Chilojnr
JF-Expert Member
- Jul 5, 2012
- 308
- 1,354
MZIGO USIO NA ANUANI
Sehemu ya 01.
Dar es Salaam, Saa 8:36 Usiku.
Mlio wa simu ndiyo uliomshtua Ashrafu Maganza kutoka katika usingizi mzito. Mwili wake ulichoka kutokana na kuchelewa kulala siku hiyo, alipoisikia simu ikiita tu, akayafumbua macho yake na kuanza kuangalia huku na kule.
Akashikwa na hasira, katika kipindi alichokuwa akichoka kama hicho hakutaka kuona akisumbuliwa na mtu yeyote yule, mara nyingi huzima simu lakini kitu cha ajabu kabisa katika siku hiyo ambayo alichoka sana, alisahau kuizima.
Akaupeleka mkono wake kwenye kidroo kidogo kilichokuwa pembeni ya kitanda na kuichukua simu hiyo, macho yalikuwa mazito, akakiangalia kioo cha simu na jina la mkuu wake wa kazi kuonekana kwenye simu ile. Haraka sana akaipokea.
“Heshima yako mkuu!” alisema kwa sauti ya kichovu.
“Najua nimekuamsha na niliahidi kutokukupa kazi nyingine kwa sababu upo likizo, ila naomba nikuone hapa Jangwani mara moja, kuna tukio moja kubwa,” alisikika mwanaume aliyekuwa upande wa pili.
“Kuna tukio kubwa?” aliuliza kwa mshtuko.
“Ndiyo! Ni kubwa sana, lile la kumfanya kila Mtanzania kulizungumzia sana, nahitaji uje mara moja,” alisikika mkuu huyo.
“Sawa! Hakuna shida.”
Ni kweli alichoka, alifanya kazi nyingi mfululizo mwezi huo lakini simu aliyoipokea ilikuwa muhimu mno kwake na ilikuwa ni lazima afanye kile alichoambiwa akifanye muda huo.
Alikuwa mpelelezi wa kutegemewa wa jeshi la polisi, aliyethubutu kufanya kazi kwa nguvu kubwa na kuwakamata watu wengi ambao walionekana kama kushindikana kwa uhalifu nchini Tanzania.
Alipambana nao kwa kipindi kirefu na kushinda vita hizo na kupata sifa kubwa katika jeshi la polisi nchini Tanzania. Kwa jina aliitwa Ashrafu Maganza, kijana aliyekuwa mrefu kidogo, mwenye mwili ulioonekana kuwa na mazoezi na muda mwingi alipenda kutoa tabasamu pana.
Simu aliyoipokea ilitoka kwa kiongozi wake wa kazi, Mrisho Masumbuko aliyekuwa amempigia na kumwambia kulikuwa na kazi aliyotaka kumpa. Hakupenda kupewa kazi kwa kuwa aliomba likizo ya mwezi mzima lakini hakuwa na jinsi, mpaka anapigiwa simu na kuambiwa aende huko Jangwani, aliamini kulikuwa na kazi nzito ambayo isingeweza kutatuliwa na mtu yeyote isipokuwa yeye.
Akainuka kutoka kitandani, akafungua kabati lake la nguo, akavalia suruali ya jinzi na fulana nyeusi kisha kuchukua bastola yake na kuanza kuelekea huko Jangwani.
Njiani alikuwa na mawazo lukuki, alikuwa akiifikiria simu ile aliyokuwa amepigiwa, alijua kulikuwa na tukio kubwa, alijaribu kulifikiria tukio hilo na uzito wake lakini hakupata jibu lolote lile mpaka pale ambapo angefika na kujionea kwa macho yake.
Kutoka Kinondoni alipokuwa akiishi, hakuchukua muda mrefu akafika Magomeni Mapipa ambapo akaunganisha mpaka Jangwani, kwa mbele aliyaona magari kama manne hivi yakiwemo ya polisi, akasogea mpaka kule na kuteremka.
