charz91
Member
- Aug 10, 2013
- 34
- 12
TANZANIA YA NYERERE SI HII YA LEO
Nimekuwa nikiandika mambo mbalimbali kulihusu taifa letu, licha yakutokuwa mwandishi kitaaluma, nimejaribu kuandika na kuchambua kile ambacho naamini kinawafikia walengwa ambao hasa ni watawala wa Nchi hii, kwa mtu makini naamini atajiuliza mara mbili mbili kwanini nimeamua kuwaita watawala na si viongozi? Hilo ni jambo pana kidogo, nitakuja kulieleza siku za mbele kadri mwenyezi mungu anavyoendelea kuniongezea siku za kuishi, lakini kwa leo wacha nijielekeze katika kuuchambua uongozi wa Baba wa taifa letu Mwalimu Julias Kambarage Nyerere nikiufananisha na huu utawala wa leo wa hawa watawala wetu tuliowazoea kuwaona wakija na vijimambo vyao vya ajabu ajabu kila uchao.
Baba wa taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere alikuwa kiongozi wa mfano wa aina yake kupata kutokea katika karne ya ishirini, akifahamika Afrika na duniani kote kama kiongozi mwenye msimamo makini, asiye mwepesi wa kuyumbishwa, mwingi wa maarifa, kiongozi aliijua vyema nchi anayoiongoza kama alijuavyo jina lake, Nyerere hakutetereshwa wala kutetereka katika maamuzi yake, hakuwa kiongozi mfuata filimbi ya mabeberu wa magharibu wanaoiliza filimbi yao hadi hii leo wakiwachezesha kundumbwendumbwe hawa watawala wetu wa sasa walioukubali mdundiko huo wa kimagharibi na kusahau kabisa utaifa wao, watawala ninaowasemea ni hawa ambao dhahiri shahiri wameshindwa kwa kiasi kikubwa kumuinua Mtanzania wa kule kijijini kwetu Mwambani kata ya Mkwajuni Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya kutoka kwenye umasikini na badala yake wameweza kumzamisha katika ufukara ulio kithiri ( tukuka), nimependa kuyatumia maneno hayo umasikinina ufukara kama vile ambavyo kaka yangu Zitto Z Kabwe huyafafanua maneno haya, tukianzia na Umasikini Zitto uelezea kuwa ni ile hali ya mtu au jamii fulani kushindwa kujimudu kupata mahitaji yake muhimu ya maisha mfano chakula, mavazi na malazi kutokana sababu za kimaafa kama vile vita, mafuriko, ukame, ama jiografia ya eneo husika kuwa tata , Lakini Ufukara ni ile hali ya mtu ama jamii fulani kushindwa kupata mahitaji muhimu kutokana na serikali kushindwa kusimamia upatikanaji wa mahitaji hayo, yaweza kuwa kwasababu ya sera mbovu, kukithiri kwa rusha, kushindwa kuyashughurikia mambo muhimu ya wananchi wake nk, kwahivyo umasikini ni ile hali tu yakuwa masikini, lakini ufukara ni ile hali ya kufukarishwa yaani kufanywa kuwa masikini.
