Hussein Massanza
JF-Expert Member
- Dec 26, 2012
- 1,016
- 2,194
NI ulevi mbaya lakini halali kwa matumizi. Wenye kuutumia na kuathirika nao hali zao ni mbaya. Usijaribu kumshauri mwanasiasa aache siasa kabla hajachoka mwenyewe, hatakuelewa.
Mfuatilie mwanasaisa ambaye alikuwa mbunge kwa miaka kadhaa, kisha akashindwa uchaguzi. Ni nadra kukubali matokeo. Anapokaa nje ya ulingo, maisha yake hutawaliwa na msongo wa mawazo au hata huzuni.
Siasa zina alosto mithili ya mtumia madawa ya kulevya anapokosa vitu vyake. Je, unayajua mateso ya teja anapokosa mihadarati? Basi kutana na mwanasiasa aliyekuwa na nafasi yake kisha akaipoteza.
Mamlaka yanapumbaza. Yanaweza hata kumpa ukichaa mwenye mamlaka. Hii ni kwa sababu mamlaka yanapumbaza kuliko mihadarati. Watu wengi wazuri walibadilika. Usichezee mamlaka!
Mgogoro wa Zanzibar ni ulevi tu wa kisiasa! Kinachobishaniwa ni vyama na mamlaka. Kama ingekuwa kinachotazamwa ni ukweli wa mambo na maridhiano kutokana na hali halisi, mgogoro ungekuwa umeshakwisha.
Maana ingekuwa ni ukweli kuthibitishwa kuwa ama uchaguzi ulivurugwa, hivyo urudiwe au Seif Sharif Hamad alishinda, kwa hiyo atangazwe. Tatizo ukweli unawekwa kando kisha yanatazamwa maslahi, Dk. Ali Mohamed Shein anavuta, Seif naye pia. Vuta nikuvute!
Badala ya kuwatazama Wazanzibar katika jicho la kwanza, kinachoangaliwa kwanza ni vyama. Wanasiasa wanajikita kwenye hatari ya kukosa utamu wa kupata. Mazungumzo yanabeba tafsiri ya faida na hasara. Siku zote uchaguzi siyo tatizo kama ridhaa ya mpigakura itaheshimiwa.
Burundi, Rais Pierre Nkurunziza tayari ameshapumbazwa na mamlaka. Haoni tatizo kwa wananchi wasio na hatia kuuawa. Kwake kuachia madaraka bora watu waendelee kupoteza maisha. Warundi wanakufa, wanakimbia nchi yao.
Chukua hii; Mamlaka yanapumbaza kuliko moshi wa bangi, na yanapita aina zote za mihadarati. Wapenda mamlaka wakishayapata na kujisikia wanayo, kisha kujiamini kuwa amri na maagizo yao ni sauti kuu ya kutekelezwa bila kuhojiwa, wanaweza kutenda mambo ambayo hata kichaa angeogopa au kuyaonea aibu.
Tatizo ni mgogoro tu wa kikatiba; Nkurunziza anang’ang’ania awe rais kwa kipindi cha tatu kwa sababu muhula wa kwanza aliidhinishwa na bunge, kwa hiyo katiba haimzuii. Kwamba katiba inaweka ukomo wa vipindi viwili vya uongozi kama rais atakuwa amechaguliwa mara mbili na wananchi. Nkurunziza anadai yeye muhula wa kwanza hakuchaguliwa na wananchi, kwa hiyo anataka amalizie kipindi cha tatu, kwani ndiyo atakuwa ametimiza vipindi viwili vya kuchaguliwa na wananchi.
Mwaka 2005, baada ya vikundi vya waasi kupata upatanisho na kukubaliana kwenda kuijenga Burundi moja, baada ya wabunge kupatikana, Bunge la Burundi lilimchagua Nkurunziza kuwa rais na mwaka 2010, ulifanyika uchaguzi na kuchaguliwa na wananchi. Hapo ndipo palipo na mgogoro!
Na kwa kutazama hali halisi, ni wazi bila shaka yoyote kuna ulevi wa kisiasa, vilevile pumbazo la mamlaka. Mamlaka za kutafsiri sheria zipo, ni kwa nini mgogoro unazidi kuchukua nafasi? Ndipo unakuja kugundua kuwa siku zote wanasiasa ambao wameshalewa siasa zao kisha wakawa wanapingana, hata siku moja hawawezi kupata mwafaka. Ni vigumu mno!
