zifuatazo:

(a) Posho ya majukumu kwa ajili ya Spika, Naibu Spika, Kiongozi wa Shughuli za
Serikali Bungeni, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Serikali Bungeni, Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Wenyeviti wa Bunge na wa Kamati za Kudumu za Bunge;

(b) Posho ya Jimbo kwa Mbunge wa Jimbo;

(c) Posho maalum kwa Wabunge wa Viti Maalum;

(d) Posho kwa ajili ya malipo ya msaidizi wa Mbunge, dereva, mhudumu wa ofisi
na matumizi mengine ya ofisi, na posho nyingine zitakazoamuliwa na rais.

Ijapokuwa kifungu cha 19 kinasema stahili hizi za Wabunge zitaamuliwa na Rais;
akishaamua na uamuzi huo kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali, Rais hana

mamlaka tena ya kutengua ama kupunguza stahili hizo; au kuamua Mbunge yupi alipwe na yupi asilipwe.

Vivyo hivyo, sio Spika Ndugai wala Katibu wa Bunge Kagaigai mwenye mamlaka ya kufuta, kusimamisha ama kuzuia malipo ya stahili hizo kwa Mbunge yeyote kwa sababu yoyote.

Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa ibara ya 71 ya Katiba, "iwapo Mbunge hatakoma kuwa Mbunge kwa mujibu wa jambo lolote kati ya mambo hayo yaliyotajwa (kwenye ibara hiyo) na kama hatajiuzulu au kufariki mapema zaidi, basi Mbunge ataendelea kushika madaraka yake kama Mbunge ... bila ya kuathiri haki na stahili zinazotokana na ubunge wake."

Mambo yaliyotajwa na ibara ya 71 yanayoweza kuathiri 'haki na stahili
zinazotokana na ubunge' hayanihusu mimi kabisa.

Sababu ya kwanza ni kukosa au kupoteza sifa za kuchaguliwa kuwa Mbunge.
Mimi sijakosa wala kupoteza sifa za kuchaguliwa kuwa Mbunge.

Jambo la pili lililotajwa kwenye ibara ya 71 ni kuchaguliwa kuwa Rais. Mimi
sijachaguliwa, bado, kuwa Rais.
Jambo la tatu ni kukosa kuhudhuria vikao vya Mikutano mitatu mfululizo ya
Bunge 'bila ruhusa ya Spika.'

Mimi sijahudhuria kikao chochote cha Mkutano wowote wa Bunge tangu
September 7, 2017, kwa sababu nilikimbizwa nje ya nchi nikiwa sijitambui,
baada ya kushambuliwa kwa risasi na wanaoitwa 'watu wasiojulikana.'

Spika Ndugai, aliyehudhuria kikao kilichoamua nipelekwe Nairobi kwa
matibabu, na aliyeahidi kuja kunitembelea hospitali mahali popote nitakapokuwa lakini hakufanya hivyo, hawezi kusema nimekuwa nje muda wote huu bila ruhusa yake.

Sababu ya nne ni kama itathibitishwa kwamba Mbunge amevunja masharti ya
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Hakuna uthibitisho wa mimi kuvunja
masharti yoyote ya Sheria hiyo.

Jambo la tano ni kuacha kuwa mwanachama wa Chama alichokuwamo
wakati alipochaguliwa au kuteuliwa Mbunge. Mimi siko tayari kujifedhehesha,
na kuwasaliti wananchi na wanachama wa CHADEMA walionipa heshima ya
kuwa Mbunge wao, kwa 'kuunga mkono juhudi.'

Jambo la sita lililotajwa kwenye ibara ya 71 ni kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa
Makamu wa Rais. Mimi sitarajii kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais.

Mambo mengine yaliyotajwa na ibara ya 71 yanayoweza kuathiri stahili
zinazotokana na ubunge ni kujiuzulu au kifo cha Mbunge. Mimi sina mpango
wowote wa kujiuzulu ubunge wangu.
Aidha, pamoja na kumiminiwa risasi 16 mwilini mwangu na wauaji wa kutumwa,
na licha ya kunyimwa stahili zangu za matibabu kwa muda wote huu, bado
niko hai.

Nje ya Katiba na Sheria ya Uendeshaji wa Bunge, namna pekee ambayo
mshahara na posho za kibunge unaweza kuathiriwa kihalali ni kwa Mbunge
kusimamishwa na Bunge kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kukiuka maadili ya
Bunge.

Hapa Kanuni za Kudumu za Bunge zimeelekeza kwamba Mbunge huyo
atalipwa nusu ya mshahara na posho za kibunge kwa muda wote wa
kusimamishwa kwake. Sababu hiyo nayo hainihusu.

Kwa vyovyote vile, uamuzi wa kuzuia mshahara na posho zangu za kibunge ni
uamuzi haramu kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu, Sheria ya Uendeshaji wa
Bunge na Kanuni za Kudumu za Bunge letu. Ni uamuzi haramu vile vile kwa
sababu haujazingatia misingi ya haki katika kufanya maamuzi yanayoathiri haki
na maslahi ya yangu.

Hadi sasa, sijaandikiwa barua au kutakiwa kujieleza kwa namna yoyote ile kwa
nini stahili zangu zisizuiliwe kwa sababu ya 'utoro' wangu Bungeni tangu tarehe 7
September, 2017.

