Nilipo mtaja bubu, si kwamba hawezi sema.
Ila ni mtaratibu, haneni kwa kulalama.
Ni mke mwenye adabu, anamuhofu kalima.
Natafuta wa kuoa, mdada alo na sifa.
Kipofu namaanisha, hatotazama wenzangu.
Mimi peke namtosha, ahahi na ulimwengu.
Sote twapanga maisha, kwa kutanguliza Mungu.
Natafuta wa kuoa, mdada alo na sifa.
Nikisema mlemavu, si kwamba hatotembea.
Ila kwangu ka ubavu, anatunza familia.
Sio kokolo la nyavu, mitaani zoazoa.
Natafuta wa kuoa, mdada alo na sifa.
Hakika nimekusoma, Ufafanuzi murua,
Fikira zilinihama, nikajua watania,
Mawazo yalishazama, lugha sikuitambua,
Utapata wa kuoa, Mola kishakupangia.
Mola kishakupangia, Utapata wa kuoa,
Wala hautojutia, Raha utajipatia,
Naye atawajalia, bora yenu familia
Utapata wa kuoa, Mola kishakupangia.
Amina amina sana, nasema tena amina,
Amina tena na tena, Tena na tena amina,
Tena nasema amina, Amina ilo amina,
Utapata wa kuoa, Mola kishakupangia.
ODM