Simulizi Ya Kweli: Usiku Wa January 20, 2015

Simulizi Ya Kweli: Usiku Wa January 20, 2015

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2016
Posts
20,746
Reaction score
25,638
USIKU WA JANUARI 20, 2005

SIMULIZI YA KWELI

INNOCENT A. NDAYANSE

KUNA MATUKIO MBALIMBALI YA KUFURAHISHA, KUSIKITISHA NA HATA YA KUTISHA YATOKEAYO KILA SIKU DUNIANI. KATIKA SIMULIZI HII NINAKULETEA MTIRIRIKO WA TUKIO HALISI LILILONIKUTA MWANZONI MWA MWAKA 2005 NA KUZUA TAHARUKI KATIKA JAMII YA ENEO NILILOKUWA NIKIISHI.

NI TUKIO LILILOIBUA MASWALI MENGI NA HISIA TOFAUTI KWA WAKAZI WA ENEO HILO NA HATA WALE WALIOKUWA WAKIISHI MAENEO MENGINE, KILA MMOJA KWA UPEO WAKE WA KUFIKIRI.

SIMULIZI HII NI YA KWELI KWA ASILIMIA MIA MOJA, TOFAUTI KABISA NA HADITHI NYINGINE ZILIZOTANGULIA NA ZITAKAZOTUJIA SIKU ZA USONI.

TIRIRIKA NAYO…

* * ***
HUDAIWA kuwa kila mtu huwa na jambo ambalo nafsi yake imejikita zaidi. Hupenda sana kulifanya jambo hilo hata kama itamlazimu kutumia gharama za ziada.

Kuna anayependa kukaa vijiweni na kupiga stori. Mwingine ni mpenzi wa kunywa pombe. Mwingine hupendelea sana kutazama televisheni. Yupo aliyebobea katika michezo ya kamari. Na yupo ambaye yeye akili yake yote ni kwenye uhusiano wa mapenzi, leo yuko na huyu, kesho yuko na yule.

Ndiyo, kila mmoja ana kile ambacho roho yake hukipenda na huwa tayari hata kuvuruga bajeti yake na kubadili ratiba zake za siku ili tu airidhishe nafsi yake.

Mimi nilitokea kupenda kupiga gitaa tangu nikiwa na umri wa miaka 14. Niliipenda fani hiyo kwa kuwa nilikuwa siachani na kaka yangu ambaye tulikuwa tukipendana sana tangu utotoni kabisa. Aliitwa Barack Ambrosse Ndayanse.

Barack alikuwa mpenzi zaidi wa gitaa, labda zaidi yangu na alikuwa akipiga na rafikiye kipenzi, Ramadhani Zahoro ‘Bangwe’, wakitoroka darasani na kwenda kujificha kwenye shamba la mihogo na kuanza kupiga gitaa lililotengenezwa kwa zana hafifu za galoni.

Wakati huo tulikuwa tukiishi kitongoji cha Bangwe, mjini Kigoma. Kwa kuwa mara kwa mara nilikuwa nashinda naye, nilishawishika na mimi kujifunza kutekenya nyuzi za gitaa hilo la kiasili.

Mwanzoni mwa mwaka 1978, tukajiunga kwenye kwaya ya Kanisa la Anglikana Mwanga mjini Kigoma, usharika wetu na ambao baba yetu mzazi alikuwa Shemasi kanisani hapo.

Katika kipindi hichohicho, wakaja wanamuziki wawili kutoka katika kwaya iliyokuwa ikitikisa ukanda wa Afrika Mashariki, Mwanza Town Choir. Wanamuziki hao walikuwa wamekuja mjini Kigoma kwa ajira za Upanuzi wa Bandari na hivyo wakaamua kuwa wanakuja kanisani hapo kupiga magitaa.

Ni hapo ndipo mimi na Barack tulipogundua kuwa viwango vyetu vilikuwa duni sana na kuanza kujifunza kwa hao vijana waliotoka Mwanza.

Tuliendelea na fani hiyo na baada ya miaka mitatu tulikuwa katika viwango vilivyokubalika kwa wapenzi wengi wa muziki. Nakumbuka kuwa tulikuwa wepesi wa kusikiliza nyimbo zilizokuwa zikitamba miaka ile.

Baadhi ya nyimbo hizo ni Nyako Konya (Orchestre Mangelepa), Memi, Moni Afinda (Orchestra Kiam), Mikolo Mileki Mingi (Orchestre Veve) na nyingine nyingi za Kikongo.

Nyimbo za Tanzania, Usia wa Baba, Mwanameka na Betty za Dar International pia zilikuwa zikituteka kwa kiasi kikubwa. Kusikiliza sana nyimbo hizo kulikwenda sambamba na uigaji ili tuweze kupiga hatua.

Mara nyingi nilikuwa nikimsikia kaka yangu akisema, “Kama wao wameweza kwa nini sisi tusiweze?”

Mwaka 1985 tukawa tumekomaa zaidi, Baraki akiwa imara kwenye upigaji wa gitaa zito la besi na rythm ilhali mimi nikikomaa zaidi katika gitaa la solo kiasi cha kujikuta tukianza kupiga katika bendi moja iliyokuwa mjini hapo ya Super Kibisa Orchestra tukiwa na Ramadhani Zahoro ‘Bangwe.’

Hata hivyo, baadaye Ramadhani aliondoka Kigoma na kulivaa Jiji la Dar es Salaam, mimi na Barack na wanamuziki wengine tukabaki tukiliendeleza ‘sebene’ kwenye bendi hiyo na wakati huohuo pia tukiupiga muziki kwenye kwaya ya kanisa. Kwa sasa Ramadhani Zahoro ‘Bangwe’ ni mpigaji gitaa tegemeo wa Msondo Ngoma Music Band ya Dar es Salaam.

Kuanzia mwaka 1990, kasi ya kupiga muziki ikanipungukia kutokana na wingi wa majukumu. Miaka miwili baadaye nikaamua kubadili mazingira. Nikahamia jijini Dar es Salaam na nikawa napiga gitaa mara chache pale nilipoliona na nilipokuwa na nafasi ya kufanya hivyo.

Siku zikaenda, hatimaye nikajiunga na Kwaya ya Amkeni KKKT Usharika wa Kinondoni mwaka 1996. Hapo sikudumu sana kwa sababu zilezile za kubanwa na majukumu.

Mwaka 1997 mwishoni nikajiunga na Kwaya ya Vijana na Uinjilisti Hananasif Kinondoni, kwa maombi ya mwalimu mmoja aliyewahi kuniona nikipiga gitaa kule Usharika wa Kinondoni KKKT.

Hapa Hananasif nimekaa sana na kwa kuwa ndipo yalipokuwa masikani yangu nikajikuta nikirudi kwenye fani kwa kasi ya ajabu.

Mapenzi yangu kwa mpiga solo mahiri wa enzi za miaka ya 90, Alain Makaba wa Wenge BCBG yakairudisha ile ari yangu ya kupiga gitaa na hasa kwa kipindi kile Wenge walipoibua albamu ya Pentagone mwaka 1994.

Sasa nikarudi kwenye gitaa kwa nguvu kubwa. Kila wimbo uliopigwa na Alain Makaba nikawa nauiga kwa kiasi kikubwa. Kiwango kikapanda.

Mwishoni mwa miaka ya 1990, bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ ikazaliwa. Nakumbuka bendi hiyo ilikuwa inapiga muziki wake kwenye viwanja wa Leaders Club bureee! Kila Jumapili mchana!

