Dar es Salaam. Ripoti ya utafiti kuhusu ujangili wa meno ya tembo imebaini kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi mbili za Afrika ambazo idadi kubwa ya tembo wanauawa.
Utafiti huo wa njia ya vinasaba (DNA) uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) ulibaini kuwa asilimia 85 ya meno ya tembo yanayokamatwa asili yake ni mbuga za Selous, Ruaha na Ruangwa, Tanzania.
Kadhalika, utafiti huo umebaini kuwa nchi nyingine ambayo tembo wengi wanauawa ni Congo.
Katika utafiti huo, Mwanabaiolojia wa Chuo Kikuu cha Washington, Samuel Wasser alitumia teknolojia ya vinasaba kujua asili ya meno ya tembo yanayokamatwa.
“Kujua maeneo ambayo meno mengi yanatoka, kunasaidia kujua eneo lenyewe na kuwekeza nguvu kazi na sheria ili kumaliza mauaji ya tembo,” alisema Wasser.
Katika utafiti huo, Wasser alitumia sampuli za vinasaba kama kinyesi cha tembo, tishu na nywele ambavyo alivikusanya kutoka katika nchi zote Afrika. Baadaye alioanisha vinasaba hivyo na meno yaliyokuwa yakikamatwa.
Maabara iliyofanya utafiti huu ilipokea meno ya tembo yanayokamatwa na shirika la kimataifa la uchunguzi (jina linahifadhiwa) kisha baadaye yalipimwa ili kujua asili yake.
Kwa mfano, Julai 2006, kilo 2,500 za meno ya tembo yenye vinasaba vya Tanzania, yalikamatwa katika Jimbo la Kaohsiung, Taiwan.
Lakini kiasi kikubwa cha meno ya tembo kutoka Tanzania kilikuwa ni kilo 6,034 zilizokamatwa Desemba 2012, Port Klang, Malaysia.
“Shehena hii ya meno ya tembo yanayovunwa na kuuzwa fedha zake zinatumiwa zaidi kufadhili makundi ya kihalifu, hasa ugaidi katika nchi za Afrika,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Wakati huohuo, Shirika la Utafiti wa Mazingira, (EIA) limechapisha ramani mpya inayoonyesha maeneo hatarishi ya tembo na kuitaja Tanzania kuwa miongoni mwa maeneo makuu.
Akizungumzia ripoti hizo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani alisema anaweza kutoa ufafanuzi zaidi iwapo ataoanisha takwimu za ofisi yake na zile za EIA, shirika la kimataifa la kuhudumia wanyama na mimea walio katika hatari ya kutoweka (CITES) na UNODC.
Hata hivyo, alisema wizara imeandaa mikakati mipya ya kupambana na ujangili ikiwamo kuunda kikosi kazi kinachojitegemea kwa ajili ya kuzuia ujangili.
“Kikosi hiki kitafanya kazi kwa kushirikiana na jeshi la polisi na taasisi nyingine za ulinzi na usalama kwa sababu kwa sasa hatutaki kuwekeza katika kukamata, bali kuzuia zaidi ujangili,” alisema.
Kadhalika, EIA ilinukuu Ripoti ya mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayoishia Juni 30, 2013 ambayo ilibaini kuwa kilo 108 za pembe za ndovu ziliibwa kwenye ghala la kuhifadhi pembe za ndovu mwaka 2013.
“Kama Tanzania watashindwa kudhibiti hata wizi wa pembe zinazokamatwa ni rahisi pembe hizi kurudi tena kwenye soko haramu,” ilisema ripoti ya EIA.
Chanzo: Mwananchi