Sikuamini

Sikuamini

Jokajeusi

JF-Expert Member
Joined
Jun 1, 2018
Posts
6,336
Reaction score
10,895
Mugonile bandugu!!

Sikuamini. Niliona yote ni ubatili. Machozi yasiyokomaa yalikuwa yakinilenga lenga machoni ingawa nilijikaza yasijekudondoka. Akili ilirudi nyuma mwili ukiwa umesimama. Sikuamini.

Ndoto huotwa na muotaji. Si uotaji wa moto bali uotaji wa kifikra wenye matarajio ya picha na sinema katika fikara. Ndivyo mimi kijana wa zama zangu. Kijana Barobaro mwenye ndoto lukuki za milenia. Nilijaza masanduku kwa masanduku. Mabehewa kwa mabehewa ya ndoto.

Nilikuwa na ndoto kubwa. Ndoto itakayoishangaza dunia. Kama haitoshi Ndoto hii ingeandikwa katika vitabu vya rekodi za kimataifa zilizopata kutokea. Siku hizo nalikuwa kijana mdogo. Kijana Chakaramu mwenye kukimbiza upepo na kuukamata. Nilikuwa hodari kwenye giza naam hata katika nuru nilishindikana. Warembo wote wa mtaa niliokuwa nikiishi nao walihitaji mhuri wangu. Na kwa hakika nilipiga chapa yangu maridhawa katikati ya pambaja zao.

Umashuhuri wangu ulizidi na kuvuka mipaka kama habari za udaku. Niligeuka kimbunga niliyebeba hata vitu vizito. Jambo hili lilinifanya nijione mfalme mwenye mamlaka chini ya Jua. Kumbe katika wakati kuna kubadilika. Fikra mpya zilipiga kichwa changu kama jiwe la mtupo. Mawazo mageni yaliupuliza ubongo wangu. "Nitaoa Mke Mzuri" ilikuwa ni sauti isiyo na maneno iliyosema kichwani mwangu.

Hii ilikuwa ndoto mpya. Mbali na ndoto nyingine ndoto hii ilinipa raha na kunifanya nitabasamu kila nikiifikria. Mara nyingi nilikuwa naifikiria nyakati za usiku niendapo kulala. Hapo nawazaga mambo lukuki kuhusu Harusi yangu.

Harusi yangu lazima itashangaza viumbe wote. Si binadamu tuu hata wanyama, ndege wa angani na samaki wa baharini. Harusi yangu itakuwa mwanzo mpya wa historia kuandikwa. Tayari nilimuona mke wangu mtarajiwa katika vasi jeupe pee mithili ya theluji. Uzuri wake ulikosa irabu za kuulezea. Nilipofika hapa nilitabasamu. Kisha niliendelea.

Siku ya harusi yangu watakuwepo watu mashuhuri. Watu wenye kila aina ya sifa zilizotukuka. Niliwaona wachezaji wa mpira wakiwa na jezi zao wakiwa katika siti zao. Hapo nilimuona C. Ronaldo, Messi, Devoe, Mo salaa, na wengine wengi. Nilitabasamu nilipomuona Gaucho akicheka huku akinipa ishara ya kunipongeza nami nilimjibu kwa ishara.

Niliwaona viongozi wakubwa wa serikali za nchi na kimataifa wakiwa katika siti zao. Hapa nilimuona Obama, Akiwakilisha bara la amerika ya kasikazini. Mugabe(Afrika), Angela Merkel(Germany) na Wengineo. Viongozi wa Tanzania walikuwepo wote. Rais Magufuli alinitazama kama mtu mwenye jambo la kusema. Sikujua ni jambo gani lakini niliwaza huenda harusi yangu itaondoka na mtu atayetumbuliwa.