Watu tukawa tunajimwaga hapo kila wikiendi na hasa kwa kuzingatia kwangu mimi pale palikuwa ni jirani sana na nyumbani. Mpangilio mzuri wa muziki wa Twanga, sanjari na upigaji wa Adolf Mbinga katika gitaa la solo vilinivuta sana na hivyo sasa nikawa nikibuni vyangu, nachanganya na vionjo vya ama gwiji Alain Makaba au mzalendo Adolf Mbinga hasa na wimbo wake wa ‘Kisa Cha Mpemba.’

Nikaendelea kuwa bora katika fani hiyo huku pia nikifanya kazi ya ajira katika Kampuni ya Uchapishaji Vitabu ya HEKO.

USIKU JANUARI 20, 2005

HII ilikuwa ni siku, kama siku nyingine ambazo niliamka na kwenda kwenye shughuli zangu za kila siku. Kwa siku hii nilizungukia mitaa ya katikati ya jiji ambako nilikuwa nafuatilia oda ya biashara kwa wafanyabiashara wakubwa wa maduka ya vitabu.

Ilipofika jioni, kitu kama saa 11 hivi nikawa nimesharudi Kinondoni na moja kwa moja nikaelekea kanisani kwa ajili ya mazoezi ya kwaya. Mazoezi yalimalizika saa moja usiku. Kijigiza kilikuwa kimekwishaitawala anga.

Baada ya mazoezi nilitoka na rafiki yangu, Kimambo aliyekuwa akiishi Kinondoni Shamba. Nilikuwa nikimsindikiza na tulikuwa na mazoea ya kuzungumza hili na lile hususan kuhusu kwaya kila tumalizapo mazoezi.

Siku hiyo, mara tulipomaliza mazoezi nilichoropoka hadi nyumbani ambako hakukuwa mbali. Nikavua viatu na kuvaa kandambili kwa kuwa siku hiyo sikuwa natarajia kwenda mbali.

Nikarudi eneo la kanisa ambako nilimkuta Kimambo akiwa nje ya uzio akizungumza na wanakwaya wengine huku akinisubiri.

Kabla hatujaondoka akaja rafiki yangu mwingine wa ‘kufa na kuzikana,’ Willy. William Jacob Kalumila. Huyu alikuwa ni mwalimu wa kwaya na nilizoeana naye kwa kiasi kikubwa na kuwa marafiki wa karibu zaidi kwa kuwa alikuwa akifundisha nyimbo zenye mwelekeo nilioupenda.

“Kocha vipi, tupandishe Mkwajuni?” Willy aliniambia.

Kwa kuwa tayari Kimambo alikuwa amenisubiri kwa muda mrefu, nikaona haitakuwa vizuri kumwacha na kuambatana na Willy. Kimambo angeona nimemdharau. Hivyo, kwa ustaarabu nikamjibu Willy, “Hapana kocha. Leo ngoja nimpe tafu mzee wa Kinondoni Shamba.”

Willy hakujali, tukaagana.

Mara tu nilipofika Kimambo alisitisha maongezi na kuniambia, “Inno, twen’zetu.”

Tukaondoka taratibu, tukipiga stori kuhusu mazoezi ya siku hiyo. Tukapita jirani na Shule ya Msingi Hananasif katika eneo lililokuwa na miti mingi iliyoongeza nguvu ya giza kwa kuwa hakukuwa na nyumba zilizokuwa kando ya barabara.

Tukawa tunapita Mtaa wa Ngano, mtaa uliokuwa umepandwa miti mingi iliyounda kivuli kizito mchana na kutengeneza giza la kuogofya usiku.

Mazingira yale tulikwishayazoea, hivyo hatukuwa na wasiwasi wowote. Tukawa tukitembea taratibu huku tukizungumza.

Hatimaye tuliuacha Mtaa wa Ngano, tukashika Mtaa wa Wakulima.
Mbele kidogo tukawa tunapita katikati ya makaburi. Tulipofika mwisho wa eneo la makaburi, tukawa kando ya Barabara ya Kinondoni, eneo lililojulikana na linalojulikana mpaka sasa kwa jina la MWEMBEJINI.

Hapo tulikuta mchanganyiko wa watu. Walikuwepo waliokuwa kituoni wakisubiri daladala na wengine kwa harakaharaka unaweza kuwaita ‘vibaka’ au ‘mateja’ kwani walikuwa ni vijana wanne wakizunguka-zunguka tu kituoni hapo huku wakizungumza kwa sauti zenye mikwaruzo inayokera, sigara na bangi zikivutwa bila ya wasiwasi.

Mimi na Kimambo hatukuwajali kama ambavyo nao hawakutujali. Mara kwa mara watu wa aina ile huwa eneo lile wakivizia daladala lililojaa ili waingie na kubanana na abiria na matokeo yake abiria ‘hulizwa.’ Au huvizia abiria atakayeteremka na kuzubaa-zubaa na wao huwa wepesi kwa kumpora chochote chenye manufaa kwao.

Magari mengi yalikuwa yakipita barabarani muda huo yakitokea katikati ya jiji hivyo ikatulazimu kusubiri. Mara daladala kutokea mjini likafika. Lilikuwa limejaa pomoni. Ile kusimama tu vijana wale nao wakasogea mlangoni kama abiria wa kawaida. Konda alipoteremka na kuwapisha abiria wateremke, vijana hawa waliokuwa chini wakawa wamesogea zaidi mlangoni.

Ndipo kilipotokea kituko. Mwanamume mmoja ambaye alikuwa amevaa nadhifu alipoteremka na kuanza kuvuta hatua akija upande huu wa Barabara ya Wakulima, alifuatwa na vijana wawili na haraka mmoja akampiga ngwara, jamaa akaenda chini kama gunia la mashudu tii!

Kabla hajajitetea, mikono ya vibaka wale ikawa imekwishatalii mifukoni mwake na kutoka na pesa na simu kisha hao wakakimbilia makaburini.

Yule jamaa aliyevamiwa alichanganyikiwa. Tukamsogelea na kumnyanyua. Tukamsihi aende tu nyumbani kwa kuwa vibaka wale wameshatokomea. Akaondoka huku akiilalamikia simu yake aliyodai kuwa kainunua siku tatu zilizopita kwa bei ya kutisha katika duka moja Mtaa wa Samora, katikati ya jiji.

Tulimwonea huruma lakini hatukuwa na namna ya kumsaidia. Mimi na Kimambo tulivuka barabara na nikaendelea kumsindikiza.

“Tuingie pale kwenye kantini tunywe maziwa moto,” Kimambo aliniambia mara tulipokuwa upande wa pili wa barabara.

Sikuwa na sababu ya kukataa. Nikamjibu, “Poa tu.”

Tukaingia. Akaagiza maziwa moto na keki mbili. Tukanywa taratibu huku tukiendelea kuzungumzia uboreshaji wa muziki wa gitaa, fani iliyokuwa inayateka maongezi yetu kila tunapokuwa pamoja.

Nusu saa baadaye, kama saa 2 hivi, tuliagana, yeye akaenda kwake ambako kwa hapo hakuwa mbali sana na mimi nikaanza safari ya kurejea nyumbani Hananasif. Kumbuka, nilikuwa nimetoka nyumbani nikiwa nimevaa makubadhi tu miguuni na sikutarajia kuwa ningetembea mpaka huko Kinondoni Shamba.

