Soma Hii:Matokeo ya uchaguzi Kenya: Nilishinikizwa, sijui kama Kibaki alishinda

kaisa079

Member
Nov 16, 2007
20
0
FROM MAJIRA TODAY
*Adai maandalizi kumwapisha Kibaki yalishakamilika
*Akubali uchunguzi ufanywe kuhusu matokeo ya urais
*Wanasheria wataka marais Afrika Mashariki waingilie
*Kivumbi chasubiriwa mkutano wa ODM Uhuru Park leo

NAIROBI, Kenya

MWENYEKITI wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK), Bw. Samuel Kivuitu, amesema alishinikizwa kutangaza matokeo.

Akizungumza juzi jijini hapa, Bw. Kivuitu alisema alishinikizwa na chama cha Rais Kibaki cha National Unity na kingine kidogo cha upinzani ambacho kilijitenga na kile cha Odinga cha Orange Democratic Movement (ODM).

"Nililazimishwa na PNU na ODM-Kenya kutangaza matokeo mara moja," alisema Bw. Kivuitu.

Wakati makamishna wanne wa Tume hiyo wameungana na miito ya kutaka uchaguzi huo na mchakato mzima uchunguzwe na chombo cha kisheria, waangalizi wa Jumuiya ya Ulaya (EU) wamesisitiza kuwa uchaguzi huo haukukidhi viwango vya kimataifa.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama kweli Rais Kibaki alikuwa ameshinda uchaguzi huo, Bw. Kivuitu alijibu: "Sijui kama Kibaki alishinda uchaguzi huo."

Aliendelea na majibu yake ya kushangaza, aliposema kuwa ndiye aliyepeleka cheti cha mshindi wa urais Ikulu jijini Nairobi, baada ya "baadhi ya watu kutishia kukipeleka huko wakati mimi ndiye mwenye mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.

"Niliwasili Ikulu kupeleka cheti hicho na kumkuta Jaji Mkuu, tayari kumwapisha Rais Kibaki," alisema Bw. Kivuitu.

Kuhusu madai kuwa kweli alikuwa katika shinikizo la kutangaza matokeo, Bw. Kivuitu alisema: "Baadhi ya viongozi wa PNU na ODM-Kenya waliniweka katika shinikizo hilo kutokana na kunipigia simu mara kwa mara wakinitaka nitangaze matokeo mara moja."

Hata hivyo, alisema shinikizo la kumtaka atangaze matokeo lilikuwa likitoka sambamba na la mabalozi wa nchi za Jumuiya ya Ulaya, na Bw. Maina Kiai wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, kutotangaza matokeo hadi malalamiko yaliyoibuka yapatiwe majibu.

"Nilishafikiria kujiuzulu, lakini nikabadili mawazo kwa sababu sitaki watu waseme mimi ni mnafiki," alisema. Bw. Kivuitu aliyasema hayo muda mfupi baada ya kukutana na makamishna 22 wa ECK.

Hata hivyo, kuhusiana na hali ilivyo, alishauri masuala hayoi ya matokeo yakafikishwa mahakamani na uamuzi uchukuliwe haraka ili kuodokana na mvutano uliopo hivi sasa nchini.

"Kama suala hili hatimaye litafikishwa majakamani, uamuzi wake utatakiwa kufanyika haraka ili kama itaamuliwa kuwa Bw. Odinga ni Rais, na iwe hivyo. Kama ni Kibaki na iwe hivyo," aliongeza.

Bw. Kivuitu alisema alifikia uamuzi wa kutangaza matokeo kwa sababu Tume yake haina mamlaka kisheria kuchunguza malalamiko yaliyotolewa na upinzani.

Hata hivyo, alishindwa kuwataja maofisa wa vyama hivyo waliomshinikiza atangaze matokeo, ila akasema tu kuwa tume yake inawasiliana na wanasheria mashuhuri kujua ni hatua ipi ya kuchukua hivi sasa, ili itakayochukuliwa iwe katika misingi ya kisheria.

