Story: True Love

Ok9

JF-Expert Member
Joined
Oct 5, 2013
Posts
4,554
Reaction score
4,171
Monrovia, Liberia "Natangaza hali ya hatari , nchi yetu imekumbwa na balaa kubwa. Sote tutakuwa mashahidi wa jinsi ndugu zetu wa karibu, familia zetu , watu tunaowapenda na majirani zetu wanavyozidi kupukutika kutokana na ugonjwa huu wa ajabu uliotukumba .

"Natangaza hali ya hatari, watu wasiruhusiwe kutoka au kuingia kienyeji ndani ya mipaka ya nchi yetu bila kupimwa. Kwa wale watakaothibitika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huu, haraka wapelekwe kwenye vituo maalum vilivyotengwa kwa ajili ya kazi hii.

"Pia nichukue fursa hii kuwapongeza wa hudumu wa afya, manesi na madaktari wa nchi nzima ambao mmejitolea kadiri ya uwezo wetu , mkiyaweka maisha yenu hatarini kwa ajili ya kupigania maisha ya wengine kama mlivyokula kiapo.

"Serikali inafanya kila kinachowezekana kuhakikisha mnapatiwa vifaa vya kujikinga ili msipate maambukizi kama ilivyotokea kwa baadhi ya wenzenu . " Nayatangaza maeneo ya Mji wa Dolo , Bomi , Bong, Grand Bassa, Grand Cape Mount, Lofa, Margibi, Montserrado, Nimba, Mto Cess na jiji lote la Monrovia kuwa chini ya karantini maalum.

"Wanausalama wote fanyeni kazi yenu kwa kushirikiana na watumishi wa wizara ya afya kuhakikisha hakuna anayeingia wala kutoka kwenye maeneo niliyoyataja, " Rais wa Liberia , Hellen Joseph, mwanamke wa kwanza kuiongoza nchi hiyo katika historia, alikuwa akilihutubia taifa katika hotuba ya dharura kufuatia kuibuka kwa ugonjwa hatari wa Ebola uliolitingisha vibaya taifa hilo.

Kila mtu alikuwa kimya , wengine wakiwa kando ya redio zao, wengine pembeni ya televisheni zao wote wakisikiliza hotuba hiyo kutoka kwa rais wao aliyekuwa akihutubia kupitia Shirika la Utangazaji la Liberia ( Liberia Broacasting System ). Utekelezaji wa alichokiagiza ukaanza kufanyika haraka ambapo miji yote iliyotajwa iliwekwa kwenye karantini , ikiwepo makao makuu ya nchi hiyo, Monrovia.

Ikawa hakuna mtu aliyekuwa anaruhusiwa kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine bila kuwa na sababu ya msingi . Hata wale waliokuwa na ulazima wa kusafiri kuingia au kutoka kwenye maeneo yaliyowekewa karantini, walikuwa wakipimwa afya zao kabla ya kuruhusiwa kusafiri.

Licha ya tahadhari kubwa zilizokuwa zinachukuliwa na serikali kupitia wizara ya afya na taasisi nyingine , bado kasi ya maambukizi ilizidi kushika kasi katika nchi hiyo iliyopo Afrika Magharibi. Mamia ya watu wakawa wanaambukizwa kila kukicha na kukimbizwa kwenye vituo maalum ambavyo vilitengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Wahudumu wa afya waliokuwa wakivaa mavazi maalum yaliyofunika miili yao yote , kuanzia juu hadi chini , waliendelea kufanya kazi usiku na mchana huku wengine wakipita kwenye makazi ya wananchi na kuwaeleza dalili za ugonjwa huo na namna ya kujikinga.

Taasisi ya Planet Link Health Care iliyokuwa na makao makuu yake nchini Marekani katika Jiji la California , Texas , nayo ilituma wataalamu wake nchini Liberia kwa ajili ya kwenda kuwaelimisha wananchi juu ya maana ya ugonjwa huo, dalili zake, jinsi unavyoambukizwa na namna ya kuuzuia.

"Ugonjwa huu unasambazwa na virusi viitwavyo Ebola Virus ambavyo husambazwa kwa kugusa mwili wa mgonjwa , damu , mate au majimaji ya mwilini, zikiwemo mbegu za kiume. "Kwa mara ya kwanza, ugonjwa huu uligundulika kwenye miili ya sokwe na popo waliokuwa wakipatikana kandokando la Mto Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan mwaka 1976 na ukahamia kwa binadamu ambako umeendelea kusambaa kwa kasi kubwa mpaka kufika hapa nchini Liberia.

"Dalili kuu za ugonjwa huu ni homa kali ya ghafla, maumivu makali ya kichwa, kutokwa damu kwenye viungo mbalimbali vya mwili , kutapika , kuhara na mwili kukosa nguvu na dalili hizo huanza kuonekana siku mbili baada ya mtu kuambukizwa. Asipopata tiba ya haraka, hufa ndani ya saa zisizozidi sita.

"Ukiigusa maiti ya mtu aliyekufa kwa Ebola au kuikaribia, nawe utaambukizwa ndani ya muda mfupi . Wagonjwa wa Ebola ni lazima watengwe ili wasiwaambukize wenzao na ni makosa makubwa kumgusa mgonjwa wa Ebola kwani lazima nawe utaambukizwa.

"Dalili za mwishomwisho kabla ya mgonjwa wa Ebola kufa ni kutapika damu, kukohoa makohozi yenye damu na kuharisha damu. Pia kutokwa na damu puani , mdomoni na masikioni. "Ni lazima maiti za watu waliokufa kwa Ebola zizikwe na wataalamu wa afya kwa kuzingatia kanuni maalum ikiwemo kuchimba kaburi refu na kumwagia madawa ya kutosha kwenye makaburi, " wataalamu wawili wa shirika la Planet Link Health Care, walikuwa wakitoa semina maalum kwa wananchi, kupitia redio na televisheni ya taifa.

Hata hivyo, elimu hiyo muhimu ilikuja kwa kuchelewa kwani tayari kasi ya maambukizi ya Ebola ilikuwa imepamba moto, vituo vilivyotengwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hao vilionekana kuzidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa, hali ikazidi kuwa tete. Ilibidi hospitali zote kubwa jijini Monrovia, nazo zianze kutoa huduma kwa wagonjwa wa Ebola.

Hospitali za John F. Kennedy Medical Center , Eternal Love Winning Africa , Redemption , St. Joseph' s Catholic , Seven Days Adventist, MSF Pediatric , E. S. Grant Mental Health, A. M. E. University Clinic na nyingine nyingi zote zilifurika wagonjwa wa Ebola.

Licha ya jitihada za madaktari na manesi , bado hali ilizidi kuwa tete , wagonjwa wakazidi kufa na kibaya zaidi, hata madaktari waliokuwa wakiwahudumia , nao walianza kuambukizwa ugonjwa huo hatari ambao mpaka muda huo, haukuwa na tiba ya uhakika . Kitendo cha madaktari kuanza kuugua na kufa, kilizidi kuifanya kazi iwe ngumu kwani wengine waliogopa na kuanza kukimbia mmoja baada ya mwingine kuokoa maisha yao.

Madaktari wachache ambao kweli walikuwa wakizingatia weledi wa kazi zao, wao waliendelea na kazi . ataifa ya kigeni ambayo yalikuwa na raia wao kwenye nchi hiyo, nayo yalianza kuwahamisha na kuwarudisha makwao baada ya kuwapima na kuthibitika kwamba hawakuwa na ugonjwa huo.

Ofisi za mabalozi wa nchi zote zikafungwa na kila mtu akaja kuchukuliwa na nchi yake kurudishwa nyumbani kwao. Siku tano baadaye tangu rais alipotangaza hali ya hatari , vifo vya wagonjwa wa Ebola vilikuwa vimeongezeka zaidi ya mara kumi ukilinganisha na awali, maiti nyingi zikawa zinazagaa mitaani na kusababisha Jiji la Monrovia na vitongoji vyake kutawaliwa na harufu za wafu.

Licha ya maagizo ya serikali kuwazuia watu kutotoka wala kuingia kwenye maeneo yaliyokuwa chini ya karantini, maelfu ya watu waliyakimbia makazi yao wakihofia kufa na ugonjwa huo , mitaa ikabaki kimya kabisa. Kelele pekee zilizokuwa zinasikika , zilikuwa ni za mbwa waliokuwa wakifaidi mizoga ya binadamu waliokufa kwa ugonjwa huo wa Ebola.

"Baby, go back to Sangabuye , please go baby!" ( Mpenzi , tafadhali rudi Sangabuye , tafadhali nenda mpenzi )"I ' m not going anywhere, if you want me to leave , we must go together otherwise let me die with you. " ( Siendi popote, kama unataka niondoke lazima tuondoke pamoja vinginevyo niache nife na wewe )"But baby, you know I ' m a doctor and I ' m devoted to my career, I can ' t leave here and let my patients die helpless . ( Lakini mpenzi , unajua kwamba mimi ni daktari ambaye nimejitolea maisha yangu yote kwa ajili ya kazi yangu, siwezi kuondoka na kuwaacha wagonjwa wangu wakifa bila msaada).

Watu wawili walikuwa wakibishana kutoka ndani ya nyumba moja iliyokuwa katikati ya Jiji la Monrovia. Mazungumzo yao yaliendelea kwa muda mrefu lakini muafaka haukufikiwa, licha ya mwanaume kumsisitiza mpenzi wake huyo aondoke ili asije akaambukizwa ugonjwa huo hatari, mwanamke hakuwa tayari.

Akawa anamng ' ang ' ania waondoke pamoja ili kama ni kunusurika, wanusurike wote kuliko kuondoka peke yake kwani alikuwa anajua nini kingetokea endapo angeondoka na kumuacha mpenzi wake huyo ambaye walikuwa kwenye hatua za mwisho za kufunga ndoa kabla ya kulipuka kwa ugonjwa huo

Je, nini kitafuatia?
 
Ugonjwa wa kutisha usio na tiba wala kinga, Ebola umeikumba nchi ya Liberia na kusababisha maafa makubwa . Hali ya hatari inatangazwa nchi nzima ambapo maeneo yaliyoathirika sana yanawekwa chini ya karantini maalum, watu wakizuiwa kuingia au kutoka bila kuwa na sababu maalum.

Licha ya serikali iliyokuwa inaongozwa na rais mwanamke, mwanamama shupavu mwenye moyo wa kipekee, Hellen Joseph, kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kupambana na ugonjwa huo, kazi inakuwa ngumu na mamia ya watu wanaendelea kupoteza maisha na kuambukizwa ugonjwa huo hatari .

Hali inazidi kuwa tete kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele, maiti nyingi za watu waliokufa kwa ugonjwa huo zinatapakaa mitaani huku maelfu ya wakazi wakiyakimbia makazi yao wakiogopa kuambukizwa ugonjwa huo hatari. Jiji la Monrovia linabaki kuwa kimya kabisa huku harufu za maiti zikizidi kuifanya hali kuwa ya kutisha mno.

Mitaa yote inakuwa kimya kabisa , kelele pekee zinazosikika ni za mbwa wanaogombea mizoga ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo . Ndani ya nyumba moja, watu wawili waliokuwa wapenzi wanasikika wakibishana. Mwanaume anamtaka mpenzi wake aondoke na kurudi nchini kwao, Sangabuye ili asije akaambukizwa ugonjwa huo lakini mwanamke anakataa akitaka waondoke pamoja au wabaki wote na kufa pamoja.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO… Tafadhali mpenzi wangu , naomba unielewe Rafiki, rudi nyumbani mpenzi wangu , mimi nikimaliza tu kazi nitakuja. " "Hapana Lawrence, siwezi kuondoka na kukuacha . Ni juzi tu tumesherehekea pamoja Sikukuu ya Krismasi hapa Monrovia kabla Ebola haijalipuka, leo unataka niondoke na kukuacha peke yako ? Umesahau nini kipo mbele yetu ?"

"Sijasahau Rafiki mpenzi wangu , najua siku chache baadaye tutafunga ndoa na kuwa mume na mke halali baada ya kusubiri kwa muda mrefu lakini hii kazi ninayoifanya ni muhimu sana. " " Unataka kusema kutibu wagonjwa wa Ebola ni muhimu kuliko mimi na wewe kufunga ndoa? Lawrence mpenzi wangu, zimebaki wiki mbili tu kabla hatujafunga ndoa leo unataka niondoke na kukuacha. Ukifa je?" "Siwezi kufa Rafiki mpenzi wangu , nitajitahidi kuwa makini . " "Huwezi kufa? Umeshuhudia mpaka sasa madaktari wangapi wamekufa? Kwani wao hawakuwa makini?" "Hapana Rafiki, nakuomba tafadhali nielewe, rudi nyumbani mimi nitakuja siku chache zijazo.

Ndugu zako , familia yako na watu wote watanichukia sana endapo utapatwa na Ebola kwani watajua mimi ndiyo chanzo kwa sababu wanajua umenifuata mimi huku Liberia . " "Kumbe hunipendi Lawrence , nimegundua kwamba nalazimisha mapenzi kwako wala hunipendi, " alisema msichana huyo huku akianza kuangua kilio kama mtu aliyepokea taarifa za msiba.