Hata hivyo, nilijifariji kuwa kwa giza lililokuwapo isingekuwa rahisi kila mtu kubaini kuwa nimevaa nini miguuni. Sikujali. Nikaanza kuvuta hatua, nikavuka barabara huku nikiwa nimekifungua kijiredio changu kidogo aina ya Panasonic nikisikiliza muziki.

Wakati niko eneo la katikati ya makaburi, nikimulikwa na mwangaza mkali kutoka kwenye taa kubwa zilizolizingira jengo moja lenye ofisi nyeti sana serikalini, mara nikakutana mwanamke mnene kiasi, mweupe akiwa amevaa gauni pana lakini lenye mvuto. Nuru ya taa za jengo hilo ilimmulika vizuri mwanamke huyo na kuuweka bayana uzuri wa sura na umbo lake.

TUTAONANA TENA SAA KUMI JIONI.....NIENDELEE KUKUJUZA KILICHOJIRI***
 
USIKU WA JANUARI 20, 2005 (SEHEMU YA PILI)

SIMULIZI YA KWELI

INNOCENT A. NDAYANSE

***** ***** *****

KUNA MATUKIO MBALIMBALI YA KUFURAHISHA, KUSIKITISHA NA HATA YA KUTISHA YATOKEAYO KILA SIKU DUNIANI. KATIKA SIMULIZI HII NINAKULETEA MTIRIRIKO WA TUKIO HALISI LILILONIKUTA MWANZONI MWA MWAKA 2005 NA KUZUA TAHARUKI KATIKA JAMII YA ENEO NILILOKUWA NIKIISHI.

NI TUKIO LILILOIBUA MASWALI MENGI NA HISIA TOFAUTI KWA WAKAZI WA ENEO HILO NA HATA WALE WALIOKUWA WAKIISHI MAENEO MENGINE, KILA MMOJA KWA UPEO WAKE WA KUFIKIRI.

SIMULIZI HII NI YA KWELI KWA ASILIMIA MIA MOJA, TOFAUTI KABISA NA HADITHI NYINGINE ZILIZOTANGULIA NA ZITAKAZOTUJIA SIKU ZA USONI.
TIRIRIKA NAYO…

*** *** ***

Wakati niko eneo la katikati ya makaburi, nikimulikwa na mwangaza mkali kutoka kwenye taa kubwa zilizolizingira jengo moja lenye ofisi nyeti sana serikalini, mara nikakutana mwanamke mnene kiasi, mweupe akiwa amevaa gauni pana lakini lenye mvuto. Nuru ya taa za jengo hilo ilimmulika vizuri mwanamke huyo na kuuweka bayana uzuri wa sura na umbo lake.

Dada huyo alipunguza mwendo na kunisogelea kisha akanichangamkia haraka, “Oyaa mambo vipi?”

“Poa tu,” nilimjibu na kumtazama kidogo kisha nikaendelea na safari yangu. Hakuniachia. “Anko, samahani kidogo,” aliniambia huku akiwa amesimama na kunigeukia.

Nikaiheshimu kauli yake. Nikasimama na kumsikiliza.

Akanisogelea. Tukawa jirani sana. Tukatazamana. Nikahisi manukato makali kutoka maungoni mwake huku tabasamu likichanua usoni pake na jino moja sijui la dhahabu au mfano wa dhahabu likajitokeza kinywani mwake.

Pale kifuani alikuwa na ujazo wa wastani uliovutia. Alipendeza kutazamwa. Katika kuonesha kuwa hataki kupoteza muda, na alikuwa mwepesi wa uchokozi kwa kunisogelea zaidi na kuniegemea, mkono wake wa kushoto ukiwa bega la kulia na wa kulia ukijaribu kutalii maungoni mwangu. Sikumruhusu sana. Nikautoa mkono huo kistaarabu.

“Vipi?” hatimaye alisema kwa mnong’ono wa kibiashara zaidi huku akinishika mkono.

Kwa kuwa nilikuwa mwenyeji wa eneo hilo sikuhitaji kujiuliza ni kipi kilichomfanya mwanadada huyu anisimamishe. Watu wa aina yake muda huo huwa wameshatanda kando ya Barabara ya Kinondoni pale Mwembejini, kule kwenye makaburi ya ‘Lang’ata’, kwenye makutano ya Barabara ya Tunisia na Kinondoni, juu ya eneo la Viwanja vya Leaders Club hadi maeneo mengine ya huko Ada Estate wakiwa mawindoni, wakiwavizia wanaume ‘wenye njaa.’

Japo alinigeuza mimi kuwa windo lake, hata hivyo sikutaka kumjibu vibaya. “Poa tu,” nami nilimjibu kwa sauti ya chini, nikimruhusu aendelee kukishika kiganja cha mkono wangu na wakati mwingine kukitomasa-tomasa.

Labda alitarajia kuwa kitendo cha kunitomasa kingenivurugia programu yangu haraka sana na hivyo kujikuta nikikubaliana na hila zake. Haikuwa hivyo. Hakunipa msisimko wowote kwa kuwa nilijua fika kuwa yuko kikazi Zaidi, yuko kibiashara zaidi.
Nilijua kuwa hata kama mimi ningediriki kumtekenya kidogo huenda angejitia kushtuka huku akitoa ukelele wa mbali akijifanya kasisimkwa kiukweli! Uongo mtupu!

“Inakuwaje?” akarusha swali na kumalizia, “Twen’zetu basi tuka…” alichomalizia kukitamka kilikaribia kunichekesha kwa kuwa nilitarajia ndivyo angesema.

Hata hivyo sikucheka. Nikaendelea kuonesha kumjali. Nikamjibu kwa upole, “Usijali, tufanye siku nyingine. Leo siko fresh,” nikaongeza huku nikijipapasa mifuko kuonyesha kuwa sikuwa na pesa.

“Una sh’ngapi?” aliniganda.

“Sina kitu,” kwa kiasi fulani nilianza kuchukia. Hawa viumbe wenye biashara hizi mara nyingi huwa ving’ang’anizi! Na ukiwachekea utajuta!

Akanitazama usoni na kugundua kuwa sasa sikuhitaji kuendelea kujadili kuhusu hiyo hoja yake na wala sikuwa nahitaji kuwa naye. Akaniachia mkono huku kwa unyonge akisema, “Poa, acha sie tukasake mkwanja viwanja…”

Sikumjibu.

Akaondoka taratibu, akijitupatupa kwa mwendo wake wa ‘bata mzoea kupata.’ Tembea yake ilitosha kudhihirisha kuwa yuko kazini, tayari kwa lolote na tayari kwa yeyote.

Nikaendelea kuvuta hatua taratibu hadi nilipofika Mtaa wa Ngano. Kama awali, mtaa huu ulikuwa umetulia lakini sasa niliona kama ukimya ulizidi. Ulikuwa ni ukimya uliotoa taswira ya kuogofya kidogo kwani mbele yangu sikuona hata mtu wala gari. Nilikuwa peke yangu! Miti mikubwa iliyokuwa imejipanga vizuri kando ya barabara hiyo ilikuwa imetulia kama inayonishangaa.

Mara ghafla nikasikia upepo mkali ukivuma, upepo ulioambatana na kimbunga kidogo. Vumbi likatimka mbele yangu, hatua kama kumi hivi! Miti ile iliyokuwa imetulia sasa ikatikisika kwa nguvu!