Naye aliwaunga mkono makamishna wake wanne, akisema ni bora kikaundwa chombo huru ili kuchunguza yaliyojitokeza, na lakini hilo linaweza kufanyika tu iwapo sheria inaruhusu.

"Sisi tume ni washukiwa. Hatuna budi kukiachia chombo huru kichunguze nini hasa kilikosewa," alisema Mwenyekiti wa ECK na kuwashangaza waandishi wa habari wa ndani na nje waliofika nyumbani kwake kumsikiliza.

Katika hatua nyingine, Afrika Kusini kama zilivyo nchini nyingine zilizoshituliwa na hali hiyo, imetuma Kenya maofisa wake wa uchaguzi kujaribu kusaidia.

Naibu Mwenyekiti wa ECK, Bw. Kihara Muttu, aliuita mkutano wa makamishna wa ECK kama 'mkutano wa kuiweka sawa nyumba yao'.

Katika tamko lao la pamoja, makamishna hao walilaani ghasia zilizoibuka Jumapili usiku na mpaka sasa zimepoteza maisha ya takriban watu 300.


Mawaziri wakana udanganyifu


Lakini Waziri wa Fedha, Bw. Amos Kimunya, alikanusha kuwapo kwa madai ya udanganyifu katika mchakato huo.

Waziri alisema: "Sina ushahidi kuwa kulikuwa na udanganyifu. Yeyote mwenye taarifa kwamba ulikuwapo hata katika jimbo moja au lingine au kwa ujumla wake, waziwasilishe kwa vyombo vya sheria."

Naye Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Bibi Martha Kirua, alitaka kuwapo maridhiano ya kitaifa na kuitaka ODM iende mahakamani kupinga matokeo isiyoridhika nayo.

Alisema washindi na washindwa katika uchaguzi hu, wote wanahitajiana na kuitaka ODM kuachana na msimamo wake unaochochea ghasia.

Waziri Karua alisema hatua ya maridhiano haiwezi kuendana na kumtaka Rais Kibaki ajiuzulu, akisema matokeo ya uchaguzi yataweza kubatilishwa na mahakama hasa baada ya kuwa yametangazwa na tume.

Kuhusu kuundwa kwa tume ya uchunguzi, Waziri Karua alisema sheria hairuhusu.

"Uchunguzi hufanywa na mahakama ya sheria na ni baada ya chama kisichoridhika kupeleka malalamiko. Hatuwezi kubatilisha matokeo. Mahakama pekee ndiyo inayoweza kufanya hivyo," Bibi Karua alisema.

Alisema si kweli kuwa kulikuwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kupiga kura katika jimbo la Rais Kibaki kuliko waliojiandikisha, na kuongeza kuwa hata wataalamu walishatabiri kuwa watu watakuwa wengi.

Bibi Karua akisema alishuhudia wakati ECK ikipitia matokeo kutoka majimbo 210 ambapo pia ODM na PNU waliwakilishwa na kukubaliwa kuwa matokeo yatangazwe.

Alizitaka PNU na ODM kutafuta njia ya kumaliza tatizo lililopo kwa maslahi ya nchi. "Washindi na washindwa lazima wasonge mbele. Bado tunahitaji kushirikiana. Na hata ndani ya Bunge tunahitaji kuwa
na Serikali na Upinzani," alisema.

Pande mbili za Serikali na Upinzani zimekuwa zikilaumiana kuhusu ghasia huku maelfu ya watu wakikimbia makazi yao wakihofia mapigano.

Takriban watu 300 wameshauawa, wakiwamo takriban 40 waliouawa kwa moto wakiwa wamejihifadhi kanisani.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Bw. John Kufuor, jana alitarajiwa kuwasili nchini Kenya, kuzungumza na Rais Kibaki, huku Marekani na Uingereza wakipaza sauti za kutaka kumalizika kwa ghasia nchini humo.

Serikali kwa upande wake ilisema wafuasi wa Odinga "wanashiriki katika kuangamiza kabila fulani kwa njia iliyopangwa kwa uangalifu mkubwa."

