Hivi bado kuna watu wanaamini kwa kocha huyu huyu Sven Simba itatwaa ubingwa wa ligi? Hivi wale wajumbe wa bodi ya Simba waliokuwa wanapitapita kwenye vyombo vya habari kumsema vibaya Uchebe wapo wapi sasa hivi? Kidogo nilimsikia mmoja juzi akiwatupia lawama wachezaji na kumtetea Sven eti wachezaji wanacheza chini ya kiwango ili kocha atimuliwe.
Kumfukuza Uchebe halikuwa tatizo kwa sababu viongozi wao ndio wanajua kwa nini walifanya maamuzi hayo ila je umemleta nani kuchukua nafasi yake? Tutakatae tukubali Sven sio kocha wa kiwango cha kufundisha Simba. Kwa kikosi kilichopo Simba inahitajika tu kuisoma timu pinzani na mfumo inaotumia basi wewe unapanga kikosi chako na mbinu zako kwa sababu Simba ina mseto wa wachezaji wenye vipaji tofauti tofauti wanoweza kukupa matokeo katika mifumo tofauti tofauti. Kwa ligi ya ndani bado kikosi cha Simba kinaweza kushindana na kutetea ubingwa iwapo kikipata kocha mzuri.
Sven mfumo wake wa kutumia mshambuliaji mmoja badala ya wawili huwa unazipa sana nguvu timu pinzani kwani zikishamkamata Kagere au Boko basi biashara imeisha. Kagere sio aina ya washambuliaji ambao unaweza kumtumia katika mfumo wa mshambuliaji mmoja kwa sababu hana kasi sana na sio mzuri sana wa kukaa na mpira mguuni. Hili Profesa Uchebe alilijua ndio sababu kubwa alikua anaanza na Boko na Kagere pamoja kwa vyovyote timu pinzani lazima ibaki nyuma kujilinda na hivyo ilikuwa inawapa nafuu viungo na mabeki wa Simba. Ndio maana mapungufu ya ukuta wa Simba yameonekana sana sasa hivi wakati yalikuwepo tangu msimu unaanza. Sasa kwa kocha wa kiwango cha Sven hata hili dogo linamshinda kuona vipi kwa mbinu nyingine za kimchezo ataweza kweli?
Mapungufu mengine makubwa kwa Sven ni kuwa hajui kupanga kikosi kwa ufanisi kulingana na ukubwa au aina ya mechi. Upangaji wake ni kama anapiga ramli. Pili si mwepesi wa kufanya "sub" kwa wakati na hata wakati mwingine akifanya hizo "sub" anazidi kuingamiza timu badala ya kuisaidia timu.
Na sasa hivi hatulalamiki tu Simba kufungwa bali hata kiwango cha timu kimekuwa cha kawaida sana. Simba ya sasa haitishi ndio sababu timu yoyote inayokuja uwanja wa Taifa inafunguka na kama haujui rangi ya jezi si rahisi uitofautishe Simba na timu pinzani kwa kiwango chake. Mpaka unajiuliza ndio uwanja huu huu Alhaly, As Vita, Soura, Nkana na wengineo walifia hapa?
Kutegemea Sven atetee ubingwa hizi ni ndoto za mchana kwa sababu hata mfumo unaompa manufaa yeye mwenye hauamini. Siku zote anaanza na mshambuliaji mmoja timu inafungwa anaingiza mshambuliaji mwingine timu inakuwa na washambuliaji wawili wanakomboa goli na kuongeza goli lingine. Kwa kuwa ni sikio la kufa mechi ijayo badala aanze alipoishia anarudi tena anaanza na mshambuliaji mmoja. Kwangu mimi huyu alipaswa kufukuzwa mara moja kwa sababu mechi kuanzia ya Mwadui, Namungo na Polisi kiukweli timu ilicheza vibaya sana kama vile haina kocha na ni kama tulifungwa tu zile mechi sasa sijui viongozi wanasubiri nini.