ITEGAMATWI
JF-Expert Member
- Jan 26, 2012
- 5,338
- 4,081
Juma Mtanda, Mwananchi jmtanda@mwananchi.co.tz
Shule ya Sekondari ya Malinyi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro ndiyo iliyofanya vibaya zaidi katika matokeo ya mtihani wa taifa kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni. Shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 56, kati yao 40 walipata daraja sifuri, 12 daraja la nne huku wanne matokeo yao yakizuiliwa. Safari kuelekea shuleni Nililazimika kuwa na moyo wa uvumilivu ili kuianza safari ya kuelekea kijiji cha Mchangani, kata ya Malinyi ilipo shule hiyo ambayo kwa kigezo cha mazingira hasa majengo yake, kinatosha kuwa sababu ya wanafunzi kufanya vibaya kitaaluma. Njiani nilikumbana na changamoto mbalimbali ikiwamo ya uduni wa miundombinu ya barabara hasa kuanzia eneo la Lupilo kwenda Malinyi.
Ni safari ya kilometa zisizopungua 130 iliyochukulia muda wa saa karibu saba kufika shuleni hapo. Ubovu wa barabara unamfanya dereva kuendesha gari kwa mwendo wa kinyonga hasa katika zile sehemu korofi zilizojaa matope na utelezi. Makamu mkuu shule atoa ya moyoni Makamu Mkuu wa shule hiyo, Ackrey Lyotela anaeleza sababu za shule hiyo kufanya vibaya kwenye matokeo hayo kuwa ni pamoja na kuwa na wanafunzi wenye uwezo mdogo, walioingia kidato cha tatu kwa ‘huruma’ ya Serikali ilipotangaza wanaofeli kidato cha pili waruhusiwe kuendelea na masomo. “Hawa wanafunzi ndiyo wameifanya sekondari ya Malinyi kushika mkia kitaifa, hebu fikiria wakiwa kidato cha pili, ni wanafunzi 24 pekee waliofaulu kuingia kidato cha tatu. Waliobaki 83 walifeli, lakini kupitia tamko la Serikali waliruhusu kuingia kidato cha tatu, unategemea nini?’’ anahoji Lyotela. Uhaba wa walimu Achana na ya Firauni ya Musa ni zaidi. Kwa miaka mitatu tangu kuanzishwa kwake, shule hii haikuwa na walimu wa Hisabati na masomo ya Sayansi. Kwa mujibu wa mwalimu wa taaluma, Reuben Wilson, uhaba wa walimu umechangia asilimia 75 ya wanafunzi wa shule hiyo kufanya vibaya. “Tangu shule ianzishwe, ilianza na walimu wawili na kuongezeka hadi kufikia walimu sita mwaka 2014, lakini mwaka 2009 hadi mwaka 2011 hapakuwapo na mwalimu wa Hisabati na Sayansi, masomo haya ndiyo muhimu zaidi kufundishwa. “Wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2015 hawakufanya mtihani wa Fizikia, kwani kipindi chao chote hawakusoma somo hilo kwa sababu hakukuwapo mwalimu,’’ anasema Wilson. Uhuni, ngono vyakithiri Unapozungumza na baadhi ya walimu na wakazi wa Malinyi, hawasiti kukutajia sifa ya utovu wa nidhamu na tabia mbaya walizonazo miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo. Mwalimu Lyotela anasema miongoni mwa wanafunzi waliomaliza mwaka jana, saba waliwahi kusimamishwa masomo kutokana na kujihusisha na uvutaji wa bangi, huku wakiunda kundi walilolipa jina la ‘Ukawa.’
“Kundi la Ukawa liliundwa na wanafunzi wengi wa kiume na ndilo lililojihusisha na uvutaji wa bangi, utoro sugu na wasichana kujiingiza katika ngono na wanaume wa kila rika. Jamii imekuwa na mwitikio mdogo kuhusu malezi ya watoto,” anaeleza Mwalimu Lyotela. Mmoja wa wazazi ambaye hakutaka jina lake lichapishwe gazetini anasema hashangazwi na wanafunzi wa kike wa shule hiyo kujiingiza kwenye vitendo vya ngono kwa kuwa ni matunda ya kazi iliyotengenezwa na mikono ya wazazi wao. Anasema wakati wa msimu wa kilimo, baadhi ya wazazi hukimbilia mashambani na kuwaacha watoto wao bila ya mahitaji muhimu. “Ni kweli wanafunzi wa kike wanajihusisha na ngono na wanaume tena waliopo katika ndoa zao. Baadhi ya wanaume wanatumia dhiki ya wanafunzi wa kike wanaokosa mahitaji kutoka kwa wazazi,” anasema na kuongeza: ‘‘Hili la kutembea na watu watu wazima siyo jambo la ajabu na imewahi kutokea mwalimu mmoja wa shule ya msingi kuishi kinyumba na mwanafunzi wa kike baada ya kumgeuza mke wake, lakini suala hilo lilipogunduliwa liliishia hewani tu.’’ Vyoo, nyumba za walimu tatizo Wakati mwongozo wa Serikali ukieleza tundu moja la choo kutumiwa na wanafunzi wa kike 20 na wavulana 25, katika shule hiyo yenye wanafunzi 485, tundu moja linatumiwa na wanafunzi wa kike 79 na wavulana 125. Hali hiyo inatokana na shule kuwa na matundu matano, kwa mgawanyo wa matatu kwa wasichana na mawili kwa wavulana. Kuna nyumba mbili za walimu huku wengine wakilazimika kupanga umbali wa kilometa 12 kutoka shuleni. Kwa siku walimu hao wanatembea umbali wa kilometa 12 kwenda na kurudi shule.
Shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa vitabu vya masomo ya Jiografia, Uraia, Kiingereza, Kiswahili na Historia. Uongozi wa shule Baadhi ya wadau wa elimu wanasema kukosekana kwa umoja miongoni mwa walimu na mkuu wa shule kutoonekana mara nyingi shuleni, kumechangia matokeo hayo. Hata hivyo, Mkuu wa shule hiyo, Alana Fungo anasema: ‘‘Uhusiano wangu na walimu ni mzuri kwani hawajawahi kunishtaki kokote. Mimi nimeokoka, ratiba za ibada ni jioni, kama sipo shuleni basi nitakuwa wilayani au sehemu nyingine kwa maendeleo ya shule. Siku ambazo niko kazini, huwa wa mwisho kuondoka shuleni. Jambo la maana tushirikiane Serikali, wazazi, wanafunzi, vyama vya siasa, wadau na walimu wote. Mkuu wa shule peke yake hawezi.’’ Kauli ya diwani Diwani wa Kata ya Malinyi, Saidi Tira anasema kukosekana kwa nguvu ya pamoja kati ya Serikali, wazazi, jamii na walimu kumechangia shule hiyo kufanya vibaya.
Haiwezekani shule iwe na walimu watano kwa kipindi kirefu halafu utegemee wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa,’’ anasema na kuongeza: “Shule ikiwa na upungufu wa walimu, wanafunzi hawawezi kusoma baadhi ya masomo. Pia uhusiano ukiwa mbaya kati ya mkuu wa shule na walimu mambo yataenda ovyo,’’ anasema Tira. Anashauri ujenzi wa mabweni na nyumba za walimu uwe sehemu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili shule hiyo kitaaluma na kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.