Kutokana na tafsiri hizo zisizo rasmi, niseme tu wazi kwamba sisi Watanzania ni mafukara kwa asilimia kubwa, kwasababu umasikini wetu ni wakusababishwa na watawala wetu, watawala wapo tayari kutuvisha pingu na kututupa Segerea ama Keko endapo ukithubutu kuwanyooshea vidole juu ya uchakachuaji wanaofanya katika rasilimali zetu, watawala wetu wamekuwa wakifanya mambo ya ovyo na yakustaajabisha sana, wamekuwa wakiyapeleka peleka mambo kama vile wehu, tumeshuhudia hivi karibuni wakitupitisha katika mchakato wa kupata katiba mpya kana kwamba Watanzania tu mapunguani wa akili ama hatujasoma na kujielimisha juu ya maswala hayo, tuliona jinsi ambavyo mambo yamekwenda yakifunikwa funikwa na hatimaye wakiibuka na Katiba pendekezwa ambayo muonekano wake umekiuka maoni ya wananchi walio wengi kama ambavyo waliyapendekeza kwa tume ya mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, nilishangazwa sana jinsi watawala wetu walivyojinadi kwa kusema misimo yao wazi wazi na kwa hisia kali yakuwa wao watapigana kufa na kupona kuakikisha wanabakiza muundo wa serikali mbili, huku wakiongeza kusema kuwa muundo wa serikali mbili ndio msimamo wa CCM, kana kwamba tunatafuta katiba ya CCM, nilishangazwa zaidi waliposema kuwa muundo huo ( serikali mbili) ulikuwa ndio msimamo thabiti wa Baba wa taifa Mwalimu Nyerere hivyo wao kuusimamia msimamo huo ni kumuenzi kwakuwa wao ndio wakumuenzi Mwalimu zaidi, huo ni unafiki wa hali ya juu na unafiki huu ukalibisha unafiki mwingine wakusema kuwa yeyote anayepinga Muundo wa serikali mbili ni mpinga Muungano kitu ambacho si kweli hata kidogo, kwahiyo dhana yakuwa wanamuenzi Mwalimu ni uongo na unafiki, hapa unaweza kuwashangaa watawala hawa jinsi walivyo waongo, tunajua kuwa Mwalimu alikerwa sana na rushwa mbona wao leo wameikomaza Rushwa na hata ikaitwa Ufisadi, Mwalimu alikuwa na watoto wengi tu lakini hata mmoja haukuwahi kusikia kampa madaraka makubwa yasiyomstahili, leo watawala wetu wanalithishana madaraka wanafanya ubunge na uwaziri kuwa usultani, Mwalimu alipinga ubwenyeye leo watawala ni mabwenyeye wamegeuka kuwa wakoloni weusi, Tunajua sote kuwa moyo wa Mwalimu ulikuwa ndani ya Azimio la Arusha, mbona watawala wetu walilifuta azimio la Arusha na kulikiuka kabisa, sasa tunaposema tunamuenzi Mwalimu tunamuenzi vipi? Je, tunamuenzi kwa itaji la serikali mbili pekee? Ama tunatakiwa kumuenzi kwa maslahi Fulani?
Niliwahi kusema na nitarudia kusema kuwa mwalimu Nyerere, hakuwa malaika na wala hakuwa mkamilifu pia, Mwalimu alikuwa mwanadamu kama nilivyo Mimi na wewe na kwa hivyo inathibitisha wazi kuwa Mwalimu alikuwa akifanya makosa kama wengine, na alikuwa akiyasahihisha makosa yake sambamba kwa kutubu, hili linathibitishwa nayeye mwenyewe kupitia imani yake kama muhumini mkatoliki, Mwalimu alikuwa akihudhuria maungamo na hivyo tunazidi kuthibitisha kuwa naye alitenda dhambi pia, Sikatahi hata mara moja kwa watawala wetu kuishi na msimamo wao huo wa Serikali mbili, ila ninachotofautiana nao ni kumhusisha Mwalimu kwa kusema kuwa wanamuenzi katika kubaki na serikali mbili, huo ni unafiki wa wazi kabisa, narudia kuwa huo ni unafiki na pengine wapo wanaoweza kudhani kuwa nasema hivi kwavile ninaamini katika serikali tatu, hapana naomba nisieleweke hivyo hata kwa makosa, kwani msimamo wangu binafsi hapo niliuweka mapema katika maoni na Tume binafsi nilipendekeza pawepo na Serikali moja kwani ninatambua kuwa utata wa Muungano wetu ni swala la sovereighty kwamba tuna sovereighty mbili ndani ya nchi moja niliona kuwa utata huo wa sovereighty ungeweza kutatuliwa kwa kuleta serikali moja na wala si kwakubakiza hizi mbili ama kuongeza nyingine ya tatu, kwangu niliona hizo ni fujo. Lakini kwavile nimo ndani ya nchi yenye kujiita inafuata mfumo wa kidemokrasia usiyofahamika nilijikuta nakubaliana na misingi ya kidemokrasia inayofahamika yakwamba wengi wape uwezo wa kuamua na wachache wape nafasi waseme. Hivyo mimi nilipata nafasi nikasema na wengi wakaamua kutaka Serikali tatu, na nikalazimika kukubali kidemokrasia hilo liko wazi, nimeona niliseme hili wale wapinzani wangu wasiku zote wasipate nafasi ya kuchapa chapa maneno yao niliyoyazoea kuyasikia.