Mamlaka yanataka unyenyekevu na kutambua kuwa alichonacho ni dhamana tu. Wapo wengine wanaweza kutenda kazi aliyonayo kwa ubora zaidi kuliko yeye, ila imekuwa bahati na kuaminiwa tu!
Mtu aliyelewa au kupumbazwa na mamlaka, huvimba kichwa mpaka kuamini kuwa zaidi yake hakuna mwingine mwenye akili, nguvu na uwezo. Na ndiyo sababu wapo viongozi hutoa maagizo kama vile baba wa familia anawaambia watoto wake wadogo.
Muangalie Robert Mugabe wa Zimbabwe! Pale alipo haamini kama kuna Mzimbabwe mwingine mwenye uwezo wa kuongoza nchi hiyo. Ameshalewa mamlaka!
Mwanasiasa hukenua na kuona maisha yanamuendea vizuri pale anapofanya mikutano ya hadhara na kupata watu. Wanasiasa wanapenda kupendwa, huhitaji wafuasi wengi. Huumia wanapokosa watu. Mwanasiasa anapokosa jukwaa la kufanyia siasa hulegea na kulendemka mithili ya teja na alosto! Mwanasiasa afanye matukio bila kuonekana kwenye vyombo vya habari, huumia kwelikweli!
Hii ndiyo sababu wanasiasa hulogana kwa wale wenye imani za kishirikina. Hupandikiziana fitina kwa wenye hulka za ufitini. Wanasiasa huwaonea wivu na kutamani kuwashusha wenzao wanaong’ara.
Ukitaka kujua kuwa mamlaka yanalevya na siasa ni uteja, msome Rais wa Sita wa Marekani, John Quincy Adams, aliyeongoza kwa muhula mmoja tu, kati ya mwaka 1825 mpaka 1829.
Baada ya kushindwa kwenye uchaguzi na Rais wa Saba, Andrew Jackson, Adams alikuwa kama teja. Maisha nje ya ulingo wa kisiasa yalimtesa. Washington DC, alipaona pagumu mno. Akaamua kurejea nyumbani kwao kwenye mji aliokulia wa Quincy, Massachusetts.
Kabla ya kuondoka Washington, Adams alisema: “The sun of my political life set in the deepest gloom.”
Kiswahili: Jua la maisha yangu ya kisiasa limewekwa kwenye giza totoro.
Alikuwa mwenye huzuni sana. Hata baada ya kufika Quincy, aliona bado hawezi kuishi nje ya siasa, akaamua kugombea ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, akashinda. Rais kwenda kuwa mbunge, hiyo ndiyo tabia ya mwanasiasa anapolewa. Mwanasiasa lake ni jukwaa, akilikosa ni kama teja.
Adams alishika vyeo vingi kabla hajawa rais lakini hakuridhika, alitaka aendelee kuongoza. Alishika nafasi mpaka ya Uwaziri wa Mambo ya Nje lakini hakutosheka. Na alishinda ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, aligombea tena na tena kabla ya kufikwa na mauti mwaka 1848, tena akiwa bado mjumbe!
Alifikwa na mauti akiwa na umri wa miaka 80. Akiwa anaugua kiharusi, aliuona kabisa mwisho wake, akasema: “This is the end of earth, but I am content.”
Kiswahili: Huu ndiyo mwisho wa dunia, lakini nimeridhika.
Kwamba kutokana na ulevi wake wa vyeo, alipokuwa anakaribia kufa, aliona kama ndiyo na dunia inakwisha. Tangu mwaka 1848, dunia bado ipo!
Kituko kingine, Adams aligoma kuhudhuria siku Jackson alipoapishwa kuongoza Marekani, kwa hiyo hakukabidhi mamlaka rami kwa mrithi wake, kutokana na kinyongo. Wanasema maji hufuata mkondo, kwani Adams ni mtoto wa Rais wa Pili wa Marekani, John Adams, aliyeongoza nchi hiyo kuanzia mwaka 1797 mpaka 1801, naye aliposhindwa na Thomas Jefferson, alisusia sherehe za uapisho.
