Siku ya Ukimwi Duniani iturejeshe kwenye maadili.
Leo ni siku muhimu duniani kwani mataifa yote yanaadhimisha kwa kukumbuka na kutathmini athari za ugonjwa wa Ukimwi tangu ulipojitokeza mwanzoni mwa karne hii. Ni siku muhimu pia ambapo jamii inawakumbuka wote waliopoteza maisha kutokana na janga hili la Ukimwi ambalo bado linaendelea kuteketeza watu wengi.
Hapa nchini, maadhimisho hayo yanayobeba kaulimbiu inayosema "Tanzania Bila Maambukizo Mapya ya Ugonjwa wa Ukimwi, Unyanyapaa na Vifo vitokanavyo na Ukimwi inawezekana", ambayo kitaifa yanatarajiwa kufanyika leo katika viwanja vya Mnazimmoja, Dar es Salaam na mgeni rasmi atakuwa Rais Jakaya Kikwete.
Katikati ya wiki hili, kulifanyika kongamano la kitaifa kuhusu utekelezaji wa kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambapo watendaji wa mikoa na wilaya wametakiwa kuweka mikakati maalumu yenye mkazo katika makundi mbalimbali yanayoongeza kasi ya maambukizo ya ugonjwa wa Ukimwi.
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein leo pia atakuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yatakayofanyika Paje mkoa wa Kusini Unguja.
Taarifa za maambukizi ya Ukimwi huko Zanzibar kwa mwaka 2012 hadi 2013 zinaonesha watu 108 walikutwa na maambukizi mapya na kufanya idadi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi visiwani humo kufikia 6,125. Maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa Zanzibar yameendelea kuwa asilimia 14 kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Wakati wa kongamano jijini Dar es Salaam, ambalo pia lilitoa fursa kwa wadau kujiandaa kabla ya maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga alisema yapo makundi ambayo yamekuwa chachu ya kuongeza maambukizo ya ugonjwa huo. Aliyataja kuwa ni pamoja na wafugaji, wafanyakazi wa utalii, wavuvi, machimbo pamoja na wajenga barabara za masafa marefu.
Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (TACAIDS), Fatuma Mrisho naye alisema lengo la kongamano hilo ni kutafakari hali halisi na mwelekeo wa udhibiti wa Ukimwi kwa jamii na taifa kwa ujumla ili kuweza kuona maambukizo ya ugonjwa huo yanapungua na kufikia asilimia sifuri.
Tunaziona jitihada za viongozi wa kitaifa kama dira ya mapambnano na janga la gonjwa hili baya nchini, kinachojaribu kudhoofisha kasi ya mapambano hayo ni wakati baadhi ya taasisi zinazojihusisha na elimu ya Ukimwi nchini kugeuza kama mradi binafsi unaowanufaisha, wakati wakiendelea kupata misaada ya fedha kwa wafadhili kupitia mgongo wa waathirika wa Ukimwi.
Nchi nyingi pamoja na taasisi za kimataifa zimeonesha nia ya kutoa misaada kupitia vikundi, asasi, pamoja na taasisi binafsi ambazo kwa nia njema zimedhihirika kuwasaidia waathirika wa Ukimwi, ingawa mwelekeo wa kutoa misaada ulibadilika pole pole na wao kugeuza kuwa mitaji yao ya ujasiriamali binafsi.
Tunaamini kwamba kupata takwimu ili kupima uzito wa tatizo la ugonjwa wa Ukimwi peke yake haitoshi kuonyesha kama ni sehemu ya mapambano, kinachotakiwa ni hatua gani zinachukuliwa kuwahudumia waathirika wa Ukimwi, pamoja na mikakati ya kupunguza maambukizo mapya.
Tunajua kuwa wapo wataalamu wengi wanaoweza kuandika michanganuo ya kutafuta misaada kwa ajili ya waathirika wa Ukimwi, wakisaidiwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini.
Hiyo peke yake kwa wataalamu hao inaonekana sawa na ajira ya kudumu. Baadhi yao wanaposikia mashirika yanayosaidia miradi ya kupambana na Ukimwi yakijiengua, wao wanapata hofu ya kutojua mustakabali wa ajira hiyo.
Mkazo mkubwa katika mapambano dhidi ya Ukimwi uwe kutokomeza kabisa janga hili, ili tuepukane kabisa na maambukizi mapya ya Ukimwi badala ya kugeuza kama mradi wa kujinufaisha kutokana na misaada ya fedha za wafadhili.
Hali ya maambukizi ya Ukimwi huko vijijini ni kubwa sana, huku baadhi ya wananchi kutokana na kukosa elimu ya Ukimwi, wamegeuza mtizamo na kuhusisha ugonjwa huo na masuala ya ushirikina.
Matokeo yake baadhi yao wamekuwa wakituhumiana na hata kuuana kutokana na imani potofu za kudhani wagonjwa wa Ukimwi wamelogwa.
Bado tunahitaji kuzidisha jitihada za dhati za kupambana na maambukizi mapya ya ukimwi ili kulinusuru taifa lisiangamie, na kwa bahati mbaya sana asilimia kubwa ya maambukizi mapya yanawapata vijana wa umri wa kati ya miaka 21 hadi 46, ambao ndiyo nguvukazi tegemezi ya taifa.
Ni imani yetu kuwa maadhimisho ya mapambano hayo yanayofanyika kote duniani leo, yatatoa mikakati mipya ya namna ya kupata ushindi dhidi ya maambukizi ili katika maadhimisho kama haya mwakani, tusiwe na takwimu ya maambukizi tena.
Rais Kikwete amewahi kutamka kuwa "Tanzania bila Ukimwi inawezekana", tunaamini hilo linawezekana ikiwa kila mmoja katika eneo analoishi atazingatia kumlinda mwenza wake kwa kuepuka vishawishi vya kufanya ngono zembe, pamoja na kuchukua tahadhari nyingine za kujikinga na maambukizi. Kila mtu achukue hatua kujikinga.
SOURCE: NIPASHE JUMAPILI