Kwa kweli nilijitamba, ijapo si mmiliki
Nikawaita washamba, hata ndugu marafiki
Nikawa mimi ni mwamba, kejeli nyingi na chuki
kisima nimekiacha, maji hanyweki tena
............................................................
Na nyinyi enyi malenga, tahadhari nawambia
Hakuna sifa kulenga, chini tutawafukia
Mimi nimeshajitenga, na kule sintarudia
kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena
Wenu
Sindano Mwana wa Ganzi. (SMG)
Pokea pole mtani:
Pokea pole mtani, kupoteza lako dili
Maji hayo kisimani, nataka tuyajadili
Tena fikiri kichwani, utafahamu dalili
Kupoteza lako dili, pokea pole mtani
Nafikiria kichwani, nahisi u m bahili
Ukateka kisimani, halafu huku kijali
Vya watu ukitamani, tafuta yake asili
Kupoteza lako dili, pokea pole mtani
Najua ulitamani, vya bure bila kujali
Vina ladha mdomoni, hakika kama asali
Wenyewe ni kina nani? kichwani uliza swali
Kupoteza lako dili, pokea pole mtani
Kisima siyo mtoni, uliza kwa wenye mali
Walochimba kisimani, iweje hukuwajali?
Busara yako kichwani, ni vipi hukujadili?
Kupoteza lako dili, pokea pole mtani
Vieleavyo majini, nasema vina asili
Mtoni pia ziwani, baharini kuna meli
Asili yake ni nani, uliza bila kejeli
Kupoteza lako dili, pokea pole mtani
Pokea pole mtani, ingawa si yako mali
Jifunze tena kichwani, kujua yake asili
Vya watu ni mtihani, usivifanye ni dili
Kupoteza lako dili, pokea pole mtani
Hati miliki muhimu;
Hati miliki muhimu, na umma kutangazia
Kufuli siyo muhimu, hati ukishikilia
Watakwepa wadhalimu, mwenyewe wakihofia
Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu
Kamwe hawata dhulumu, safari ukianzia
Heshima pia nidhamu, kwa kina kuheshimia
Utadhania mwalimu, nidhamu kitapatia
Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu
Uianze kwa salamu, wakati wakizengea
Wajuwe siyo dhalimu, mwanzoni ukianzia
Washenga na mabinamu, watume kwa asilia
Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu
Ni muungwana wa hamu, na wao watahisia
Wenyewe kukuheshimu, mwanzo mzuri anzia
Wakuone si mgumu, na posa kuwatumia
Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu
Tano zilizo muhimu, ni mwisho ninaishia
Nahisi umefahamu, kosa usije rudia
Utaupata wazimu, wengine wafanyizia!
Sikia kaka sikia, hati miliki muhimu
Mwenzenu ninajongea, taratibu nawajia
Kwa haya yalotokea, ya kisima nawaambia
Hofu menisogelea, na nguvu zimeishia
kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena
Kisima nilitumia, na mtu sikuchangia
Usafi lizingatia, kwa ndani nikiingia
Nilionyesha na nia, kufuli kukifungia
Kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena
Nanikiwa kisimani, mwenzenu ninafurahi
Mengine siyatamani, siwezi wahadithia
Ni raha iso kifani, moyo unavyotulia
Kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena
Nilikunywa nikaoga, na mengi nikafanyia
Sikuwa hata na woga, madhara sikudhania
Na watu nikawakoga, raha zilivyozidia
kisima nimekiacha, Maji hayanyweki tena
Kwa kweli nilijitamba, ijapo si mmiliki
Nikawaita washamba, hata ndugu marafiki
Nikawa mimi ni mwamba, kejeli nyingi na chuki
kisima nimekiacha, maji hanyweki tena
udhuru ulinipata, kwa mbali kusafiria
Nyuma yaliyofuata, machungu kusimulia
Waovu walikamata, mabaya kukusudia
Kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena
Kisima liharibiwa, waovu watu wabaya
Tope walivyochimbuwa, kweli walikosa haya
Umbole kahujumiwa, 'saizi' sasa yapwaya
Kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena
Kwa sasa kimepoteza, umbole lile asili
Waovu nao wabeza, wasema hakina 'dili'
Usijaribu penyeza, utazama wako mwili
Kisima nimekiacha, maji hanyweki tena
Kisima sasa hatari, wadudu wamejibanza
kutumia kwa hadhari, fikiri kabla kuanza
Nimeacha jivinjari, tamaa sije niponza
kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena
Na nyinyi enyi malenga, tahadhari nawambia
Hakuna sifa kulenga, chini tutawafukia
Mimi nimeshajitenga, na kule sintarudia
kisima nimekiacha, maji hayanyweki tena
Wenu
Sindano Mwana wa Ganzi. (SMG)
Nasema pole sindano; wahenga hukusikia
Maisha ni mashindano, si ajabu kutindikia
Wajinadi kwa maneno, mrembo wajipatia
Kususa uhayawani; ya bahari huyawezi.