Lawrence akasimama dirishani na kutazama nje, maiti nyingi za wagonjwa wa Ebola zikiwa zimezagaa kila sehemu na kuifanya hali iwe ya kutisha mno . Akamgeukia Rafiki aliyekuwa amekaa kwenye kochi dogo, akiendelea kulia kwa kwikwi kiasi cha kuufanya uso wake ubadilike rangi na kuwa mwekundu. Akajikuta akibaki njia panda, akishindwa kuamua nini cha kufanya.

Kutokana na hali mbaya iliyokuwa inaendelea kulitingisha taifa la Liberia , Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa ( WHO) ilibidi liingilie kati kwa kutangaza hali ya hatari duniani kote kwamba watu hawatakiwi kabisa kuvuka mipaka ya Liberia na kuingia kwenye nchi hiyo kwa sababu ya ugonjwa huo . Safari zote za ndege zilizokuwa zikiingia kwenye nchi hiyo zilifutwa mara moja na kuwaacha mamia ya abiria wakisuasua kwenye viwanja mbalimbali vya ndege.

Shirika hilo pia lilituma timu ya madaktari wake wengi waliokuwa na vifaa vya kisasa zaidi vya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwenda kutoa msaada kwa madaktari wa Liberia walioonesha kuzidiwa na kazi hiyo. Ndege maalum zikasafiri zikiwa na madaktari, vifaa, madawa na vitu vyote muhimu kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo na baada ya kusafiri kwa saa nyingi angani, hatimaye zilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Roberts International Airport ( Zamani Robertsfield ). Madaktari hao walipokelewa na wenzao wa Liberia na kupelekwa moja kwa moja mpaka kwenye Hospitali Kuu ya Monrovia ( JFK) ambayo ndiyo ilikuwa kambi kubwa ya madaktari waliokuwa wakihaha kupambana na Ebola na muda mfupi baadaye, walianza kazi ya kuhakikisha wanapambana na Ebola.

Jamhuri ya Sangabuye , ilikuwa miongoni mwa nchi zilizokuwa zikipatikana katika Ukanda wa Afrika Mashariki , ikipakana na nchi za Rwanda , Burundi, Kenya, Zambia na Malawi huku upande wa Mashariki, ikiwa imepakana na Bahari ya Hindi.

Baada ya kudumu kwenye siasa za chama kimoja kwa kipindi kirefu, huku rais wake akisimamia mfumo wa ujamaa ambao ulikuwa ukipingwa na watu wengi, nchi hiyo ilijikuta ikiingia kwenye machafuko makubwa baada ya watu waliokuwa wanapinga mfumo wa ujamaa kuanza kuizidi nguvu serikali.

Martin Wela alikuwa ni mwanaharakati ambaye kwa kipindi kirefu alikuwa adui namba moja wa serikali iliyokuwa madarakani kutokana na msimamo wake wa kumtaka rais kuachana na mfumo huo kwani haukuwa na tija yoyote. Badala yake, Martin Wela alishauri utumike mfumo wa kibepari ili kuleta maendeleo ya haraka na kuwakomboa wananchi wa Sangabuye waliokuwa wanateseka na umaskini uliokithiri.

Misimamo yake ilimfanya kujulikana sana ndani na nje ya nchi huku wananchi wengi wa Sangabuye wakimuunga mkono na kumuona kama mkombozi wao wa kweli . Hata wakati vurugu za kuukataa mfumo wa ujamaa zilipopamba moto, Martin Wela ambaye alikuwa akiishi uhamishoni kutokana na hofu ya kuuawa na wafuasi wa rais wa nchi hiyo, alikuwa akitajwa na wananchi wengi kwamba ndiye anayefaa kuingia madarakani kuiongoza nchi hiyo.

Vurugu zilipozidi, Jeshi la Wananchi wa Sangabuye liliamua kuchukua nchi kwani serikali iliyokuwepo, ilionekana kushindwa kabisa kukabiliana na wananchi wake.

Kwa kuwa hata viongozi wa juu wa jeshi walikuwa wakimfahamu vizuri Martin Wela na kukubaliana na harakati zake, walikubaliana kwamba ndiyo apewe jukumu la kuiongoza nchi kwa usaidizi wa karibu wa jeshi hilo. Martin aliyekuwa mafichoni nchini Rwanda, akafuatwa na maafisa wa jeshi hilo na kurudishwa mpaka Sangabuye ambapo siku mbili baadaye, alitangazwa na jeshi kuwa rais mpya wa nchi hiyo mpaka uchaguzi wa kidemokrasia utakapoitishwa.

Wananchi wengi waliipokea taarifa hiyo kwa shangwe kubwa, vigelegele na shangwe za kila aina zikawa zinasikika kila sehemu ya nchi hiyo huku kila mmoja akiwa na imani kubwa juu ya rais huyo mpya ambaye licha ya umri wake mdogo wa miaka 26 tu, alionekana kuwa na busara za hali ya juu.

Rais huyo mpya akavunja rekodi ya kuwa rais mdogo zaidi duniani, huku akipewa jukumu kubwa la kuipitisha nchi hiyo katika mageuzi makubwa ya kiitikadi kutoka ujamaa hadi ubepari na kisiasa kutoka kwenye mfumo wa chama kimoja hadi wa vyama vingi ambao ulionekana kuwa kielelezo cha demokrasia ya kweli.

Martin Wela aliyaanza maisha mapya akiwa rais wa nchi hiyo , baada ya kuwa amehangaika kwa kipindi kirefu, akikamatwa , kuteswa na kupigwa na polisi, akitishiwa kuuawa na kujeruhiwa kwa risasi mara kadhaa mpaka alipofikia hatua ya kukimbilia uhamishoni. "Ili uiongoze nchi vizuri, ni lazima uwe na mke mheshimiwa rais, " mshauri mkuu wa rais, Alfred Msole alimwambia rais siku chache baada ya kuapishwa kuiongoza nchi hiyo, wazo ambalo hata yeye alilikubali haraka kwani tayari alikuwa na mchumba wake wa siku nyingi, waliyekutana wakiwa masomoni.

Sophia Marcel , mwanamke mrembo kuliko wote nchini Sangabuye, aliyekutana na Martin Wela wakiwa masomoni nchini Uingereza ndiye aliyekuwa chaguo la rais huyo kijana kuliko wote.