Nikashangaa kisha nikajawa na hofu! Haukuwa upepo wa kawaida! Huwa imezoeleka kuwa kama kuna upepo basi pia mawingu ya mvua hutanda angani na kuashiria mvua muda mfupi ujao. Kwa usiku huu, anga ilikuwa imetakata sana, nyota zikionekana kwa uwazi sanjari na mbalamwezi iliyonona vilivyo.

Mara mbele kidogo, kushoto ambako kulikuwa na kijibaa kidogo chenye wateja wachache kukazuka kelele kali, sauti kama ya mwanamke. Punde msichana aliyevaa blauzi pana na suruali akatoka mbio akikimbilia barabarani, akija huku nilikokuwa!
Nikabaki nimeduwaa!

Aliponifikia, akanitazama kidogo kisha akanipita na kuendelea kukimbia akielekea Mwembejini. Nikageuka kumtazama. Nikaona akizidi kukimbia akielekea makaburini. Akaingia eneo hilo la makaburi na kunifanya nizidi kushangaa. Nikajiuliza ni kipi kimemtoa mkuku humo ndani ya baa? Na mbona amenitazama kidogo kwa macho makali na bila hata ya kuomba msaada kanipita kama hajaniona na kuendelea kukimbia?

****TUKUTANE KESHO ASUBUHI.*
 
USIKU WA JANUARI 20, 2005 (SEHEMU YA TATU)

SIMULIZI YA KWELI

INNOCENT A. NDAYANSE

***** ***** *****

Aliponifikia, akanitazama kidogo kisha akanipita na kuendelea kukimbia akielekea Mwembejini. Nikageuka kumtazama. Nikaona akizidi kukimbia akielekea makaburini. Akaingia eneo hilo la makaburi na kunifanya nizidi kushangaa. Nikajiuliza ni kipi kimemtoa mkuku humo ndani ya baa? Na mbona amenitazama kidogo kwa macho makali na bila hata ya kuomba msaada kanipita kama hajaniona na kuendelea kukimbia?

Je, kuna usalama kwangu kama nitaendelea kwenda mbele ambako nitakuwa naisogelea baa hiyo? Kwa nini nisigeuze njia nikarudi kule mwembeni na kupanda daladala hadi Kinondoni ‘A’ kisha nikatembea taratibu hadi nyumbani? Au kwa nini nisiifuate Barabara ya Wakulima hadi kwenye Kanisa la Wasabato na kuendelea hadi Shule ya Hananasif ambako nitakutana na barabara ya kuelekea nyumbani kwangu?

Maswali mengi yalinijia kwa muda mfupi. Nikajikuta nikikosa uamuzi wa haraka. Nikaendelea kutulia palepale nikiangalia mbele yangu ambako upepo uliokuwa ukivuma sasa ulianza kupungua taratibu. Hatimaye hali ikatulia. Nikapiga moyo konde na kujipa ujasiri. Nikaanza kutembea tena. Nikavuta hatua taratibu huku nikihisi kutokuwa na utulivu moyoni. Kwa mbali nikahisi mapigo ya moyo yakizidisha kasi. Naogopa? Naogopa nini? Na kwa nini niogope?

Nilipofika jirani na kile kijibaa, upepo ukaanza kuvuma tena! Kwa msaada wa mwangaza mdogo wa taa zilizokuwa zikiwaka ndani ya baa hiyo nikafanikiwa kuona kitu kama kamba ndefu mbele yangu. Kamba nyeusi. Nilijenga imani kuwa ni kamba kwa kuwa kitu hicho kilikuwa kimetulia tuli kandokando ya barabara.

Sikuwa na wazo lolote tofauti kuhusu kitu hicho, nikaendelea kutembea hadi nikawa hatua kama mbili hivi kutoka mbele ya kitu hicho.

Haikuwa kamba!

Alikuwa ni nyoka! Na hakuchelewa, alijivuta kwa kasi na kutua kwenye kiganja cha mguu wangu wa kulia, akadonoa haraka kisha kwa kasi ileile akajivuta na kuingia nyasini, kando ya barabara! Eneo aliloingia kiumbe huyo hatari kulikuwa na ua kubwa lililounda chaka la aina yake hivyo niliishia kusikia sauti ya “Shhhhh…ssshhhhh….” ishara ya kutokomea ndani ya chaka hilo lililokuwa jirani sana na kijibaa hicho!

Lilikuwa ni tukio la haraka sana na hata maumivu yake pia yalikuja kwa kasi vilevile! Sekunde kama kumi za awali baada ya kuumwa na nyoka huyo niliweza kukanyaga chini na kuvuta hatua moja tu. Kitendo cha kuvuta hatua ya pili na kukanyaga tena chini kilizua maumivu makali sana! Ndiyo, hayakuwa maumivu ya kawaida! Yalikuwa makali kuliko unavyoweza kukadiria!

Simulizi kuhusu madhara ya sumu ya nyoka zilinijia akilini papohapo na kuzua kumbukumbu za kutisha. Zipo sumu za nyoka ambazo hufanya kazi haraka sana kiasi cha kuua kwa dakika moja au mbili! Sumu nyingine huweza kumtia mtu ulemavu wa maisha! Sumu za nyoka kama Hongo au kwajina lingine Futa, japo huweza kuua kuanzia muda wa nusu saa na kuendelea tangu ipenye mwilini, hata hivyo bado inaaminika kwa wataalamu kuwa ni sumu ambayo huweza kumtia mtu ulemavu wa viungo.

Nikahisi uhai unakaribia kuniacha! Jasho likaanza kunitoka! Sikuona mtu yeyote mbele wala nyuma! Ndani ya sekunde kama tano hivi kukawa na ongezeko la maumivu maradufu! Nikalazimika kuushika mguu ulidungwa jino na joka lile, nikaukunja juu-juu kwa nyuma na kusimamia mguu wa kushoto pekee japo kwa shida. Nikawa nikihemea juu-juu. Nilipozidiwa nikajikuta nikianguka chini, katikati ya barabara huku kwa mbali nikisikia sauti ya mtu akicheka. Sauti ya kike!

Nilianza kukata tamaa ya kuishi. Simulizi nyingi nilizokwishazisikia tangu utoto kuhusu madhara ya kuumwa na nyoka ziliniletea kumbukumbu ya kuogofya akilini mwangu. Nikatulia chini, katikati ya barabara huku nikiangalia huku na kule na kuomba Mungu atokee mtu wa kunisaidia.

Hatimaye haikutimu hata dakika moja, mtu mmoja, mwanamume akatokea ndani ya kile kijibaa, akitembea kwa kasi lakini akionekana kutokuwa na wasiwasi wowote. Aliponiona, akashtuka na kunisogelea.

“Vipi?” ndivyo alivyoniingia.

“Nyoka!” nilimjibu. Sasa maumivu yalikuwa yakizidi na kwa hali hiyo nikawa najikunja na kujikunjua pale chini huku nimeushika mguu uliojeruhiwa.

“Hee!” alibwata kwa mshtuko. “Atakuwa ni yule nyoka tu….duh!”
Akanishika mkono na kunisaidia kunyanyuka. “Jitahidi kujikokota tufike hata pale kwenye ile nyumba!”

Mbele yetu kulikuwa na nyumba ambayo nilisikia kuwa ilikuwa ikimilikiwa na Meya wa moja ya manispaa za Jiji la Dar.

Nilitembea kwa mguu mmoja wa kushoto huku wa kulia nimeukunja juu kwa nyuma na jamaa yule kapenyeza mkono wake kwapani kwangu kulia ili kuwa mhimili mzuri wa kutembea. Nikawa narukaruka hadi kwenye hiyo nyumba ambayo ilikuwa hatua kama kumi na tano au ishirini hivi kutoka pale nilipokumbwa na zahama.

Tulipofika kwenye nyumba ile tukapokewa na binti mmoja na kijana mmoja wa kiume waliosadikiwa kuwa walikuwa wakiilinda tu nyumba hiyo. Taarifa za kuumwa kwangu nyoka zikazidi kuenea tangu nilipofika hapo. Dakika tano baadaye watu saba walikuwa ndani ya nyumba hiyo, mmojawao akiwa ni mzungu wa asili ya Uholanzi, ambaye alikuwa akiishi jirani na nyumba hiyo akiwa pia na ofisi ya shirika lake binafsi hapohapo.

Yule mzungu ndiye aliyeonekana kutaharuki zaidi alipoisikia taarifa yangu. Akawa akihaha huku na kule kusaka kamba ya kunifunga mguuni ili sumu isisambae. Vijana wengine waliokuwa pale nao walikuwa wakihangaika kivyao, baadhi yao wakionekana kuogopa kuwa labda nyoka huyo atazuka tena na kumdhuru yeyote kati yao. Baada ya dakika kadhaa mmoja akaja na waya wa umeme na wembe.

“Mchanje kwanza!” mmojawao alisema.

Nikachanjwa juu kidogo ya kiganja cha mguu! Damu nzito kama tope, damu nyeusi tii, ikatoka kama mabonge fulani hivi. Wote walioshuhudia wakashtuka! Mshtuko wao ukaniongezea hofu. Simulizi nyingi nilizokwishazisoma na kuzisikia kwa watu mbalimbali kuhusu kasi ya madhara ya sumu ya nyoka mwilini mwa mwanadamu sanjari na taharuki iliyowakumba hawa watu walionizunguka ilinifanya nijione kuwa niko katika dakika za mwisho za uhai wangu. Hofu ilizidi kunitawala!

“Chanja tena juu yake!” ushauri ukatolewa na mtu mwingine.

Mwenye wembe akachanja mara mbili umbali kama wa inchi tatu, juu ya pale alipochanja awali.

“Heee…” wakazidi kubwata kwa mshangao. Hata hapo ilitoka damu nzito na nyeusi kama tope!

Wakachanja sehemu kama nne tofauti mpaka jirani sana goti lakini bado hakukuwa na nafuu yoyote, pote pakaonyesha kuwa tayari pameathiriwa na sumu ya joka lile.
Mguu ukatapakaa damu! Haukupendeza kutazamwa! Mabonge bonge hayo ya damu yakawa yakishuka taratibu na kunitisha hata mimi mwenyewe! Maumivu yakazidi kuwa makali!

Kilichonitia woga ni kuwaona hata hawa vijana waliokuja kunisaidia nao wakionekana kutaharuki. Baadhi walikuwa wakinikodolea macho tu bila ya kufanya chochote. Hatimaye yule aliyekuwa akinichanja mguuni akasema, “Kunja suruali zaidi bro!”

Nikafanya alivyotaka. Nilikunja suruali hadi mapajani.

Akachanja kwenye paja mara tatu. Damu iliyotoka hapo ni ile ambayo wenyewe tumeizoea kuwa ni damu ya kawaida ya mwanadamu yeyote. Haraka jamaa huyo akaamua kuitumia kamba ya katani iliyokuwa imeletwa hapo na kijana mmoja wa Kiarabu ambaye alitoka kwenye nyumba kama ya tano hivi baada ya kusikia kuhusu tukio hilo.

Nikafungwa kamba hiyo kama vile ni mtu ninayezuiwa kutoroka. Ilikazwa imara kwenye paja ikiaminika kuwa itasaidia kuizuia sumu kupanda zaidi na kuleta madhara zaidi.

“Usiogope,” yule jamaa aliyenifunga kamba aliniambia baada ya kuona jinsi nilivyotaharuki. “Hapa tumekomesha. Sumu haipandi tena. Imebaki kazi ya daktari.”

Kilichofuata ni kukabidhiwa fimbo ya kunisaidia kutembea mpaka nje, kando ya barabara ambako yule kijana wa Kiarabu alikuwa kaegesha gari dogo aina ya Toyota Mark 11 na nikaingia ili wanipeleke hospitali.

“Usihofu tena,” yule kijana wa Kiarabu ambaye nilikuwa nimeketi naye katika kiti cha nyuma naye aliongeza kunipa matumaini. Kisha akavuta suruali juu na kunionyesha mguu wake wa kushoto ulivyobabuka! Ulikuwa unatoka magamba kuanzia chini mpaka kwenye goti!

“Unaona hii?!” aliniuliza huku akinitazama usoni kwa macho makali.

Sikumjibu, nikautazama tu ule mguu, tendo nililoamini kuwa lilitosha kumfanya ajue kuwa nimemsikia.

*****TUKUTANE TENA KESHO***
 
USIKU WA JANUARI 20, 2005 (SEHEMU YA NNE)

SIMULIZI YA KWELI

INNOCENT A. NDAYANSE

***** ***** *****
“Usihofu tena,” yule kijana wa Kiarabu ambaye nilikuwa nimeketi naye katika kiti cha nyuma naye aliongeza kunipa matumaini. Kisha akavuta suruali juu na kunionyesha mguu wake wa kushoto ulivyobabuka! Ulikuwa unatoka magamba kuanzia chini mpaka kwenye goti!

“Unaona hii?!” aliniuliza huku akinitazama usoni kwa macho makali.

Sikumjibu, nikautazama tu ule mguu, tendo nililoamini kuwa lilitosha kumfanya ajue kuwa nimemsikia.

“Ni hilo joka!” alisema. “Nina wiki kama tatu hivi tangu linidonoe! Nilikuwa nimekaa hapo nyumbani, nje nikipunga hewa. Likatokea huko lilikotoka, spidi ya kufa mtu dadek! Liliponifikia tu likaning’ata na kuteleza msh’kaji wangu. Jeusi na refu kishenzi! Nilipiga kelele msh’kaji wangu, akaja faza na kijiwe f’lani hivi sijui kakitoa wapi… akaniwekea mguuni, nasikia huwa kinafyonza sumu!

“Halafu wakanipeleka Aga Khan Hospital. Wallahi Ningekufa! Yaani ni kama niliponea chupuchupu! Wiki nzima sikuweza kutembea. Sasa nimepona lakini cheki mwana nimekuwa kama nyoka au kenge kudadek! Magamba haya nd’o yanatoka…sijui nd’o ngozi iliyoharibiwa na sumu?! Nimekuwa ka’ nyoka mwenyewe!”

Nilimwelewa lakini sikumjibu kitu. Mawazo yangu yalikuwa juu ya zahama iliyonikuta. Nikamkumbuka mke wangu. Nikawaza, je, atawaza kuwa niko wapi? Anaweza kuwa na mawazo dhaifu akafikiria kuwa nimekwenda kwa mwanamke wa pembeni? Nimpigie simu?

