Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,483
Mh Frederick Sumaye
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye (63), amesema hatua ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuzuia wanachama wake wanaotaka kuwania urais kujitangaza mapema ina madhara zaidi kuliko faida. Akizungumza katika kipindi cha televisheni cha Dakika 45 kilichorushwa na ITV juzi usiku, Sumaye alisema wagombea wakijulikana mapema ni faida kwa wananchi maana watapata nafasi ya kuwachambua ili wakati ukifika, wafanye uchaguzi sahihi wa wanayemtaka.
"Hivi karibuni, kuna baadhi ya vyombo vilimkariri Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akiwaambia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), kwamba ni ruksa kwa wanaotaka urais kuanza kujipitisha kwa wanachama. Kwa kweli nilifurahi sana niliposoma. "Hata hivyo, kesho yake Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, alizungumza na waandishi wa habari na akasema mwanachama atakayeanza kujipitisha au kufanya kampeni kabla ya wakati atafukuzwa chamani.
"Kwa bahati mbaya sikuwepo kwenye mkutano ule wa NEC na hivyo sasa sijui nani anasema kweli kati ya Nape na magazeti yaliyoandika. "Hata hivyo, mtazamo wangu mimi ni kwamba ni kheri chama kikaruhusu watu wajitangaze kama wanataka urais. Waambiwe tu kwamba wajitangaze halafu wakae kimya na wasivuruge chama.
"Hii itatoa fursa kwa wananchi kuanza kudadisi kuhusu watu hao. Wakati wa uchaguzi ukifika, watu wanakuwa wanamfahamu kila mgombea kiundani na hivyo hata uchaguzi unafanyika katika mazingira ambayo watu wanafahamu wanachagua nini," alisema Sumaye. Alisema utaratibu wa sasa unaleta matatizo kwa vile inabidi watu wafanye mambo yao kwa siri na mambo mengi yanayofanyika kwa siri huwa na matatizo. Pia alisema mfumo unawanyima fursa wananchi kuwajua wagombea wao.
"CCM kwa mfano kinachagua mgombea wake kwenye mwezi Mei hivi. Uchaguzi ni miezi mitano baadaye na hivyo watu wanakuwa na miezi sita tu kumjua mgombea. Hii si vema kabisa," alisema. Jina la Sumaye limekuwa likitajwa miongoni mwa wale wanaotarajiwa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ingawa katika mahojiano hayo hakukubali wala kukana kuhusu hilo alipoulizwa na mwendesha kipindi, Ibrahim Semunyu.
Kuhusu rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania ambayo imetolewa mwezi huu, Sumaye alikuwa na machache ya kueleza kuhusu masuala ya mgombea binafsi na serikali tatu. Akizungumzia mgombea binafsi, Sumaye alisema anaunga mkono suala hilo kwa vile litatoa fursa ya kugombea kwa watu ambao hawatakuwa wakitendewa haki kwenye vyama vyao.
Alisema hadhani kama kuna uwezekano wa mgombea urais binafsi kushinda urais hapa nchini lakini kuna uwezekano mkubwa kwenye nafasi za ubunge na udiwani. "Kuna watu walikuwa wanawania ubunge na udiwani kwenye vyama vyao wakakataliwa lakini walipoenda vyama vingine wakashinda. Hii maana yake ni kwamba wapiga kura waliwachagua wao na si vyama vyao," alisema.
Kuhusu serikali tatu, Sumaye alitabiri kwamba kutakuwa na mvutano mkubwa baina ya rais wa Tanzania na wa Tanganyika kuliko ule wa sasa baina ya wa Muungano na wa Zanzibar.
Alisema ingawa suala la serikali tatu halikwepeki kwa sasa, ni muhimu kwa baadhi ya mambo kufahamika mapema ili isij e kuibuka mivutano isiyo na sababu chini ya mfumo wa serikali tatu. "Kijiografia, Zanzibar iko mbali na Tanganyika. Ni kisiwa kile. Lakini rais wa Tanganyika na mwenzake wa Tanzania watakuwa wapo ndani ya eneo moja (kama makao ya rais wa Jamhuri ya Muungano yatakuwa Dar es Salaam). (Hiyo ni sawa na) kuwa na marais wawili ndani ya nchi moja. Hili si suala dogo hata kidogo," alisema.
Alisema pia kwamba kuna suala la gharama kubwa za kuendesha serikali tatu ambapo itabidi sasa wananchi wagharamie serikali tatu badala ya mbili za sasa.
Katika mahojiano hayo, Sumaye pia alizungumzia mapendekezo ya kwenye rasimu yanayotaka makamu wa rais kuchukua nafasi ya urais ikitokea rais aliyechaguliwa akafariki au kupoteza sifa za kuwa rais. "Hili naona ni pendekezo la hatari kidogo. Wakati watu wanakwenda kuchagua rais, hawachagui makamu. Wanamchagua rais. Kama akifariki, ni lazima tu uitishwe uchaguzi mwingine.
"Utaratibu unaopendekezwa una hatari sana. Kama makamu wa rais atakuwa na nia ya urais anaweza kufanya taratibu za kumwondoa ili yeye achukue nafasi. Inawezekana yeye asiwe na nia hiyo lakini wapambe wake wakijua kwamba watafaidika zaidi iwapo mtu wao atakuwa rais," wanaweza kufanya hivyo, alisema
- See more at: Raia Mwema - Sumaye aikosoa CCM