Kwa kuwa naye alikuwa mafichoni kwa kipindi chote hicho pamoja na mchumba wake huyo , taratibu za kumfuata nchini Rwanda zilifanyika haraka na siku chache baadaye , akaletwa ikulu. Harakaharaka mipango ya harusi ikaanza kupangwa huku uzuri wa mwanamke huyo , ukiwa gumzo kubwa miongoni mwa wananchi wa Sangabuye.

"Anastahili kabisa kuwa mke wa rais, unamuona jinsi alivyo mzuri ! Mtoto mrefu kama twiga , mtazame alivyoumbika vizuri sehemu za nyuma na kifuani , dah ! Kweli rais wetu anajua kuchagua, " vijana wawili waliokuwa wakifuatilia habari juu ya ndoa hiyo kwenye runinga, walikuwa wakijadiliana na kucheka kwa furaha . Mipango ilizidi kupamba moto , kwa jinsi rais huyo alivyokuwa akipendwa na wanachi wake , wengi walijitokeza kumuunga mkono kwa hali na mali kuhakikisha harusi hiyo inakuwa ya kihistoria.

Hatimaye maandalizi yote yalikamilika na kilichokuwa kikisubiriwa, ilikuwa ni siku ya tukio kufika . Kila mtu akawa na shauku kubwa ya kumuona rais mpya, Martin Wela akimvalisha pete mwanamke mrembo kuliko wote, Sophia Marcel.

Je, nini kitafuatia?
 
Ebola, ugonjwa usio na tiba wala kinga umeikumba nchi ya Liberia na kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wake. Watu wengi wanaambukizwa ugonjwa huo na ndani ya muda mfupi tu, mamia ya wananchi wanapoteza maisha. Hali ya hatari inatangazwa nchi nzima ambapo maeneo yaliyoathirika zaidi yanawekwa chini ya karantini maalum, watu wakizuiwa kuingia au kutoka bila kuwa na sababu maalum.

Licha ya serikali iliyokuwa inaongozwa na rais mwanamke, mwanamama shupavu mwenye moyo wa kipekee , Hellen Joseph, kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kupambana na ugonjwa huo, kazi inakuwa ngumu na maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha na kuambukizwa ugonjwa huo hatari. Hali inazidi kuwa tete kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele , maiti nyingi za watu waliokufa kwa ugonjwa huo zinatapakaa mitaani huku maelfu ya wakazi wakiyakimbia makazi yao wakiogopa kuambukizwa ugonjwa huo hatari.

Jiji la Monrovia linabaki kuwa kimya kabisa huku harufu za maiti zikizidi kuifanya hali kuwa ya kutisha mno. Mitaa yote inakuwa kimya kabisa , kelele pekee zinazosikika ni za mbwa wanaogombea mizoga ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo. Ndani ya nyumba moja, watu wawili waliokuwa wapenzi wanasikika wakibishana.

Mwanaume anamtaka mpenzi wake aondoke na kurudi nchini kwao, Sangabuye ili asije akaambukizwa ugonjwa huo lakini mwanamke anakataa akitaka waondoke pamoja au wabaki wote na kufa pamoja. Upande wa pili, historia ya nchi ya Sangabuye inamulikwa ambapo Rais Martin Wela anaingia madarakani baada ya serikali iliyokuwepo kupinduliwa.

Kwa kuwa Martin alikuwa bado hajaoa , anapewa ushauri wa kutafuta mke na kura yake inamuangukia mpenzi wake wa siku nyingi, Sophia Marcel . Mipango ya ndoa inaanza kufanyika. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO.

Maandalizi yote muhimu kuelekea kwenye ndoa ya kipekee kati ya Rais Mteule wa Sangabuye, Martin Wela na mwanamke mrembo kuliko wote, mrefu kama twiga, aliyejaaliwa umbo lenye mvuto wa aina yake, Sophia Marcel, yalizidi kupamba moto. "Siamini kama unaenda kuwa mume wangu Martin, siamini, " Sophia alimwambia mpenzi wake huyo wa muda mrefu waliyedumu pamoja kwenye shida na raha mpaka kufikia hatua ya kutorokea mafichoni wakikwepa kukamatwa na serikali kutokana na itikadi za kiuanaharakati alizokuwa nazo Martin.

"Wewe ndiyo mwanamke wa maisha yangu , umenivumilia kwa muda mrefu sana Sophy , nakupenda sana na naahidi kukupenda maisha yangu yote , " alisema Rais Martin na kumbusu Sophia kwenye shavu lake, akamkumbatia kimahaba, jioni ya siku moja kabla ya ndoa yao iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa. "Kwa hiyo na mimi nitakuwa first lady? Na mimi nitakuwa naishi ikulu?" "Ndiyo Sophy, kama uliweza kuishi na mimi uhamishoni kwa nini isiwezekane kuishi ikulu? Huu ni wakati wetu wa kuwatumikia watu wa Sangabuye na kurejesha imani yao kwa serikali, naamini utakuwa mshauri mzuri kwangu kama ambavyo siku zote umekuwa .

"Ahsante sana mpenzi wangu , nitakupenda daima Martin, " alisema Sophy kisha wakakumbatiana tena . Waliendelea kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu maisha yao ya baadaye, wakiwa wamekaa kwenye viunga vya ikulu, kila mmoja akionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya moyo wake .

Hatimaye siku ya harusi iliwadia , viunga vyote vya ikulu kuanzia kwenye bustani za nje mpaka ndani kukapambwa na wapambaji maalum waliokodiwa maalum kwa ajili ya kazi hiyo na kuifanya Ikulu ya Sangabuye kubadilika mno.

Wageni wengi maarufu walialikwa , wakiwemo marais wa nchi jirani , viongozi wa juu wa taasisi mbalimbali za kimataifa , viongozi wa majeshi ya nchi mbalimbali na vigogo wengi kutoka ndani na nje ya nchi.

Hatimaye Martin akafunga ndoa ya kifahari iliyohudhuriwa na wageni wengi mashuhuri na kuweka historia ya kipekee katika historia ya maisha yake. Kutokana na jinsi alivyokuwa akikubalika miongoni mwa wananchi wa Sangabuye, ndoa hiyo ilivuma mno . Kila redio , runinga, magazeti na mitandao vikawa vinaripoti tukio hilo huku watu wengi wakikata vipande vya magazeti vilivyokuwa na picha za maharusi hao na kubandika kwenye vyumba vyao kama kumbukumbu.

Furaha kubwa zaidi ilikuwa kwa Martin mwenyewe na mkewe mpya , Sophia ambao kwa pamoja walionesha kuwa na raha za ajabu ndani ya mioyo yao kwani ndoa hiyo waliisubiri kwa kipindi kirefu na sasa hatimaye ilikuwa imetimia. Baada tu ya ndoa kuisha , Rais Martin na mkewe walisafiri kwa ndege maalum mpaka Comoro walikokaa kwa siku saba wakila fungate.