Hata hivyo Bw. Odinga amekuwa akikaririwa akisema Serikali ya Rais Kibaki ina hatia moja kwa moja katika mauaji ya kimbari."

Wengi wa waliouawa kanisani ni Wakikuyu, kabila la Rais Kibaki na zimekuwapo taarifa kuwa kuna watu wanalengwa kwa misingi ya kikabila.

Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya, Bw. Abbass Gullet, alisema ni wale tu wanaotoka katika kundi linalotakiwa la kikabila ndio wamekuwa wakiruhusiwa kupita kwenye vizuizi barabarani katika baadhi ya maeneo.

Wachunguzi wa masuala ya siasa, wanasema ingawa uchaguzi ulikuwa ukihusu zaidi masuala ya kiuchumi na siasa zaidi ya ukabila, ipo hatari kwamba jinsi ghasia zinavyoongezeka tatizo sasa litakuwa la kikabila zaidi.

Mashirika ya misaada tayari yanahofia kuibuka kwa janga la kibinadamu iwapo ghasia hizo hazitakomeshwa.

Wengi wa watu waliouawa kanisani Eldoret walikuwa ni miongoni mwa mamia ya waliokimbilia humo kujihifadhi na walioshuhudia walisema kundi la watu wenye hasira lilivamia kanisani na kumwaga petroli kabla ya kuwasha moto.

Wakazi wa mji huo wamekuwa wakielezea kujawa na hofu, kwani hata waliojihifadhi majumbani wamekuwa wakifungiwa milango na nyumba zao kuwashwa moto na vijana wenye silaha ambao pia wanapora mali.

Mwanamke mmoja alidai kufungiwa katika kituo cha kulelea watoto yatima, na wale wakubwa wakiamriwa kujihami kwa silaha kwani chochote kinaweza kutokea, "hivyo wana marungu na silaha yoyote wanayoweza kuipata," alisema mwanamke huyo.

Juzi zilikuwapo taarifa za kuibuka upya kwa mapigano katika vitongoji vya Nairobi huku Chama cha Msalaba Mwekundu kikisema katika eneo la Bonde la Ufa, takroiban watu 70,000 hawana makazi, na kuielezea hali hiyo kama janga la kitaifa.

Maofisa wa Uganda nao wamekaririwa wakisema mamia ya Wakikuyu wanavuka mpaka kuingia nchini humo kutoka Kenya.


Wanasheria wawazindua marais EAC

Wakati huo huo, Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS), kimelaani machafuko yaliyogubika sehemu nyingi za nchi na kuwataka Wakenya kurejesha amani.

Rais wa EALS, Bw. Tom Ojienda, alisema amewaandikia marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki- Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi – kuingilia kati na kurejesha amani kabla machafuko hayo hayajavuka kiwango.

Katika hatua nyingine, Chama cha Wamiliki wa Matatu (daladala), kimeungana katika kulaani machafuko hayo na kuitaka Serikali kuimarisha usalama.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Simon Kimutai, alisema machafuko hayo yamevuruga kabisa huduma za usafiri.

Aliitaka Serikali kuwahakikishia usalama watoa huduma ya matatu, ili waendelee kutoa huduma zao, hasa ikizingatiwa kuwa shule zinafunguliwa wiki ijayo.

Nacho kikundi cha Wadau wa Amani kiliwataka viongozi wa PNU na ODM kuwaasa wafuasi wao kurejesha na kudumisha amani nchini kote.

Kikundi hicho, kinachoundwa na wasanii wa burudani na mashirika yasiyo ya kiserikali, kiliwataka Wakenya hususan vijana, kusema 'HAPANA' kwa machafuko.

Ofisa wa wadau wa burudani, Bw. Dan Odhiambo, alisema amani ni kitu muhimu sana ambacho Kenya ilikuwa nacho na ikijivunia siku zote.