Jirani kajihifadhi; maji shinda kajitekea
Kisima hakina maradhi; janga limekutokea
Wamlaumu mahadhi; maji amejinywea
Kususa uhayawani; ya bahari huyawezi
Tuliza akili yako, maji hayana makombo
Jitwalie kata yako, kisimani rudi zako
Kunywa maji yako; ikate kiu yako
Kususa uhayawani, ya bahari huyawezi.
Yakisima yamezidi, utamu hauna mfano
Mahadhi kajirudi, hana shari ya maneno
Sindano nyumbani rudi, jilie raha zako
Kususa uhayawani, ya bahari huyawezi.
Chama
Gongo la Mboto DSM.
Uamuzi nilochukua, hakika niwa busara
Jaribu kudadavua, sindano sina papara
Hili ukishalijua, huwezi pata madhara
Tope lishavurugwa, maji hayo sinywi tena
Tope zilichimbuliwa, maji sasa karaha
Sipendi kushutumiwa, nasema hayana raha
Kisima lifumiliwa, tena pasi na staha
Tope lishavurugwa, maji hayo sinywi tena
Kisima kimechafuka, na tope kila sehemu
Nduguyo nimeshituka, kwa pale sinayo hamu
Siwezi kuwa mzuka, kujitoa ufahamu
Tope lishavurugwa, maji hayo sinywi tena
Vipi nikitia kata, tope likang'ang'ania
kipi kitakachofata, kama sio kujutia
Na maradhi nikipata, nani tanihudumia?
Tope lishavurugwa, maji hayo sinywi tena
Kisima tadumbukia, cha maji yalo salama
Humo nitafurahia, na wala sintolalama
Mbizi nitazidishia, kwa ndani ninavyozama
Tope lishavurugwa, maji hayanyweki tena
wako
SMG
Nduguyo bado nasita
Mtani nimekupata, hati wasisitizia
Ila ni tabu kupata, kisima kiso kadhia
vingi kwa kweli matata, lengo hutolifikia
Visima viwango duni, nduguyo bado nasita
.......................................................
Kipata chenye viwango, choveki nitakwambia
Huu ndo wangu mpango, ubora kuzingatia
Hapa sirushi madongo, mwenzio nasubiria
Visima viwango duni, nduguyo bado nasita
wako
SMG
Kususa si uunngwana, busara kufikiria
kisima chako bayana, hakuna wa kubishia
Hakuna kulaumiana, hilo nakazania
Mso hili analile, kaa chini fikiria
Makosa uliyatenda, mwenyewe hukusikia
Kisima hazina linda, vingapi utasusia
Nasema njia panda, sindano wajitakia
Mso hili analile, kaa chini fikiria
Kosa kutendeana, hilo mbona halina shida
Waungwana kusamehana, jambo hilo kawaida
Jitulize na rehana; hata wewe umeranda
Mso hili analile, kaa chini fikiria
Kisima chako maridhawa, hakina msimu wa maji
Hakika nakuweka sawa, usiwe mropokaji
Waugopa ugonjwa, hali wewe msakaji
Mso hili analile, kaa chini fikiria
Chama nipo safarini, nikija nitakuona
Usionione hayawani, hilo nimeshaliona
Umepata mtihani, jaribu kushauriana
Mso hili analile, kaa chini fikiria.
Chama
Gongo la Mboto DSM.
Ukiona vyaelea;
Ukiona vyaelea, ujuwe vimeundiwa
Nami nakukumbushia, si kwamba vimejaliwa
Tafuata chako tunzia, mengine ni majaliwa
Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea
Nimeanza na msemo, kukumbusha ya wahenga
Tena kipate kisomo, twakujulisha malenga
Ama waleta mgomo, kufuga wipiga chenga?
Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea
Ni vingi vyenye viwango, machoyo ukifungua
Tumia wako ubongo, kwa dhati utajulia
Wala huhitaji hongo, vinono kujipatia
Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea
Tafuta chako utunze, utashangaa mavuno
Tena kutunza jifunze, utafaidi vinono
Kisima chako kitunze, kwa yako hiyo mikono
Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea
Hapa nasema tamati, nahisi umenipata
Mradi ujizatiti, nasema utakipata
Na tena cha madhubuti, kisima na yake kata
Ujuwe vimeundiwa, uonavyo vyaelea
KIPI ZAIDI YA KIPI?
Kuna visima vya pwani, wengi wavisimulia
vyajua mambo fulani, raha hazitaishia
Hata kiwe cha zamani, mwenyewe utaridhia
Vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?
...........................................
Na kuna vya kule bara, sifaze sijazipata
Labda navyo imara, Choveki unazo data?
Vipi kikiri kakara, vyaweza kweli kunata?
Vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?
SMG
SI KAMA NIMESUSIA
Mengi nilifikiria, wala sikukurupuka
Busara nimetumia, ndo kisa cha kufunguka
Na wala sitojutia, hili halina mashaka
si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho
Ni vipi wanishutumu, ukweli hutaki ona
Hivi nikilamba sumu, wadhani naweza pona?
Napingana na dhalimu, walojaa kila kona
Si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho
Mbona nimeshasamehe, madhila nilofanyiwa
Kwao wao iwe sherehe, kila jambo majaliwa
Nangoja yangu tarehe, kwa lile nilopangiwa
Si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho
siwezi jilazimisha, moyo wangu umzito
kisima tabadilisha, nataka umotomoto
Nianze yangu maisha, niachane na majuto
si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho
safari nakutakia, ufike huko salama
Na tena ukirudia, sikose kunitazama
Ndio mambo ya dunia, ngoja niache lalama
si kama nimesusia, lenye mwanzo lina mwisho
SMG
KIPI ZAIDI YA KIPI?
cha kwangu nitatafuta, hili nimedhamiria
Tena nikisha kipata, walahi nitatulia
Vya watu sitafuata, mola tanisaidia
vya pwani na kule bara, kipi zaidi ya kipi?
Kuna visima vya pwani, wengi wavisimulia
vyajua mambo fulani, raha hazitaishia
Hata kiwe cha zamani, mwenyewe utaridhia
Vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?
Majiye kama nanasi, walonavyo meniambia
Havipatikani nkasi, mombasa ndo asilia
utatulia kwa nafsi, usijute na dunia
vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?
Na kuna vya kule bara, sifaze sijazipata
Labda navyo imara, Choveki unazo data?
Vipi kikiri kakara, vyaweza kweli kunata?
Vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?
Visima vya asilia, kwa sasa tabu kupata
mchina kaingilia, soko amelikamata
Na kama hujajulia, kundini waweza fata
vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?
Mtani usinichoke, nduguyo nahangaika
Naomba nihifadhike, niache kulalamika
salama nisalimike, maisha yenye mashaka
vya bara na kule pwani, kipi zaidi ya kipi?
SMG
Muhimu Kuridhika nacho tu;
Chongo kuita kengeza, msemo ushasikia?
Si fundi wa kueleza, ni wapi kulobobea
Uzushi sitoeneza, na hilo kaka julia
Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima
Nchini kote uliza, majibu siyo sawia
Wa pwani wanidokeza, visima vyao hulea
Sauti utaipaza, kwa ladha ya asilia
Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima
Bara ni kama baraza, visima hivyo sikia
Na kiu utamaliza, na mazingira sawia
Kwa macho utaangaza, wakati wakodelea
Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima
Wasema hutopoteza, na bara utarudia
Visima vyao vyajaza, kwa maji yalo sawia
Mchina hajakatiza, vya bara ni asilia
Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima
Vya pwani siyo vilaza, mtani hapo julia
Kwa mengi vinashangaza, ufundi wa asilia
Kwa ndugu utaapiza, kisima kutoachia
Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima
Ridhika nimeeleza, muhimu hiyo sikia
Chongo kuita kengeza, ishara ilo timia
Utabaki waapiza, na mali ukagawia
Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima
Mtani ninamaliza, mwishowe ninaishia
Ni mengi nimeeleza, wajibu kwako kujua
Muhimu maji kujaza, kisima kilo tulia
Ridhika nacho kisima, muhimu hiyo lazima
ZAFANANA
Sikiliza kwa makini, hasira ziweke kando
Lako jipe tumaini, kisima safi ni kondo
Utajitia mtoni, utaumudu mkondo
Watanga walinena, hizo zote zafanana
Bara na visiwani, kote nimepitia
Wamiliki visimani, hakuna asiyejutia
Wamelala malindoni, wajuvi wamepitia
Watanga walinena, hizo zote zafanana
Usijitie jutoni, rudi zako kisimani
Busara zako sioni, fikiri tena makini
Mapenzi yapo moyoni, hayapotei gharikani
Watanga walinena, hizo zote zafanana
Visima vina maudhi, na kweli vina madhara
Usiogope maradhi, vitamu vina madhara
Hatima yetu faradhi, nalo si masikhara
Watanga walinena, hizo zote zafanana
Maji tamu kisimani, sote twakimbilia
Kila mtu atamani, hakuna pakulilia
Asipoyanywa Hassani, chura atakimbilia
Watanga walinena, hizo zote zafanana
Tamati namalizia, rudisha zako hisani
Tanga nakaribia, nijiendee kisimani
Tuliza zako hisia, waulize makuhani
Watanga walinena, hizo zote zafanana
Chama
Gongo la Mboto DSM
Mwanangu Yakuonea, sikiza wangu usia
Ni mengi umeongea, yaani karibu kulia
Kobisi nilikulia, nimeshindwa kuvumilia
Nyumba wakaa mwenyewe, Kisima gharama tupu
Hujaona ya kununua, Maji yapo sikia
Kubaki jishebedua, kisima kujichimbia
Umekua ka Ngamia, Maji mengi kujinywea?
Nyumba wakaa mwenyewe, Kisima gharama tupu
Ungeweza jipatia, Kilimanjaro maji sawia
Kwa bei ya kutupia, Uhai wajimwagia
Na ladha ilo sawia, Sayona wajionjea
Nyumba wakaa mwenyewe, Kisima gharama tupu
SIO ZOTE ZAFANANA
Mgosi nafurahika, kwa wewe kurudi tena
Mwenzio nahangaika, maisha hayajafana
Hujafa hujaumbika, angalizo la rabana
Sio zote zafanana, chunguza utanambia
wembamba sio upana, jaribu kupambanua
Na usiku si mchana, hivi kweli hujajua?
Kikongwe hawi kijana, naomba kufafanua
sio zote zafanana, chunguza utanambia
Na fupi kamwe si ndefu, vipimo vi tofauti
Hata uwe umpofu, gogo huliiti jiti
Mfupa sio mnofu, tuulize watafiti
Sio zote zafanana, chunguza utanambia
Vya mombasa si vya bara, kimaisha na fikira
Na pwani haiwi ngara, mwembe hauwi mpera
Tafiti acha papara, uone kilicho bora
sio zote zafanana, chunguza utanambia
kuna zile za minato, nyingine zimeachia
Na hata kwa manukato, huwezi badilishia
utapatwa machafuko, na mengi yenye kadhia
sio zote zafanana, chunguza utanambia
SMG