Waliporudi , kila mmoja alikuwa mpya kabisa , wakiwa mume na mke halali . "Sasa umekamilika mheshimiwa rais, unaweza kuendelea na majukumu yako kama kawaida, " mshauri wa rais alimwambia bosi wake wakiwa kwenye ofisi yake, siku moja tangu arejee kutoka fungate . Wote wakacheka na kugongesheana mikono kwani mshauri huyo ndiye aliyempa wazo la kufunga ndoa kabla hajaanza rasmi kazi ya kuiongoza Sangabuye.

Siku hiyo ilipita, Rais Martin akaendelea kufanya kazi kwa juhudi kubwa kuhakikisha anaiongoza vyema nchi hiyo . Mageuzi makubwa yakaanza kufanyika ambapo mfumo wa ujamaa ambao ndiyo uliokuwa ukitumika kwa kipindi kirefu tangu nchi hiyo ilipopata uhuru, ulianza kufutwa hatua kwa hatua.

Viwanda vingi vilivyokuwa vikimilikiwa na serikali vilibinafsishwa kwa wazawa ambao walikuwa wakiingia mikataba na wawekezaji wa nje ya nchi katika kuviboresha. Leseni za kuanzisha viwanda vingine vipya nazo zikawa zinatolewa kwa wingi huku mara kwa mara rais huyo kijana na mchangamfu akiwasisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi bila woga na kuzitumia vizuri fursa zilizokuwa zikipatikana.

Ndani ya kipindi kifupi tu, viwanda vingi vilivyobinafsishwa vilipanuliwa na kuongezwa ufanisi ambapo sasa bidhaa nyingi zilianza kuzalisha ndani ya mipaka ya Sangabuye . Wananchi wengi ambao awali walikuwa wakitegemea kilimo kama uti wa mgongo , sasa wakaajiriwa viwandani ambako walikuwa wakilipwa mishahara mikubwa tofauti na vipato walivyokuwa wanapata kupitia kilimo.

Taratibu maisha ya kila mwananchi yakaanza kubadilika, bei ya bidhaa mbalimbali ikashuka madukani kutokana na viwanda vya ndani kuzalisha bidhaa nyingi na serikali kuvipunguzia kodi, kila mtu akawa anayaona mabadiliko ya waziwazi yaliyokuwa yanatokea. Mabadiliko yaliendelea kupamba moto , vijana wengi na wanawake wakawa wanapewa elimu ya ujasiriamali ambayo iliwafanya wengi kujiajiri na kuwaajiri wengine huku mikopo iliyokuwa ikitolewa na serikali na taasisi nyingine za kifedha kwa riba nafuu ikizidi kurahisisha maisha ya wengi.

"Mume wangu wewe ni kiongozi mzuri sana, najivunia kuwa na mume mzuri kama wewe , " Sophia alimwambia mumewe wakiwa ikulu, asubuhi moja wakati akimuandaa kuelekea kwenye ziara ya kikazi sehemu mbalimbali za Sangabuye. "Kwa nini unasema hivyo mke wangu ?" "Umeyabadilisha sana maisha ya Sangabuye , yaani laiti kama baada tu ya kupata uhuru tungekupa wewe jukumu la kutuongoza huenda leo tungekuwa tunakaribiana na Marekani kwa maendeleo . "Ndani ya muda mfupi tu umebadilisha mno maisha ya wananchi wa.

" Sophia hakumalizia sentensi yake, ghafla akajishika mdomoni na kutoka mbio mpaka kwenye sinki lililokuwa kwenye korido ya ikulu. Rais Martin Wela alishtuka mno kumuona mkewe akiwa kwenye hali hiyo , akaacha kila kitu na kumkimbilia pale kwenye sinki alipokuwa amejiinamia , akazidi kupatwa na hofu baada ya kugundua kumbe mkewe alikuwa akitapika.

"Pole mke wangu , umepatwa na nini?" alisema Martin huku akimshika mkewe kwa upole na kumsaidia kuinuka. Akafungulia maji na kumnawisha kisha akambeba kwenye mikono yake na kumrudisha mpaka sebuleni , akamlaza kwenye sofa la kifahari huku akitoa simu yake na kuwapigia wasaidizi wake waliokuwa ndani ya jengo hilohilo.

Harakaharaka wanawake wanne waliokuwa wakifanya kazi ya kumlinda mke wa rais wakaingia na kwenda mpaka pale mke wa Rais Martin alipokuwa amelazwa. Akawaeleza kilichotokea na kuwataka wahakikishe wanamsaidia haraka. Daktari wa rais akapigiwa simu haraka huku wale wanawake waliokuwa wamevalia mavazi maalum wakiendelea kumpa huduma ya kwanza Sophia . Japokuwa muda wa kuondoka ulikuwa umefika na tayari msafara wa rais ulikuwa tayari nje ya ikulu, Rais Martin hakuweza kutoka mpaka ajue nini kilichokuwa kinamsumbua mke wake.

Muda mfupi baadaye , daktari aliwasili akiwa na vifaa vyote muhimu , harakaharaka akaanza kumpima Sophia aliyekuwa ametulia kwenye sofa , huku akiendelea kulalamika kusikia kichefuchefu. Baada ya kumpima vipimo vyote vya msingi , daktari huyo hakubaini tatizo lolote , akamruhusu Rais Martin aendelee na kazi zake wakati yeye akiendelea kumchunguza mgonjwa taratibu.

"Hakikisha anakuwa sawa daktari, tafadhali msaidie mke wangu , " alisema Rais Martin na kumbusu mkewe kisha akatoka nje ambako msafara wake ulikuwa ukimsubiri . Akaingia kwenye gari lake na safari ya kwenda kuwatembelea wananchi wa sehemu mbalimbali na kusikiliza matatizo yao ikaanza . Je, nini kitafuatia?
 
AKIWA kwenye ziara yake ya kikazi, mara kwa mara Rais Martin alikuwa akipiga simu ikulu kuulizia maendeleo ya mkewe ambaye alimuacha akiwa na hali ya kutatanisha . "Mume wangu , naendelea vizuri ila nina habari njema kwako. " "Ooh afadhali mke wangu kama unaendelea vizuri, unataka kunipa habari gani ?" aliuliza Rais Martin huku akionekana kuwa na shauku kubwa.