Naye kiongozi wa chama cha Safina, Bw. Paul Muite, alimtaka Rais Kibaki kuanzisha mazungumzo na Bw. Odinga haraka inawezekanavyo.

Bw. Muite alisema ajenda ya kwanza na muhimu sharti ielekezwe katika kumaliza ghasia, machafuko na upotevu wa maisha ya watu na mali zao.


Makamishna ECK wapingwa

Nao makamishna wanne wa ECK wanaotaka kuundwa kwa tume ya uchunguzi kuhusiana na matokeo hayo, imepingwa kwa kuambiwa masimamo wao huo umetolewa ukiwa umechelewa.

Kamishna wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Kenya (KNHCR), Bw.
Hassan Omar, alisema juzi: "Ingawa tunafarijika na ujasiri wao, Taifa lingekuwa limetendewa vema zaidi kama wangekuja na hoja yao hiyo kabla ECK haijatangaza matokeo."

Jumatatu iliyopita, makamishna Bw. Jack Tumwa, Bw. Joseph Hamisi Dena, Bw. Daniel Ndambiri, Bw. Samuel arap Ng’eny na Bw. Jeremiah Matagaro, waliwambia waandishi wa habari kuwa nao wana shaka na kilichojitokeza katika mchakato wa uchaguzi na kutaka uchunguzi ufanywe.

Juzi Bw. Omar aliunga mkono kuwapo kwa tume huru ya uchunguzi na kusema KNHCR itaiunga mkono.

"Tunaunga mkono wazo hilo la kufanyika uchunguzi huru dhidi ya baadhi ya maofisa wa ECK na matokeo yote kwa ujumla," alisema.

Alidai kuwa shaka kutoka kwa waangalizi wa uchaguzi imetia dosari uhalali wa mchakato mzima na misingi ya demokrasia nchini.

"Ni muhimu sasa pande zote zihakikishe zinalinda maslahi ya Taifa hili hasa katika kipindi hiki kigumu cha nchi yetu tunayoipenda," alisema.

Mbali na watu takriban 40 kuchomwa moto kanisani Eldoret juzi, jijini Mombasa ilitaarifiwa kuwa watu 11 wengi wao wakiwa wa familia moja, walichomwa moto ndani ya nyumba yao.


Uhuru Park kuzizima

ODM kwa upande mwingine, imeanza mikutano yake ya maombi ambayo itafikia kilele leo katika mkutano mkubwa kwenye viwanja vya Uhuru Park jijini Nairobi.

Mbunge mteule wa Ugenya, Bw. James Orengo, ambaye alianzisha maombi hayo katia makanisa yote ya All Saints Cathedral, alisisitiza jana kuwa mkutano wa leo upo kama ulivyopangwa.

Hatua hiyo inaelezwa itaibua mapambano mengine kati ya wafuasi wa ODM na wanausalama katika eneo hilo la kihistoria, kutokana na onyo la Polisi kwamba mkutano huo ni batili.

Serikali ilishasema kuwa mkutano huo wa ODM si halali na kuwaonya wananchi kutosogelea eneo hilo.

"Serikali haina msingi kwa vyovyote kuzuia mkutano wetu wa maombi. Walituomba tuwataarifu na napenda kuwambieni kuwa tulifanya hivyo tena katika muda muafaka waliotupa," alisema Bw. Orengo.

Mlolongo huo wa maombi ulianza juzi mchana kabla ya kuhamia katika Kanisa la Holy Family Basilica.

Jana walitarajiwa kuwa katika msikiti wa Jamia kuanzia saa 7 mchana huku mikutano mingine kama hiyo ikifanyika katika misikiti mingine sehemu mbalimbali za nchi.

Kwingineko viongozi wa kiislamu juzi walitangaza kampeni ya kukomesha ghasia zinazoendelea na uharibifu wa mali kwa kuhubiri amani.

Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kenya (CIPK) katika taarifa yake ilisema hasira ambazo zinaelekezwa kwa jumuiya fulani nchini, hazina tija na zinatakiwa kukomeshwa.

Katibu Mkuu wa CIPK, Shekhe Mohammed Dor, alisema maimamu walio katika Baraza hilo, wametakiwa kuhubiri amani.

"Tumewaelekeza maimamu wetu kuhubiri amani na kuhakikisha uharibifu wa mali na vifo vinavyoendelea vinakoma," alisema Shekhe Dor.

CIPK ilimlaumu Mwenyekiti wa ECK na Rais Kibaki kwa kuchukua uamuzi ambao hivi sasa umeiingiza nchi katika machafuko.

"Kama Bw. Kivuitu angekubali uhakiki wa karatasi zote za kura, tatizo hili lisingekuwapo na shaka ya udanganyifu ingeshatoweka," alisema Shekhe Dor.

Alimtaka Rais Kibaki akubali kura za urais zihesabiwe upya, ili kuiokoa nchi na machafuko yanayoendelea.

Kanisa lilivyochomwa

Wakazi wa mji wa Eldoret wamesimulia tukio la kutisha ambapo watu wapatao 30 waliungua moto juzi na kufa katika Kanisa walimokuwa wamekimbilia na kujihifadhi kutokana na mapigano yanayoendelea.

Bw. George Karanja, aliliambia shirika la habari la Associated Press jana, kwamba aliweza kuopoa watu 10 katikati ya ndimi za moto, lakini akashindwa kuokoa maisha ya mwipwa wake mwenye umri wa miaka 11.

"Alikuwa akilia 'mjomba, mjomba ... alikufa," alisema Bw. Karanja.

Kundi la watu wenye hasira lilivamia Kanisa la Assembilies of God na kulimwagia mafuta ya petroli kabla ya kuliwasha moto, walionusurika na polisi waliiambia AFP.

"Magodoro waliyolalia watu hao yalishika moto. Kulikuwa namsongamano mkubwa na watu walilaliana katika juhudi za kujiokoa," alisema Bw. Karanja (37).

Mamia ya watu, wengi wao kutoka Kabila la Rais Mwai Kibaki la Wakikuyu, ndio wanaoaminika kujihifadhi ndani ya Kanisa hilo.

Taarifa zilisema miili ya watu hao ilikutwa imejiviringa ndani ya mabati huku mbao zilizoungua kiasi, zikiwa zimefunikwa na majivu na vifaa mbalimbali vya watu hao vikiwa vimetawanyika huku na huko.

Baadhi ya miili iliungua kiasi cha kutotambuliwa, alisema Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu cha Kenya, Bw. Abbass Gullet.

"Hili ni moja ya matukio ya kutisha ambayo sijawahi kuyashuhudia maishani mwangu. Kuona wanawake na watoto waliotafuta usalama wao ndani ya nyumba ya Mungu wanauawa, ni kitu ambacho si rahisi kuamini," alisema ofisa mmoja wa Chama hicho mjini Eldoret.

Mwandishi mmoja aliyefika kwenye eneo la tukio aliliambia Shirika la Habari la Uingereza, Reuters, kwamba kundi la vijana lilifika kanisani hapo na kuwazidi nguvu vijana waliokuwa wakilinda usalama na kuchoma moto jengo.

Mchungaji wa Kanisa hilo, Bw. Jackson Nyanga, aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kwamba wengi wa watu hao walipiogwa kwanza kabla ya Kanisa kuchomwa moto.

"Watoto walikufa-takriban 25 kwa idadi - wazee wanne. Na watu wetu waliojaribu kukabiliana nao walijeruhiwa," alisema Mchungaji.

Mfanyakazi wa kujitolea wa Chama cha Msalaba Mwekundu, alisema idadi ya waliokufa ilifikia 50, huku vyombo vya habari nchini Kenya vikiripoti kuwa watu 20 walijeruhiwa.

"Mji wa Eldoret uliomo katika mkoa wa Bonde la Ufa, una historia ya mapigano ya kikabila na umegubikwa na macahuko ,mabaya sana tangu kutangazwa kwa matokeo ya urais JUmapili iliyopita.

