HOJA binafsi iliyowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyik (CHADEMA), kutaka hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na uondoaji wa maji taka jijini Dar es Salaam, itatolewa uamuzi katika kikao kijacho cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya jiji hilo.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na katibu wa mbunge huyo, Aziz Himbuka, ilieleza kuwa Mnyika aliwasilisha hoja hiyo kwa Mkurugenzi wa Jiji, Mussa Natty.
Himbuka alisema kuwa katika hoja hiyo, Mnyika alieleza kwamba kati ya mwaka 2003 mpaka 2010 serikali ilitekeleza mradi wa ukarabati na upanuzi wa miundombinu ya majisafi na majitaka jijini Dar es Salaam na maeneo ya Bagamoyo na Kibaha.
Alisema kuwa mradi huo ulitumia dola za Kimarekani milioni 164.6, lakini hata hivyo hadi sasa katika maeneo mengi mabomba yake hayatoi maji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wizara ya Maji iliandaa waraka maalumu wa kuiomba serikali kutenga kiasi cha sh bilioni 653.85 katika mpango maalumu wa 2011-2013 wa kuboresha huduma za majisafi na uondoaji wa majitaka uliopitishwa na Baraza la Mawaziri.