"Wala usishtuke mume wangu kipenzi , mwenzio nime. . . nime. . . " alisema First Lady huyo lakini akashindwa kumalizia sentensi yake, akasikika akicheka kwa furaha, jambo lililozidi kumuweka Rais Martin njia panda. "Unaniweka roho juu mke wangu , tafadhali niambie, " alisema Rais Martin huku akionesha dhahiri kuwa na shauku kubwa ndani ya moyo wake, mke wake akamwambia jambo ambalo lilimshtua na kumfurahisha mno. "Nimenasa ujauzito mume wangu , miezi michache ijayo na wewe utakuwa unaitwa baba, " alisema Sophia , hali iliyomlazimu mumewe kukatisha ziara muhimu aliyokuwa anaifanya . Msafara ukageuza na kurudi ikulu huku Rais Martin akiwa bado haamini alichokuwa anakisikia.

Hakuna kitu alichokuwa anakisubiri kwa hamu kama mkewe kupata ujauzito wake , jambo ambalo sasa lilikuwa limetimia . Msafara wake ulipowasili ikulu tu, harakaharaka alishuka na kwenda moja kwa moja kwenye chumba mkewe alichokuwa amepumzika . Akaingia mbiombio na kwenda kumkumbatia huku akiachia mvua ya mabusu. "Daktari , eti ni kweli ?" Rais Martin alimuuliza daktari aliyekuwa amesimama pembeni, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, akatingisha kichwa kukubali kwamba alichokuwa akiambiwa na mkewe kilikuwa kweli.

"Hongereni sana, " alisema daktari huyo kabla hajatoka na kuwapisha wawili hao walioonesha kuwa na furaha ya hali ya juu ndani ya mioyo yao . Wakakumbatiana tena na kuendelea kupongezana kwa hatua hiyo kubwa waliyokuwa wameifikia. Siku zilizidi kusonga mbele huku ujauzito wa First Lady , Sophia ukizidi kuwa mkubwa. Kama ilivyokuwa kipindi cha ndoa yake, waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali walikuwa wakimfuatilia kwa karibu na kuripoti kuhusu maendeleo ya ujauzito wake.

Ratiba ya rais nayo ilibidi ibadilike , kazi nyingi za usiku akawa anazifanya mchana ili apate muda wa kutosha kukaa na mkewe ambaye alikuwa akideka sana kutokana na hali yake. Rais Martin aliajiri wafanyakazi wengi kuhakikisha mke wake anapewa huduma zote muhimu mpaka siku ya kujifungua itakapowadia . Mapenzi kati ya wawili hao yaliongezeka maradufu na kadiri ujauzito ulivyokuwa unazidi kuongezeka ndivyo furaha ilivyokuwa ikizidi kuchanua kwenye familia hiyo.

Hatimaye miezi tisa ilitimia, Sophia akashikwa na uchungu wa kujifungua na kukimbizwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Sangabuye ambako alilazwa kwenye wodi ya VIP, iliyokuwa na ulinzi mkali na huduma za kiwango cha juu . Akajifungua salama mtoto wa kiume . "Whaooo ! Amefanana na wewe, mtazame alivyo mzuri ! Macho, pua, sura vyote kachukua vyako. " "Mh! Mi naona kafanana na wewe , mcheki alivyo ' handsome' , kama baba yake!" Rais Martin na mkewe walikuwa wakijadiliana na kutaniana kwa furaha ndani ya wodi ya wazazi, baada ya rais huyo kuwa mtu wa kwanza kuingia wodini na kumjulia hali mkewe pamoja na mtoto, muda mfupi tu baada ya kujifungua salama.

Habari juu ya kujifungua salama kwa mke wa rais zilisambaa kwa kasi kama moto wa nyikani , salamu za pongezi zikaanza kumiminika kama mvua ya mawe kutoka kila kona ya nchi. Wananchi wengi wakawa wanampongeza Rais Martin na mkewe kwa kupata mtoto mzuri mwenye afya njema. Vyombo mbalimbali vya habari navyo viliendelea kuripoti tukio hilo na kumfanya mtoto huyo awe maarufu akiwa bado mchanga. "Nataka tuzae mwingine wa kike kisha ndiyo nitulie, bado hamu yangu haijaisha mpaka nitakapokuzalia mtoto wa kike, najua unampenda sana, " alisema Sophia wakiwa chumbani na mtoto wao mchanga, wazo ambalo Rais Martin alilikubali kwa haraka kwani ni kweli alikuwa akitamani sana mtoto wa kike kuliko wa kiume . Wakakubaliana kuwa mtoto huyo atakapofikisha umri wa miaka miwili tu, wamtafutie mdogo wake.

Furaha ilizidi kuongezeka kwenye familia hiyo , wakakubaliana kumpa mtoto huyo jina la Charles. Kutokana na malezi mazuri aliyokuwa akiyapata mtoto huyo, alinawiri vizuri na akawa anakua kwa kasi kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele . Naye Rais Martin Wela alizidi kuchapa kazi ya kuitumikia nchi yake kwa uzalendo na uadilifu wa hali ya juu.

Hali za kimaisha za wananchi wa Sangabuye zikawa zinazidi kuimarika kila kukicha, ule umaskini uliowatesa kwa kipindi kirefu sasa ukawa unapotea kama theluji iyeyukavyo juani. "Hii ndiyo Sangabuye tuliyokuwa tunaitaka, tunamuombea mwanao akue haraka ili siku moja na yeye aje kuiongoza nchi yetu kama wewe baba yake ulivyofanya , " mshauri wa rais alimwambia mheshimiwa Martin Wela jioni moja wakiwa wamepumzika kwenye bustani za ikulu, rais akichezacheza na mwanaye.

Kauli hiyo ilimfurahisha sana Rais Martin, akashusha pumzi ndefu na kuanza kujadiliana na mshauri wake huyo aliyekuwa akimuongoza vyema kwenye mambo mbalimbali yaliyokuwa yakiihusu nchi hiyo. "Nafikiri sasa nchi yetu imeshatulia vizuri na huu ndiyo muda muafaka wa kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia utakaomaliza utawala wa kijeshi ulioniingiza mimi madarakani. "

"Ni kweli kabisa mheshimiwa , nadhani huu ndiyo muda muafaka wa wananchi kuamua wenyewe kwa demokrasia rais wanayemtaka ingawa najua bado chaguo lao namba moja utakuwa ni wewe. " "Hahaaa ! Hapana mimi sitagombea tena , nitawapisha wenzangu nao waoneshe uwezo walionao, mimi nitaelekeza nguvu zangu kuitunza familia yangu kwa sababu nikiwa hapa ikulu nakosa uhuru wa kutosha wa kukaa na familia yangu. "

"Wananchi hawatakubali kabisa , yaani ni bora uendelee kuongoza wewe kijeshi kuliko kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia halafu usigombee. Mimi siwasemei wananchi lakini amini nakwambia bado wanakuhitaji sana, " alisema msaidizi huyo wa rais, wakaendelea kuzungumza mambo mbalimbali lakini bado Martin alionesha kutokuwa na nia ya kugombea tena urais . Siku chache baadaye , Rais Martin Wela aliwahutubia wananchi wa Sangabuye ambapo mbali na mambo mengine , alitangaza nia yake ya kuirejesha nchi hiyo katika mfumo wa kiraia baada ya yeye kuiongoza kwa muda, akiwa amewekwa madarakani na jeshi.

