dubu
JF-Expert Member
- Oct 18, 2011
- 3,500
- 3,481
Serikali imewataka wauzaji wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi (mobile devices) kuacha mara moja tabia ya kubadilisha namba tambulishi (‘kuflash’) za vifaa hivyo kwani watakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka 10 au faini isiyopungua Sh. milioni 30 au vyote viwili.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
“Namba tambulishi (IMEI) za vifaa vyote vya mawasiliano ya mkononi ambavyo vimeibiwa,vimeharibika,kupotea au visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaruhusiwa kuunganishwa kwenye mitandao ya watoa huduma ifikapo tarehe 16 June 2016, "alisema Mungy.
Akizungumzia kampeni ya kuelimisha umma kuhusu matumizi ya simu zote zisizokidhi viwango, Mungy alibainisha kuwa idadi ya simu hizo imeshuka kutokana na elimu ambayo wameitoa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.
Alisema lengo la elimu hiyo kwa umma ni kujenga uwezo kwa wananchi kutambua simu zisizokidhi vigezo kabla ya kufika ukomo wa matumizi ya simu bandia nchini.
Mungy alifafanua kuwa uchambuzi wa IMEI unaonyesha kuwa hadi Februari,2016 idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa hazina viwango zilikuwa sawa na asilimia tatu ambapo namba tambulishi ambazo zimenakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 18 na simu halisi zilikuwa sawa na asilimia 79.
“Kwa mwezi Machi 2016 ulionyesha kuwa Idadi ya namba tambulishi ambazo hazina viwango ni asilimia nne, na idadi ya zile zilizonakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 13 ambapo uchambuzi huu umehusisha taarifa za kampuni zote za simu nchini,’’. alifafanua Mungy.
Aliongeza kuwa matokeo hayo mazuri ni matunda ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya mamlaka hiyo, Shirika la Viwango Tanzania (TBS),Tume ya Ushindani (FCC),kampuni za simu, pamoja na wadau wengine katika kuelimisha umma juu ya uhakiki wa simu walizonazo ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kununua simu ikiwemo kuzihakiki ubora wake.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, Injinia Gabriel Mruma amesema kuwa ni vyema Watanzania wakajenga utamaduni wa kununua simu zenye ubora kuepuka usumbufu wakati Tanzania inapoelekea ukomo wa matumizi ya simu bandia.
TCRA ina dhamana ya kusimamia shughuli za mawasiliano ya Kielektroniki na Posta hapa nchini.
Kuwepo kwa Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 na kanuni zake za mwaka 2011 kumewezesha kutekelezwa kwa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.
Mfumo huu wa kielektroniki ulizinduliwa tarehe 17, Desemba 2015 na unahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi kwa lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vilivyoibiwa,kuharibika au kupotea, bandia vya mawasiliano katika soko.