Nieleweke katika hili kuwa, Mwalimu hakuwahi kusema kuwa CCM isimamie muundo wa Serikali mbili milele, ninaimani kuwa kama Mwalimu angelikuwa hai hadi hii leo asingelipinga maoni ya wengi ama vile vile asingelisita kuwashahuri wana CCM wa leo kuwa wakati umefika kwa yale mambo yalioshindakana nyuma kuwezekana, ni lazima tutambue kuwa Mwalimu alibadilika kadri nyakati zilivyokuwa zikibadilika, tutakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 1990s ni mwalimu aliyekuwa wa kwanza kuunga mkono kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi Mwaka 1992 licha ya Tume ya Jaji Francis Nyalali kutoa matokeo yakuwa Watanzania wengi zaidi ya 80% hawakuwa tayari kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi, Mwalimu alikuwa wa kwanza kuwashauri wana CCM wenzake kukubali na kujiandaa na mfumo wa vyama vingi, ingawa ni yeye mwenyewe alifuta vyama vingi Mwaka 1965, niwaambie tu wazi watawala wangu nikiwa ninajua hata wao pia wanajua kuwa Mwalimu hakuwa static, ipo mifano mingine mingi inayoonesha kuwa Mwalimu alikuwa mtu wakubadilika na kusahihisha makosa yake ya nyuma, tazama Mwalimu aliwahi kuiunga mkono Jamhuri ya Biafra ilipokuwa ikipigana vita kujitenga na Nchi mama yao Nigeria, hapa Mwalimu alikosea na alikuja kujisahihisha baadae.
Mwaka 1994 mwalimu aliandika kijitabu chake kidogo kilichoitwa UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA ndani ya kijitabu hicho mwalimu alionyesha ufa mkubwa uliopo katika chama na Serikali, Mwalimu alieleza mengi yaliyopelekwa ovyo na watawala wetu wakati huo nchi ikiongozwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi, Waziri mkuu akiwa John Malecela na huku kwenye chama katibu mkuu akiwa Hayati Horace Kolimba, si lengo langu kusimulia kitabu chote hicho bali nilitaka niwaonyeshe ushahidi kuwa mwalimu hakuwahi kuenziwa na wana CCM wake, si wakati hakiwa hai wala baada ya kufa kwahiyo si wana CCM wa wakati huo akiwa hai wala wana CCM hawa wa leo wanaojitamba na kujinadi wazi wazi bila soni ati wanamuenzi baba wa taifa, hoja ile yakusema kuwa muundo wa serikali mbili ndio muundo sahihi uliopigiwa chepuo na Mwalimu inakufa kwa maandiko yake mwenyewe Mwalimu Mwaka 1995, Mwaka huo Mwalimu aliutanabaisha ulimwengu kwamba muundo wa serikali mbili unafaa kuendelea kuwa msimamo wa CCM walau hadi Agosti 01, 2004 {Ushahidi: Our leadership and destiny of Tanzania, ISBN: 1-77901-091-5, uk. 04, aya ya 03, sentensi ya kwanza}. Sasa wanaosema wanamuenzi Mwalimu leo Mwaka 2014, kwa kulazimisha Serikali mbili kwa kusema Mwalimu aliutaka uwe ndio Muundo wa milele basi nawashauri wakasome vizuri kitabu hicho ili wajielimishe.