Ona mamlaka yanavyopumbaza na kusahaulisha watu. Robert Guei aliongoza mapinduzi yaliyomuondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Henri Konan Bedie Desemba 1999.
Yalikuwa mapinduzi ya kikundi kidogo kisicho na ridhaa ya wengi (coups d'etat). Hata hivyo, Guei alitetea dhamira ya mapinduzi kuwa ni kujenga demokrasia, haraka sana akatangaza na tarehe ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Rais.
Uchaguzi ulifanyika Oktoba 22, 2000. Baada ya mahesabu Guei aliyejitangaza kama msimika demokrasia nchini kwake, alishindwa na Laurent Gbagbo wa Chama cha Ivorian Popular Front (IPF).
Hata hivyo, Guei hakutaka kukubali matokeo, kwanza alijitangaza kuwa mshindi, kisha akasema aliongoza matokeo ya awali kwa idadi ya kura pungufu ya asilimia 50, hivyo ilitakiwa uchaguzi urudiwe kati yake na Gbagbo. Hesabu zilipopigwa vizuri, zilionesha Gbagbo alishinda kwa asilimia 59.
Idadi hiyo ya kura za Gbagbo zilitosha kumfanya atangazwe kuwa mshindi bila kufanyika marudio ya uchaguzi. Tatizo ni kipindi ambacho Guei alikuwa ameshapumbazwa na mamlaka, hakutaka kuachia ngazi. Wananchi wa Ivory Coast waliingia barabarani, waliandamana mpaka kwenye makazi ya rais na kumuondoa Guei madarakani, kisha Gbagbo aliapishwa kuiongoza nchi hiyo.
Hii ina maana kuwa Gbagbo alijionea kilichompata mtangulizi wake (Guei). Na ni yeye aliyesababisha mwisho mbaya wa Guei ambaye aliuawa kinyama, akiwa na mkewe pamoja na watoto wake, Septemba 19, 2002, Cocody, Abidjan.
Mamlaka yanapumbaza kuliko mihadarati! Kipindi cha uongozi wa Gbagbo, kilitakiwa kufika ukingoni mwaka 2005 kisha aitishe uchaguzi mwingine, lakini kwa makusudi aliahirisha. Malalamiko yalikuwa mengi lakini alivimba kichwa. Tayari alishalewa!
Hakukumbuka tena kilichompata mtangulizi wake! Baada ya kusemwa sana, mchakato wa uchaguzi ulianza na uchaguzi wenyewe ulifanyika Oktoba 31, 2010 lakini Gbagbo alishinda kwa asilimia 38, huku mpinzani wake, Alassane Ouattara akiambulia asilimia 32. Hakuna aliyezidi asilimia 50.
Uchaguzi ulirudiwa kwa mafahari wawili, Gbagbo na Ouattara. Matokeo yakamuonesha Ouattara mshindi kwa asilimia 54. Gbagbo akakataa kuachia madaraka. Mwisho aliondolewa kwa aibu, ikiwa pamoja na kudhalilishwa mno yeye na mkewe. Siku zote kumbuka, mwisho wa ubaya ni aibu!
Kimsingi kama kuna aina ya mihadarati inayopumbaza ubongo lakini wakati huohuo aliyepumbazika akawa anaonekana ana akili nzuri, basi ni mamlaka. Ni hatari sana! Yupo mtawala aliwahi kusema wakifa watu wawili kwa ajili ya kulinda mamlaka siyo jambo baya. Mantiki yake ni kuwa bora watu wafe lakini utawala ubaki kwa mtawala.
Uongozi umetawaliwa na ghiliba. Katiba zinavunjwa, vyama vya siasa vinajaza masultani badala ya viongozi. Unakuta mwenyekiti wa chama hataki kupisha, anang’ang’ana. Ulevi wa madaraka!
Imekuwa fasheni sasa, mtu akikaribia kumaliza muda wake wa uongozi, eti wanatokea watu, wanaanzisha vuguvugu la kumshawishi asiachie ngazi, agombee tena.
Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipong’atuka, Watanzania hawakuandamana kumshinikiza atengue uamuzi wake. Siku hizi kuna watu wanapendwa ndani ya vyama, kuliko Nyerere kwa Watanzania. Kiongozi mzuri ni yule anayetambua kuhusu maono, kwamba yapo ya kwake, vilevile kuna ya mwingine. Ongoza kwa kipindi chako, baada ya hapo unapisha wengine.
Kiongozi mzuri hutumia muda wake wa kikatiba kufanya kile hasa ambacho anatakiwa kufanya. Maono yake yote huyafanyia kazi katika kipindi ambacho amehalalishwa. Hii ina maana kuwa utakuja muda mwingine kwa ajili ya uongozi wa mtu mwingine.
Jambo la msingi ni kutambua ukishapewa mamlaka, yakulevye na yakupumbaze lakini yasikudanganye kuwa ni wewe pekee ndiye mwenye haki, uwezo na nguvu za kuongoza na wengine ni wa kuongozwa na kutawaliwa tu.
Ulevi wa mamlaka ni mbaya sana! Tena mamlaka yenyewe ya urais katika nchi ambayo rais ndiye kila kitu. Frederick Chiluba ni marehemu hivi sasa lakini aliwahi kupumbazwa na mamlaka mpaka akasahau kuwa zipo nyakati za baadaye, hatakuwa tena rais.
Katika Bara la Afrika ambalo mtu kuachia madaraka anaonekana wa ajabu mno, Kenneth Kaunda alionesha njia. Kaunda ambaye ndiye Baba wa Taifa la Zambia, alipigania uhuru wa taifa hilo kutoka kwa Muingereza, kipindi hicho nchi hiyo ikiitwa Rhodesia ya Kaskazini.
Kwa amani kabisa, Kaunda akaridhia mfumo wa vyama vingi vya siasa na uchaguzi ulipofanyika mwaka 1991, Chiluba alishinda, kisha Kaunda akakubali matokeo na kumkabidhi usukani wa uongozi mshindi.
Chiluba akasahau yale amepewa ni mamlaka ambayo msingi wake ni dhamana kutoka kwa wananchi, siku wakiamua kuyadai wanayachukua. Chiluba akamtesa Kaunda, akawa fisadi na kukiuka misingi ya utawala bora na haki za binadam.
Muda wa Chiluba ulipokwisha alitaka kufanya fujo ya kubadili katiba, aliposhindwa, alitaka kumuweka kibaraka, Levy Mwanawasa ambaye alipoapishwa tu, aliamua kumtambua na kumuenzi Kaunda kama Baba wa Taifa la Zambia.
Ni kipindi cha Mwanawasa, Chiluba alikutana na mateso makubwa kutokana na fujo ambazo alizifanya kipindi cha utawala wake. Maisha yalikuwa magumu mno. Mke wa Chiluba, Regina Mwanza Chiluba, alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu na nusu kwa wizi wa mali za umma, kipindi mumewe alipokuwa madarakani.
Leo hii Paul Kagame anajiona malaika, kwamba bila yeye Rwanda hakuna utulivu! Amesahau yaliyompata hayati Juvenal Habyarimana, aliyeitawala Rwanda miaka 21 na kujiona kuwa hakuna mtu mwingine wa kuongoza zaidi yake.
Baada ya wananchi kukerwa kwa muda mrefu, mwaka 1994 walimuua kwa kuitungua ndege aliyokuwa amepanda, ilipokuwa inakaribia kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kigali, Rwanda. Na baada ya hapo, yalifuata mauaji ya kimbari (genocide).
Tatizo ni kuwa mamlaka yakishampumbaza mtu, hufurahia kusifiwa na hukasirika kuambiwa ukweli. Mlevi wa madaraka hujiona mtu mkubwa mno, kwa hiyo kukosolewa huwa haitakiwi. Unaweza kuwaza Kagame anafikiria nini leo na usipate majibu. Haoni utamu kuachia madaraka kipindi ambacho bado anapendwa. Anataka mpaka wananchi wamchoke, wamdhalilishe.
Mwalimu Nyerere aliachia madaraka kipindi ambacho Watanzania walikuwa bado wanampenda na kumwamini. Hata yeye angekaa mpaka kuwachosha wananchi, asingekuwa na heshima ambayo ameondoka nayo. Wanasiasa wachukue somo!