Swali hili la mwisho nikaona ndilo linapaswa kufanyiwa kazi. Hata hivyo, usalama kwanza! Ndivyo nilivyoamini. Nikatulia huku nikiyasikilizia maumivu ya jeraha na zile chale ambazo nazo ziliongeza maumivu huku nikizidi kutishika kila nilipoutazama mguu huu na kushuhudia damu hiyo yenye mabonge-bonge mazito ikizidi kutoka kwenye yale maeneo yenye chanjo za wembe.

Gari likaenda hadi eneo la Mkwajuni ambako tuliingia katika zahanati moja ya MICO. Daktari akatupokea kwa moyo mkunjufu na kuniangalia kwa macho ya huruma.

Baada ya kupata maelezo akasema, “Ni tatizo kubwa kwa upande wetu hapa kwenye zahanati. Sisi hatuna uwezo wa kukuhudumia lakini kwa kupunguza tatizo ili sumu isiende kudhuru figo, nitakuchoma sindano moja ya kinga halafu itabidi uende Mwananyamala.”

Wale wasamaria walionileta waliposikia hivyo wakamshukuru daktari na kuniambia kuwa wao wanarudi nyumbani kwa kuwa hata gari lao halina mafuta ya kuweza kunipeleka huko Mwananyamala.

Nikajua kazi ninayo. Hata hivyo, nikawashukuru kwa msaada huo wa kunifikisha hapo. Nikajali kwanza kupata huduma hiyo ya sindano. Na nilipokwishachomwa, nikatoka nje na fimbo yangu dhaifu huku bado damu ikizidi kunitoka kwa wingi na baadhi ya watu wakawa wakiniangalia kwa mshangao bila ya msaada.

Nikaanza kujikokota nikielekea kituo cha daladala huku nikiwaza je, kuna daladala itakayonikubali kwa hali ile niliyokuwa nayo? Guu limeshavimba na limetapakaa damu nyeusi ti! Nikajisikia kukata tena tamaa!

Nikajikokota tu bila ya matumaini hatua kama kumi hivi, jamaa mmoja akanisimamisha na kuniuliza, “Vipi aisee?”

Nikamtazama na kugundua kuwa ni fundi makenika ambaye tulikuwa tukikutana mara kwa mara jirani na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Usharika wa Azania katikati ya jiji akitengeneza magari katika kijigereji bubu kilichokuwa katika eneo hilo. Jamaa huyo ambaye siwezi kulisahau jina lake, Lyimo, alikuwa msaada mkubwa kwangu kwa siku hiyo.

Japo tulifahamiana, lakini hatukuwa na ukaribu, ni kule kujuana-juana tu kimjini-mjini kama ilivyo kwa wakazi wengi wa Jiji la Dar. Lakini usiku huu wa saa tatu kasoro, jamaa huyu alisitisha kuendelea na safari pale tu nilipomdokeza mkasa ulionikuta.

Hatua chache kutoka pale tulipokuwa kulikuwa na teksi mbili zimeegeshwa. Haraka akamwita dereva mmoja na kumwambia, “Danny, mpeleke msh’kaji wangu Mwananyamala Hospital haraka.”

Dereva yule aliniangalia kwa mshangao na kuniuliza, “Umekumbwa na mkasa gani?”

“Huu sio muda wa maswali!” Lyimo aliingilia kati. “Mpeleke halafu ukirudi uje kuchukua pesa yako.”

Dereva alinifungulia mlango wa kushoto, mbele huku akiniambia, “Ingia msh’kaji.”

Kisha Lyimo akaniuliza, “Nyumbani wana taarifa?”

Ni hapo nilipojiwa na kumbukumbu kuhusu umuhimu wa kufikisha taarifa nyumbani. Nikamjibu kuwa hakuna taarifa na nikampa namba mbili za simu, moja ya rafiki yangu na nyingine ya mke wangu.

“Simu yangu haina salio na haina chaji, inaweza kuzima muda wowote,” nilimwambia. “Tafadhali, ukiweza nisaidie kuwapigia kuwapa taarifa.”

“Usijali nitahakikisha taarifa inafika. Nikishindwa basi nitapita hata pale kanisani na kuwataarifu.”

*****
TEKSI iliondoka na kwa kweli yule dereva alikuwa na moyo wa kibinadamu zaidi kwani tulipofika Hospitali ya Mwananyamala hakuniacha getini. Alinishika mkono na kunipeleka hadi kwa daktari huku wagonjwa wengine wakituruhusu kuwapita kwa kuwa hali yangu iliwatisha na kuonekana kuwa napaswa kupewa kipaumbele katika huduma.

Baada ya kutoa maelezo kwa daktari, nikakalishwa kwenye kiti maalum na dereva huyohuyo wa teksi, akanisaidia kwa kukisukuma kiti hicho hadi wodi namba 5 ambako nilikabidhiwa kitanda. Usiku huo wa Alhamisi ukanikuta hapo hospitali na ukaisha nikiwa hapo hospitali.

Siku iliyofuata ilikuwa ni Sikukuu ya Maulid. Siku ya mapumziko. Mimi nilikuwa wodini. Ndugu, jamaa na rafiki walifika hospitali kuniona. Wanakwaya wengi pia walifika kuniona. Lakini hadi kufika jioni sikuwa nimepata huduma yoyote kubwa kuhusu jeraha hilo zaidi ya kupewa tembe za kutuliza maumivu! Mguu ulizidi kuwa mweusi hususan eneo la kiganjani. Na uvimbe ulizidi!

Kila nilipojaribu kuhoji kwa nesi kuhusu kuhudumiwa nilipata majibu yasiyoelewaka. Mara, “Dokta atapita…” mara “vuta subira madokta wako kwenye kikao…” mara hili mara lile ilimradi yalikuwa ni majibu yasiyokuwa na msaada wowote kwangu.

Hatimaye usiku ukaingia bila ya kupata huduma yoyote! Ilipofika saa 4 nesi mmoja akaniletea vidonge vya vallium ili nipate usingizi. Nikanywa na vikanisaidia kwa kiasi fulani.

Asubuhi ya siku ya Jumamosi mambo yakawa vilevile. Hadi saa 4 asubuhi bado sikuwa nimemwona daktari yeyote aliyefika kunihudumia. Kungekuwa na mgomo rasmi uliotangazwa na madaktari labda ningeelewa lakini hakukuwa na mgomo wa wazi, labda wa siri.

Hatimaye saa saba mchana ikatinga, bado sijaona mtu. Nilipoletewa chakula kutoka nyumbani nikala kama kawaida kwani jeraha lile halikunifanya nishindwe kula. Lakini nilishangazwa na huduma za hospitalini hapo.

IIipotimu saa tisa hivi nikamwona mwanamume mmoja amevaa joho jeupe la kidaktari akipita kitanda kimoja hadi kingine. Hatimaye akafika kwangu na kukiangalia cheti kwa muda. Akaandika-andika maandishi aliyoyajua mwenyewe kisha akawa anauangalia mguu, akibonyeza taratibu pale penye uvimbe. Hatimaye akaondoka. Sikumwona tena kwa siku hiyo na wala sikumwona muuguzi yeyote mwingine!

Usiku saa 4 nikapewa tena vallium ili nisinzie!

Nikasinzia.

JUMAPILI ASUBUHI

Kulipopambazuka nikawa nimekwishakata tamaa ya kuhudumiwa katika hospitali hiyo kubwa zaidi ya serikali wilayani Kinondoni.

Wakati kaka yangu Barack (sasa ni marehemu) alipokuja akifuatana na rafiki yangu mkubwa, askari wa JWTZ, Mathew Mapunda saa saba mchana, tayari nilikuwa nimekuwa na uamuzi wa kuondoka hospitalini hapo. Na wao walipofika walikuwa na wazo kama langu.
Hata hivyo, kabla ya kuchukua uamuzi, tulimuuliza nesi mmoja aliyekuwa akirandaranda humo wodini, nesi ambaye kwa kiasi fulani nilikuwa nimekwishazoeana naye.

“Ni kwa nini sijahudumiwa mpaka leo?”

Nesi yule alitabasamu kidogo kisha akaniambia kwa sauti ya chini, “Kaka, si kwamba madaktari hawapo …wapo sana…wamejaa tele ka’ pishi ya mchele! Wanajichimbia kule theatre (chumba cha upasuaji) wakingoja dili. Kama una pesa leta nikamwone daktari aje akuhudumie. Vinginevyo kaka’angu…!” akaiacha sentensi hiyo ikielea.
Nilimwelewa.

Kaka yangu na rafiki yangu walikuwa na pesa lakini kwa hasira yule rafiki yangu alisema, “Hapa hapafai! Hakuna kutoa pesa wala nini…tuondoke zetu!” akamgeukia yule nesi na kumwambia kwa ukali, “Tunaondoka na mgonjwa wetu!”

****TUONANE KESHO KATIKA TAMATI YA MKASA HUU WA KWELI..***
 
USIKU WA JANUARI 20, 2005 (SEHEMU YA TANO)

SIMULIZI YA KWELI

INNOCENT A. NDAYANSE

***** ***** *****

Nilimwelewa.

Kaka yangu na rafiki yangu walikuwa na pesa lakini kwa hasira yule rafiki yangu alisema, “Hapa hapafai! Hakuna kutoa pesa wala nini…tuondoke zetu!” akamgeukia yule nesi na kumwambia kwa ukali, “Tunaondoka na mgonjwa wetu!”

Nesi alikuwa mpole. Akasema, “Hatukatai lakini subirini basi tufanye utaratibu wa kumdischaji.”

“Nini?! Hatuna muda mchafu!” kaka yangu alifoka huku akipunga mkono hewani. “Hatusubiri chochote! Tunaondoka naye! Mkawadischaji ndugu zenu mnaopenda kuwahudumia!”

Mathew na kaka yangu wakatoka, wakielekea nje ya geti. Wakati huo wanakwaya takriban kumi na watano nao walikuwa nje ya wodi wakiwa wamekuja kunijulia hali na kujua hatima ya sakata lililonikabili.

Dakika chache baadaye kaka yangu na Mathew wakarejea wakiwa ndani ya gari pick-up, nikapanda na wanakwaya wengine wakapanda tukasepa!

Moja kwa moja hadi Kinondoni, Mtaa wa Sekenke ambako kulikuwa na zahanati iliyokuwa ikisifiwa kipindi hicho; Nyamongo. Ile kufika tu nikapewa tembe moja ndogo kisha nikachomwa sindano moja. Nikapewa kitanda ndani ya chumba nikiwa peke yangu!

Nikalazwa kwa mara ya pili!

Wauguzi wakanihudumia haraka na kwa namna iliyonitia faraja kwa kiwango kikubwa. Nikatundikiwa dripu tatu mfululizo!

Jumatatu asubuhi, daktari mkuu wa zahanati hiyo akaja kunitazama.

Unajisikiaje, mgonjwa wangu?” ndivyo alivyoanza mara tu alipoketi kitini kando ya kitanda.

“Nina nafuu dokta,” nilimjibu huku nikimtazama kwa makini.

Daktari huyo ambaye kutokana na jina lake nilijenga hisia kuwa ni mzaliwa wa Mkoa wa Mara, alishusha pumzi na kuendelea kunitazama sana. Sijui alikuwa akiwaza nini. Hatimaye akasema, “Una nyota nzuri sana. Kwa namna mguu huu ulivyo, ingewezekana kabisa ukapoteza maisha siku ileile ulipoumwa kwa sababu ulisema kuwa ulichelewa kufikishwa hospitali.”

Sikutamka neno, nilitikisa kichwa tu kuashiria kukubaliana na alichosema.
“Hivi ulimwona vizuri nyoka aliyekung’ata?” aliniuliza.

“Nilimwona.”

“Alikuwa wa aina gani?”

“Mweusi.”

“Urefu wake?”

Nikamwonesha kwa ishara ya mkono wa kulia na kushoto.
Daktari akaonesha mshangao. “Mweusi?”

“Ndiyo.”

“Nimeshawaona sana kwetu Musoma nyoka wa aina hiyo,” alisema. “Nashangaa hapa Dar tena kwenye huo mtaa kama wa Ngano ambako ni mjini sana eti kunakuwa na nyoka wa aina hiyo! Na asipouawa atawadhuru wengi. Anajulikana kwa kushambulia kwa usahihi na nguvu kubwa, na ana uwezo wa kugonga mara kumi na mbili kwa mpigo mmoja.

“Kwa utaalamu wangu, kwa jinsi ninavyouona huu mguu wako, naamini sumu iliyokuingia ni ya nyoka aina ya Black Mamba ambayo ina kitu kinachoitwa ‘post-synaptic neurotoxin’ na ana uwezo wa kuidunga sumu hiyo kwa ujazo wa 1/250 oz.

“Kiasi hicho kinatosha kusababisha kifo kwa asilimia hamsini. Ikiwa itatokea umegongwa na nyoka huyu basi huenda ukapatwa na tatizo la upumuaji na kutokwa jasho sana na kama hutapata tiba mapema, unapelekwa ‘mwembejini’ (akimaanisha makaburini) kupumzika milele. Kama wasingekufunga kamba zile, basi ndani ya robo au nusu saa ungekuwa katika sayari nyingine.”

Daktari alizungumza mengi na akanifariji kuwa tatizo langu siyo kubwa sana na jioni angeniruhusu niondoke.

Ndivyo ilivyokuwa. Jioni niliruhusiwa kuondoka.

SIKU MBILI BAADAYE

Wakati nikiwa nyumbani nikiuguza jeraha walikuja watu kadhaa kunijulia hali. Baadhi yao ndio waliozungumza kuhusu tukio la nyoka yule na imani za kishirikina. Kuna waliodai kuwa nyoka yule alikuwa akifugwa na mama mmoja wa Kiarabu aliyekuwa akiishi jirani sana nyumba ya Shule ya Msingi Hananasif, na kwamba mama huyo alikuwa amechoka kuendelea kumfuga hivyo akamwachia.

Ikadaiwa kuwa nyoka huyo amekwishawauma watu wanne, mimi nikiwa mmojawao kwa kipindi cha wiki mbili! Na ikaendelea kudaiwa kuwa mara kwa mara kila ifikapo usiku pale kwenye makutano ya Barabara za Wakulima na Ngano, jirani na kile kijibaa, husikika kelele za kicheko cha mwanamke asiyeonekana!

Taarifa hizo zikaegemea zaidi kwenye imani za ushirikina, imani ambayo haikuniingia akilini asilani. Ndiyo, sikujenga imani kuwa yule nyoka aliyening’ata ni wa kishirikina. Sikuwa tayari kuamini hivyo.

