Usanii at its best!
Posted Date::12/20/2007
Meghji atetea kucheleshwa ya ripoti BOT
*Asema bado ipo katika mchakato
Ramadhan Semtawa na Kuruthum Ahmed
Mwananchi
SERIKALI imetetea hatua ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuendelea kukumbatia ripoti ya ukaguzi wa tuhuma za ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Msimamo huo wa serikali umekuja siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kuhoji ukimya katika kuitangaza ripoti hiyo na kudai kwamba unaweza kufanya serikali ipike matokeo.
Akizungumza jijini Dares Salaam jana, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, alisema ripoti hiyo ilipaswa kupitia kwa CAG kwani ndiye msimamizi wa mchakato mzima.
Meghji alisema CAG ndiye ametoa kazi na kuteua kampuni hivyo lazima kwanza aipitie kwa kina ripoti hiyo.
"Siyo kwamba CAG ameikumbatia, ni lazima ripoti iwe kwake, aisome na kupitia hatua kwa hatua," alisema Meghji na kuongeza:,
"Kwa sababu yeye CAG ndiye ametafuta kampuni na kusimamia mchakato mzima wa ukaguzi huo."
Waziri Meghji aliongeza kwamba, hakuna ukimya bali ni mchakato kwani awali ripoti hiyo ilikwenda kuandaliwa London,Uingereza.
Kuhusu lini atakabidhiwa, alisema CAG Ludovick Utouh, ambaye kwa sasa yuko nje kikazi anatarajiwa kurejea nchini kesho, hivyo atumaini kukabidhiwa ripoti hiyo siku yeyote mara baada ya kuwasili kwake.
Alipoulizwa kwamba haoni ukimya huo unatia shaka na kuleta uwezekano wa serikali kupika matokeo, alijibu " Serikali haiwezi kupika matokeo."
"Kama serikali ingekuwa haitaki kufanya ukaguzi isingeamua kufanya hivyo, kwani yenyewe ndiyo iliamua, sasa tufiche nini?" alihoji Meghji.
Waziri Meghji aliongeza kwamba, serikali haiwezi kukurupuka tu kuitoa ripoti hiyo bila kuipitia kwa kina.
Alisema serikali inapaswa kulinda heshima yake kwa kuangalia kama maagizo yake katika uchunguzi huo, yamezingatia mambo yote ya msingi ambayo yalipaswa kuchunguzwa.
"Serikali iko, makini lazima ipitie ripoti kwa umakini, kuona kama kweli mambo ya msingi yamezingatiwa ili kulinda heshima yake kwa umma," alisisitiza.
Waziri huyo alisema lengo la serikali ni kuona ripoti hiyo inakamilika ili iweze kutolewa kwa wananchi na kusisitiza kila kitu kitaelezwa bayana wakati wowote ikikamilika kupitiwa.
Juzi katika tamko la Chadema ambalo limetolewa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho, alisema wamefikia uamuzi huo wa kuitaka serikali itangaze ripoti hiyo hadharani na kuacha kuikumbatia kwani kitendo hicho kinatiashaka kwamba inaweza kufichwa.
Ukaguzi wa akaunti hiyo umefanywa na Kampuni ya Ernst & Young, ambayo ilikabidhi ripoti hiyo kwa CAG mwezi uliopita, lakini hadi sasa kukiwa na ukimya huku taarifa za ndani zikielezwa kuwapo ubadhirifu wa zaidi ya dola 50 milioni.
Ukimya huo umekuwa ukifanya watu wa kada mbalimbali nchi kudhnai kwamba serikali kwamba ina nia ya kugeuza matokeo hayo.