Taarifa hiyo ilipokelewa kwa mikono miwili na wananchi wengi ambao walipendekeza kuwa Rais Martin agombee kupitia mfumo wa kidemokrasia kwa sababu bado wananchi wengi walikuwa wakihitaji aendelee kuwaongoza. "Naona mheshimiwa umeamini mwenyewe , unaona watu wanavyotoa maoni yao kuhusu mpango wa kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia?

Wewe ndiyo nyota ya Sangabuye , una mvuto wa kipekee kwa jamii na hakuna anayeweza kushindana na wewe, " mshauri wa rais alimweleza Martin wakiwa wamekaa kwenye ofisi ya rais, ikulu wakifuatilia mahojiano ya watu mbalimbali waliokuwa wakitoa maoni yao kuhusu uchaguzi wa kidemokrasia.

Ilibidi Martin arudi kwa uongozi wa juu wa jeshi ambao ndiyo uliomuweka madarakani, akawaeleza kwamba hafikirii kugombea tena kwa sababu atakuwa bize na ulezi wa familia yake, wazo ambalo lilipingwa vikali na viongozi hao waliomtaka kugombea ili aendelee na kazi nzuri aliyokuwa ameianza.

Martin hakuwa na ujanja, ilibidi afanye kama alivyokuwa ameelekezwa , mchakato wa kuunda serikali ya kidemokrasia ukaanza ambapo vyama mbalimbali vya siasa vilianza kusajiliwa upya. Martin Wela akaunda Chama cha Sangabuye Alliance for Democracy and Transparency ( SADT) .
 
Ebola, ugonjwa hatari usio na tiba wala kinga, unaikumba Liberia , nchi iliyopo Magharibi mwa Bara la Afrika na kusababisha maafa makubwa kwa wananchi wake. Watu wengi wanaambukizwa ugonjwa huo na ndani ya muda mfupi tu, mamia ya wananchi wanapoteza maisha . Licha ya serikali kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kupambana na ugonjwa huo , kazi inakuwa ngumu na maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha na kuambukizwa ugonjwa huo hatari.

Hali inazidi kuwa tete kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele , maiti nyingi za watu waliokufa kwa ugonjwa huo zinatapakaa mitaani huku maelfu ya wakazi wakiyakimbia makazi yao wakiogopa kuambukizwa ugonjwa huo hatari . Jiji la Monrovia linabaki kuwa kimya kabisa huku harufu za maiti zikizidi kuifanya hali kuwa ya kutisha mno.

Mitaa yote inakuwa kimya kabisa , kelele pekee zinazosikika ni za mbwa wanaogombea mizoga ya watu waliokufa kwa ugonjwa huo . Ndani ya nyumba moja, watu wawili waliokuwa wapenzi wanasikika wakibishana . Mwanaume anamtaka mpenzi wake aondoke na kurudi nchini kwao, Sangabuye ili asije akaambukizwa ugonjwa huo lakini mwanamke anakataa akitaka waondoke pamoja au wabaki wote na kufa pamoja.

Upande wa pili, historia ya nchi ya Sangabuye inaelezewa ambapo Rais Martin Wela anaingia madarakani baada ya serikali iliyokuwepo kupinduliwa na jeshi . Muda mfupi baadaye anamuoa mpenzi wake wa siku nyingi, Sophia Marcel na baada ya miezi tisa, ndoa yao inajibu ambapo wanapata mtoto mzuri wa kiume , jambo linaloongeza furaha kwenye familia hiyo . Rais Martin Wela anaendelea kuwatumikia wananchi wa Sangabuye na sasa yupo kwenye mchakato wa kuibadilisha serikali ya kijeshi kwenda kwenye demokrasia ya kweli.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO… Licha ya Rais Martin Wela kuonesha nia ya kutogombea tena kwenye uchaguzi wa kidemokrasia, shinikizo kutoka kwa wananchi na viongozi wa juu wa jeshi ambao ndiyo waliomuweka madarakani lilikuwa kubwa mno kiasi kwamba akawa hana ujanja zaidi ya kukubaliana na matakwa ya wengi.

Ikabidi afanye kama alivyokuwa ameelekezwa, mchakato wa kuunda serikali ya kidemokrasia ukaanza ambapo vyama mbalimbali vya siasa vilianza kusajiliwa upya. Martin Wela akaunda Chama cha Sangabuye Alliance for Democracy and Transparency ( SADT) . Muda mfupi tu tangu kuanzishwa kwake , chama hicho kilipata umaarufu mkubwa huku wananchi wengi wakijiunga nacho kumfuata Rais Martin Wela, kipenzi na chaguo la wengi.

Kama ulivyo utaratibu wa serikali za kiraia , vikao vya ndani vya kila chama vilianza kufanyika kwa lengo la kila kimoja kujiwekea sera zake , ilani na kuteua wagombea katika ngazi mbalimbali. Kama ilivyotarajiwa na wengi, Chama cha SADT kilimteua Rais Martin Wela kuwa mgombea wake wa urais huku akipewa pia jukumu la kuteua vijana alioona wanafaa kugombea nafasi za ubunge katika majimbo yote ya uchaguzi.

Kwa kuwa Rais Martin alikuwa mwanaharakati kwa kipindi kirefu kabla hajapewa nafasi ya kuiongoza nchi hiyo , alikuwa akiwajua vizuri vijana wenye uchungu na nchi yao.

Kwa kuwa alipewa nafasi ya upendeleo ya kuteua wagombea wa nafasi za ubunge ambao aliona wanafaa, aliifanya kazi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu , akawateua vijana waliokuwa na sifa zote za kuwa viongozi bila upendeleo wa aina yoyote. Tume huru ya uchaguzi nayo iliundwa na kupewa jukumu la kuandaa na kusimamia uchaguzi huo ambao ulipangwa kuwa huru na wa haki. Maandalizi yaliendelea kufanyika huku familia ya Martin Wela nayo ikizidi kuwa na furaha.