Ni wazi kuwa mambo yanavyokwenda sasa ni tofauti kabisa na enzi zile za Mwalimu Nyerere, watawala wetu wa sasa wanapeleka mambo ovyo sana, wakati Mwalimu akiiongoza Nchii hii hakukuwa na utofauti mkubwa kati ya aliye nacho na asiye nacho, wakati ule wakina Samweli Sitta wakiwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam ( UDSM ) wakiandamana kudai maslahi yao sambamba na kutaka usawa wa kimaisha, wakipinga income gap kuongezeka, Mwalimu hakuona shida kupangua 20% ya mshahara wake wa Tsh. 5000/= bila kujali ugumu wa maisha atakaoupata Nyumbani kwake Msasani, leo unadhani Sitta anaweza kuthubutu kulilia kile alichokililia miaka ya 1960's? na hata akaupunguza mshahara wake ili kuwafariji Walimu na wale Madaktari wa Muhimbili wanaogoma kila leo? Je, unadhani inawezekana hata kwa mkuu wa kaya? Jibu ni ngumu sana, ukirejea wakati ule wa Mwalimu maadili ya uongozi yalifuatwa kikamilifu, viongozi waliheshimu raia wao na hata raia pia waliwaheshimu viongozi, hakukuwa na uhuni kwa viongozi, ile dhana ya kuongoza ni kuonyesha njia basi ilijidhiirisha wazi wakati huo tofauti na sasa watawala hawa wanavyopeleka mambo kihuni na wao pia wakiwa wahuni sambamba na matendo yao, tumeshuhudia jinsi watawala wetu wakidharirisha nafasi tulizo wapa, tumeona baadhi ya wabunge na mawaziri wetu wanavyoshinda wakianikwa mitandaoni wakiwa uchi wakifanya vitendo vya ajabu kabisa vya kudharirisha bunge na Serikali yao, wamekuwa wakifanya hivyo bila hata kukemewa, si Spika wa Bunge wala si Raisi wa Nchi aliyewahi kutoa kauli yakukemea upuuzi huo unaofanywa na baadhi ya wateule wake, kitu ambacho hakikuwahi hata kudhaniwa kingetokea katika miaka 25 yote baba wataifa akiwa madarakani.
Leo watawala wetu bado wanachezesha ndimi zao kusema kwamba wanapambana na rushwa eti leo bado kuna chombo kinaitwa TAKUKURU, hii yote ni kudanganya Watanzania kuendelea na lile wanaloliita funika kombe, kuendelea na ujanjaujanja, Serikali inajua tatizo la rushwa na yenyewe ni sehemu ya tatizo hilo ni wao wamelea rushwa ndogondogo hadi ikakomaa na kuwa beberu "UFISADI" Serikali ikiwa ndio mlezi mkuu, leo Serikali imeshindwa kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wakuu wa ufisadi wa kuanzia lile sakata la MEREMETA, RICHMOND, EPA, DOWANS na hata sasa hili la TEGETA ESCROW limekwisha zimwa. Leo serikali imeshindwa kutoa maelezo sahihi ya jambo Dogo tu kama nani? anamiliki UDA nakujua hisa zake katika shirika hilo lililogeuzwa danguro la kujitajirisha watawala. Mambo yote ninayoyaeleza hapa yasingeweza kutokea enzi zile za Mwalimu akiwa mkuu wa nchi, tukumbuke kuwa mwalimu hakuwa akisubiri mahakama ithibitishe yakuwa umekula rushwa yeye ulikuwa ukisha kudhaniwa tu kama ulitoa ama kupokea rushwa kwake ulikuwa hauwezi kupona, ni lazima hakutimue kazi na kukufilisi au la ujiudhuru mwenyewe mapema, hiyo ndiyo ilikuwa desturi ya Baba wa taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere
Wapo baadhi ya watu hadi hivi leo wanamtafsiri Mwalimu Nyerere kama Dikteta, sawa naweza nisiwapinge lakini nao watapaswa kukubaliana nami kuwa nao wajitathmini wakoje? na waliutazama udikteta wa Mwalimu kwa jicho lipi? je la utaifa ama la ubinafsi? binafsi niseme kwa mbavyo nimepata kumsikia Mwalimu Nyerere, kufuatilia kazi zake na kuyatafiti maisha yake, nimegundua na nimejiaminisha kwa kutumia dhana ya hao Mabwana wapinzani wake kuwa, Mwalimu alikuwa Dikteta mwema ( Benevolent Dictator) na ndiyo imani yangu juu ya Mwalimu na sitetereki kwenye imani hii, Mwalimu alikuwa tayari kufa kwa niaba ya taifa lake, aliakuwa tayari kufanya lolote kuakikisha misingi ya umoja na amani ya taifa letu inalindwa na kusimamiwa vyema, aliwaweka watu vizuizini alipoona watu hao kwa uwepo wao ama wao binafsi ni sehemu ambayo kama itaachwa basi umoja wetu unaweza kufa na hata kupelekea mparanganyiko katika taifa, hayo ni makosa ukiyahoji na zaidi ni dhambi ukizama katika theologia, lakini ni ushujaa mkubwa katika uzalendo wa mtu na taifa lake, Mwalimu hakuwa Malaika, hakuwa Mtume wala hakuwa Nabii, Mwalimu alikuwa Kiongozi, Mwanafalsafa na Mtabiri wa mambo yatakayotokea katika taifa lake, navunja hoja ya wale ninaowaita wapinzani wa Mwalimu kwa kusema kwamba, Mwalimu alikosea kama binadamu wengine ila makosa yake hayakuwa na athari kwa taifa lake ama athari zake ni chache na zinatetewa na ubinadamu wake.