Tayari mkanda wa njano uliosomeka ‘Do not Cross’ yaani usivuke ulikwishazungushiwa sehemu ya tukio, kwa kuwa alijulikana, akaunyanyua na kuuvuka ambapo mbele kidogo macho yake yakatua kwa kiongozi wake, Masumbuko.
“Nimefika mkuu!” alisema baada ya salamu.
“Kuna mtu ameuawa na mwili wake kutupwa hapa!” alisema Masumbuko huku akimwangalia Maganza ambaye hakuonekana kushtuka kwani kile alichokitarajia ndicho kilichotokea mahali hapo.
“Ni nani?” aliuliza.
“Veronica!” alijibu Masumbuko.
“Veronica yupi?” aliuliza.
“Sebastian!”
“Unamaanisha yule Miss Utalii?”
“Ndiye huyohuyo!” alijibu Masumbuko.
Maganza akashusha pumzi nzito, hakutegemea alichokisikia. Alimfahamu sana Veronica, alikuwa mmoja wa wasichana warembo mno nchini Tanzania. Mbali na uzuri wake, Veronica alikuwa msichana mpole kupita kawaida, muda mwingi uso wake ulikuwa na tabasamu pana, hata alipokuwa akikasirika, aliutumia uso wake mzuri kuonyesha tabasamu hilo.
Masumbuko akamchukua Maganza na kumpeleka mahali ulipokuwa mwili wa Veronica, haukuwa umefunikwa na chochote kile mpaka watu wa kitengo cha CSI yaani Crime Scene Investigation wafike mahali hapo na kuchukua ushahidi na picha nzima ya tukio hilo.
Maganza aliuangalia mwili wa Veronica mahali pale, yule msichana mrembo aliyekuwa akitamba kwenye magazeti mpaka mitandao ya kijamii alikuwa chini, tumbo lake lilikuwa wazi, kulikuwa na unga fulani mweupe ambao kwa uzoefu wake wa macho tu alipoungalia aligundua yalikuwa ni madawa ya kulevya.
Masikitiko mazito yakaukumba moyo wake, hakuamini alichokuwa akikiona mahali hapo. Tanzania ilimpoteza msichana mrembo, mwenye sifa kubwa ambaye ndoto yake kubwa baadaye alitamani kuwa Miss Tanzania, leo hii ndoto yake ilizimwa ghafla.
“Ni nani amefanya hivi?” aliuliza Maganza kwa sauti ya chini iliyoonyesha kuumizwa na kile kilichotokea.
“Bado hatujajua ni nani aliyefanya hivi! Ila natumaini kwa uzoefu wako wa kazi, utatuambia ni nani na kwa nini amefanya hivi,” alisema Masumbuko huku naye macho yake yakiwa katika mwili wa Veronica.
Hapohapo Maganza akaagiza kupewa glovusi, akapelekewa na kuzivaa kisha kuanza kuugusa mwili ule kwa umakini mkubwa kabisa huku akiumulika kwa tochi ya simu yake.
Aliuangalia kwa sekunde kadhaa na ndipo macho yake yakatua katika sehemu ya kifua ambapo kulikuwa na neno MZIGO IV ambalo liliandikwa na kalamu yenye wino mwingi (Marker pen)
“Mzigo IV!” alisema Maganza huku akilisoma neno hilo mara nyinginyingi.
“Neno gani hilo?” aliuliza Masumbuko, kwa mbali aliliona neno hilo.
“Mzigo namba nne!”
“Mzigo namba nne?”
“Yeah! Ni mzigo usiokuwa na anuani!” alisema Maganza.
“Unamaanisha nini?”
“Ulikuwa unapelekwa wapi? Unadhani hapa ndipo ulipokuwa unaletwa? Hapana! Kuna sehemu ulikuwa unapelekwa! Ni wapi huko? Kwa nini haukufika salama? Kwa nini umetelekezwa hapa?” aliuliza Maganza huku akiendelea kuuangalia mwili ule.
