ng'ombo
JF-Expert Member
- Dec 1, 2014
- 418
- 619
Kila siku nilijiona kama Baba bora, nikifanya kazi kwa bidii kuhakikisha kua watoto wangu watatu wanaishi katika mazingira mazuri. Sikutaka wakose chochote kwani walikua wanamaanisha kila kitu kwangu.
Lakini nilikua na tatizo moja, kumnyanyasa mke wangu. Kusema kweli sababu kubwa ya kumnyanyasa na wakati mwingine kumpiga mke wangu ilikua ni uoga na wivu uliopindukia.
Mke wangu ni mzuri, Mama bora na ana akili nyingi sana pengine kuliko hata mimi na nadhani hilo ndiyo lilikua tatizo kubwa. Baada ya kumuoa nilimlazimisha kuacha kazi, akiwa na elimu yake nzuri tu.
Nilimuahidi kumfungulia biashara lakini si kufanya hivyo, kila siku nikimuambia kuwa hana akili, nilimtukana kuwa kazi yake ni kufua nepi tu ndiyo kitu anachokiweza mpaka akafikia hatua kuamini na kunivumilia kwa ujinga wangu.
Lakini ukweli nilikua najua mke wangu ana akili, sana, ana bahati ya biashara na anaweza kufanikiwa kuliko mimi na hicho kiliniogopesha. Pamoja a manyanyaso yote hayo kwa mke wangu lakini mimi ni Baba bora,.
Nawapenda wanangu, nikiwaletea zawadi kila siku, kufanya nao homework, kucheza nao na kamwe hata siku moja sikuwahi kumtukana Mama yao, kumnyanyasa wala kumpiga mbele yao.
Mbele ya wanangu nilijiona kama shujaa, nikiigiza nikitaka wanione kama malaika. Nikiamini nimeweza, nikiamini mke wangu naye anaficha maumivu na nikijiona mwanaume, kidume kabisa kwamba nampiga mke lakini napenda watoto.
Nikiamini watoto nao wananipenda na hawajui kinachoendelea, siku moja mke wangu aliumwa sana na kulazwa hospitalini. Nakumbuka mwanangu, binti wa miaka mitano, mtoto wangu wa pili tulienda naye kumuangalia Mama yake.
Sasa tukiwa nje baada ya daktari kutuambia tutoke nje mtoto wangu huyo alianza kulia sana, alikua akimlilia Mama yake na nilimtuliza nikimuambia Mama yake atakua salama, lakini majibu yake ndiyo yalinifanya nisijione Baba mbaya tu bali nijione ni Baba mkatili.
Wakati namtuliza namwambia Mama yake atakua sawa aliniambia. “Baba Mama akifa na mimi nataka nife naye…” Nilistuka, mwili mzima ulipigwa na ganzi, lakini nilijizuia nisihamaki nikamtuliza, nikijua ni mapenzi yake kwa Mama yake aliendelea.
“Nitakunywa sumu au kujirusha kwenye ghorofa nife na Mama..” hapo nilistuka zaidi kwani mwanangu alikua akiwaz akujiua. Nilimkumbatia kumuliza kisha nikamuambia kuwa Mama yake hatakufa na kumuuliza kwanini anasema hivyo.
“Sasa Baba kama Mama akifa wewe utampiga nani tena, si utaanza kutupiga na sisi. Mimi sitaki kupigwa kama Mama, si bora tu nife, Mama yeye anajifungia tu chumbani analia hata hasemi, mimi ningesema, Mama hasemi…”
Utumbo ulianza kusokota, nilisikia tumbo la kuhara, kidogo nijikojolee. Kusema kweli nguvu ziliniishia na sikujiona kama mwanaume tena. Nilitamani kunyanyua mdomo kuongea lakini haukufunguka.
Kabla sijasema chochote Daktari alituita, tuliruhusiwa kwenda kumuona. Nilivyofika alikua macho, nilipiga magoti mbele yake na kumuambia mke wangu nisamehe. "Nimekutendea mengi mabaya lakini leo ndiyo mwisho."
"Nimegundua kuwa sikuumizi wewe tu nawaumiza na watoto" mwanangu mkubwa alipokuja nilimuuliza akaniambia hata yeye anajua, ndiyo kijana wa miaka tisa alikua anajua kua na mnyanyasa Mama yake lakini hakua na nguvu za kumtetea.
Niliwaomba msamaha na kuamua kubadilika. Baada ya wiki moja mke wangu aliruhusiwa, tangu siku hiyo ni mwaka wa pili sasa sijawahi hata kumtukana mke wangu.
Nilikua najifanya kuwa nina hasira za karibu lakini sasa nikikasirika tunaongea. Mambo yanaenda vizuri, nimemfungulia mke wangu biashara na kama nilivyosema awali mke wangu ana akili kuliko mimi.
Biashara inaenda vizuri na mapato yake ni mara tano kuliko mshahara wangu, hakuna dharau kama nilivyokua nikidhani labda akipata pesa atanidharau zaidi ya upendo.
Wanaume hata hawamsumbui wanamuogopa kwani ana hela. Nampenda sana mke wangu na namshukuru Mungu nimegundua mapenzi kuwa haikufanyi mwanaume zaidi kumpiga mkeo bali inakufanya mwanaume mpumbavu.
Naamini kuna wanaume huko nje bado wanaamini kua kumpiga mwanamke ndiyo uanaume. Kwamba ukimnyanyasa labda ndiyo atakuheshimu hapana anakugopa lakini hakuheshimu.
Lakini kuna ambao wanajifanya Baba bora kwa kudekeza watoto huku wakiwanyanyasa Mama zao wakidhani labda watoto hawaoni. Niwamabie kitu tu, watoto wanaona Mama yao anateseka na wao wanateseka pia kwani wanampenda Mama yao kuliko hata wewe mwanaume.
Sasa hivi nimebadilika, sasa naweza kujiita mume na Baba bora. Kila mke wangu akiniudhi na nikitamani hata kunyanyua mdomoni kuna maneno yananijia kichwani na naacha kabisa. “Baba Mama akifa na mimi nataka nife naye…”