Mwalimu amekufa akiwa masikini tofauti na watawala wengine wa Afrika, kwa nafasi yake kama angechagua kutaka kuwa tajiri basi leo tungeanza kutamka jina lake tukiweka neno "Bill" mwanzoni, Mwalimu aliwalea viongozi wa sasa bila kujua analea mafisi akizani mbuzi, aliwaita watoto wake kwa kuwalea kisiasa, lakini Mwalimu amakuja kufa akiwa hana amani hakiteswa na watoto wake aliowalea kisiasa, Mwalimu amekufa akisononeka moyo kuona taifa alilolipigania likiacha misingi ya umoja na usawa tena chini ya wale aliowaamini kwamba wangeweza kulinda maadili ya utaifa ndio hao hao waliomgeuka na kuanza kuibomoa Nchi na kuitafuna badala ya kuijenga na kusimamia misingi ile bora ambayo yeye kama mwasisi na mlezi aliiweka, Mwalimu akiwa hai alishaanza kuumizwa taratibu baada ya kuona Nchi yake inabomolewa angali yu hai, bila haya watawala wetu waliamua kuachana na mifumo ya kweli na usawa wakaua Azimio la Arusha na hatimaye kuingiza mifumo nyonyaji ya kibeberu, Mwalimu alishangaa taifa chini ya watawala aliwalea kama watoto wake wakiachana na mifumo ya usawa na uwajibikaji na kuingiza utandawazi wa kiliberali, mfumo wakinyonyaji, waziwazi wakiukaribisha ukoloni mamboleo, mfumo uliokaribisha ufisadi na wizi wa Mali za umma, na kuziacha jamii nyingi za watanzania zikilia juu ya kupokonywa ardhi yao na kupewa wawekezaji, kitu ambacho hata kwa bahati mbaya tu kisingeweza kutokea wakati ule wa Mwalimu, ukiuliza wakati ule wa mwalimu, Je? ni jamii gani iliyolia juu ya wawekezaji kuchukua mashamba yao na wao kubakia mikono mitupu? Jibu ni hakuna, Lakini leo raia wazawa wa Tanzania wanalalama kila kona kuhusu kunyang'anywa ardhi yao na kupewa wawekezeji huku serikali yao ikiongoza kuwakandamiza kwakuto kujali maslahi yao, ndio Tanzania hii ya sasa ilivyo, ndivyo raia wake wanavyopata taabu katika ardhi ya nchi yao walimo zaliwa, viongozi ndio hivyo tena wamekwisha kuwa kama "Mbwa yule Oysterbay" aliyesimuliwa na Mwalimu Nyerere huko nyuma.