Wanamuziki wakimataifa na wa ndani walizingira eneo lote wakitoa burudani za kila namna. Ilikuwa ni harusi iliyomfanya mke wangu SIKOMOYONI atabasamu kila mara kwa furaha.
Nilishtuka Kumuona Mange akiwa kavalia kijisketi kilichombamba. Mara kwa mara Mange alikuwa akimkata kijicho upembe JPM.

Kwa kifupi harusi yangu ilivunja rekodi kwani Baada ya shughuli. Shirika la Marekani la mambo ya anga NASA lilituchukua na kutupeleka mwezini kula fungate.

Ilikuwa ni ndoto tu niliyokuwa nikifikiri nikiwa mdogo. Umri ulikimbia mambo yalienda kombo. Sikuwa na maisha mazuri. Sasa nilikuwa na umri wa miaka thelesini na saba. Ndoto ya kufanya harusi kubwa iliota mbawa na kupaa katika anga la Abunuasi.

Sikuamini siku ya harusi yangu kama ndio itakuwa hivi. Ilikuwa harusi mbaya haijapata kutokea. Si ile harusi iliyosheheni mafogo niliowaota nikiwa mdogo. Ilikuwa harudi iliyosheheni wazamiaji watafuta kitenesi alimaarufu kama mpunga. Mbaya zaidi ni kuwa hakukuwa na chakula siku ile.

Mke wangu SIKOMOYONI alikuwa kakaa kwa huzuni kama mkiwa. Kijigauni alichokivaa kilikuwa kama kioja na dhihaka kwa waliomtazama. Make up haukwa na ushirikiano usoni. Nilimuonea huruma sanal. Nilijiona mwenye hatia kumtenda mwanamke mzuri kama yeye mambo yale. Zile ndoto za yeye kuvaa gauni lenye kung'aa kama jua ziligeuka hekaya za Fumo Lyongo.

Sikuamini kama kweli siku ya harusi yangu nitavaa kiatu nilichokivaa miaka mitatu iliyopita wakati nilijua nitavaa kila kitu kipya kasoro mwili tuu ndio ungekuwa wa zamani. SIKOMOYONI alinitupia macho ambayo yalionyesha dalili zote za chuki na hasira alizokuwa nazo moyoni. Nisamehe SIKOMOYONI zile ndoto zangu za milenia ziliraruliwa.

Harusi iliisha na tuliondola pale kwenye ukumbi wa kanisa na bajaji badala ya chombo maalumu cha NASA. Tukapotelea huko vichochoroni uswahilini badala ya kwenda mwezini kula fungate.

Sikuamini kuwa wakati mwingine ndoto hugeuka adhabu kwa muotaji.

JOKA JEUSI
 
Joka u nataka kufanana Na Seneta wa mtwizi kila mpishana vitu kadha.
Nyote mmesoma Udsm
Nyote mmesoma art has a lugha.
Nyote mmesomea ualimu
Nyote ni wachejeshaji pia ni watunzi wa mashairi. Nyote mmehitimu zaidi ya miaka 3 iliyopita aumiwili.

Utofauti.
Seneta ni mmakonde kila we inawezekana ni mchaga au MTU kutoka uchagani au mbeya.
Seneta mwislam we mkristo
 
Joka u nataka kufanana Na Seneta wa mtwizi kila mpishana vitu kadha.
Nyote mmesoma Udsm
Nyote mmesoma art has a lugha.
Nyote mmesomea ualimu
Nyote ni wachejeshaji pia ni watunzi wa mashairi. Nyote mmehitimu zaidi ya miaka 3 iliyopita aumiwili.

Utofauti.
Seneta ni mmakonde kila we inawezekana ni mchaga au MTU kutoka uchagani au mbeya.
Seneta mwislam we mkristo


Nyekundu umenoa japokuwa unakaribia ukweli.
Watu tunaozaliwa Mwezi Machi tupo hivi Mkuu. Angalia asilimia kubwa ya wanaopost humu vitu amaizing wamezaliwa mwezi huo
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom