Dotto C. Rangimoto
JF-Expert Member
- Nov 22, 2012
- 1,985
- 1,284
Tumbo laniunguruma, ninaharisha matata,
Kichwa nacho chaniuma, kitovu kinanikata,
Kila siku mie homa, ngozi yote yafukuta,
Si bure nimeupata, hizi dalili za ngoma.
Mbavu zina chomachoma, mgongo wanichonyota,
Naenda kwa kuinama, mwili ninaukokota,
Vikizidi kunichoma, mwendo sina ninasota,
Si bure nimeupata, hizi dalili za ngoma.
Chakula siwezi uma, kooni tabu kupita,
Majipu yasiyo koma, mwilini yameniota,
Nimekonda sina nyama, hema yangu ya kukuta
Si bure nimeupata, hizi dalili za ngoma.
Kupenda kwangu kulima, kila shamba nilokuta,
Ninaingia mazima, naanza piga matuta,
Nimekuwa kiserema, leo sasa ninajuta,
Si bure nimeupata, hizi dalili za ngoma.
Hapa tupu sijapima, peke yangu mwaniwata,
Vipembeni mwanisema, gari limegonga kuta,
Siko tayari kupima, kwa nguvu mnganivuta,
Si bure nimeupata, hizi dalili za ngoma.
Dotto Rangimoto Chamchua(Njano5)
whatspp/call 0622845394