Mtoto Charles akawa anaongezeka ukubwa na akili kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele . Hatimaye tume ya uchaguzi iliyoundwa , ikatangaza kuanza rasmi kwa kampeni za kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani. Japokuwa kulikuwa na vyama zaidi ya kumi na mbili, vikiwa na wagombea wenye sifa tofautitofauti katika ngazi zote, Alliance for Democracy and Transparency ( SADT ) kilichokuwa kinaongozwa na Rais Martin Wela kilionekana kuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi.

Katika mikutano ya kampeni ya chama hicho, idadi kubwa ya watu walikuwa wakihudhuria na kuwashangilia wagombea wa nafasi mbalimbali kwa tiketi ya chama hicho , hali iliyotoa majibu ya mapema juu ya jinsi matokeo yatakavyokuwa. Kwa kuwa Rais Martin Wela katika kipindi chote cha uongozi wake alikuwa na desturi ya kufanya ziara za mara kwa mara mpaka vijijini, hakupata shida wakati wa kampeni kwani tayari alikuwa akivijua vijiji karibu vyote .

Kila alipokuwa akipita na wagombea wenzake , wananchi walikuwa wakimpokea vizuri na kumuona kama mkombozi wao kwani ndani ya kipindi kifupi tu alichokaa madarakani, aliweza kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi , tofauti na waliomtangulia ambao licha ya kukaa kwa miaka mingi , hakuna chochote cha maana walichokifanya . Kampeni ziliendelea kila sehemu , umaarufu wa chama hicho ukazidi kuwa mkubwa huku maelfu ya wananchi wakijiandikisha na kupewa kadi za chama hicho.

Baada ya kuzunguka karibu nchi nzima, Rais Martin alihitimisha kampeni za chama chake kwenye Jiji la Katwe ambalo ndiyo lilikuwa makao makuu ya nchi hiyo. Viwanja vya Nyika ambavyo mara kwa mara ndivyo vilivyokuwa vinatumika kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu , siku hiyo vilionekana kutotosha kutokana na jinsi watu walivyokuwa wengi.

Hata spika kubwa zilizofungwa kila sehemu , zilionekana kutokidhi mahitaji ya watu wote, wagombea mbalimbali wa chama hicho wakawa wanahutubia kwa zamu na mwisho kabisa, alipanda Rais Martin Wela ambaye kabla hata hajasema chochote, umati wote ulilipuka kwa shangwe , nderemo na vigelegele , huku kila mmoja akilitaja jina lake. Alichokuwa anakiona mbele ya macho yake, kilisababisha atokwe na machozi ya furaha kwani licha ya kukubalika sana sehemu zote alizopita kufanya kampeni, hakuwahi kudhani kwamba wananchi wa Sangabuye , hasa wakazi wa Jiji la Katwe walikuwa wakimkubali kiasi hicho.

Moyoni akajihisi kuwa na deni kubwa la kuhakikisha anayabadilisha kabisa maisha ya kila mmoja . Hata alipoanza kuhutubia, kila baada ya kuzungumza kidogo , watu walikuwa wakishangilia mno. Mpaka anahitimisha hotuba yake, bado wananchi walikuwa na shauku ya kuendelea kumsikiliza . Mkutano ukaahirishwa huku kila aliyehudhuria akiahidi kukipigia chama cha SADT kura na kumchagua Martin Wela kuendelea kuiongoza nchi hiyo . Hatimaye kampeni zilifungwa rasmi, Martin akarudi kutulia na familia yake kwani kwa kipindi chote hicho, alikosa muda wa kukaa na mkewe na mwanaye . "Pole sana mume wangu, najua ni kwa jinsi gani umechoka, " alisema mkewe, Sophia baada ya mumewe kurejea, akamkumbatia kwa furaha na kumpeleka mpaka kwenye chumba cha mtoto wao ambaye alikuwa amelala baada ya kulishwa chakula cha usiku.

"Kila siku anazidi kuwa mkubwa, nawapenda sana wewe na mwanangu, " alisema Martin na kwenda kumbusu mwanaye kwenye paji la uso . "Tunakupenda pia baba, anakua haraka kwa sababu anajua nimekuahidi kumletea mdogo wake siku chache zijazo, " alisema Sophia na kumkumbatia tena mumewe, wakamwagiana mabusu kisha wakarudi chumbani kwao kupumzika, huku Sophia akiendelea kumsisitiza mumewe kwamba lazima amzalie mtoto mwingine wa kike haraka iwezekanavyo.

Hatimaye ile siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa , ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani iliwadia . Wananchi wengi wa Sangabuye walijitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura. Foleni ndefu za watu waliokuwa wamejipanga tangu alfajiri, zilionekana kwenye vituo vyote vya kupigia kura . Kwa mara ya kwanza uchaguzi wa kidemokrasia ukafanyika tangu jeshi lilipoipindua nchi hiyo , wananchi wote waliokuwa na sifa za kupiga kura wakaitumia vizuri nafasi hiyo.

Mpaka ilipotimu saa sita za usiku, zoezi hilo lilifungwa baada ya kuwa watu wote wameshapiga kura. Zoezi la kuhesabu kura lilianza haraka chini ya ulinzi mkali wa askari wa kawaida na wanajeshi waliokuwa wakipita kila sehemu kuhakikisha amani na utulivu vinadumishwa. Mpaka alfajiri ya siku ya pili ilipowadia , tayari baadhi ya vituo vilikuwa vimekamilisha zoezi la kuhesabu kura.

Chama cha SADT kilianza kung' ara tangu kwenye matokeo ya awali ambapo wagombea wake wengi wa nafasi za udiwani na ubunge waliwazidi kwa mbali wapinzani wao kutokana na wingi wa kura . Yote tisa, kumi ilikuwa ni kwenye nafasi ya urais ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo, Martin Wela alikuwa akiongoza kwa zaidi ya asilimia tisini ya kura zote zilizopigwa.

Zoezi liliendelea kwa siku mbili mfululizo na baada ya siku ya tatu, Tume ya Uchaguzi ya Sangabuye ( SEC) ikatangaza rasmi matokeo ya urais ambapo Martin Wela alishinda kwa kishindo baada ya kupata asilimia tisini na tatu ya kura zote . Shangwe , nderemo na vigelegele vikawa zinasikika kila kona ya nchi hiyo, huku waangalizi wa uchaguzi huo kutoka mataifa mbalimbali, wakishangazwa na jinsi Martin Wela alivyokuwa akikubalika miongoni mwa wananchi wake .

Je, nini kitafuatia?

Usikose Jumatatu
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…