Mazingira ya eneo la Hananasif yalinifanya niamini kuwa alikuwa ni nyoka wa kawaida kama nyoka wengine. Nikayakumbuka yale mafuriko ya mvua za El-Nino mwaka 1998 yaliyolitikisa Jiji la Dar es Salaam.

Yalikuwa ni mafuriko yaliyosadikika kuwa yalizikumba samani mbalimbali kwenye makazi ya watu kuanzia Manzese, bonde la Magomeni, Msimbazi na kuja hadi kwenye hilo bonde la Hananasif huku baadhi ya vyombo hivyo vikikwama kwenye mikoko iliyoshamiri katika bonde hilo na vingine vikipitiliza hadi kwenye Daraja la Selander ambako vilitokomea baharini.

Ni katika mafuriko hayo ilipobainika pia kuwa nyoka wakubwa kwa wadogo walisukumwa na kuja kukwama kwenye mikoko hiyo na baada ya maji kupungua viumbe hao wakaanza kutambaa hapa na pale, huku na kule nchi kavu, wakapanda juu Kinondoni Moscow, wakazaliana na kuishi kwa uhuru kama viumbe wengine.

Japo sikupingana waziwazi na hawa wakazi wenzangu wa Hananasif walioamini kwa asilimia mia moja kuhusu ushirikina wa nyoka wa ajabu, hata hivyo nilibaki na msimamo wangu wa kutoamini kuwa niling’atwa na nyoka wa ajabu.

*****
SIKU ya tatu gazeti maarufu kwa siku zile lililoitwa ALASIRI, lililokuwa likiingia mitaani kila siku alasiri, likachapa kwa kirefu habari yenye kichwa cha: JOKA LA MAAJABU LAITIKISA HANANASIF. Habari hiyo ikawafanya wakazi wengi wa eneo hili wagwaye kuitumia Barabara ya Ngano iwe asubuhi, mchana hata jioni au usiku.

Ni wengi walioogopa, siyo wote. Baadhi walipita lakini wakiwa na hadhari kubwa na kikafika kipindi kila mtu alikuwa akipita mtaani hapo macho yake yanakuwa juu ya miti akihofia kuwa huenda joka hilo liko mtini na linaweza kumshukia mtu yeyote.

Siku mbili baada ya gazeti hilo kutoa habari hiyo, dada mmoja (sasa ni marehemu) aling’atwa na nyoka njiapanda ya barabara hizo za Wakulima na Ngano zikiwa ni kama hatua hamsini tu kutoka pale nilipong’atwa mimi!

Huyo hakuwa peke yake, alikuwa na mdogo wake ambaye alihadithia simulizi isiyotofautiana na madhila yaliyonikuta mimi ile Januari 20. Kwamba, muda mfupi baada ya dada yake kuumwa na nyoka, kicheko kikali kikasikika kutoka kwenye mkusanyiko wa miti uliounda chaka zito kwenye makutano hayo.

Kisha kukazuka upepo mkali kwa muda mfupi na kutoweka. Lakini tofauti ndogo ni kuwa siku hiyo hakukuwa na mtu aliyeibuka na kutimua mbio na kuwapita kama ile siku alipotokea yule mwanamke na kunipita mbio!

Hata hivyo, dada yule ambaye alikuwa akiishi hukohuko Hananasif, alikata roho muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali huku mwili wote ukiwa umebadilika rangi na kuwa mweusi ti!

Wiki moja baada ya dada huyo kufariki nikapata taarifa kuwa hata yule kijana wa Kiarabu ambaye alinipa msaada wa kunipeleka Hospitali ya MICO pale Mkwajuni kwa huduma ya awali, akiwa na mguu wake uliobabuka ngozi kutokana na sumu ya nyoka naye alifariki dunia!

Sababu, mguu wake ulivimba tena na kubadilika tena rangi, ukawa mweusi zaidi kisha mwili wote ukavimba na alikata roho ndani ya saa ishirini na nne tu!

Nikahofia kuwa labda na mimi niko kwenye mkumbo huohuo kwa kile kilichoaminika kwa wakazi wa hapo kuwa yule hakuwa nyoka wa kawaida, ni joka la miujiza. Ni jini!

Mtaa huo ukawa ukiogopwa na wakubwa kwa wadogo na nilithibitisha hivyo siku nilipopewa lifti ya gari nikielekea maeneo ya Posta Mpya. Tukiwa barabarani nikashangaa kutomwona mtu hata mmoja akitembea barabarani hapo hadi Mwembejini!
Hata kinamama waliokuwa wakipeleka biashara mjini maarufu kwa ‘mamantilie’ iliwalazimu kukusanyana hadi kufikia kumi au zaidi kisha wanasindikizwa na wanaume wawili au watatu wakiamini kuwa ndiyo salama yao!

Mtaa wa Ngano ukageuka kuitwa kimasihara kwa jina la ‘Mtaa wa Nyoka!’

*****
GUU langu liliendelea kuwa jeusi tii! Ndiyo, lilikuwa jeusi lakini halikubabuka. Mwezi ukaisha nikiwa siwezi kuvaa kiatu. Mwezi wa pili ukakatika, lakini nafuu ilizidi kupatikana. Hatimaye siku ya Jumapili ya Pasaka mwezi Aprili, nikafumba macho na kuvaa viatu huku nikijisemea liwalo na liwe, kama ni kukatwa mguu basi na ukatwe.

Nilifikia hatua ya kuchukua uamuzi huo kwa kuwa kuna daktari mmoja alinihadharisha kuwa nikivaa kiatu wakati bado sumu haijateketea mguuni basi mguu utapata joto kali na joto hilo litaleta madhara! Mguu utaoza! Matokeo ya kuoza ni kukatwa!

Nilimwelewa daktari, lakini akili ilishachoka! Akili ilishapinda! Nilishachoka kupita mitaani na makubazi!

Nikachukua uamuzi mgumu!

Siku hiyo ya Pasaka nikavaa viatu na kwenda kanisani. Hadi natoka kanisani sikuwa nimehisi mabadiliko yoyote ya ajabu mguuni! Ukawa mwanzo wa kupona. Badala ya maumivu kuongezeka, yakawa yanapungua kila kukicha. Taratibu rangi ya ngozi ikaanza kurudi. Hadi leo niko vizuri na mtaani hapo kuko kawaida. Mtaa unapendeza maradufu!

Hakuna wa kung’atwa na nyoka, ng’e wala tandu! Tofauti ni kuwa ile miti iliyopandwa kando ya barabara imekuwa mikubwa zaidi na imestawi zaidi, kiasi cha kutoa taswira ya kuvutia machoni mwa yeyote apendaye mazingira ya aina hiyo.

Mchana ni kivuli mwanzo-mwisho na usiku ni giza zito! Kama utaliwazia tukio na simulizi za joka lile hutapita hapo, lakini kama utahitaji burudani ya kivuli basi mtaa huo wa Ngano ni jibu la mahitaji yako.

Kijani kitupu!

Sasa ukipita usiku barabarani hapo giza lake ni zaidi ya giza. Kama una moyo mwepesi, utageuza njia urudi ulikotoka!

MWISHO.
 
hadithi nzuri sana kama ina kaa ukweli!!!
maana ina kichwa bila miguu
  • tarehe zinewekwa ningeamini ni ya ukweli
  • uponyaji tiba yake (solution) ingewekwa km ni Maombi kanisani, au Daktari kaweka Pennicyllin ningeamini imekamilka kichwa, tumbo na miguu
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom