Serikali yetu ijifunze kwa China kuhusu suala la kuzalisha ajira

Donatila

JF-Expert Member
Oct 23, 2014
7,563
21,665
Ndugu wana JF, Nimeyakuta haya mawazo Mahali nikaona si vibaya nikawaletea hapa msome na mjadili.

Na Elias Mhegera, Beijing

Miongoni mwa mambo niliyojifunza hapa China na hasa baada ya kuwa nimetembelea majiji manne tofauti katika kipindi cha mwezi mmoja ni jinsi serikali ilivyo makini katika kuzalisha ajira.

Kwa mfano hivi karibuni nilitembelea katika Jimbo la Hainan ambako hali ya hewa ni ya ukanda wa tropiki sawa na ilivyo kwa nchi nyingi za Bara la Afrika.

Historia ya Jimbo la Hainan ni ya kufurahisha kidogo, hasa kutokana na ukweli kwamba China kuna kipindi ilikuwa katika umaskini kama tuliokuwa nao sisi Tanzania kwa kiwango fulani.

Katika kipindi hicho maendeleo yalijikita katika baadhi ya maeneo ya mijini na mengine yakasahaulika. Jimbo la Hainan ni kama lilitelekezwa na vijana wengi walianza kulikimbia wakitafuta maisha kule walipoona kuna ridhiki zaidi.

Lakini wokovu wa jimbo hili ulitokana na baridi kali inayokuwapo katika majimbo mengine msimu wa baridi na kuliacha jimbo hili likiwa na hali ya joto kama ilivyo katika nchi nyingi za Kiafrika. Matokeo yake ni watu mbali mbali kukimbilia huko katika msimu wa baridi kali.

Walikuwa wanakuja watu kutoka mataifa mbali mbali kuanzia Urusi, Korea, Japan na hata Marekani na Uingereza ingawaje kwa idadi kubwa zaidi walitoka Urusi.

Watu hao wakati mwingine waliweza hata kujenga majengo ya muda ili wapate kuwa na makazi. Ndipo serikali ya China ikauchukua mwanya huo na kuanza kujenga majengo mengi yakiwamo mahoteli ya nyota saba.

Pia serikali ikakaribisha watu binafsi wenye mitaji yao waweze kujenga huko na mpango huo ukawa na tija kubwa. Serikali ikahama hata katika uwanja wa ndege wa zamani wa kimataifa wa Hainan ili kupisha ujenzi wa majengo ya uwekezaji katika eneo hilo.

Matokeo yake watu wakaanza kurejea kutafuta ajira mahali ambako walipata kupakimbia. Ukienda Hainan ya leo utapata picha ya miji kama vile Bagamoyo au Lindi kwani hiyo ni miji iliyowahi kuvuma na kisha ikakimbiwa.

Tofauti iliyopo sasa Hainan ni kwamba majengo ya kizamani yamehifadhiwa kwa ajili ya utalii wakati nchini Tanzania kila siku majengo ya zamani yanadondoka kutokana na kukosa utunzaji ni hivi karibuni tu hali hiyo ilijitokeza haijulikani ufadhili wa UNESCO katika uhifadhi wa majengo hayo ni wa kiwango gani.

Serikali ya China kwa upande wake imejizatiti kama ilivyokuwa kwa Marekani na Hawaii ndivyo serikali hii inawekeza Hainan. Miongoni mwa miji maarufu ya kitalii katika jimbo hili ni Jiji la Sanya ambapo mashindano ya kumtafuta mlimbwende wa dunia yamewahi kufanyika mara mbili.

Lakini pia ukiwa katika jimbo hili utakutana na maajabu mengine ya dunia ikiwamo kijiji cha kitalii cha Miao. Katika kijiji hiki imehifdhaiwa historia ya kale ya watu wa kabila la Li.

Watu hawa walikuwa na asili ya kuweka alama katika ngozi zao sehemu mbali mbali za miili na hasa usoni na mikononi kama ilivyokuwa kwa wamakonde wa Tanzania na Msumbiji.

Pia watu hawa walikuwa wakifuma nguo zinazotokana na magome ya miti. Utamaduni huo umehifadhiwa kwa sasa na serikali ya china na ndani ya kijiji hicho cha kitalii kuna watu takribani 2000 wakiwa wameajiriwa na kujiajiri.

Miongoni mwa mambo yanayofanyika humo ni mauzo ya kazi za kiasili kama vile dawa za Kichina, nguo zinazotokana na magome ya miti, mabegi, bangili lakini pia kuna kikundi kikubwa sana cha ngoma za asili.

Inapofikia kuzalisha ajira wachina hawana aibu watafanya kila jambo ili mradi watu wao wapate ajira. Ni katika jimbo hilo hilo la Hainan katika Jiji la Boao tulifika kuoneshwa dawa za asili.

Miongoni mwa watu waliokuwa wakisimama na kutoa ushuhuda kwa kundi kubwa la wanahabari wa ndani na nje wapatao 500 ni mabalozi wastaafu kila mmoja akieleza jinsi alivyoponywa na dawa zinazotokana na tiba asilia za China.

Wapo waliosema walipona macho, kisukari, shinikizo la damu na hata kurudisha kizazi. Dawa zao zimepakiwa katika muundo wa kisasa kabisa kiasi kwamba mtu utashawishika kuzinunua bila wasi wasi wowote.

Ni katika jimbo hilo hilo kuna bustani maarufu iitwayo; ‘Xinglong Tropical Botanical Garden’ ambayo nayo imekuwa ni kuvutio kikubwa na watu wengi za sasa wanakwenda hapo ili kuangalia mitishamba ambao baadhi ilihamishwa kutoka Afrika. Nina hakika baadhi ya miti hiyo ukija katika Bara la Afrika iliotoka wala unaweza usiipate na hata kusikia historia yake tu.

Katika bustani hiyo kunalimwa aina mbali mbali ya michai chai takribani aina tano. Lakini pia kuna maji mazuri ya matunda yatokanayo na madafu ambayo yamechanganywa na mitishamba, na kupata harufu na ladha nzuri bila hata kupitia kiwandani.

Lakini pia ni katika jimbo hilo ambako kuna kijiji cha Zhongliao kilichopo jirani na Jiji la Sanya. Kutokana na kubana matumizi watalii wengi walipendelea kufikia kwenye hoteli lakini walienda kula majumbani kwa wanavijiji.

Mara serikali ya China ikaligundua hilo ikaanza kukarabati nyumba za wanavijiji hao, ikaboresha mazingira yao na hata kuwajengea hoteli nyumbani kwao hapo hapo na kutoa mikopo ya friji na majiko.

Leo kijiji hicho kilichoanzishwa na ‘mama lishe’ ni mtaa mzuri kabisa wa sasa tayari hata mabwawa ya kuogelea yamejengwa ili watalii wakitoka kupata mlo wao wapitilizie kuogelea kabla ya kurejea hotelini walikofikia.

Je kwetu nini kimeua Muungano Dancing Troupe? Nini kimeiua Tanzania One Stars (TOT)? tutafakari pamoja…

Tuwasiliane: mhegera@gmail.com simu:
+86-18510699262
Maelezo ya picha
Kikundi cha ngoma za utamaduni katika kijiji cha asili cha kitalii cha Miao.
 
Back
Top Bottom