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, anaongoza nchi ambayo alipata kutokea jabali, aliyejitangaza kuwa rais imara duniani, Idd Amin Dada ambaye mwisho wake ulikuwa mbaya sana. Akitambua kila kitu, Museveni hafikirii kabisa kukabidhi uongozi wa nchi kwa mtu mwingine. Naye anasubiri siku wananchi wakasirike, waamue kumvunjia heshima na wamadhalilishe. Kama ingekuwa kila mwanasiasa anakumbuka mwisho mbaya wa wengine, hakika wangejirekebisha sana.
Thabo Mbeki wa Afrika Kusini alijisahau kidogo na kujikuta anaondolewa madarakani na chama chake, African National Congress (ANC). Nidhamu ya uongozi inawashinda wengi.
Alikuwepo Jenerali Sani Abacha wa Nigeria, alikufa na kuzikwa kama mgonjwa kipindupindu! Kifo usiku, asubuhi mazishi. Wengi wanaamini aliuawa lakini alikimbiziwa kaburini bila hata maiti yake kufanyiwa uchunguzi (autopsy).
Tafakari kuhusu ubabe wa Abacha na jinsi alivyofariki dunia na kuzikwa. Utakuja kugundua kuwa mengi ni fahari ya macho tu pindi mtu anapokuwa na madaraka yake. Vinginevyo, maisha yanataka watu wawe wanyenyekevu.
Fungua faili la Afrika ya Kati, utamkuta mtu mzito na aliyeogopwa hasa. Anaitwa Jean-Bedel Bokassa. Mwenyewe alipenda aitwe Bokassa I. Yote kuhusu ukatili na kuwaua wapinzani wake yalikwisha, mwisho alifariki dunia akiwa mtu mnyonge kabisa. Hata siku moja mtu hatakiwi kudanganywa na mamlaka!
Wapo huvimba vichwa kwa sababu ya ushauri wa wake zao. Wakumbuke kuwa Mfalme Louis XVI wa Ufaransa aliponzwa na mke wake, Marie Antoinette. Lugha za kuudhi na kuumiza nyakati za dhiki ndiyo sababu kuu.
Ilikuwa Karne ya 18, wananchi waliandamana kudai chakula, maana njaa ilikuwa kali na kwenye nyumba zao hakukuwa na chakula. Maandamano yalipofika kwenye jumba la mfalme, Marie Antoinette alihoji: “Mbona kelele nyingi, wana matatizo gani?”. Walinzi wa jumba la mfalme walimjibu Marie: “Wanalalamika njaa, wameishiwa mikate.”. Marie akajibu kwa dharau: “Sasa hapo tatizo nini? Kama mikate hawana si waende wakale keki?”
Wananchi wa Ufaransa walikasirika mno kwa jibu hilo, wakahimizana kuuondoa utawala wa Mfalme Louis XVI madarakani. Na huo ndiyo ukawa mwisho wa tawala za kifalme nchini Ufaransa.
Kilichomponza Marie ni kupumbazwa na raha zilizokuwepo ndani ya jumba la mfalme. Kwamba vyakula vipo na ni vya kuchagua tu. Keki na mikate vipo vingi. Hakujua kuwa maisha hayo hayapo kwa mwananchi wa kawaida. Kama amekosa mkate ambao ni rahisi, keki ambayo ni ghali anaipataje? Ndiyo maana wananchi waliona hayo ni matusi.
Kila mtu awe mnyenyekevu anapokuwa na mamlaka. Akumbuke kesho na hatari zake. Kwa kuweka mbele kesho, ni rahisi kutambua kuwa madaraka si vitu vya kung’ang’ania wala kupigania.
Usiache pia kumkumbuka Mobutu Sese Seko na utajiri wake. Urais wake aliuona ndiyo kila kitu. Akajilimbikizia mali. Akawa kiongozi tajiri kupita mfano. Akaharibu nchi. Lakini akawa mtu mwenye kuogopwa mno. Mwisho wake alipinduliwa na kufariki dunia akiwa hata hajui wapi panaweza kuwa mahali salama kwake kuishi. Mali zake zote zilifilisiwa.
Madaraka ni matamu ila yakikulevya shauri yako.
By Luqman Maloto