Tujikumbushe kisa kile alichopata kukisimulia Mwalimu katika hotuba yake aliyopata kuitoa huko nyuma mwanzoni mwa Miaka ya 1980 katika sikukuu ya wafanyakazi yaani May Mosi pale uwanja wa taifa Dar es salaam nitanukuu, "Ndugu zangu watu wa Dari salama ebu nisikilizeni; kulikuwa na Mbwa wa wiwili, mmoja wa Manzese na mwingine wa oysterbay. ikatokea siku moja ,Mbwa Manzese akatembea hata akafika Oysterbay
kwenye moja ya nyumba za huko Oysterbay akamwona Mbwa mwenzake aliye ndani ya geti. Mbwa yule wa Manzese akasogea getini; huku akimshangaa mbwa wa Oysterbay.
Mbwa yule wa Oysterbay alinenepeana huku manyoya yake yakiwa yameteremka hadi machoni. Mbwa wa Oysterbay naye alimshangaa mwenzake wa Manzese. Mbwa yule wa Manzese alionekana kukondeana huku masikio yake yakiwa yameteremka hadi shingoni.
Mbwa wa Oysterbay kwa mshangao akamwuuliza mwenzake ; "hivi nawe ni Mbwa kama Mimi?!
"naam, miye ni Mbwa kama wewe alijibu Mbwa wa Manzese. " sasa mbona umekondeana hivyo, njoo humu ndani kwa bwana wangu nawe uwe kama Mimi " Mbwa wa Manzese akajibu; "lakini wewe umefungiwa, mwenzio niko huru"
kwenye moja ya nyumba za huko Oysterbay akamwona Mbwa mwenzake aliye ndani ya geti. Mbwa yule wa Manzese akasogea getini; huku akimshangaa mbwa wa Oysterbay.
Mbwa yule wa Oysterbay alinenepeana huku manyoya yake yakiwa yameteremka hadi machoni. Mbwa wa Oysterbay naye alimshangaa mwenzake wa Manzese. Mbwa yule wa Manzese alionekana kukondeana huku masikio yake yakiwa yameteremka hadi shingoni.
Mbwa wa Oysterbay kwa mshangao akamwuuliza mwenzake ; "hivi nawe ni Mbwa kama Mimi?!
"naam, miye ni Mbwa kama wewe alijibu Mbwa wa Manzese. " sasa mbona umekondeana hivyo, njoo humu ndani kwa bwana wangu nawe uwe kama Mimi " Mbwa wa Manzese akajibu; "lakini wewe umefungiwa, mwenzio niko huru"
Nimejifunza jambo moja kubwa sana kupitia kisa hiki na ninaamini pia kila mtu atakifikiria zaidi na mwisho kitampa picha akifananisha na maisha na hali ya sasa ya nchi yetu na hata nitaungwa mkono kwa kuwafananisha watawala wetu wasasa na yule dog wa Oysterbay.
Sing'ati ng'ati maneno wala sisemei pembeni, ni lazima niwe wazi hapa, ingawa Mwalimu alikuwa akitoa mfano ule siku ile ya Mei Mosi katika Miaka ile ya 1980 akiwafariji wafanyakazi waliokuwa wakilalama juu ya hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na Serikali yake kukataa kufuata zile sera za shirika la fedha la Dunia ( IMF ) na Benki ya dunia ( WB ) zilizowataka Nchi za kiafrika kufuata sera walizoiweka ili wapate kusaidiwa ni wakati huo ambapo hali ya uchumi kwa nchi nyingi za kiafrika zilikuwa mahututi. Mwalimu na serikali yake walikataa kufuata Sera zile na hata kupelekea Nchi kukumbwa na misukosuko na vikwazo kutoka kwa wakubwa wa dunia, Mwalimu aliutaka uhuru, Uhuru kama ule aliokuwa nao Mbwa wa manzese, hakutaka nchi yake na wananchi wake wana Watanzania waishi maisha kama aliyokuwa nayo Mbwa yule Oysterbay, yaani kupata misaada kutoka kwa wakubwa wa dunia ili hawadidimize wananchi wake, Mwalimu hakutaka hata kwa bahati mbaya tu aonekane kama msaliti wa Nchi yake na Sera zake za ujamaa na kujitegemea, ni wazi kuwa Mwalimu hakupenda kuwa mtumwa tena.