Aidha, licha ya Waraka wa Tume ya Utumishi wa Bunge kuelekeza kwamba
madaktari wa Bunge, au mwambata wa kitabibu wa ubalozi husika wa
Tanzania, wanawajibika kufuatilia matibabu ya Mbunge anayetibiwa nje, na
kutoa taarifa za mara kwa mara kwa uongozi wa Bunge, hadi sasa
sijatembelewa na daktari yeyote wa Bunge, au mwambata husika wa ubalozi
wa Tanzania.

Vile vile, pamoja na kwamba huu ni mwezi wa pili sijalipwa mshahara na posho
zangu za kibunge, Bunge la Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai
halijanipa taarifa yoyote kuhusu jambo hilo na sababu zake.

Kama ambavyo imekuwa kawaida katika Tanzania ya Magufuli, Bunge la Spika
Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai linaendeshwa kwa matakwa na utashi

binafsi, bila kujali Katiba, Sheria wala Kanuni za uendeshaji bora na wa haki wa
shughuli za umma.

Kwa sababu zote ambazo nimezielezea kwa kirefu, ninautaka uongozi wa
Bunge, yaani Spika Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai, kurudisha mshahara
na posho zangu za kibunge mara moja na bila masharti yoyote.

Aidha, kama uongozi wa Bunge unataka kufahamu hali yangu ya kiafya kwa
muda wote ambao sijahudhuria vikao vya Bunge hadi sasa, basi utume
madaktari wa Bunge au mwambata wa kitabibu wa ubalozi wa Tanzania nchini
Ubelgiji, kuja kunijulia hali na kulipatia Bunge taarifa sahihi za hali yangu ya
afya.

Hivi ndivyo inavyotakiwa na Waraka Na. 1 wa 2016 Kuhusu Utaratibu wa
Matibabu ya Wabunge Nje ya Nchi wa Tume ya Utumishi wa Bunge.

Kama mhimili muhimu wa dola ya Tanzania, Baraza la kutunga sheria na
chombo cha kuisimamia na kuishauri Serikali, Bunge lina wajibu wa kuonyesha
mfano bora wa kuheshimu Katiba, Sheria na taratibu zake na kuzingatia misingi
ya haki katika utendaji kazi wake.

Ili kuhakikisha sheria za nchi yetu zinaheshimiwa na haki inatendeka katika suala
hili, nimewaelekeza mawakili wangu nchini Tanzania, kuanza mchakato wa
kufungua mashauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania, ili kudai Bunge la Spika
Ndugai na Katibu wa Bunge Kagaigai lirejeshe stahili zangu zote zilizozuiliwa, na
kulizuia lisiziingilie au kuziathiri tena kwa namna nyingine yoyote.

Mwisho, lakini sio kwa umuhimu, nawaomba Wasamaria Wema, Watanzania na wasiokuwa Watanzania, popote pale walipo duniani, waingilie kati tena katika
suala hili.

Kama mlivyofanya wakati niliposhambuliwa na wauaji wa kutumwa na kama
ambavyo mmeendelea kuniuguza na kunitunza kwa kipindi chote hiki,
nawaombeni muendelee kunichangia kwa chochote mlichobarikiwa, hadi
hapo matibabu yangu yatakapokamilika na mimi kurudi Tanzania ili kuendelea
kuwatumikia Watanzania.

Nawaombeni msiwaruhusu wale walioshindwa kuniua kwa risasi, na kwa
kuninyima gharama za matibabu na za kujikimu, kufanikisha malengo yao
maovu, kwa kuninyang'anya stahili zinazotokana na ubunge wangu.

Nawashukuruni sana na Mungu awape baraka zake.

Tienen, Ubelgiji
Machi 13, 2019
 

Attachments

  • TUNDU LISSU - YA SPIKA NDUGAI MSHAHARA WANGU 1.pdf
    56.8 KB · Views: 41
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ameibuka tena na waraka mwingie kuhusu kunyanganywa mshahara wake pamoja na posho zote
Tundu Lissu anasema alikuwa ameshasitishiwa mshahara wake huo kabala hata ya Spika Ndugai kutangaza Bungeni
Lissu ameeleza kuwa kama hawkumtingisha kwa kukosa kosa kumuua kwa risasi 16 basi hawatamtingisha kwa kumnyima mshahara wala posho
Tundu Lissu ameendelea kusema mshahara wake umesitishwa kwa chuki tu na wala hajavunja kanuni wala sheria yoyote ambayo angestahili kuondolewa mshahara na posho

Hado sasa hajaandikiwa barua yoyote ya kumueleza kuwa sababu ya mshahara wake kusitishwa

Tundu Lissu amemtaka Spika Ndugai kumrudishia mshahara wake huo kwa kuwa ameuondoa isivyo halali
pia amewaomba watanzania kumchangia ili aendelee na matibabu yake kama walivyofanya awali


Kwani bado anatibiwa au anafanya kazi za chadema ughaibuni. Mgonjwa gani anahojiwa kwenye vipindi maalum vya tv na radio huko ulaya pia kufanya mihadhara vyuo vikuu marekani. Tena anataka nchi iwekewe vikwazo. Huyo si mgonjwa amepona kama harudi kuwakilisha jimbo lake safi kusimamisha malipo.
 
Kama hafati sheria walizonazo huko Bungeni.. anyamaze tu.
Blah blah zote hizo anafikiri wenye chama watampa mwanya wa kuwania uraisi..
Tangu aombe ombe pesa kwa kudanganya vipi.. bado anazo? Kama gangwe kweli asingelia lia tena..
 
Back
Top Bottom