KARIBU TANGA
Mola wangu karima, hakika kanijalia
Kanipa nyingi hekima, macho kanifungulia
Sina ujanja wa kima, hilo nakubalia
Karibu mtani nyumbani, uingie mahabani
Ukweli nakwambia, sina nikifichacho
Maneno yangu sikia, nasema bila mipasho
Fadhila nasadikia, pasina roho ya korosho
Karibu mtani nyumbani, uingie mahabani
Sindano nakualika, nyumbani karibia
Ule mseto hakika, na nguru wa kunukia
Utoe zako hamaka, upate jifurahia
Karibu mtani nyumbani, uingie mahabani
Usiogope fadhila, watanga ni jadi yetu
Fadhila kwetu jalala, jione mtu wa kwetu
Na kitanda utalala, upate raha za kwetu
Karibu mtani nyumbani, uingie mahabani
Mchumba nikupatie, mwenye adili sawia
Ndoa iangukie, halali upate jilia
Furaha zikurudie, Mola atakujalia
Karibu mtani nyumbani, uingie mahabani
Na dini tukufundishe, akili ipate tulia
Maadili turudishe, tusije pata kulia
Tamaa zako ziishe, nuru ipate jazia
Karibu mtani nyumbani, uingie mahabani
Mjadala naufunga, Chama najiendea
Karibu nyumbani Tanga, ubaki kujisemea
Usije tia nanga, Tanga ukafemea
Karibu mtani nyumbani, uingie mahabani
Chama
Gongo la Mboto DSM
NA TANGA NDIO NYUMBANI
Binadamu si kamili, tuombe istifara
Mola wetu muhimili, tujaze yenye busara
Tuepushe na batili, na nyoyo ziwe imara
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Yarabi tupe shufaa, tuondoshe matatani
Tukinge na mabalaa, akhera na duniani
Maisha haya hadaa, tuepushie shetani
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Namshukuru jalia, muongozo nilipata
Chuoni kuhudhuria, suna hadithi nafata
Si kama najisifia, ya dini sina utata
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Mtani ninashukuru, Tanga kunikaribisha
Mji uso na kufuru, ni mengi yenye bashasha
Kibwando Bada na Nguru, hamu haiwezi kwisha
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Ni chuda ninatokea, ndio kwenye maskani
Bakwata nilisomea, miaka ya themanini
wewe wapi mebobea, nijuze basi mtani
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Vitongoji navijua, vyote vya Tanga mjini
Na kote wanitambua, Tanga mimi si mgeni
Uliza hata washua, mabawa na chumbageni
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Nadhani tukaribishe, ndugu zetu wa kusini
waje wajipumzishe, kwa raha za jasmini
wasahau mishemishe, wakandwe mdalasini
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Mapenzi yale ya Tanga, hayahitaji vileo
Mambo udi kungu manga, kitandani kipepeo
Na kuna mambo ya kanga, waoshwa na pembejeo
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Swahiba basi nambie, ni wapi unatokea
Nataka nijipangie, niweze kuja tembea
Na mengi tujadilie, tujenge na mazoea
Tanga nishakaribia, na Tanga ndio nyumbani
Sindano Mwana wa Ganzi (SMG)