“Ni lazima tupate jibu la kila swali!” alisema Masumbuko.
“Na kuna moja kubwa zaidi!” alisema Maganza.
“Lipi hilo?”
“Huu ni mzigo namba nne, namba moja, mbili na tatu iko wapi? Je, namba zinaishia hapa kwenye nne au napo kuna mzigo namba tano mpaka kumi?” aliuliza Maganza maswali kadhaa ambayo hakupata jibu lolote lile kutoka kwa mkuu wake.
Ni ndani ya dakika kadhaa tayari watu wa kitengo cha CSI wakafika mahali hapo na kuanza kufanya kazi yao. Kila mtu aliyeuona mwili huo alishtuka, hapakuwa na aliyeamini kama kweli msichana mrembo, Veronica aliuawa na mwili wake kutupwa huku ukiwa na madawa ya kulevya tumboni mwake.
Picha zikapigwa mahali hapo na kila kitu kilipokamilika, wakauchukua mwili huo na kuelekea hospitalini. Hawakutaka kuwapigia simu wazazi wake, ilikuwa ni lazima wajue pa kuanzia na ndipo ambapo wangepiga simu na kuwapa taarifa ili kujua zaidi kilichotokea.
Waliamini bila kuwashirikisha wazazi hao wangeweza kupata taarifa ya hilo lililotokea hivyo, walihitaji kuwapa taarifa huku wakiwa tayari wamekwishapata mahali pa kuanzia.
Maganza hakurudi nyumbani kwake, aliunganisha mpaka ofisini na kutulia huko. Saa yake ilionyeha tayari ilikuwa ni majira ya saa 9:05 alfajiri lakini kitu cha ajabu hakuwa na usingizi hata kidogo.
Muda mwingi alikuwa akimfikiria huyo Veronica huku akiangalia picha za msichana huyo kwenye mitandao ya kijamii, aliangalia enzi za uhai wake, alivyokuwa akitanua na marafiki zake, alivyoonekana kuwa na furaha tele bila kujua kama siku hiyo angekuwa maiti.
“Ni msichana mrembo sana,” alijisemea Maganza huku akimwangalia kwenye akaunti yake ya Instagram.
Wakati akipitia kuangalia picha moja baada ya nyingine huku kila sura alizokuwa akiziona zikiwa na Veronica akizihifadhi kichwani mwake, akapata wazo kwamba lingekuwa jambo la lazima kuangalia posti yake ya mwisho ilikuwa ikisema nini.
Kwa wasichana kama Veronica ambao walihitaji sana umakini wa watu, walipenda kuweka kwenye mitandao kila kitu kilichokuwa kikiendelea, hivyo akapata wazo la kuangalia picha yake ya mwisho aliyopiga na kuiweka kwenye akaunti yake.
Akafanya hivyo, picha hiyo ilimuonyesha akiwa ndani ya gari huku kwa chini kukiwa na maneno yaliyosomeka ‘Paradise 590 with my gang’.
Maganza akaangalia vizuri, picha hiyo iliwekwa kwenye mtandao saa nne zilizopita yaani ilionyesha majira ya saa tano aliiweka picha hiyo na baadaye kuuawa, akaanza kuhisi endapo angefanya safari ya kuelekea katika ukumbi wa Paradise 590 basi angepata angalau pa kuanzia.
Hakutaka kubaki ofisini, haraka sana akasimama, akachukua kila kitu kilichokuwa chake na kuondoka mahali hapo.
Mbele yake aliiona kazi hiyo kuwa ngumu mbele yake, alipapata pa kuanzia lakini hakutaka kuamini kama angepata kila kitu alichokuwa akikihitaji muda huo. Aliendesha gari kwa mwendo wa kawaida mpaka alipofika Paradise, akateremka na kufuata mlango wa kuingia katika klabu hiyo.
Je, nini kitaendelea?