Hii serikali hata haijifunzi kutokana na makosa yake ya nyuma. Baada ya mikataba ya IPTL, Songa na Richmond tungetegemea wawe makini sana katika mikataba iliyofuata ili wasirudia upumbavu waliofanya ambao umeliingiza Taifa hasara kubwa wa kuingia mikataba ambayo Watanzania tulikuwa tunalanguliwa kwa bei mbaya na makampuni yaliyopewa mikataba yalikuwa hayana uwezo wa kusimamia mikataba hiyo. Tungekuwa na uwezo tungefukuza serikali nzima kuanzia Kikwete na baraza lake la mawaziri lote. Haya makosa mnayoyafanya lini yatakoma? Ufisadi kila kukicha. kila mnachokifanya lazima kitawaliwe na ufisadi. Mnaipeleka nchi pabaya kwa uroho wenu.
TRL yaliza wapinzani
na Kulwa Karedia na Happiness Katabazi
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
HATUA ya serikali kuendelea kuinusuru Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kwa kulipa mishahara ya wafanyakazi waliotaka kugoma, imeibua maswali huku baadhi ya wananchi wakitaka mkataba huo uchunguzwe.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alitaka mkataba huo upitiwe upya kwani kampuni hiyo imeonyesha kila dalili za utapeli.
Alisema lengo la serikali kulibinafsisha lililokuwa Shirika la Reli nchini (TRC), ilikuwa kuboresha huduma za usafiri pamoja na kuwalipa vizuri wafanyakazi wake.
Kwa sababu hiyo, Slaa alisema iwapo hata baada ya kulikodisha serikali ndiyo inayoendelea kulipa mishahara, hakuna sababu ya kuwa na mwekezaji huyo.
"Mkataba huo umeonyesha kila dalili za utapeli. Wawekezaji wameshindwa kuleta teknolojia mpya, wameshindwa kuwalipa wafanyakazi mishahara mipya, wameshindwa kila kitu na badala yake serikali ndiyo inayofanya kila kitu.
'‘Nafikiri tuamue kuuvunja mkataba huo au uchunguzwe tujue namna gani waliweza kupata zabuni hiyo wakati hawana uwezo," alisema Dk. Slaa.
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, alisema anashangazwa na huruma ya serikali ya kuibeba kampuni hiyo ya wawekezaji, kwa kulipa mishahara ya wafanyakazi kila mara, kwani kuna makundi mbalimbali, wakiwemo walimu wanaodai malimbikizo yao, lakini serikali imekuwa ngumu kulipa madeni hayo.
Profesa Baregu alisema umefika wakati wa serikali kuwaeleza wananchi mchakato wa kuipata kampuni hiyo ulikuwaje na kwa nini mazingira yake kiteundaji yanafanana na mkataba wa kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond.
"Tuelezwe wakala aliyeipigia debe kampuni hii, maana haiingii akilini mwekezaji amekuja kuwekeza na mara mbili mfululizo, ashindwe kulipa mishahara ya wafanyakazi.
'‘Wananchi tuamke na tuhoji mkataba huu, kwani una kila dalili ya ufisadi. Kama anashindwa kulipa mishahara, ataweza kuiendesha kampuni? Ifike mahala tuangalie, kampuni inapaswa kuendelea kufanya kazi au la," alisema Profesa Baregu.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wananchi hawana imani kama fedha zinazotolewa na serikali zinaweza kurejeshwa kwa sababu hazijaidhinishwa na Bunge.
"Sasa kuna kila sababu ya serikali kutoa maelezo ni jinsi gani TRL inaweza kurejesha fedha hizi ambazo ni kodi za wavuja jasho wa Tanzania wakati hali ya kipato chao ni cha chini," alisema Profesa Lipumba.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha wapinzani kuipigia kelele serikali kwamba hawapaswi kukurupuka kumpa mtu au mwekezaji rasilimali muhimu ya taifa kama hii ya TRC, bila kufanya uchunguzi wa kina juu ya uwezo wake.
"Jinsi hali ilivyo, ni wazi tunaelekea kwenye matatizo makubwa, tofauti na ilivyokuwa mwanzo, haya ni mambo yaliyotokea Kenya na Uganda walipobinafsisha reli zao, sasa hali imekuwa ngumu mpaka serikali inatafuta wawekezaji wengine," alisema.
Naye Mwenyekiti wa Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, alisema anashangazwa na uamuzi wa kumbeba mwekezaji huyo, wakati dalili zinaonyesha kuwa hana uwezo wa kujiendesha.
Mrema alisema mkataba wa TRL na serikali, hauna tija kwa taifa na kwamba ni bora shirika lingeendelea kuendeshwa na Watanzania wenyewe kuliko mwekezaji mbabaishaji.
"Serikali imebinafsisha mashirika kwa kigezo kwamba, Watanzania hatuwezi kuyaendesha, sasa kama hatuwezi kuyaendesha, mbona serikali imemleta mwekezaji huyo wa kigeni ambaye anashindwa kulipa hata mishahara ya wafanyakazi, kuleta mabehewa bora na kuboresha huduma za kampuni hiyo?" alihoji Mrema.
Alisema mkataba huo ni ufisadi mwingine na kuwataka wananchi kuanza kuupeleleza ni kina nani waliiwezesha kampuni hiyo kushinda zabuni na kuitahadharisha serikali kuacha tabia ya kuibeba kampuni hiyo, kwani kwa kufanya hivyo, inajidhalilisha mbele ya wananchi wake.
Akizungumzia mkataba huo, mkazi wa Mwenge, Jerome Steven, alihoji kwanini hadi sasa serikali haijauvunja mkataba huo kutokana na ubabaishaji iliokwishaonyeshwa.
Alisema serikali inapaswa kuueleza umma kwamba sh bilioni 3.6 ilizoikopesha TRL Machi mwaka huu, zilisharejeshwa, kwani ilitakiwa izilipe ndani ya miezi mitano.
Alipohojiwa na Tanzania Daima jana endapo serikali imeshatoa fedha hizo na kiasi ilichoahidi kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa miezi miwili, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, kwanza alimjia juu mwandishi kwa kumuuliza swali hilo, lakini kama hiyo haitoshi, alikataa katakata kusema chochote kwa madai kuwa suala hilo halimhusu.
"Nasema huu siyo wakati wa kuniuliza suala hili, leo (jana) hapa tumekuja kuzungumzia masuala ya fedha za wafadhili kwa ajili ya bajeti yetu," alisema Mkulo.
Baada ya majibu hayo, Mkulo akiwa ameambatana na maafisa wake, aliamua kuondoka.
Juzi Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), kiliahirisha mgomo waliokuwa wameutangaza kuanza jana, baada ya serikali kuingilia kati na kuahidi kuwalipa malimbikizo ya fedha zao pamoja na mishahara mipya ya miezi miwili, kuanzia Agosti hadi Septemba mwaka huu.
Uamuzi huo wa serikali, ulitangazwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Omar Chambo, baada ya kuongoza majadiliano kati ya menejimenti ya TRL, TRAWU na serikali.
Chambo alisema serikali imekubali kulipa mishahara ya wafanyakazi wote kima cha chini kutoka sh 160,00 hadi sh 200,000 kutoka Agosti hadi Septemba mwaka huu.
Alisema baada ya serikali kulipa malimbikizo hayo, TRL itaendelea kubeba mzigo wa kuwalipa wafanyakazi wake kama kawaida.
Machi mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliingilia kati mzozo huo na kutangaza hatua ya serikali kuikopesha TRL sh bilioni 3.6 kwa kipindi cha miezi mitano.
Zaidi ya wafanyakazi 3,200 walitoa notisi ya saa 48 juzi kwa uongozi wa shirika hilo kuwalipa nyongeza za mishahara yao na malimbikizo mengine, vinginevyo wangeanza mgomo wa nchi nzima leo.