Waandishi wa habari walisema tangu siku chache zilizopita, mamia ya Wakikuyu katika eneo la Eldoret wamekuwa wakikimbuilia makanisani na katika vituo vya Polisi kujihifadhi.

Wakazi wa mji huo ambao wamezungumza na BBC wameelezea kuwapo kwa hali ya wasiwasi, watu wakitafuta mahali pa kujihifadhi kutokana na nyumba zao kuchomwa moto huku makundi ya vijana wenye silaha wakiiba mali mbalimbali.

"Tumeshindwa kupata usingizi kwa siku kadhaa zilizopita. Niko katika nyumba ya mjomba takriban mwendo wa dakika 10 kutoka mjini. Usiku ziku zote hapa umetawaliwa na milio ya risasi, moshi na vilio vya watu," alisema Chemu Mungo (22).

"Usiku wa jana, wanawake 20 na watoto wao wengi wao wakiwa ni Wakalenjin, walikimbilia nyumbani kwa mjomba, kwani walikokuwa wakiishi nyumba zao zilichomwa moto na kuhofia maisha yao.

Padri raia wa Ayalandi aliyeko mjini Eldoret, Bw. Paul Brennan, aliiambia Reuters, kwamba makundi ya hatari yalikuwa yakiranda mitaani. "Nyumba zinachomwa. Ni hatari sana kutoka nje kuhesabu maiti," alisema Padri huyo.

"Makanisa yamefurika watu. Katika Kanisa Kuu la Katoliki kuna takriban watu kati ya 4,000 na 5,000." (Mashirika)
 
Bora huyo ametamka waziwazi kuwa alishinikizwa.... kuliko wakina Ballali wetu ambao hawataki hata kusema...

Ni makosa kufanya kazi kwa kushinikizwa lakini kwa kuthamini jinsi tu yeye alivyothamini uhai wake kuliko wa wale waliokufa baada ya matokeo kutangazwa, inabidi tu kumpongeza kinamna kwa kulitamka hili swal hadharani na bila kuchelewa sana.

Angalia mwenzetu Balali aliyeshinikizwa (naamini hivyo), sijui atakuja kusema lini hivyo au ni lini atakuja kuwa taja walio mfanyia hivyo.... anasubiri mauti au?!

Najua ni vitu viwili tofauti, lakini nadhani ni mfano hai wa tofauti tulizo nazo sisi na wao.. tukikumbuka jinsi yule mwingine pia, aliyeenda kule Uingereza kuwataja BBC wala rushwa wote waliohusika kwenye scandal mojawapo.

SteveD.
 
Bora huyo ametamka waziwazi kuwa alishinikizwa.... kuliko wakina Ballali wetu ambao hawataki hata kusema...

Ni makosa kufanya kazi kwa kushinikizwa lakini kwa kuthamini jinsi tu yeye alivyothamini uhai wake kuliko wa wale waliokufa baada ya matokeo kutangazwa, inabidi tu kumpongeza kinamna kwa kulitamka hili swal hadharani na bila kuchelewa sana.

Angalia mwenzetu Balali aliyeshinikizwa (naamini hivyo), sijui atakuja kusema lini hivyo au ni lini atakuja kuwa taja walio mfanyia hivyo.... anasubiri mauti au?!

Najua ni vitu viwili tofauti, lakini nadhani ni mfano hai wa tofauti tulizo nazo sisi na wao.. tukikumbuka jinsi yule mwingine pia, aliyeenda kule Uingereza kuwataja BBC wala rushwa wote waliohusika kwenye scandal mojawapo.

SteveD.

kwa matamshi ya huyu kivuitu kama ni ya kweli hapo juu ,basi yeye ndie anaepaswa kuwajibishwa kwanza na kama inawezekana kuhukumiwa kisheria. ni vipi mtu utakubali kushinikizwa katika kazi yako? roho zaidi ya 300 zimepotea kwa uzembe wa mtu mmoja.
 
Back
Top Bottom