Kwa watawala wa leo dhana ya Mwalimu inaonekana kwao kama ni dhana ya kizamani zana ya kijima, wao wamekuwa tayari kuwauza wananchi wao na utaifa wao, wamekuwa wakiyafuata yale ya wakubwa wa dunia bila hofu wala haya wamediriki hata kupambana na wenzao wa Afrika kwa pendezo la watu wanene wa dunia, watawala wetu wamekuwa washinda huko kwa wanene eti wakidai wanakwenda kuemea na wakirudi wanarudi na kibaba, hayo ndio maneno ya watawala wetu, maneno yanayonipa jeuri ya kusema kuwa ama kweli akili zinazotuongoza ni ndogo na za ovyo kabisa, najiridhisha kusema hivyo kwa kuwa maneno hayo yalitoka kinywani mwa bwana mkubwa mwenyewe (head, sovereign) hii ni ithibati tosha kwangu na kwenu kuamini kuwa watawala wetu kweli wamatuchagulia maisha ya yule mbwa wa Oysterbay na kutuaminisha kuwa ndiyo maisha salama.
Nikiacha nyakati hizo za kukua kwangu na chereko chereko za kuukaribisha mfumo mzuri kwa watawala wetu yaani kuingia kwa ubinafsishaji, wacha sasa tutazame matokeo yake katika Serikali hii na watawala wetu wa awamu hii ya nne, ni ubinafsishaji ule uliokuja kwa shangwe ukipigiwa ving'ora ndio uliodhalisha tatizo sugu hivi leo tatizo la UFISADI, leo Watanzania tunalia na watawala wetu kutajirika kuliko kiwango cha kawaida tuliona wale wengine waliokutwa na mabilioni huko nje ati wakiyaita vijisenti (Mungu umeziona kufuru hizi), Watawala wamekuwa madalali wa rasilimali zetu, Watanzania tunalia tukijiuliza je? angekuwepo Mwalimu yangewezekana haya? je wakati wa Mwalimu watawala wetu hawa wa leo wangeweza kunusulika na vile viboko kumi na viwili vya wala rushwa? majibu tunayo.
Nihitimishe makala yangu kwa kutoa msimamo wangu kwamba, Mwalimu Nyerere alikuwa mzalendo wa taifa letu hakuwa muhuni, hakuwa fisadi mwalimu alikuwa mwanafalsafa, mwalimu kitaaluma, kiongozi (alionyesha njia), mwandishi na mwanafasihi mahiri, mpatanishi na mlinzi wa utaifa wetu, wanaomwita mwalimu Nyerere dikteta narudia tena kuwa siwapingi hata kidogo lakini niwaombe tu waweke wazi udikteta huo ni udikteta wa namna ipi? kama nilivyokubaliana nao nami nitapenda wakubaliane nami kuwa Mwalimu hakuwa Adolf Hitler , hakuwa Mabutu Seseseko wala mwalimu hakuwa Benito Mussolin hata kwa makosa tu mwalimu hauwezi kumfananisha na Idd amin Dadau wa Uganda, kwahiyo mwalimu akuwa Dikteta katili ( Ruthless tyrant ). Basi na kwavile hamuwezi kuondoa neno dikteta kwa Mwalimu Nyerere basi na itoshe kusema kuwa mwalimu alikuwa Dikteta mwema ( Benevolent dictator ) kama nilivyoeeleza hapo juu, kwakweli na tukubali kuwa Tanzania ya mwalimu Julias kambarage Nyerere si Tanzania hii ya sása.
Na pengine ni malize makala yangu kwa kusema kuwa tunaitaji Nyerere mwingine, tunaitaji Dikteta mwema mwingine atakaye kuwa tayari kuwashughurikia watawala wa aina hii tulionao leo, tunaitaji Nyerere mwingine atakaye kuja kutupa majibu ya hali ngumu tulizo nazo, tunaitaji uvumilivu na umakini ili kuweza kumpata.
Mungu ibariki Tanzania mungu ibariki Afrika, Mungu ilaze mahala pema peponi roho ya Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Burito Nyerere.
[SUP]MZALENDO91[/SUP]
[SUP]
[/SUP][SUP]0653947211[/SUP]